USHUHUDA MUHIMU KWA MWANAMAOMBI YEYOTE DUNIANI.

Siku moja nikiwa nimejitenga pembeni kwa wiki moja ya kuomba na kufunga na kujifunza Neno la Mungu, Nilikuwa na swali nililomuuliza Mungu katika muda wa utulivu baada ya kusoma Neno na kuomba. Swali lenyewe lilikuwa, "BWANA mbona nikiomba mbele zako inachukua muda sana kupata matokeo kuliko muda ninaochukua kumwamuru pepo amtoke mtu [Maana pepo hachukui hata robo saa na humtoka mtu haraka kila nikimwamuru kwa jina la Yesu]?" Halafu kwa sauti ya upole, Mungu alinijibu kitu ambacho kiligeuza maisha yangu ya maombi.

 Aliniambia, "Tatizo lako una imani kubwa kwa Yesu kujibu ombi la kumtoa pepo papo kwa papo lakini hautumii imani hiyohiyo unapoombea vitu vingine kama fedha, ugonjwa, tatizo, jaribu au kingine chochote kilichokutokea" Nilibaki mdomo wazi maana alikuwa AMENIUMBUA!! Nikamuuliza, "Unamaanisha nini BWANA?" Akanijibu kwa ufupi, "Yesu anayejibu na kumtoa pepo papo kwa papo kwa sababu unaamini kinapaswa kutokea papo kwa papo NI YESU YULEYULE ANAYEJIBU LOLOTE JINGINE PAPO KWA PAPO UNAPOLIOMBEA KWA IMANI, Tatizo lako HUWA HUPOKEI PAPO KWA PAPO KAMA UNAVYOPOKEA UKIMWOMBEA MWENYE PEPO" Tangu siku hiyo, Nilipata siri kubwa ya ajabu kuhusu Kuomba na Kupokea. Kama ninavyopokea papo kwa papo linapokuja swala la mwenye pepo Vivyo hivyo ndivyo ninavyofanya nikiombea pesa, tatizo la mtu, changamoto, jaribu au chochote.

 Yesu anayejibu na kumtoa pepo papo kwa hapo huwa anajibu pia papo kwa hapo kila tukiombea lolote jingine. Kinachotuponza ni kwa vile "havionekani (no reaction)" tofauti na kesi ya pepo, tunadhani haijatokea hivyo badala ya kuweka IMANI YA KUPOKEA KWENYE MATENDO (Kuanza kuongea kana kwamba kimetokea tayari, kuanza kumshukuru Mungu kwa kutupa hicho badala ya kuendelea kukiombea tena na tena eti kwa vile hakionekani machoni)... Badala ya kupokea tunaishia kupangua mkono wa Mungu ulioleta jibu kwa kuombea alichokijibu tangu siku ya kwanza tulipoomba! "Na huu ndio ujasiri sisi tulionao kwake ya kwamba tukiomba kitu chochote sawasawa na mapenzi yake anatusikia; Na kama anatusikia, TAYARI tunazo haja zote tulizomwomba" (1Yoh 5:14-15). "Yoyote muyaombayo mkisali AMININI YA KUWA MNAYAPOKEA [Muda uleule wa maombi] nayo yatakuwa yenu [yatatokea kwenye uhalisi]" (Marko 11:24). Siri hii iligeuza maisha yangu jumla, Itumie ikusaidie! 

Mwl Dickson Cornel Kabigumila
 www.yesunibwana.org

Comments