WALIKUSUDIA KUTUUA

Miaka kadhaa imepita, lakini bado nakumbuka tukio lililotupata mimi na ndugu zangu. Ni tukio la kutisha, lakini Mungu ni mkuu! Kwa ufupi ilikuwa hivi:
 
Siku moja tulikuwa tumepanga kwenda katika mji mmoja mdogo nje ya jiji la Dar es Salaam. Tukaweka vizuri kila tulichotaka kwenda nacho kisha tukaingia ndani ya gari, aina ya Toyota Pickup. Tukaanza safari. Barabara tuliyoipitia ilikuwa mbaya, yenye mashimo mashimo, hata hivyo baada ya muda tulifika katika mji ule. Tukafanya kile kilichotupeleka, kisha tukaanza tena safari ya kurudi nyumbani. Wakati huo ilikuwa jioni, na giza lilikuwa linakaribia kuingia.
 
Baada ya kusafiri kwa dakika kadhaa, mbele yetu tukaona gogo moja refu limewekwa barabarani kuzuia magari yasipite! Na pembeni mwa barabara kulikuwa na vijiti vimesimikwa ili kuzuia magari yasipite pembeni. Loo tulishikwa na mshangao na kuanza kujiuliza maswali kwanini gogo lile limewekwa pale.
 
Nikajipa moyo, nikashuka kwenye gari na kuliondoa gogo lile kisha tukapita na kuendelea na safari.  Baada ya mwendo kidogo, tukakuta tena gogo limewekwa barabarani kuzuia tusipite, na safari hii lilikuwa gogo kubwa zaidi ya lile la mwanzo. Tulipotazama upande wa kulia wa gari mita kama saba hivi, tukamuona mtu mmoja ameshika upanga! Eneo hilo lilikuwa na miti mingi na nyumba za watu hazikuwepo karibu.
 
Sote kwa pamoja huku tukiwa tumejaa nguvu za Roho Mtakatifu, tulianza kukemea kwa Jina la Yesu. "Kwa jina la Yesu, kwa jina la Yesu Shetani umeshindwa..." Jina la Yesu lilifanya maajabu. Mtu yule hakuweza kutukaribia. Akawa kama anakata kata matawi ya miti.
 
Baada ya kukemea, nilipata ujasiri usiokuwa wa kawaida, nikashuka tena kwenye gari naa kuliondoa gogo lile. Nikaingia kwenye gari kisha tukapita na kuendelea na safari ya kurudi nyumbani. Ndani ya gari tulienda huku tukimshangilia na kumsifu Mungu kwa jinsi alivyotuokoa na wale waliokuwa wamekusudia kutuua na kuiba vile tulivyokuwa navyo. Hatimaye tulifika nyumabni salama
Hakika jina la Yesu lina nguvu. Ni jina lipitalo majina yote (Wafilipi 2:9). Unapokabiliwa na mabaya, liitie jina la Yesu.                                                                                                              By Daniel Chiza

Comments