SABABU 11 ZA KUJIFUNZA NENO LA MUNGU.



BWANA YESU asifiwe.

Karibu tena siku ya leo tujifunze ujumbe usemao ‘’sababu za sisi kujifunza neno la MUNGU.’’

Mathayo 7:24-25  ‘’Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba. ‘’

Si rahisi kujifunza kitu kama huna umuhimu nacho.

Sio rahisi kutenga muda wako kwa ajili ya kujifunza jambo Fulani kama huna umuhimu na jambo hilo.

Sio rahisi kulipa gharama iwe ni pesa yako au muda wako ili tu kujifunza kitu Fulani, kama kitu hicho hakina umuhimu kwako.

Kama jambo ni la muhimu kwetu lazima tu tutenge muda wa kujifunza jambo hilo.

Mwaka 1994 nikiwa na miaka  miaka 8 nilianza kufundishwa kilimo, masomo haya ya kulima hayakuihitaji hiari yangu bali ilikuwa ni lazima, Walezi wangu walikua na lengo zuri tu kwamba kama nikifanikiwa kuwa mkulima mzuri basi ningeishi maisha mazuri kijijini kwetu Isambara, kilimo ni uti wa mgongo wa kijiji kile, Mwaka 1 baadae yaani mwaka 1995 nilianza darasa la kwanza, shuleni ilikuwa ni mbali sana zaidi ya kilomita 9 na wakati huu bado nilikuwa naendelea na kujua kulima,  Kila siku nilitakiwa kuwahi kurudi nyumbani  kutokea shuleni ili tu kuendelea na  kilimo, Kama nitachelewa kufika basi nijue lazima tu nikute matuta 5 hadi 8 ya kulima ambayo lazima niyamalize ndipo niende nyumbani, kilimo hakikuwa na mchezo, hivyo ilikuwa ni wajibu wangu kuwahi nyumbani nikitokea shuleni ili kumalizia viporo vya matuta. Walimu wangu wa nyumbani walitimiza wajibu wao wa kuhakikisha nakua mkulima bora ili nisiwasumbue baadae. Walinisaidia sana maana miaka 2 baadae nikiwa darasa la 3 nililima majaruba mawili ya mbunga na kutoa magunia 3 ya mchele  na hivyo kupelekea mimi na kaka yangu kuwa wanafunzi wa kwanza kutoka kitongoji chetu kununua baiskeli ili tuwe tunawahi shuleni ambako ni mbali sana na walimu ni wakali kupita kawaida. Kujifunza kulima  kule kulinisaidia na kunifanya niwe mkulima mzuri.  Darasa lile la kilimo hata kama lina magumu yake lakini lilinisaidia sana, Vile vile kujifunza neno la MUNGU ni darasa jema na lenye manufaa kwa roho yako na uzima wako. Luka 11:28 ‘’ Afadhali, heri walisikiao neno la Mungu na kulishika. ‘’

Nimesema huwezi kutoa muda wako kujifunza kitu ambacho hakina manufaa kwako,  lakini kama kina manufaa basi utajifunza kwa gharama zozote.  Kilimo nilijifunza kwa gharama kubwa lakini kilinisaidia sana hivyo hivyo napenda kukuambia kwamba hakuna kitu muhimu kujifunza kama neno la MUNGU maana .

-Ahadi ya MUNGU kwako utaikuta ndani ya neno.

-Baraka zako utazikuta ndani ya neno la MUNGU.

-Ushindi wako utaukuta ndani ya Neno.

-Ulinzi wako unatokana na ahadi ya MUNGU kwako, ambayo iko ndani ya neno.

Neno la MUNGU( Biblia) ni muhimu sana katika maisha yako. MUNGU kila siku anaandaa watumishi wake kwa ajili tu ya neno likufikie, yaani hakuna ambako hutapata mafundisho ya neno la MUNGU, Kama uko chumbani kwako ukifungulia tu Wapo FM au Redio yeyote ya dini lazima utakutana na mahubiri, Semina ndio zipo kila sehemu, Nyimbo za dini ziko kila sehemu hadi kwenye simu yako hapo ulipo, Mikutano ya injili ipo kila mahali, Kanisani ndio kabisaaaaa mahubiri kila siku. Ni MUNGU anazungumza na wewe, hata mitandaoni wapo watumishi wengi sana ambao MUNGU amewaagiza kulipeleka neno lake huko. Yaani kama kuna mtu ataenda jehanamu, basi ataenda kwa kupenda kwake mwenyewe ila kama maonyo na neno la MUNGU lazima tu alilipata.

Huu ni upendo mkuu sana wa MUNGU kwetu.

Nimetoa mfano na maelezo ili tu uone umuhimu wa kujifunza neno la MUNGU na faida zake.

Na sasa nakuletea kiini kabisa cha somo letu yaani SABABU AMBAZO ZINATUFANYA SISI WATEULE WA KRISTO KUJIFUNZA NENO LA MUNGU SIKU ZOTE.

Ziko sababu nyingi sana za kujifunza neno la MUNGU lakini muda huu nakuletea sababu 3 kuu za wewe na mimi kujifunza neno la MUNGU kila mara.

SABABU 11 ZA KUJIFUNZA NENO LA MUNGU KILA MARA.

              1.KWELI YA INJILI YA YESU.

 2 Timotheo 2:1-2 ‘’Basi wewe, mwanangu, uwe hodari katika neema iliyo katika KRISTO YESU. Na mambo yale uliyoyasikia kwangu mbele ya mashahidi wengi, hayo uwakabidhi watu waaminifu watakaofaa kuwafundisha na wengine. ‘’
-Tunajifunza neno ili tukawafundishe na wengine maana hii ndio kweli ya injili.


Matendo 19:9-10 ‘’Lakini wengine walikaidi, wakakataa kuamini, wakiitukana ile Njia mbele ya mkutano; basi, akaondoka akawaacha, akawatenga wanafunzi, akahojiana na watu kila siku katika darasa ya mtu mmoja, jina lake Tirano. Mambo haya yakaendelea kwa muda wa miaka miwili, hata wote waliokaa Asia wakalisikia neno la BWANA, Wayahudi kwa Wayunani. ‘’
-Huwezi ukanyamaza ikiwa BWANA amekupa agizo, MUNGU anataka watu wajifunze neno hivyo huwapamzigo watumishi wake ili tu neno litufikie na tujifunze.
  Matendo 20:20 ‘’ya kuwa sikujiepusha katika kuwatangazia neno lo lote liwezalo kuwafaa bali naliwafundisha waziwazi, na nyumba kwa nyumba, ‘’
-Mitume walipewa mzigo na MUNGU wa kufundisha neno la MUNGU.
-Na hata leo MUNGU anainua maelfu ya watumishi ili tu neno lake litufikie.
-MUNGU anataka tujifunze neno lake. 

              2. MITUME WALIAMLIWA NA BWANA YESU.

Mathayo 28:19-20 ‘’ Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la BABA, na MWANA, na ROHO MTAKATIFU; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari. ‘’

Marko 16:15-16 ‘’Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa ‘’

                 3.TUTAKUWA NA MSINGI IMARA KWA AJILI YA IMANI YETU.

 2 Timotheo 3:16-17 ‘’ Kila andiko, lenye pumzi ya MUNGU, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa MUNGU awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema. ‘’

                4. YESU KRISTO  ATAKUWA NA SISI.

Marko16:20 ‘’ Nao wale wakatoka, wakahubiri kotekote, BWANA akitenda kazi pamoja nao, na kulithibitisha lile neno kwa ishara zilizofuatana nalo.] ‘’

           5.TUNAKUWA TUNASHIRIKI PENDO LA MUNGU.

 Yohana 14:21-24 ‘’Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na BABA yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake. Yuda (siye Iskariote), akamwambia, BWANA, imekuwaje ya kwamba wataka kujidhihirisha kwetu, wala si kwa ulimwengu? YESU akajibu, akamwambia, Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na BABA yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake. Mtu asiyenipenda, yeye hayashiki maneno yangu; nalo neno mnalolisikia silo langu, ila ni lake BABA aliyenipeleka.

           6. TUNAKUWA NA UHURU WA KIROHO.

 Yohana 8:31-32 ‘’ Basi YESU akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru. ‘’, Warumi 8:1 ‘’Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika KRISTO YESU. ‘’.



            7. ILI TUWE NA HOFU YA MUNGU AMBAYO ITATUFANYA TUSITENDE DHAMBI.

Zaburi 36:1 ‘’Kuasi kwake yule mwovu hunena moyoni mwake, Hakuna hofu ya MUNGU mbele ya macho yake. ‘’

            8. NENO LA MUNGU HUTUONGOZA  KUTENDA MEMA.

Zaburi 119:105 ‘’ Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu. ‘’
-Likituongoza hili neno la MUNGU tunalojifunza, tutamaliza safari salama.

          9. NENO NI CHAKULA CHA KULETA AFYA KATIKA ROHO ZETU.

Mathayo 4:4 ‘’ Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha MUNGU. ‘’

             10.  KWA SABABU NENO LA MUNGU HALITAPITA KAMWE.

Mathayo 24:35 ‘’ Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe. ‘’

Waebrania 4:12 ‘’ Maana Neno la MUNGU li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo. ‘’

             11. NENO LA MUNGU HUTUPA UJASIRI KATIKA YOTE,

Matendo 4:31 ‘’ Hata walipokwisha kumwomba Mungu, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri. ‘’
Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. ROHO MTAKATIFU aliyenipa ujumbe huu ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
                     MUNGU akubariki sana .
                      Ni mimi ndugu yako
                       Peter M Mabula
                 Maisha ya Ushindi Ministry.
                           0714252292 
                     mabula1986@gmail.com
                 MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.
 MUNGU Akubariki.

Comments