Askofu aungana na Kakobe kutaka Tanganyika

Mtumishi wa MUNGU, Askofu Zacharia Kakobe
Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge Ngara, Severin NiweMugizi ameungana na Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zachary Kakobe kupigia debe Serikali ya Tanganyika.




Akizungumza katika mahojiano ofisini kwake mwishoni mwa wiki iliyopita, NiweMugizi alitaka Serikali kutobeza maoni ya wananchi wanaotaka Serikali ya Tanganyika kwa kuwa muungano uliopo unaunganisha nchi mbili.

Kauli hiyo inarandana na ile iliyotolewa na Askofu Kakobe juzi wakati akitoa mahubiri ya Pasaka, aliposema anaungana na Watanzania wanaodai Serikali ya Tanganyika na kuahidi kuwapa ari na shauku ya kuhakikisha inapatikana.

NiweMugizi ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), alisema ukosefu wa elimu ya uraia kwa Watanzania wasomi na wananchi, ndiyo kikwazo cha kutetea uzalendo kwenye muundo wa Muungano.

Alisema katika miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kumeibuka mambo mengi ya mpasuko wa umoja uliokusudiwa na waasisi wa kufanya mataifa mawili kuwa moja.

Alisema ili kuhakikisha Tanganyika inapatikana, lazima Serikali ya Jamhuri ya Muungano ikubali kuwa shirikisho, kwa kila nchi kupoteza baadhi ya mamlaka na masilahi ya taifa.

Pia, alisema katika kuanzisha Taifa la Tanzania, mamlaka zilizokuwapo Umoja wa Mataifa (UN), ziliondolewa kwa nchi ya Tanganyika na Zanzibar na kuunda kiti kimoja cha Tanzania.

“Zanzibar kutangaza kuwa ni nchi ndani ya nchi nyingine kwa mamlaka kamili ya Serikali na kutaka kujiunga na taasisi za kimataifa, inaonyesha kuwa Tanzania imemeguka kipande katika Muungano,” alisema Askofu NiweMugizi.

Alisema Muungano wa sasa una nyufa nyingi zaidi ya zile alizoona Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na viongozi wengine.

Alisema miongoni mwa mambo yanayosukuma wananchi kudai Tanganyika ni kupewa elimu ya uraia kufahamu vyema historia ya Muungano na nyufa zilizopo, hasa baada ya Zanzibar kuwa na mamlaka kamili ya dola.

Alisema wananchi wanatakiwa kuelimishwa zaidi manufaa ya Muungano, fursa zinazopatikana na changamoto zake katika kuutetea na kuulinda.

Askofu NiweMugizi alisema serikali mbili ni maoni ya viongozi waliopo ndani ya CCM, ambao asilimia kubwa hawawakilishi Watanzania, ingawa ni sehemu ya Wazanzibari na Watanganyika.
Kuhusu mchakato wa Bunge Maalumu la Katiba, huyo alisema kupatikana kwa Katiba Mpya lazima kuwepo misingi inayotetea haki za raia, demokrasia ya kweli na utashi wa watawala bila kuingiliwa na msimamo kisiasa.
Alionyesha wasiwasi wa kupatikana kwa Katiba Mpya, kwani wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanatetea misimamo ya vyama vyao na hawapo tayari kumsaliti aliyewateua kwa sababu alitangaza msimamo wake alipolizindua.
“Rais (Jakaya Kikwete) wakati anazindua Bunge hilo kwa sababu ana mamlaka kisheria, alivunja taratibu, kwani asingelihutubia Bunge kwa kushinikiza Jaji (Joseph) Warioba kutangulia kuwasilisha Rasimu ya Katiba,” alisema Askofu NiweMugizi na kuongeza:  “Hotuba ilijikita kutangaza msimamo na mtazamo wa CCM kutaka serikali mbili, kwa kile tunachokiona ni kukumbatia madaraka ili viongozi waliopo wasipoteze nafasi, watawale milele, hata waanzilishi wa Tanganyika wapo hadi leo.”
 
Alisema mchakato wa kuwapata wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba ulipata hitilafu baada ya kuingiza wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na Wawakilishi wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, ambao kwa kiwango kikubwa ndiyo wasemaji kuliko wajumbe 201 waliotokana na taasisi mbalimbali za kiraia.

Chanzo:Mwananchi

Comments