SIRI ZOTE ZA WANADAMU ZITALETWA HUKUMUNI.




BWANA YESU asifiwe ndugu yangu.

Karibu tujifunze.

Mhubiri 12:14 ‘’Kwa maana MUNGU ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au likiwa baya. ‘’

Kila kazi, kila neno la siri  vitaletwa hukumuni.

Kila mtu ana kazi yake, kila mtu anapenda kuwa na kazi yake , Kila mtu ana matarajio ya kuwa na kazi yake.

Kazi hapa inamaanisha yote tunayoyatenda ikiwemo na kazi zetu za kuajiriwa zitaletwa hukumuni.

-        Huwa najiuliza hivi Daktari unayetoa mimba kisa tu umesomea, Je MUNGU anakuchukuliaje?

-        Askari unaye kula rushwa, je MUNGU anakuchukuliaje?

-        Wakili unayetetea uongo ambao ni dhahiri, Je MUNGU anakuchukuliaje?

-        Hakimu unayepotosha hukumu ili tu kuwapendezesha watu Fulani, Je MUNGU anakuchukuliaje?

-        Wewe unayetumia kazi yako ili tu kuwanyanyasa wengine, je MUNGU wa mbinguni anakuchukuliaje?

-        Mganga wa kienyeji ndio kabisa umembeba shetani kuanzia mwilini mwako hadi kwenye hirizi unazotumia, Je MUNGU aliye hai anakuchukuliaje?

Neno la MUNGU linasema kila kazi italetwa hukumuni.

Wengi wamepelekwa motoni na kazi zao walizokua wanazifanya wakiwa duniani.

Kazi nyingi ni njema  lakini zikiingiliwa na shetani zinakuwa mbaya sana.

Badala ya kutenda haki , wengi hutenda uovu kupitia kazi zao. MUNGU atusaidie.

Kazi nyingi hata neno la MUNGU linazikubali mfano Luka aliyeandika kitabu cha Luka mtakatifu na matendo ya mitume alikuwa Daktari lakini hakutoa mimba na tena kazi yake ilikuwa njema kwa MUNGU.

-Watu wa TRA ni muhimu sana kwa taifa lakini neno la MUNGU linasema juu yao kwamba ‘’ Msitoze kitu zaidi ya mlivyoamriwa-Luka 3:12’’

-Wanajeshi, Polisi, mgambo na askari magereza ni muhimu sana katika taifa letu lakini neno la MUNGU linasema juu yao kwamba ‘’ Msimdhulumu mtu, Msimshitaki mtu kwa uongo, tena mtoshewe na mishahara yenu- Luka 3:13’’

Ndugu yangu

-usikubali kazi yako ikutenge na MUNGU wako.

-Usikubali kazi yako ikutenge na uzima wa milele.

-Usikubali kazi yako ikutenge na mbingu.

-Usikubali kazi yako ikutenge na uwepo wa MUNGU maishani mwako.

Kina Daudi walikuwa wafalme lakini walimpendeza MUNGU, Kina Yusufu walikuwa mawaziri wakuu lakini walimpedeza MUNGU, Kazi yako ndugu isikutenge na MUNGU wako.

Nemesema kila mtu ana kazi yake, haijarishi ni kazi nzuri au ni kazi mbaya. Wengine kazi zao ni uzinzi, wengine kazi zao ni kujiuza, wengine kazi zao ni ulevi , wengine kazi zao ni uongo. Hizo zote ni kazi na zitaletwa hukumuni.

Hakuna asiye na kazi, yawezekana wewe hujaajiriwa serikalini lakini kazi yako ikawa ni umbeya na uchonganishi.

Kila kazi italetwa kwenye mizani ya MUNGU ili kuhukumu.

Usikubali kazi yako ikawa machukizo kwa MUNGU.

Baada ya kuongelea kazi sana tugeukie Neno la siri.

Nen la siri nalo litaletwa hukumini.

Haijarishi neno hilo ni jema au baya.

BWANA YESU anasema katika Mathayo 12:36  kwamba ‘’Basi , nawaambia, kila neno la siri watakalolinena wanadamu, Watatoa hesabu ya neno hilo siku ya hukumu. Kwa kuwa kwa maneno yako utahesabiwa haki na kwa maneno yako utahukumiwa.’’

Nachopenda ujue pia ni kwamba kila neno liwe zuri au baya huanzia moyoni na baada ya hapo ni kitendo.

Mawazo yako yote kwa MUNGU yanafahamika. Ndugu hata kile ambacho ni siri ya moyo wako tu, hujawahi kumwambia mtu lakini napenda utambue kwamba kwa MUNGU kinafahamika.

Ndugu zangu tuchunge sana maneno ya vinywa vyetu, tusicheke na watu kwa nje tu huku mioyoni mwetu tunawachukia , na mioyoni mwetu tunatamani wafe kabisa.

Kazi yako itahukumiwa na pia maneno ya kinywa chako yatahukumiwa. Ndugu zangu tuwaze mema na tutende mema. Tuwabariki watu na usithubutu kuwalaani watu kwa kinywa chako.

Ila Kama kuna jambo la siri baya ambalo unalo, na uovu huo umeshindwa kabisa kuacha nakushauri usifanye siri, waone watumishi wa MUNGU waaminifu na watakuombea utapona juu ya hilo.

Kusikitika tu kwamba uongo imekuwa sehemu ya maisha yako na umeshindwa kuacha, haitakusaidia, ni heri kwenda kanisani na kumwona mchungaji ili akuombee.

Kinywa chako kisikutenge na MUNGU wako.

Tumia kinywa chako kwa mazuri, maana kinywa chako kinaweza kusababisha uzima au mauti.

Hata kuokoka tunaokoka baaya ya kumkiri BWANA YESU kwa vinywa vyetu na kuanza kuukulia wokozi katika mafundisho kanisani.

Warumi 10:9-11 ‘’ Kwa sababu, ukimkiri YESU kwa kinywa chako ya kuwa ni BWANA, na kuamini moyoni mwako ya kuwa MUNGU alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika. ‘’

Njia nzuri ya kukitumia kinywa chako  ni katika;


1. Kuwaongoza watu kutenda mema.

               2.  Kuwafundisha watoto wetu kumjua MUNGU  na wajue MUNGU anataka nini kwao.

          3.  Kuwafariji wengine katika upendo wa KRISTO
                  4.  Kuwashirikisha wengine  wokovu wetu.

       5.  Kuwaombea wengine ili MUNGU awasaidie.

               6.   Kukemea dhambi na kuonya watenda mabaya.

7.  Kumshukuru MUNGU kwa maombi.


Tumia kinywa chako kwa hayo na MUNGU akubariki sana.

Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
                     MUNGU akubariki sana .
                      Ni mimi ndugu yako
                       Peter M Mabula
                 Maisha ya Ushindi Ministry.
                           0714252292 
                     mabula1986@gmail.com
                 MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.
 MUNGU Akubariki.

Comments