MWANANDOA HAKIKISHA SIKU ZOTE ZA NDOA YENU UPENDO WA KWANZA UPO.

Mr and Mrs Peter Michael Mabula.
 KWA KILA MUME.

 Kumbuka upendo wako wa kwanza kwa mkeo. Kumbuka yule binti uliyekuwa unakosa usingizi kwa ajili yake, ulivyokuwa unapita pita karibu na kwao ili walau umuone moyo wako utulie. Uliyekuwa huwezi kulala kabla hujaisikia sauti yake. Kumbuka jinsi moyo ulivyokuwa unadunda siku ya kwanza kumueleza ya moyoni na jinsi gani ulivyojaa furaha alipokubali kuwa nawe siku zote za maisha yako.
Je kwanini leo hii unamuona hafai tena? Leo hii msichana aliyekuwa mpenzi wa moyo wako unamtendea visivyo tena bila hata kujali? Je ule upendo wa kwanza umeenda wapi? Amka katika usingizi wako, huyo mkeo ndiye yule yule binti uliyekuwa huambiwi wala husikii juu yake, uliyeapa kumlinda, kumfurahisha na kuwa naye siku zote za maisha yako.
Chukua dakika chache ufikirie mwanzo wa penzi lenu, na pia andika kabisa vitu ambavyo ulikuwa unamfanyia na uso wake unachanua kwa furaha. Sasa azimia kuyafanya hayo yote kuanzia sasa. Hata kama kuna uzito ndani yako, jisukume kutenda na hakika hutajuta. Usiangalie amefanya nini na amekosa nini bali angalia ule upendo wako wa kwanza na dhamiria kuurudisha upya katika ndoa yako.
Nakwambia ukifanya hivi utakuja kunishuhudia jinsi furaha ya ndoa ilivyoongezeka mara dufu.

KWA KILA MKE.

Uko wapi ule upendo wako wa kwanza kwa mumeo. Kumbuka jinsi gani ulivyojaa furaha baada ya kijana uliyempenda kukuvalisha pete ua uchumba na kuja kwa wazazi wako kutoa mahari? Unakumbuka jinsi gani ulivyokuwa umejiandaa kumpenda na kumtii mumeo siku zote za maisha yako. Mwanzoni ulikuwa unaona raha kumhudumia mumeo na kumfurahisha lakini kwanini sikuhizi imekuwa ni kama msalaba kwako?
Chukua muda ufikirie jinsi gani ulikuwa unajibidiisha kupata muda wa kuwa na mwenzio siku hizi uko busy na watoto na marafiki basi. Ule upendo wa kummtendea mema kila siku umeenda wapi? Haijalishi amekuumiza kiasi gani, uliapa kumpenda, na hakika upendo hugeuza hata moyo wa chuma.
Kuanzia leo dhamiria kumtendea matendo ya upendo, kumuonyesha upendo hata asipostahili kabisa na utaona furaha itakavyozidi katika ndoa yako na amani kutawala daima. Upendo hufunika wingi wa dhambi na hauhesabu mabaya.

MUNGU akubariki sana.
By Women of CHRIST.

Comments