CHANGAMOTO ZA MCHUMBA ALIYEZAA NA MTU MWINGINE KABLA YA NDOA!!

Na Mchungaji Peter Mitimingi, Mkurugenzi wa The Voice of Hope Ministry(VHM) Ya jijini Dae es salaam.

i. Matokeo ya Maisha yetu ya Nyuma Husafiri na Sisi
Sehemu ya matokeo ya aina ya maisha yetu ya siku za nyuma hubakia katika mfumo wa safari yetu ya maisha. Kuna mambo ambayo tuliyafanya katika siku zetu za zamani ambazo maandiko yanaita “zama za ujinga” baadhi ya mambo hayo hutuachia alama na kila tunapokwenda katika safari ya maisha yetu inakuwa ni vigumu kwa mambo kama hayo kufutika katika historia ya maisha yetu na hata katika uhalisia wa maisha yetu kwa ujumla.


ii. Watoto Waliotokana na Mahusiano ya Nyuma
Uwepo wa mtoto au watoto waliotokana na mahusiano ya kimapenzi kabla ya ndoa huweza kusababisha changamoto mbalimbali aambazo nimuhimu zikaangaliwa kwa kina. Endapo changamoto hizi hazitaangaliwa kwa kina zinaweza kulete athari kubwa zaidi kwa wahusika kama:
Zinaweza kulete athari kwa mtoto mwenyewe
Zinaweza kulete athari kwa mzazi aliye ondoka
Zinaweza kulete athari kwa mzazi aliyebaki na mtoto
Zinaweza kulete athari kwa mzazi mpya anayetarajiwa kuoana na huyo mzazi wa huyo mtoto
Zinaweza kulete athari kwa familiya ya wazazi wa huyo mtoto kwa pande zote mbili.
Zinaweza kulete athari kwa huyo mtoto pindi atakapokuja kuwa mtu mzima kwa maana ya kwamba mambo aliyotendewa alipokuwa mtoto kwa sehemu kubwa kuna uwezekano na yeye akawatendea wengine watakaokuwa chini ya himaya yake.


iii. Huu ni Wakati Muafaka wa ninyi Kuambiana Ukweli juu ya Watoto mliowapata kabla ya ndoa.
Endapo mmoja wenu alipata mtoto kabla ya ndoa basi huu ni wakati muafaka kwa wachumba hawa kuweza kufahamishana na kujulishana juu ya idadi ya watoto waliozaliwa kabla ya wao kuanza mahusiano haya ambayo wanataka kuyafanya kuwa ya mume na mke. 


iv. Eleza Ukweli Juu ya Aina na Kiwango cha Mahusiano na Yule au Wale Uliozaa nao Huko Nje
Mweleze mwenzi wako ukweli juu ya watoto ulionao na kama bado unamawasiliano na yule mtu uliyezaa naye mtoto huyo na pia ueleze ni mahusiano gani ambayo bado yapo kati yako wewe na huyo uliyezaa naye. Ni mahusiano ya kimajukumu kwamfano huwa unawasiliana naye kwajili ya kutuma au kupokea matumizi ya huyo mtoto au kuna mmoja wenu anajaribu kuvuka mpaka kwa kuzidisha kiwango cha mahusiano kama njia ya kujaribu kumvuta mwenzake katika hali ya kimapenzi tena katika hali isiyo rasmi. Hii itasaidia sana kumponya huyo mwenzako ili asidhanie kwamba huenda labda mmerudiana kinyemela kama njia ya kujikumbushia mapenzi ya zamani.


v. Kabla ya Maamuzi Pata Muda wa Kuomba na Kufikiri.
Baada ya kumueleza mchumba wako juu ya mtoto au watoto ulionao kabla ya kuanza mahusiano naye, sasa mchumba apewe muda wa kuomba na kufikiri kwa kina na kisha apewe uhuru wa kuamua kama atakuwa tayari kuoana nawe pamoja na watoto ulioza nje ya ndoa. Inahitaji muda wa kutosha kwa wahusika wote wawili kupata muda wa utulivu wa kuomba na kutafakari kabla ya kuchukua maamuzi maana kulingana na mazingira ya mahusiano yenyewe kuna mahusiano mengine ambayo yanaweza kugharimu wahusika hawa wanaotarajia kuoana. Sasa kabla ya kujifunga kitanzi ni vema mkapata muda wa kulitafakari tena kwa undani ndipo baadaye mnaweza kurudiana na kila mmoja akawa na jibu kamili baada ya kuomba na kutafakari.


vi. Endapo Mmoja Wenu Hasikii Amani ya Kuendelea na Jambo Hilo
Ikitokea kwamba mmoja kati yenu baada ya muda wake wa utulivu wa maombi na kutafakari akaona hasikii amani au hajapendezwa na jambo hilo, basi awe huru na wazi kueleza ukweli bila ya aibu badala ya kuingia hivyo hivyo kwa kuogopa kumuhuzunisha mtarajiwa wake. Na huyu mtarajiwa awe tayari kupokea jibu la aina yeyote kutoka kwa huyo mtarajiwa wake nahata kama jibu litakuja la hapana basi asijisikie vibaya na kulazimisha kwamba iwe kama alivyokuwa amekusudia yeye.


vii. Tuoane Ila Siko Tayari Kulea Watoto wa Nje
Endapo Mmoja wenu yupo tayari kuendelea na mambo ya kuoana ila hayupo tayari kukaa na mtoto au watoto. Basi jambo hilo litahitaji kuzungumzwa kwa kina juu ya kwamba kama katika familia yenu mpya hamtakaa na huyo mtoto -basi baadhi ya mambo ya msingi ni lazima myazungumze na kukubalina kwa mfano:
Mtoto atakuwa akiishi na nani ?
Mchakato mzima wa matunzo yake utakuwaje?
Mipaka ya mahusiano baina ya yeye na mzazi wake itakuwaje?
Kuna wakati ataruhusiwa kuja kutembelea pale na kukaa kwa muda au ndio mzazi wake itabidi yeye ndio amfuate huko aliko?
Gharama zake za kimasomo na kujikimu zitakuwaje? Nk.

Comments