MAMBO MATATU(3) YANAYOKUTAMBULISHA KWAMBA WEWE NI MTU WA MUNGU ALIYE HAI.


BWANA YESU atukuze ndugu zangu.
Leo nina ujumbe mtamu sana ambao unamhitaji kila mtu.
Leo tunazungumzia mambo 3 ambayo yanamtambulisha mtu kwamba huyo ni mtu wa MUNGU yaani ni mtumishi sahihi wa BWANA YESU.
Ukimuona mtu yeyote lazima baada ya muda kidogo utatambua kwamba ananuka manukato ya nani. Wapo watu wananuka manukato ya KRISTO na kuna watu wananuka manukato ya shetani. 2 Kor2:15 '' Kwa maana sisi tu manukato ya KRISTO, mbele za MUNGU, katika wao wanaookolewa, na katika wao wanaopotea; ''
Kuna watu wananuka manukato ya KRISTO mbele za watu wote na kuna watu wananuka manukato ya shetani mbele za watu.
Anayenuka manukato ya KRISTO lazima ukimtazama au ukikaa nae lazima tu utaona nia ya KRISTO ndani yake, lazima utaona hofu ya MUNGU kwake, lazima utaona utakatifu usio wa kuigiza, lazima uone matendo mema. Biblia inasema kwamba sisi wateule wa KRISTO ni manukato ya KRISTO kwa watu wote wawe wa kanisani au ambao hawajaokoka. Manukato lazima yatoe harufu na kila aliyempa BWANA YESU maisha yake anatakia awe na manukato ya KRISTO yaani anukie utakatifu ambao anautaka MUNGU, bila matusi wala hatumii mwili wake kwenye dhambi.
Lakini pia kuna watu wana manukato ya shetani, mtu mwenye manukato ya shetani ukikaa nae tu dakika 2 lazima ujue kwamba huyo ananuka ushetani, yaani dakika 2 tu utaona mara anatukana, mara anapiga simu kwa kujificha maana anataka amdanganye mtu kwamba yuko Dar kumbe yuko morogoro, mwenye manukato ya shetani hakawii kupiga simu na kumweleza mwanaume au mwanamke kwamba yeye hajaolewa au kuoa kumbe ukweli ni kwamba ameshaolewa au ameshaoa na ana watoto watatu.
Mwenye manukato ya shetani matusi kwake ni kawaida kabisa, hakawii kukuambia kwamba usiku wa leo ataenda disko, hakawii kusema kwamba yeye sio mlevi ila ni muonjaji tu, huyo ana manukato ya shetani. Hata kwenye commet yake hakawii kutukana, huyo ana manukato ya shetani, hata kama anahudhuria ibada na tena ni mwimbaji lakini kama ni mzinzi na mwasherati huyo bado ana manukato ya shetani. Ndugu yangu uliye na manukato ya shetani nakuomba leo kaoge kwenye damu ya YESU kwa kumpokea BWANA YESU upya na ndipo utakuwa manukato ya KRISTO kama neno la MUNGU linavyosema hapo juu. sisi tuliookoka tuna manukato ya BWANA YESU  mbele ya watu wote, wawe washirika au hata kama ni wapagani.
Nimetaka sana uyajue hayo kwanza na sasa ndio naingia kwenye kiini cha ujumbe wangu kwamba mambo 3 yanayokutambulisha kwamba wewe ni mtu wa MUNGU.
Siku moja katika ndoto nilimuona Askofu mkuu mmoja  wa makanisa ya kipentekoste  akiniambia '' Peter amka uombe''  
Niliamka na kuomba kidogo kisha nikalala siku hiyo ilikuwa jumapili, kesho yake yaani jumatatu ilianza mikasa ambayo ilidumu kwa wiki nzima, nilipitia magumu sana maana nilipanda gari na baadae gari lile  tulifika sehemu kwenye kituo watu waliokuwa nje ya gari walianza kukimbia na kusema '' Mnakufaaa'' baada tu ya maneno hayo tuanza kuona moshi ukiingia ndani ya costa ile tulishuka salama na tukaondoka tukiiacha gari inawaka moto na ile sauti ikajirudia tena kwamba Natakiwa kuomba sana wiki hiyo. Ilikuwa ni wiki ngumu sana maana mara kusingiziwa mara kutukwana bila sababu, kila mtu akiwa kinyume changu lakini moyoni nilihakikisha kabisa kwamba MUNGU yuko upande wangu, aliniponya na kunilinda na wiki iliisha salama, nilimshukuru sana BWANA kwa kunipenda na kunitumia ujumbe wa kunitaka kuomba kupitia ndoto, adui alikuwa amepanga mabaya sana lakini BWANA aliyakataa hayo na akanipa uzima. Kumcha MUNGU kuna faida sana. Kuna watu wake yaani wenye manukato yake na kuna watu ambao bado wako upande wa adui na wanamanukato ya adui. MUNGU anatutaka wote tuwe na manukato ya KRISTO mbele ya watu wote.

 MAMBO 3 YANAYOKUTAMBULISHA KWAMBA WEWE NI MTU WA MUNGU.

1.   IMANI YAKO YA UTII.

 MUNGU anaangalia utii wako kwake.
Je ufahamu wako umegeuzwa kiasi gani ili kumjua YESU KRISTO na kumtii? 
Warumi 10:17 '' Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la KRISTO. ''
Kile unachokisikia unaweza kukitumikia.
Wengi walisikia uponyaji wa babu wa Loliondo kwa sababu imani chanzo chake ni kusikia walijikuta wakikitumikia kile walichokisikia ndio maana walimwendea mzee yule, Ndio maana unachokisikia unaweza ukajikuta unakitumikia. Imani chanzo chake ni kusikia, Hata imani yako ni vile vile ulisikia kwanza ndipo ukachukua hatua na kuitumikia imani hiyo. Ndugu zangu Imani ya kweli ipo moja tu yaani KRISTO YESU  ndio maana Imani sahihi hii chanzo chake ni kusikia na kusikia huko lazima kuwe kusikia neno la KRISTO na ukiamua kuishika imani hiyo una heri MUNGU atakupenda sana. Sasa imani yako ya utii ni ipi? Ndugu imani yako ya utii inatakiwa iwe KRISTO YESU na mtu wa MUNGU kwenye mambo 3 ya kumtambulisha kwamba huyo ni mtu wa MUNGU lazima awe na imani ya utii kwa BWANA YESU. Kama huna imani ya utii kwa BWANA YESU bado wewe hujawa mtu au mtumishi wa MUNGU. Ndugu mtii KRISTO na utabarikiwa milele.

2.    MANENO YAKO UNAYOTAMKA.   

Maneno yako yanaweza kabisa yakawafanya   watu wajue kwamba ndani yako kuna MUNGU au kuna shetani.
Warumi 6:16 ''Hamjui ya kuwa kwake yeye ambaye mnajitoa nafsi zenu kuwa watumwa wake katika kumtii, mmekuwa watumwa wake yule mnayemtii, kwamba ni utumishi wa dhambi uletao mauti, au kwamba ni utumishi wa utii uletao haki. ''
Ndugu, uliyejitoa kumtumikia kwa kinywa chako wewe ni mtumwa wake huyo. Kama shetani anakitumia kinywa chako kwa mabaya basi wewe bado ni mtumwa wa shetani lakini kama kinywa chako kinatumika na ROHO MTAKATIFU Basi wewe ni mtumwa au mtumishi sahihi wa MUNGU aliye hai.
Mtume Petro Katika Mathayo 16:16 alitumika vyema alisema, Biblia inasema  ''Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe KRISTO, Mwana wa MUNGU aliye hai. ''
Lakini Petro huyo huyo Kwenye Mathayo 16:23 alikosea, Labda alikuwa hajajazwa nguvu za ROHO MTAKATIFU, Biblia inasema Mathayo 16:23 ''Akageuka, akamwambia Petro, Nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya MUNGU, bali ya wanadamu. ''.
Vinywa vyetu vinatakiwa vinene sahihi ya MUNGU. 
Mhubiri 12:14 ''Kwa maana MUNGU ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au likiwa baya ''

3.   MAWAZO.

Mawazo yana nguvu ya kutenda jema au baya.
Mtu wa MUNGU hatakiwi kuwa na mawazo mabaya.
Mwanzo 6:5 '' BWANA akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu sikuzote. '' 
Mawazo mabaya ni hatari sana, mawazo mabaya yanaweza kuchota nguvu ya MUNGU ndani yako, Mawazo mabaya yanaweza kuondoa hata upako ulioko ndani yako.
-Mawazo mabaya yana mbegu za shetani.
-Mawazo mabaya huzaa matendo mabaya.
Ndugu yangu, linda moyo wako kuliko yote uyalindayo, usikubali moyo wako uwaze mabaya. Mche BWANA MUNGU na tamani kumtii BWANA YESU peke yake.
Mithali 4:23 '' Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima. ''

Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani.
ROHO MTAKATIFU aliyenipa ujumbe huu ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
MUNGU akubariki sana
Ni mimi ndugu yako katika BWANA YESU.
Peter M Mabula
Maisha ya ushindi Ministry.
+255714252292
Bali wote waliompokea(YESU KRISTO) aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; -Yohana 1:12
 

Comments