MASWALI SABA(7) MUHIMU KWA KILA MWANADAMU KUJIULIZA NA KUJIJIBU.



 
BWANA YESU asifiwe.
Mhubiri 3:1-2a  ‘’Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu. Wakati wa kuzaliwa, na wakati wa kufa’’
MUNGU amenipa ujumbe kwa ajili yako na kwa ajili yangu pia. Kila mtu ajiulize na kujijibu. Maswali haya yatakufanya ujitambue na utambue unaishi kwa sababu gani na pia kama ukiondoka leo utaenda wapi.
A. Mimi ni nani?
             B. Kwanini niko hai leo?
                         C.  Kwanini MUNGU aliniumba?
                                   D.Dunia imejaa dhambi, je nitaponaje?
                                         E.Je natakiwa kufanya nini muda ambao niko hai?
                                F.   Nikiondoka duniani nitaenda wapi?
               G.Nitakuwa wapi milele ijayo?

Karibu.
1.   Mimi ni nani?

‘’MUNGU akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.
MUNGU akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa MUNGU alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba. MUNGU akawabarikia, MUNGU akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi.-Mwanzo 1:26-28.
-Kila mwanadamu aliumbwa na MUNGU. Mwanzo MUNGU alimuumba Adamu na Eva na kupitia hao sisi sote tuliumbwa.
-Muumbaji ni MUNGU ndio maana sio kila mwanamke anazaa. Sio kila mwanamume anazaa. Mtoto huja kwa kibali cha MUNGU na kwa makusudi ya MUNGU. Ndio maana kila mara makanisani tunasikia wanandoa wakishuhudia kwamba ‘’Tunamshukuru MUNGU kwa kutupa zawadi ya mtoto’’ Sijawahi kumuona binadamu hata mmoja anayejisifia kwamba ‘’Najishukuru kwa sababu nimezaa’’ bali wote kwa kutambua kwamba aliyeleta mtoto ni MUNGU na sio mwanadamu. Ayubu 10:8 ‘’Mikono yako imeniumba na kunifinyanga; Nawe utageuka na kuniangamiza?’’

Mpe MUNGU utukufu na heshima kwa sababu yeye ndiye aliyekuumba. Tambua kwamba
-MUNGU anakupenda kuliko wote wanaokupenda.
-MUNGU hataki uangamie.
-MUNGU anakupa pumzi ya uhai bure.
-MUNGU ameandaa njia ya wokovu kwa ajili yako.

2.  .Kwanini niko hai leo?

Maombolezo 3:22 ‘’Ni huruma za BWANA kwamba hatuangamii, Kwa kuwa rehema zake hazikomi.’’
Ndugu yangu kama unadhani kwamba uko hai kwa sababu ya dawa uliyopewa na mganga pole sana.
Kma unadhani uko hai kwa sababu ya pesa zako pole sana.
Kama unadhani uko hai kwa sababu mlinzi uliyemwajiri pole sana.
Wanaokufa wengi wana walinzi kama wewe,  wanatumia dawa za kienyeji kama wewe lakini wamekufa na kingine hakuna mganga wa kienyeji ambaye anaishi siku zote bali hata wao hufa tu. Ndugu uko hai kwa sababu ya Neema na ulinzi wa MUNGU BABA wa mbinguni.
Ndugu mpe utukufu yeye na tena amekuacha uwe hai leo kwa sababu maalumu, Tumika kwa BWANA , Mche MUNGU, Tengeneza maisha yako na tumika katika kuwasaidie wengine ili wamjue BWANA anayeokoa.
-Ndugu unaishi kwa sababu MUNGU anataka ubadilike na kumrudia yeye.
- MUNGU amekuhifadhi hai ili umtumikie. Ndiposa Mtume Paulo anasema katika nyaraka zake kwamba ‘’ Kuishi ni KRISTO na kufa ni faida’’ Yaani kama ataendelea kuishi basi atamhubiri KRISTO kwa mataifa na kama akifa basi ataenda kupumzika mbinguni ambapo huenda watakatifu baada ya kumaliza kazi yao ambayo MUNGU aliwapa duniani. Huyu alikuwa ni mtakatifu, Vipi kwa upande wako ndugu?
Kwanini uko hai leo? Tafakari na tambua kwamba uko hai kwa sababu kuna sababu ya MUNGU kukuweka hai yawezekana MUNGU anakuvumilia kwamba labda utapata ufahamu na kuacha dhambi, anakuvumilia japokuwa ni kwa kitambo tu. 

3.  Kwanini MUNGU aliniumba?

Ndugu MUNGU alikuumba kwa kusudi maalumu na kwa ajili ya kumwabudu. Ona jinsi MUNGU alivyomwambia Yeremia Katika Yeremia 1:5 ‘’ Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa.’’
Yeremia wa leo ni wewe, umeumbwa kwa kusudi jema la MUNGU.
Ndugu yangu nakuomba liishi kusudi la MUNGU la kukuumba na sio kuishi kwa kulitumikia kusudi la shetani. Maana wengi wamejitenga na MUNGU aliyewaumba na kujiungamanisha na shetani, ni mbaya sana kumsahamu aliyekuumba na kuanza kumtukuza adui yako.
Shetani ni adaui wa kila wanadamu, ndiye aliyesababisha kifo, ndiye aliyeleta dhambi, ndiye aliyesababisha laana na hata ukimtumikia hana shukrani na kama ukifa katika dhambi ataanza kukutesa kuzimu. Ndugu zangu tumkimbilie BWANA YESU ili tuokoke na moto wa milele.
-Ndugu umeumbwa kwa kusudi jema la MUNGU.
-Litumikie kusudi la MUNGU.
-Kataa dhambi, ogopa dhambi, ikimbie dhambi na usitende dhambi.

4.  Dunia imejaa dhambi, je nitaponaje?

 Warumi 5:6-8 ‘’Kwa maana hapo tulipokuwa hatuna nguvu, wakati ulipotimia, KRISTO alikufa kwa ajili ya waovu. Kwa kuwa ni shida mtu kufa kwa ajili ya mtu mwenye haki; lakini yawezekana mtu kuthubutu kufa kwa ajili ya mtu aliye mwema.  Bali MUNGU aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa KRISTO alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi.’’

Ndugu yangu japokuwa dunia imejaa dhambi lakini yupo Simba wa kabila la Yuda YESU KRISTO anayeokoa.
-Huu ni upendo wa MUNGU wa ajabu sana kwetu. MUNGU ameandaa uzima wa milele ambao umo ndani ya Mwanaye pekee YESU KRISTO.
-Kama tunataka kuliishi kusudi la MUNGU basi tumpe YESU maisha yetu.
-MUNGU hataki hata mmoja apotee ndio maana anatualika bure kabisa kushiriki uzima wa milele kupitia Mwanaye YESU KRISTO.
Kuna watu wengine hudhani kwamba MUNGU ameandaa njia nyingi za kuwapeleka uzimani wanadamu lakini kumbe njia ni moja tu yaani YESU KRISTO. Yohana 14:6 ‘’ YESU akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji  ila kwa njia ya mimi. ‘’ Matendo 4:12 ‘’ Wala hakunakwa BABA, wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.   ’ Ila ni jina la YESU KRISTO tu , Warumi 10:13 ‘’ kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la BWANA ataokoka.  ‘’

5.  Je natakiwa kufanya nini muda ambao niko hai?


Mathayo 28:19-20 ‘’ Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la BABA, na MWANA, na ROHO MTAKATIFU; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.’’
Ndugu zangu huu ni wakati wa kumtumikia MUNGU. Huu ni wakati wa kuwaambia wanadamu kwamba YESU KRISTO anaokoa. Ni wakati wa Mama kuihubiri familia yako ili ijisalimishe kwa YESU, ni wakati wa mtoto kuwaombea wazazi wako na kuwashauri kuokoka maana hizi ni nyakati mbaya.
Wafilipi 2:13 ‘’ Kwa maana ndiye MUNGU atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema. ‘’
MUNGU analo kusudi kwa wanadamu wote ndio maana anataka kukutumia wewe ili watu wote waokoke. Wewe utajiona kama unatumika / unahubiri/ unafundisha/ unawaonya watu ili wakimbilie kwa YESU na kupona kumbe ni MUNGU anayetenda kazi ndani yako ili tu kulitimiza kusudi lake jema.
Muda huu ukiwa hai ndio muda wa kumtumikia MUNGU, hakuna wakati mwingine wowote.

6.  Nikiondoka duniani nitaenda wapi?

Warumi 14:8-9 ‘’Kwa maana kama tukiishi, twaishi kwa BWANA, au kama tukifa, twafa kwa BWANA. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu mali ya BWANA. Maana KRISTO  alikufa akawa hai tena kwa sababu hii, awamiliki waliokufa na walio hai pia.''
Kuna wanaokufa kwa BWANA  YESU na kuna wanaokufa kwa shetani. BWANA YESU yuko mbinguni hivyo na wanaokufa katika yeye huenda mbinguni. Na shetani yuko kuzimu hivyo wanaokufa katika shetani/ dhambi huenda kuzimu. Unaweza kutazama mfano wa Lazaro na Yule tajiri, Lazaro alipokufa alienda mbinguni kuungana na akina Ibrahimu na tajiri alipokufa alienda kuungana na majini kuzimu.

7.   Nitakuwa wapi milele ijayo?

1 Thesalonike 4:16-17 ‘’Kwa sababu BWANA  mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya MUNGU; nao waliokufa katika KRISTO watafufuliwa kwanza.  Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki BWANA hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na BWANA milele.’’
Ni heri kufa katika KRISTO.
Ni heri kumpokea BWANA YESU leo.
Ni heri kumwishia BWANA YESU.
Ufunuo 20:12-13 ‘’Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao.  Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Waka Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake; na Mauti nahukumiwa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake.’’
Kuna watakaoishi uzimani milele na kuna watakaoishi motoni milele.
BWANA YESU atuokoe.
BWANA YESU atusaidie maana hakuna njia nyingine ya uzimani nje na BWANA YESU.

Yakobo 5:8 ‘’  Nanyi vumilieni, mthibitishe mioyo yenu, kwa maana kuja kwake BWANA kunakaribia. ‘’
 Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
                     MUNGU akubariki sana .
                      Ni mimi ndugu yako
                       Peter M Mabula
                 Maisha ya Ushindi Ministry.
                           0714252292
 
              mabula1986@gmail.com
  MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.
  MUNGU Akubariki.

Comments