TAMASHA LA MATUMAINI, NKONE, MWAIPAJA KUACHA HISTORIA TAIFA



Mkali wa muziki wa Injili, Upendo Nkone.

GUMZO kubwa kwa sasa mjini ni tamasha la Usiku wa Matumaini linalotarajiwa kufanyika Agosti 8, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar ambapo burudani kabambe kutoka kwa wakali wa muziki wa Injili, Upendo Nkone, Martha Mwaipaja, Ambwene Mwasongwe, Angel, Paul Clement na wengine kibao watawalisha mashabiki Neno la Mungu.


Ambwene Mwasongwe.

Usiku wa Matumaini ni tamasha kubwa ambalo hutumika kuwaunganisha Watanzania huku asilimia 20 ya mapato yake ikichangia mamlaka ya elimu na kuhusisha burudani tofauti kwa kuwaunganisha mastaa kibao kutoka ndani na nje ya nchi katika jukwaa moja.

Mkali wa wimbo wa Hapa Nilipo, Upendo Nkone, atakuwa mstari wa mbele katika kulitikisa jukwaa kwa kuimba nyimbo zake zote kali ikiwa ni pamoja na Haleluya Usifiwe, Mwambie Yesu, Unastahili Kuabudiwa, Usinipite Bwana na nyingine nyingi.

Nkone ambaye amekuwa akisifika kutokana na kuwa karibu na mashabiki wake, amelithibitishia Championi Jumatatu kuwa, Agosti 8 atakata kiu ya burudani kwa mashabiki wa nyimbo za Injili kwa kuimba nyimbo zake zote kali zinazotikisa.

“Mashabiki wangu waje kwa wingi Uwanja wa Taifa siku ya tukio ili kukata kiu ya muziki wa ‘Gospo’ kwa sababu nitaimba nyimbo zangu zote kama Haleluya Usifiwe, Unastahili kuabudiwa, Mwambie Yesu na nyingine zote,” alisema Nkone.


Mkali wa muziki wa Injili, Martha Mwaipaja,

Baada ya kinara huyo wa muziki wa Injili kushuka, jukwaa litashambuliwa na mwanamuziki mkali kutoka Mbeya, Martha Mwaipaja ambapo atahakikisha anakata kiu ya mashabiki kwa kutoa burudani babkubwa kupitia nyimbo zake zinazotamba ambazo ni Tusikate Tamaa na Ombi Langu kwa Mungu.

Martha ambaye husifika kwa sauti ya kuvutia, amekuwa akifanya vizuri katika tasnia hii ya muziki wa Injili, hasa anapocheza na jukwaa kuwaburudisha mashabiki wanaojitokeza katika shoo zake mbalimbali, ameliambia Championi Jumatatu kuwa, tayari ameanza mazoezi kwa ajili ya kuhakikisha siku hiyo mashabiki wanaridhika kwa Neno la Mungu kupitia muziki wa Injili.

“Nipo nafanya mazoezi ili kuwa vizuri na kufanya kitu cha tofauti siku hiyo jukwaani, muda mrefu mashabiki wamekuwa na hamu na nyimbo za Injili katika jukwaa moja, naamini kabisa siku hiyo watafaidi sana sambamba na kumtukuza Bwana.

“Unajua mashabiki wa muziki wa Injili wanakosa shoo za mara kwa mara, kwa hiyo inapotokea nafasi kama hii, tunahakikisha tunakonga vilivyo nyoyo za mashabiki na hatubakizi kitu kwa kweli,” alisema Mwaipaja.

Ukiachilia mbali na uwepo wa Martha na Nkone, wanamuziki wengine watakaolipamba tamasha hilo kubwa ambalo hutokea mara moja kwa mwaka ni pamoja na Ambwene Mwasongwe ambaye atajumuika uwanjani hapo kuachia nyimbo zake zote kali zinazotikisa kama Tangulia Mbele, Misuli ya Imani, Kaa Nami Bwana na nyingine nyingi huku wengine Angela na Paul Clement nao wakihitimisha burudani jukwaani kwa nyimbo za injili.

Mwaka jana, Tamasha la Matumaini lilikuwa na wakali wa nyimbo za injili kama vile Bahati Bukuku, Flora Mbasha, Boni Mwaitege, Christina Shusho ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Jakaya Mrisho Kikwete.

Burudani ya Usiku wa Matumaini 2014 inaletwa kwenu kwa udhamini wa Vodacom, E-FM, Times FM, Clouds FM na Azam TV. Hii si ya kukosa!!!!!

Comments