NA BARAKA HIZI ZOTE ZITAKUJIRIA NA KUKUPATA USIKIAPO SAUTI YA BWANA,MUNGU WAKO.(Kumb. 28 : 2 ) * Sehemu ya mwisho *


Mtumishi Gasper Madumla


Haleluya…
Bwana Yesu asifiwe…

Labda tuangalie wale waliobarikiwa :
01.IBRAHIMU

Tukimtizama Ibrahimu anatupa mfano mzuri wa mtu aliyebarikiwa.Kamwe hutaona Ibrahimu akiomba BARAKA kwa Bwana Mungu bali yeye aliishi maisha ya Imani tu ,akilishika neno la Mungu na yote ambayo Bwana Mungu amuagizayo na Baraka za Mungu zikamfuata pale alipo.

Tazama kwa makini Habari za Ibrahimu pale Bwana Mungu alipomjaribu kwa kumuambia amchukue mwanae,mwana wake wa pekee,ampendaye,ISAKA,ili aende kumtoa sadaka.
Jambo hili ni gumu katika hali ya kawaida.
Maana ISAKA alikuwa ni kipenzi cha Ibrahimu,mtoto wa pekee.

Labda tungelisema kama hali hiyo ingelitokea kwa mlokole wa siku hizi,kwamba asikie sauti imuambiayo,amtoe mwanae,mwana wa pekee.Ninakuambia hakika angekemea sauti hiyo na kusema hiyo sio sauti ya Mungu inayomtuma kumtoa mwanaye wa pekee,Bali ni sauti ya shetani.
Lakini hali haikuwa hivyo kwa Ibrahimu,yeye Ibrahimu alitii sauti ya Mungu.Kutokana na kutii kwake Ibrahimu, kulimfanya ABARIKIWE.

Sasa chukulia habari hiyo kwa upande wa pili,tuseme kama Ibrahimu asingetii sauti ya Bwana Mungu.
Wewe unafikili ingekuwaje ?
Angebarikiwa ?

Basi ni dhahili kabisa asingepokea BARAKA kama asingetii sauti ya Bwana Mungu.Na ndio maana nakuambia BARAKA haziombwi!
Bali ni kutii sauti ya Bwana Mungu tu.

Tunasoma Mwanzo 22 : 17-18
“katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao;
na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; KWA SABABU UMETII SAUTI YANGU .”

Sikia :
Wengi tunadandia Baraka za Ibrahimu mpaka leo kwa sababu sisi wenyewe hatuishi maisha ya UTII wa sauti ya Mungu. Neno la Mungu linatuambia katika
Wagalatia 3 : 14
“ili kwamba baraka ya Ibrahimu iwafikilie Mataifa katika Yesu Kristo, tupate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani. ”

• Hivyo basi mkondo/njia ya Baraka ni UTII wa sauti ya Bwana Mungu.

Mfano :
Fikilia kuwa wewe ni mzazi wa watoto wawili katika familia yako. Katika watoto wako,mmoja ni mtii sana wa sauti yako na mwingine hatii kabisa kwa chochote umuambiacho.Unapowatuma kazi,mmoja hufanya mwingine hafanyi kabisa na wala hana muda kuisikiliza sauti/maagizo yako.
Ukweli ni kwamba utampenda sana Yule wa kwanza mwenye kutii,na kumchukia Yule wa pili asiyetii,ingawa wote ni wanao.
Kwa kumchukia mwanao haimaanishi kwamba utamnyima chakula Bali Chakula utampa lakini kuna upendo Fulani ataukosa.

Upendo huu ndio ule unatoa zawadi kwake hata kama hajaomba,bali utajikuta tu unachilia BARAKA kwake yeye anayesikia sauti yako.Na ndivyo ilivyo kwa Mungu kwetu sisi wanae.Tutakapoufurahisha moyo wa Bwana,Bwana atachilia Baraka kwa watu wake.

Haleluya…

Ipo sababu ya kuwepo kwa fundisho hili mahali hapa,Kwamba kanisa libadili muelekeo wake wa KUOMBA BARAKA maana wengine hufunga na kuombea BARAKA,hii ni makosa sana kiimani.

Nasema hivi :
Itakuwa utakaposikia sauti ya Bwana, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo yake yote ndipo Bwana, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani; na baraka zote zitakujilia na kukupata usikiapo sauti ya Bwana, Mungu wako.

Tumuangalie mtu wa pili aliyeshika neno la Mungu,kisha AKABARIKIWA

02. AYUBU.
Tunasoma Ayubu 1 : 1
“ Palikuwa na mtu katika nchi ya Usi, jina lake alikuwa akiitwa Ayubu; mtu huyo alikuwa mkamilifu na mwelekevu, ni mmoja aliyemcha Mungu, na kuepukana na uovu. ”

Chanzo kikuu cha mali za Ayubu ilikwa ni kwa sababu Ayubu alikuwa mtu mkamilifu mbele za Bwana.
Hata ile namna ya ulinzi wa mali zake ilikuwa ni kwa sababu Mungu alizungusha wigo wake,akalinda mali zake.

Sasa umeona namna Ayubu alivyokwenda na Mungu kwa kusikia sauti ya Bwana Mungu,kisha baadaye tunaona wingi wa mali zake zikiongezeka hata pale shetani alipoziangusha lakini Biblia inatuambia akapata mali nyingine zaidi ya zile za mwanzo.
Tunasoma
Ayubu 42 : 10

“ Kisha Bwana akaugeuza uteka wa Ayubu, hapo alipowaombea rafiki zake; Bwana naye akampa Ayubu mara mbili kuliko hayo aliyokuwa nayo kwanza. ”

• Ukitaka kubarikiwa basi ukubali kulishika neno la Mungu kwa usahihi na kuliishi,nawe utabarikiwa.

MWISHO.
UBARIKIWE.

Comments