JE UTASTAHILI TAJI YA MFIA IMANI?




BWANA YESU KRISTO asifiwe ndugu yangu.

Karibu tujifunze ujumbe wa MUNGU unaoleta mabadiliko, kufunguliwa na uponyaji.

Leo tunajifunza kuhusu taji ambazo tutapewa wateule wa MUNGU tukifika mbinguni. Ufunuo 3:11 {  Naja upesi. Shika sana ulicho nacho, asije mtu akaitwaa taji yako. }

BWANA YESU kwenye hilo andiko anasema ‘’Shika sana ulichonacho asije mtu akaitwaa taji yako’’
1 Kor 9:25 ''Na kila ashindanaye katika michezo hujizuia katika yote; basi hao hufanya hivyo kusudi wapokee taji iharibikayo; bali SISI TUIPOKEE TAJI ISIYOHARIBIKA.''

Taji atakayotoa BWANA YESU ni muhimu sana.

Kuna taji nyingi  ambazo watapewa watakatifu baada ya kushinda ya dunia.
Mathayo 13:43 ''Ndipo wenye haki watakapong'aa kama jua katika ufalme wa BABA yao. Mwenye masikio, na asikie.'' 
 

Kuna

-Taji ya uzima(Yakobo 1:12)

-Taji ya haki(2 Timotheo 4:7-8)

-Taji ya utukufu(1 Petro 5:4)

-Taji isiyoharibika( 1Kor 9:25)

-Taji ya mfia imani.(Ufunuo 2:10)





Taji hizi saba watapewa watakatifu wa MUNGU, Kila mtu sawasawa na sifa ya taji yake ila taji ya uzima tutapewa wote tutakaoingia uzimani yaani wote waliokombolewa kwa Damu ya YESU KRISTO na kufanyika watoto wa MUNGU kwa yeye tena wameliishi neno la MUNGU.

-Taji ya uzima ni ya wote wateule wa KRISTO watakaovumilia mpaka mwisho.

-Kuna watu watapata taji zaidi ya moja kulingana na kile walichokifanya duniani.

-Kwa sehemu ndogo sana naomba nizungumzie Taji ya utukufu.

Taji ya utukufu watapewa wateule wa BWANA YESU ambao  waliwaongoza wengine katika kutenda mema, Daniel 12:3 ''Na walio na hekima watang'aa kama mwangaza wa anga; na hao waongozao wengi kutenda haki watang'aa kama nyota milele na milele.''
Taji ya utukufu ni muhimu sana, na Biblia inaendelea kusema.

 1 Petro 5:4 ‘’ Na Mchungaji mkuu(YESU)  atakapodhihirishwa, mtaipokea taji ya utukufu, ile isiyokauka. ‘’

Ndugu yangu, hapa unaweza ukajiona kabisa kwamba unastahili taji gani na kama ukivumilia hadi mwisho wa maisha yako BWANA YESU atakupa taji Zako au yako  unayostahili.

Taji ya utukufu wataipata wale ambao walikuwa wanawaongoza wengine katika kutenda mema.
 

Leo nazungumzia TAJI YA MFIA IMANI.

Hii ni taji ngumu kidogo maana kunahitajika uvumilivu na kujaa ROHO MTAKATIFU. Ufunuo 2:10-11  ‘’Usiogope mambo yatakayokupata; tazama, huyo Ibilisi atawatupa baadhi yenu gerezani ili mjaribiwe, nanyi mtakuwa na dhiki siku kumi. Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima.  Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye hatapatikana na madhara ya mauti ya pili.’’

Sifa muhimu ili kuipta taji hii ni ‘’UWE MWAMINIFU KWA YESU HATA KUFA’’

Taji hii wataipata wale ambao licha ya mateso waliyoyapata kwa sababu ya KRISTO lakini walivumilia hadi mwisho. Kuna mambo yanaweza kuruhusiwa kabisa maishani mwako lakini BWANA leo anakutaka uvumilie mpaka mwisho. Mitume na manabii walivumilia. Kuna ambao kwa kujitoa kwako na kuvumilia kwao ndio maana leo injili umetufikia mimi na wewe, haikuwa kirahisi hivyo. Kuna ambao waliwekwa kwenye mapipa ya mafuta yanayowaka moto mkali  lakini bado walisema ‘’YESU ni BWANA’’. Kuna watumishi walikatwa mikono na kukata na mapanga na bado walibaki katika BWANA YESU. Hakika walifanya kazi inayohitaji TAJI YA MFIA DINI. Ndugu yangu, swali kwako ni hili, je utavumilia na kumkiri YESU KRISTO kama BWANA na MWOKOZI wa maisha yako hata kama ni katika kipindi kigumu?

-Je utasema YESU ni BWANA na Mwokozi wako hata kama ukoo wako watakufukuza na kutaka kukuua kwa sababu tu umeamua kuokoka?

-Je utasema ‘’Kufa ni faida na kuishi ni KRISTO’’ Hata kama unataka kunyongwa kwasababu ya kumtumikia BWANA YESU?

Stephano alivumilia hadi mwisho, alikuwa mwaminifu hata kufa. Biblia inasema hivi juu ya yaliyomtokea Stephano na bado akavumilia hadi mwisho. Matendo 7:54-60 ‘’ Basi waliposikia maneno haya, wakachomwa mioyo, wakamsagia meno. Lakini yeye akijaa ROHO MTAKATIFU, akakaza macho yake, akitazama mbinguni, akauona utukufu wa MUNGU, na YESU akisimama upande wa mkono wa kuume wa MUNGU.  Akasema, Tazama! Naona mbingu zimefunguka, na Mwana wa Adamu amesimama mkono wa kuume wa MUNGU. Wakapiga kelele kwa sauti kuu, wakaziba masikio yao, wakamrukia kwa nia moja,  wakamtoa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni pa kijana mmoja aliyeitwa Sauli.  Wakampiga kwa mawe Stefano, naye akiomba, akisema, BWANA YESU , pokea roho yangu.  Akapiga magoti, akalia kwa sauti kuu, BWANA, usiwahesabie dhambi hii. Akiisha kusema haya akalala. Na Sauli alikuwa akiona vema kwa kuuawa kwake. ‘’

Ndugu zangu, mtumishi huyu alivumilia hadi mwisho.

-Yawezekana wewe hata hupitii jaribu gumu kama hili lakini umekubali kabisa kumkana BWANA YESU na kuirudia dunia.

-Yawezekana umesemwa tu kidogo na watu walioshiba makande na umelia sana na kurudi nyuma, wewe wala hujapitia jaribu kama la Stefano lakini kwanini kurudi nyuma?

-yawezekana muumini mwenzako kakukwaza kidogo lakini hadi umeacha wokovu, ndugu hivi unaijua jehanamu au unaisikia tu? Ndugu je uzima wa milele umeuchukia kwa sababu tu ya kusemwa kidogo na wanadamu wanaomwakilisha shetani?

Ndugu yangu, haijalishi kuna nini.

Haijalishi nani kasema nini.

Haijalishi dunia inasema nini.

Tusikubali kumwacha BWANA YESU maana hakuna uzima kwingine kokote nje na BWANA YESU(Matendo 4:12).

Ndugu zangu, taji ya mfia dini haipatikana kwa kupigana na mtu yeyote na wala haipatikani kwa kuitetea dini yeyote ile, ila itapatikana kwa kuvumilia mateso yote  kwa ajili ya KRISTO.  Vita vyetu sisi sio juu ya damu na nyama Waefeso 6:12 ‘’ Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. ‘’. 

 Na hata ninaposema neno Dini simaanishi dini  tunazozifahamu bali naamisha Dini yaani njia ya kumwelekea MUNGU(Ayubu 4:6) Na njia ni moja tu ya kweli yaani YESU KRISTO(Yohana 14:6,YESU akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa BABA, ila kwa njia ya mimi. ).

Wanaojitoa mhanga hawawezi kupata taji kutoka kwa MUNGU aliye hai.

Wanaotetea dini zao wala hawahusiani na MUNGU aliye hai. Wateule wa KRISTO ni watu wa rohoni na hawatafuti taji kimwili.

BWANA anatutaka tuvumilie kwa yote ambayo tutapitia, tuwe waaminifu mpaka kufa kwetu. Pia kama tutapitiamagumu Fulani maishani mwetu ambayo  ni hila tu za shetani tunalo jina la YESU KRISTO la kutupa ushindi, lakini kama kuna jambo ambalo litaruhusiwa kwetu kama lilivyoruhusiwa kwa Stefano basi tuvumilie.

Ufunuo 6:9 ‘’ Na alipoifungua muhuri ya tano, nikaona chini ya madhabahu roho zao waliochinjwa kwa ajili ya neno la MUNGU, na kwa ajili ya ushuhuda waliokuwa nao.  ‘’

-Ndugu yangu vumilia yote unayopitia.

-Kuna mengine yanakupata kwa sababu yako mwenyewe maana ulijisahau kuomba.

-Mengine yanakupata kwa sababu ya kutoitii sauti ya MUNGU.

-Wala usiseme unajaribiwa na MUNGU bali omba kupitia jina la YESU KRISTO aliye hai, ila pale kunapohitaji uvumilivu uwe mwaminifu hata kufa na BWANA atakupa taji ya mfia dini.

Vumilia ndugu na ongeza sana maombi.

Dada mmoja alipoamua kuokoka ndugu zake walitaka kumuua, walimtisha sana na kumfukuza, alikuja kanisani na tukajitolea kumhifadhi kwa muda. Alivumia na sasa ni mke wa mtumishi mmoja kule Zanzibar, kwa sasa maisha ni mazuri na mama yake ndio kwa sasa wanamuona wa muhimu kuliko watoto wengine.

Ndugu vumilia yote na MUNGU yu pamoja na wewe.

 Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.

                     MUNGU akubariki sana .
                      Ni mimi ndugu yako
                       Peter M Mabula
                           0714252292
 

              mabula1986@gmail.com
  MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments