KUTUMIA UHURU KUWA HURU.




YALIYOMO
  1. Utangulizi
  2. Uhuru wa Hiyari
  3. Madhara ya Uhuru
  4. Hitimisho

ANDIKO KUU: Kumbu Torati 30:15-20
….nimekuwekea mbele yako leo uzima na mauti, Baraka na laana….

LENGO LA SOMO:
            i.Ni kuonyesha uhuru wa kuwa huru   
                (ii). Kufichua kichaka cha Haki za Binadam

1.UTANGULIZI

•►Haki za binadamu,ni msemo ambao upo mdomoni mwa watu na taasisi nyingi, umoja wa mataifa wanakazia haki za binadamu,serikali na taasisi zake, mashirika na mtu binafsi-binafsi wamekuwa macho kwenye haki za binadamu

►Kuna nini hasa nyuma ya haki za binadamu? Kuna ajenda gani ya siri inayoendelea?
Katika fundisho hili la haki za binadamu,utajifunza maneno yanayoambatana na haki za binadamu,kama UHURU, HIYARI NA MAAMUZI, pia utajifunza kutumia uhuru wako kutokuwa huru.


2.UHURU WA HIYARI
-►Linapotumika neno HAKI ZA BINADAMU, UHURU, HIYARI, maneno haya ni kama kivuri au kichaka kinachoficha uhalisia wa nia ya moyoni. Nia ya moyo wa mwanadamu toka enzi na enzi ni kutaka kutumia uhuru kuwa huru, mbali na Mungu na sheria na amri zake,hitaji hili la moyo linajificha ndani ya HAKI ZA BINADAMU na UHURU WA HIYARI.

-►Uhuru wa hiyari ndio jambo la pekee ambalo mwanadamu amepewa na Mungu uhuru asilimia 100, Mungu hana haki ya kuvunja uhuru wa hiyari wa mwanadamu hata nukta moja. Kwa uhuru wa hiyari alionao Mwanadamu, maamuzi yapo mikononi mwake. Kuwa na uhuru sio dhambi,lakini kutumia uhuru ili kuwa huru ndio dhambi.

A) UHURU WA HIYARI YA MAAMUZI TUMEPATA WAPI?
►Tunafahamu kuwa mwanadamu wa kwanza ni Adam na Eva, kabla ya kuasi kwao uhuru wa hiyari zao zote walimkabidhi Mungu, hivyo walitumia uhuru wao kutokuwa huru,lakini siku walipoamua kutumia uhuru wao kuwa huru ndipo walipoharibu.

- Mwanzo 3:1-7, Shetani kabla hajawa shetani, alikuwa malaika, lakini baadae akatumia uhuru wake kuwa huru, awe mbali na Mungu. Eva nae akachagua kuwa HURU mbali na Mungu na Adamu nae akawa ndani ya mstari. Toka mwanadamu wa kwanza alipochagua kutumia uhuru wake kuwa HURU mbali na Mungu, ndio wote tukapata uhuru wa hiyari.

B) KWANINI UHURU?
►Kuna sababu zinazomfanya mwanadamu atake kuwa huru, na hizi sababu zimejificha nyuma ya neno HAKI ZA BINADAM na neno UHURU,toka Adamu alipoasi kwasababu ya kutaka kuwa huru na ndio mpaka leo dhambi kubwa ya wanadamu ni kutaka uhuru wao kuwa huru, mbali na Mungu na sheria zake na amri zake.

► Mambo matano(5) yanayomdanganya mwanadamu kutaka kutumia uhuru wake kuwa huru bila Mungu: Maarifa, Pesa, Dini, Tamaduni, Serikali. Haya mambo 5 ambayo ninayaita M’BADALA WA UFALME siyo mabaya wala sio dhambi isipokuwa namna yanavyotafutwa kwa kudhaniwa kuwa kuna uhuru ndio tatizo.

MAARIFA
►Mwanadamu anadhani kuwa siku atakapopata maarifa ya kutosha atakuwa huru,tena atajitoshereza mahitaji yake mbali na Mungu. Hii dhambi ndio ya Adamu na Eva hasa, ule mti ulikuwa unafaa kwa maarifa, neno maarifa limetokana na neno la kilatini (sciencia) likimaanisha sayansi(elimu).

► Nenda chuo chochote muulize mwanachuo mmoja kwanini anatafuta sana maarifa,atakupa majibu mazuri ambayo hayataonyesha waziwazi kuwa anataka kuwa huru mbali na Mungu,ndio maana nikasema hii dhambi niya moyoni zaidi. Kwanini elimu imepewa kipaumbele sana kuliko ufalme wa Mungu? Tatizo nini? …. Uhuru.

PESA, DINI, TAMADUNI NA SERIKALI
► Kwakifupi,mambo yote ambayo mwanadamu anadhani kuwa niya muhimu sana kuliko Mungu, ni kumkataa Mungu na kutaka kuwa huru kwa jina halali la pesa,dini,tamaduni na serikali. Kitendo cha kutafuta sana haya mambo 5 n’nje ya Mungu ni sawa na kumwambia Mungu unataka ujiendeshe mwenyewe asikuchoshe na amri zake.

3.MADHARA YA UHURU
► Toka Adamu, moyo wa mwanadamu unamchukia Mungu, hivyo huwa unatafuta njia m’badala wa kumtoa Mungu katika maisha ya mwanadamu,kama nilivyosema hapo juu,m’badala ambao mwanadamu amejitafutia ni yale mambo 5 hapo juu. Haki za binadamu zinajaribu kumwambia mtu atumie uhuru wake kuwa huru na Biblia (Mungu)

-JUHUDI ZA KUTUMIA UHURU KUWA HURU

A) ADAMU-Mwanzo 3:23-24
► Shetani alitumia uhuru wake kuwa huru mbali na Mungu,akafukuzwa mbinguni, Adamu na Eva walitumia uhuru wao kuwa huru mbali na Mungu,wakafukuzwa Edeni.
Haya ndio matokeo ya kutumia uhuru wa hiyari kuwa huru, kila maamuzi anayoyafanya mwanadamu, Mungu atahakikisha mwanadamu anapata matokeo ya maamuzi yake.

B) WANA WA ISRAELI NA MUSA –Hesabu 14:26-28
► Moyoni mwa wana Israeli hawakumtaka Mungu wa mababa zao,ambae Musa alimtambulisha kwao, sasa ili wawe huru na miungu yao ya Misri, wakataka kurudi Misri kwa kisingizio cha njaa, vita , kifo na magonjwa. Baada ya Musa kuwa mlimani kwa siku 40 ndipo wakaonyesha kilichokuwa moyoni,waliabudu sanamu.

►Utagundua dhambi ya uhuru siku zote huwa inajaribu kujificha kwenye jambo ambalo litaonekana kuwa halali, uhalali ukishapatika ndipo utakapogundua kilichokuwa nyuma ya uhuru. Mpaka sasa ni nani asiyejua umuhimu wa elimu na pesa? Hizi ni sababu halali

C)  ISRAELI NA SAMWELI —1 Samweli 8:4-7
► Ile dhambi ya kutaka kuwa huru haikuishia jangwani kwa Musa, ikaendelea mpaka wakati wa Samweli. Kutaka mfalme ilikuwa ni kisingizio tu,lakini dhumuni hasa ilikuwa ni kuwa huru mbali na Mungu waliyedhani anamashariti na masheria mengi. Mungu akawapa walichokitaka na matokeo ya maamuzi yao akawabebesha.

► Baadhi ya madhara ya maamuzi yao mpaka leo tunayaona hata hapa Tanzania, kodi,ushuru, ajira kuwa serikalini, maisha kuwa juu ili viongozi walipwe. Yote haya ni matokeo ya Mwanadamu kutaka kuwa huru mbali na Mungu kwa kisingizio cha kutaka Raisi na serikali isiyofungamana na dini yoyote. Serikali haina dini? Kwanini?

D) WANA WA ISRAELI NA YESU – Yohana 8:21-23
►Toka kwa Adam, wakati wa Musa,na wakati wa Samweli mpaka nyakati za Yesu kale kamchezo ka mwanadamu kutaka kuwa huru bado kalikuwa kanamkeleketa moyoni. Wakamkataa Yesu kwa njia halali ya Uhuru na Haki ya mwanadamu ya kuchagua.

E) NYAKATI ZETU
►Nyakati hizi niza wasomi wengi, lakini ile dhambi ya kutaka kutumia uhuru kuwa huru bado ipo moyoni, ingawa dhambi ni ileile lakini miaka hii imetengenezewa mazingira na majina mazuri (Haki za Binadamu), na nyimbo zimetungwa – Freedom Song, na filamu zimetengenezwa – Independent Day, na vyuo vimejengwa – Liberty University, na Luninga hazipo mbali – Independence Television(ITV), Na nyimbo za Taifa(Anthem)--♫...dumisha uhuru na umoja…♫,pia …♫.utumwa wa nchi nyerere ameukomesha…♫

4.HITIMISHO
►Wana siasa na watu mbalimbali wanapopigania haki za binadamu, usidhani ya kwamba wanauzalendo sana, hapana,wana ajenda yao ya siri,ipi hiyo? Wanataka utumie uhuru wako uwe huru katika maamuzi yako bila kuingiliwa na misingi ya Mungu na Biblia


► Ungeniambia nikushauri, ningekushauri mambo mawili ;
            i) Usitumie uhuru wako kuwa huru, na 
            (ii) Tumia uhuru wako kutokuwa huru.
MUNGU akubariki sana.
 By Apostle eliya simon-

    .......HOSE………THE BEST HAS COME………….

Comments