OMBA KWA MUNGU LEO UTAPOKEA

BWANA YESU asifiwe.
Leo nakuletea Neno la uzima.
Maombi ni maisha, maombi ni mkono mrefu kuliko yote wa kupokea kutoka kwa MUNGU.
 Maana ya maombi ni kusema na MUNGU au kuhitaji msaada toka kwa MUNGU. Isaya 43:26, ''Unikumbushe, na tuhojiane; eleza mambo yako, upate kupewa haki yako. '' Sehemu pekee ya kueleza mambo yako ni kwa Mungu,
Maombi yanayojibiwa ni yale yaliyoombwa katika jina la YESU KRISTO pekee Yohana 14:13-14 '' Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili BABA atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya. ''

Hakuna mwanadamu hata mmoja ambaye hana hitaji kwa MUNGU hata asiombe. kama una pesa bado unatakiwa kumwomba MUNGU akupe afya njema, kama una kazi nzuri bado unatakiwa umuombe MUNGU ili ailinde kazi yako. Kama una nyumba nzuri 10 bado unamhitaji MUNGU akupe uzao na awalinde watoto wako, Kila mtu anatakiwa amuombe. Wapo matajiri sana lakini wanaumwa hivyo bado wanamhitaji MUNGU awaponye. Kama wewe huombi unakosea sana. Hata kama huna la kuombea ni heri kuomba maombi ya kumshukuru MUNGU kwa kukulinda miaka yako yote, Mshukuru hata MUNGU kwa kukupa wazazi wazuri, Maombi ni maisha. maombi hayakomi yaani siku zote za maisha yetu lazima tuombe.
Kumuomba MUNGU ni kudumisha uhusiano wako na MUNGU na kutokuomba ni kuharibu  uhusiano wako na BWANA MUNGU maana MUNGU husema na sisi kwa njia ya neno lake kupitia watumishi wake au sisi wenyewe kusoma neno lake, hapo MUNGU anakuwa anasema na sisi  na kwa upande wa sisi wanadamu tunasema na MUNGU muumba wetu kwa njia ya maombi Hivyo ili uhusiano wako na MUNGU uwepo lazima muwe mnawasiliana. MUNGU atawasiliana na wewe kwa njia ya neno lake kama hivi sasa kupitia ujumbe huu na wewe lazima uwasiliane na MUNGU kwa njia ya Maombi katika KRISTO YESU. omba ndugu siku zote za maisha yako.
 Tuombe kwa jina la YESU KRISTO tu.
Hata kama utaomba maombi gani na kwa muda gani , lakini kama hujaomba katika jina la YESU KRISTO usahau kujibiwa .
MUNGU ameamuru tuombe katika jina la YESU KRISTO pekee. hakuna jingine

Hapa nakuletea sehemu ndogo tu ya maandiko yanayotutaka tuombe siku zote.

= Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; Mathayo 7:7 

= Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa. - Yohana 15:7 

= Niite, nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua. - Yeremia 33:3

 =Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote. - Yeremia 29:13

 =Na itakuwa ya kwamba, kabla hawajaomba, nitajibu; na wakiwa katika kunena, nitasikia. - Isaya 65:24

 = Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lo lote watakaloliomba, watafanyiwa na BABA yangu aliye mbinguni. Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao. - Mathayo 18:19,20

= Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba. - I Yohana 5:14,15 

= ombeni bila kukoma; I Wathesalonike 5:17 

=Kama ningaliwaza maovu moyoni mwangu, BWANA asingesikia. Hakika MUNGU amesikia; Ameisikiliza sauti ya maombi yangu. - Zaburi 66:18,19

 =Akasema, Simoni, Simoni, tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano; lakini nimekuombea wewe ili imani yako isitindike; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako. - Luka 22:31,32

 =Naye(YESU), kwa sababu hii, aweza kuwaokoa kabisa wao wamjiao MUNGU kwa yeye; maana yu hai sikuzote ili awaombee. - Waebrania 7:25

=Kadhalika ROHO naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini ROHO mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Na yeye aichunguzaye mioyo aijua nia ya Roho ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo MUNGU. - Warumi 8:26,27 

=Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu. - Marko 11:24 

 =na lo lote tuombalo, twalipokea kwake, kwa kuwa twazishika amri zake, na kuyatenda yapendezayo machoni pake. - I Yohana 3:22 

= Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifulifuli, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe. -Mathayo 26:39

= Bali wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za BABA yako aliye sirini; na BABA yako aonaye sirini atakujazi. Nanyi mkiwa katika kusali, msipayuke-payuke, kama watu wa mataifa; maana wao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu ya maneno yao kuwa mengi. - Mathayo 6:6,7

 =Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji. - Waebrania 4:16 

=kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika ROHO, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote; - Waefeso 6:18

=Jioni, asubuhi, na adhuhuri nitalalama na kuugua, Naye(MUNGU) ataisikia sauti yangu. - Zaburi 55:17

 =Atakapoyaelekea maombi yake aliye mkiwa, Asiyadharau maombi yao. - Zaburi 102:17

 = Haleluya. Nampenda BWANA kwa kuwa anaisikiliza Sauti yangu na dua zangu. Kwa maana amenitegea sikio lake, Kwa hiyo nitamwita siku zangu zote. - Zaburi 116:1,2

 = Dumuni katika kuomba huku na shukurani, mkituombea na sisi pia, kwamba MUNGU atufugulie mlango kwa lile neno lake, tunene siri ya KRISTO, ambayo kwa ajili yake nimefungwa, ili niidhihirishe, kama inipasavyo kunena.-Wakolosai 4:2-4

  Maombi ni hali ya kuongea na MUNGU
 
= Zaburi 4:3 "Bali jueni ya kuwa BWANA amejiteulia mtauwa BWANA atasikia nimwitapo." 
Ndugu mwite MUNGU leo kwa maombi ili upokee majibu yako.

 Tunahitaji msaada wa MUNGU  kwa kila jambo tunalolifanya katika maisha yetu na  Msaada unapatikana kulingana na Mahusiana yaliyopo baina ya muombaji  na mtoaji, kwa kawaida unalolitaka kwa kwa mtu ili ulipate mahusiano yanatakiwa yawe mazuri,

 SABABU 4 ZA KWANINI TUNAMUOMBA MUNGU:

1. Kujinyenyekesha mbele za MUNGU.
2. Kuonyesha kuwa yeye ni MUNGU wetu.
3. kuonyesha kuwa vyote viko mikononi mwake
4. Tunampa heshima kama BABA mwenye familia ya watoto watakatifu.

 Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako
Peter M Mabula
Maisha ya Ushindi Ministry.
0714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.
MUNGU Akubariki.

Comments