ONDOA MAJITU MAISHANI MWAKO.



 
BWANA YESU asifiwe ndugu yangu.
Leo nina ujumbe wa ajabu sana ambao MUNGU amenipa ili nikuletee. Ujumbe unahusu MAJITU.
Watu wengi wanatamani kufika mahali fulani kimaisha lakini  kuna vitu ni vikwazo vya kuwakwamisha, hivyo vikwazo ndio JITU ninalozungumzia leo.
1 Samweli 17:31-46 ‘’Na maneno hayo aliyosema Daudi yaliposikiwa, watu wakamweleza Sauli; naye akatuma mtu kwenda kumwita. Daudi akamwambia Sauli, Asizimie moyo mtu ye yote kwa ajili ya huyu; mimi mtumishi wako nitakwenda kupigana na Mfilisti huyu. Sauli akamwambia Daudi, Huwezi wewe kumwendea Mfilisti huyu upigane naye; maana wewe u kijana tu; na huyu ni mtu wa vita tangu ujana wake. Daudi akamwambia Sauli, Mtumishi wako alikuwa akichunga kondoo za baba yake, na alipokuwa akija simba, au dubu, akamkamata mwana-kondoo wa lile kundi, mimi hutoka nikamfuata, nikampiga, nikampokonya kinywani mwake; na akinirukia, humshika ndevu zake, nikampiga, nikamwua. Mtumishi wako alimwua simba na dubu pia; na huyu Mfilisti asiyetahiriwa atakuwa kama mmoja wao, kwa sababu amewatukana majeshi ya MUNGU aliye hai. Daudi akasema, BWANA aliyeniokoa na makucha ya simba, na makucha ya dubu, ataniokoa na mkono wa Mfilisti huyu. Sauli akamwambia Daudi, Enenda, na BWANA atakuwa pamoja nawe. Ndipo Sauli akamvika Daudi mavazi yake ya vita, akamtia chapeo cha shaba kichwani, akamvika dirii. Naye Daudi akajifunga upanga juu ya mavazi yake, akajaribu kwenda; maana alikuwa hajavijaribu. Daudi akamwambia Sauli, Siwezi kwenda na vitu hivi, maana sikuvijaribu. Basi Daudi akavivua. Akaichukua fimbo yake mkononi, akajichagulia mawe laini matano katika kijito cha maji, akayatia katika mfuko wa kichungaji aliokuwa nao, maana ni mkoba wake, na kombeo lake alikuwa nalo mkononi mwake, akamkaribia yule Mfilisti. Huyo Mfilisti naye akamsogelea Daudi na kumkaribia; na mtu yule aliyemchukulia ngao yake akamtangulia. Hata Mfilisti alipotazama huku na huku, akamwona Daudi akamdharau; kwa kuwa ni kijana tu mwekundu, tena ana sura nzuri. Mfilisti akamwambia Daudi, Je! Mimi ni mbwa hata umenijia kwa fimbo? Mfilisti akamlaani Daudi kwa miungu yake. Mfilisti akamwambia Daudi, Njoo huku kwangu; nyama yako nitawapa ndege wa angani na wanyama wa mwituni. Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la BWANA wa majeshi, MUNGU wa majeshi ya Israeli uliowatukana. Siku hii ya leo BWANA atakuua mkononi mwangu, nami nitakupiga, na kukuondolea kichwa chako, nami leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya majeshi ya Wafilisti, ili kwamba dunia nzima wajue ya kuwa yuko MUNGU katika Israeli. ‘’.
-Umepanga kwenda mkoa Fulani ili ukaanze ajira yako ambayo umetafutiwa huko lakini nauli ikawa kikwazo, nauli hiyo ndio Jitu linalokukwamisha.
-Watu wengi wamezuiliwa na majitu katika maisha yao.
Wana wa Israeli walikuwa na nguvu sana ila tu wakisikia jina Goliathi wanaogopa maana Goliathi lilikuwa ni jitu ambalo hawakuwahi kulishinda.
-Mfalme Sauli aliliogopa jitu Goliathi.
-Kaka zake Daudi waliliogopa hili jitu.
-Waisraeli waliliogopa hili jitu lakini Daudi kijana mdogo  aliijua siri ya kuliondoa hili jitu.
-Wewe ndugu yangu najua una majitu mengi tu maishani mwako je unajua siri ya kuyaondoa?
Kuna watu majitu yao ni madeni, yaani umeshindwa kuyaondoa majitu madeni katika maisha yako.
Jitu ukiliogopa litakusumbua sana, ona jinsi ambavyo Goliathi aliwadharau Wanajeshi wa Israeli hadi mfalme wao Sauli. Walikuwa wanaweza kusema chocgote walichotaka kusema lakini akitokea tu jitu Goliathi wote wanakimbia mbio. Jitu huyu alitisha na kuwasumbua sana wana wa Israeli kama ambavyo wewe leo unavyosumbuliwa na majitu. Majitu yako leo yanaweza kuwa kiburi, yaani kila ukiomba hupokei kwa sababu una kiburi na kila siku wewe ni mtu wa kwanza kuwatukana watumishi wa MUNGU. Kumbuka kwamba kwa MUNGU kila jambo litatolewa hesabu yake, na yawezekana kabisa hesabu yako imeanza kutolewa ndio maana hupokei hadi pale ambapo utaliondoa jitu kiburi na kuacha kuwatukana watumishi wa MUNGU.
Je unataka kuyaondoa majitu yote katika maisha yako?
1 Yohana 3:8b inasema ‘ Kwa kusudi hili Mwana wa MUNGU alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi.  ‘’.
BWANA YESU alikuja ili tu kila kazi yote ya  shetani iondoke kwa wanadamu na katika kazi zake shetani, majitu ni sehemu muhimu ya kazi hizo za shetani na kwa kutumia majitu hayo, shetani huwatesa sana watu wa MUNGU.
Je unataka kuyaondoa majitu maishani mwako?
Mathayo 11:28 inasema ‘’Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. ‘’
BWANA YESU leo anatutaka  tuyapeleke kwake majitu yote yanayotusumbua ili atupumzishe.
Kaka na Dada nakuomba kimbilia kwa YESU kwenye uzima. Majitu yatakuachia na utakuwa huru tena huru kweli kweli.
Bartimayo upofu ndio ulikuwa jitu lake lakini aliijua siri ya kuliondoa jitu hilo la upofu na ndio maana bada ya kukimbilia kwa YESU uzima uliingia kwake.
Ndugu kimbilia kwa YESU leo na majitu yote yataondoka kwako.
Kipindi cha nyuma mimi nilikuwa mhudhuriaji mzuri sana wa ibada kanisani, sikujua kuokoka ni nini na sikutaka kuokoka, nilijua kuokoka ni kuhama dhehebu langu zuri  na sikuona faida kabisa ya kuokoka, niliendelea kusali lakini bila uwepo wa MUNGU wala hofu ya MUNGU hata kidogo, ilikuwa ni jambo la kawaida sana kwenda kanisani ni nikitoka tu kanisani naanza kutenda dhambi hata nyumbani sijafika, siku nyingine nilikua nawahi kutoka kanisani ili tu nikafanya machukizo mbele za MUNGU, dhambi ilikua jitu baya sana kwangu, nilitamani kuacha lakini sikuweza, na licha ya dhambi kuwa jitu kwangu, jitu jingine kwangu lilikuwa ni uzingizi yaani kila nikiingia tu kanisani usingizi unanisumbua hadi ibada inaisha, nilidhani ni jambo dogo kumbe hili jambo lilikuwa ni jitu kubwa sana, yaani adui alihakikisha kila jumapili sipati neno la MUNGU. Licha ya hayo majitu mawili, kulikuwa na jitu jingine kubwa sana ambalo ni kusinzia kila nikianza kusoma Biblia, yaani kila nikianza kusoma Biblia hata kabla sijamaliza mistari miwili lazima nisinzie, hali hii ilinitesa sana na kuniumiza sana maana nilitamani sana kuisoma Biblia na kuielewa lakini jitu usingizi alinishinda, ndipo baadae kabisa nikiwa Zanzibar niliisikia sauti ya MUNGU ikiniambia niende kanisani maana nisipoenda kuna kifo mbele yangu, niliogopa sana lakini sauti hiyo ilizidi na kuzidi na kupelekea kwenda kanisani, na wakati huu MUNGU aliniongoza kutafuta kanisa kwa masaa 4 maana kila kanisa nikienda ndani yangu naambia kwamba  ‘’ Sio hapo nilipokuagiza uende’’ hadi kwa baadae nikajikuta nakutana na mchungaji wangu wa Zanzibar ambaye MUNGU alimuandaa anisubiri stand, tukaenda naye kanisani na siku hiyo nikaokoka. Na tangu nimeokoka mwaka 2008 sijawahi kusinzia kanisani, sijawahi kusinzia kwa sababu ya kusoma Biblia na dhambi zile zilizokuwa zinanisumbua zamani kwa sasa haziniwezi tena. Tangu siku nimeokoka , majitu hayo BWANA YESU ameyaondoa maishani mwangu.
Ndugu yangu tambua neno hili ya kwamba ukitaka majitu yakukimbie basi mpe BWANA YESU maisha yako na liishi neno la MUNGU.
-Majitu mengi yanayokubabili maishani mwako ni kwa sababu hujajua tu jinsi ya kuyaondoa.
Siri ya kuyaondoa ni kumkabidhi YESU majitu hayo na yeye atayaamuru yarudi kuzimu na kukuacha wewe ukiwa huru.
Ni kweli kabisa Goliathi alikuwa ni jitu linalotisha sana kwa waisraeli lakini Daudi kijana mdogo alijua jinsi ya kuliondoa majitu kama haya. Ndio maana Daudi akakumbuka jinsi ambavyo MUNGU alimshindia kwenye majitu makubwa kama simba na dubu. Nampenda Daudi kwa maneno haya aliyoliambia jitu Goliathi  ‘’BWANA leo atakuua mikononi mwangu, na Dunia nzima itajua kwamba yuko MUNGU katika Israeli.’’
Hata wewe leo yaambia hayo majitu kwamba ‘’ Ewe jitu ugonjwa leo utajua kwamba yuko MUNGU kwangu, na kwa sababu MUNGU yuko upande wangu basi leo majitu yatatoka yote.’’
Kwa jina la YESU KRISTO majitu yote yatoke kwangu.
Kwa jina la YESU umeshinda.

Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
                     MUNGU akubariki sana .
                      Ni mimi ndugu yako
                       Peter M Mabula
                 Maisha ya Ushindi Ministry.
                           0714252292 
                     mabula1986@gmail.com
                 MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.
 MUNGU Akubariki.

Comments