NI NINI MAANA YA MUNGU KUMUUMBA MTU KWA SURA MFANO WAKE


Na Abel Sileiman Shiriwa
Watu wengi huchanganyikiwa kwa kitendo cha Mungu kusema alimuumba mtu kwa mfano wake na kwa sura yake,, yaani mwanaume na mwanamke wote hawa waliumbwa kwa mfano na sura ya MUNGU,
mawazo yao huyapeleka kwenye Nyuso (Face) na hata kufikia hatua ya kuuliza Mungu ana jinsia gani? Ya kike au ya kiume? Au ana jinsi zote 2? Kwa sababu tu MUNGU alimuumba mwanaume na mwanamke kwa mafano na sura yake.

Hayo ni mawazo ya wajinga na wapumbavu ambao hawatambui makusudi na mawazo ya Mungu, maana Daudi alishawatambua watu hao, nae akasema:
Zaburi 92:5 Ee Bwana, jinsi yalivyo makuu matendo yako! Mawazo yako ni mafumbo makubwa.
6 Mtu mjinga hayatambui hayo, Wala mpumbavu hayafahamu.

Mawazo ya Mungu ni mafumbo makubwa mtu mjinga hayatambui, wala mpumbavu hayafahamu hayo, ndiyo maana wanafikia kuuliza Mungu ana jinsia gani ya kiume au ya kike? Mungu ana sura gani ya kiume au ya Kike? Huo ni ujinga na upumbavu aliousema Daudi,
NI NINI SASA MAANA HALISI YA MUNGU KUMUUMBA MTU KWA MAFANO NA SUA YAKE?
Mwanzo 1:26 Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.
27 Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba.

Maana halisi ya Mungu kumuumba mtu kwa mafano na sura yake, ni ‘UTAKATIFU’ utakatifu ndiyo sura ya Mungu,
Kama Mungu angekuwa na Sura (Nyuso) za Kibinadamu, basi leo tungeuliza, Mungu ni mweupe au Mweusi?
Mungu ni Mzungu au Mchina, Ni Mwarabu au Muhindi? Ni MWAFRICA au Mkorea? Tungruliza Mungu ni mfupi au Mrefu? Mnene AU mwembamba? Lakini Mfano na sura ya Mungu si katika maumbile ya Mwili, Bali Utakatifu; Utakatifu, haubagui, rangi, wala kabila, haubagui Jinsia, huu ni kwa kila mtu autakae,

Adamu na Hawa walipoumbwa, walikuwa watakatifu, watu wasiokuwa na dhambi, ndiyo maana Mungu akasema wakatawale samaki wa baharini, ndege na wanyama, na kila kitu kilichopo duniani…. Hapo unaweza kuona ni kwa namna gani Mtu alivyo mfano na sura ya Mungu, maana Mungu ni mtawala wa vitu vyote, mtu nae akapewa utawala huo huo, Simba, Dubu, Mamba, Chui, Duma, Nyoka, na wanyama wote wakali tunaowashuhudia wakiwatafuna wanadamu leo, wakawa chini ya utawala wa mtu, hawakuwa na uwezo wa kumuua wala kumdhuru mtu, (Adamu na Hawa)kwa sababu walimuogopa, kama ambavyo wanamuogopa Mungu… kwa sababu hao walikuwa watatakatifu, (Wenye sura na mfano wa Mungu)…
“KITU GANI SASA KILICHOPELEKEA WANYAMA WAKALI WASIWAOGOPE WATU LEO KAMA ILIVYOKUWA MWANZO?”
DHAMBI: Adamu na Hawa walipomkosea Mungu kwa kukubali kuyafanya yale ambayo Mungu aliwakataza, yaani wasile matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya, ambao Mungu hakutaka waule, soma Mwanzo 2:16 wao wakala, baada ya shetani kumrubuni Hawa, Mungu alikasirika, na kuwanyang’anya Utawala aliokuwa amewapa, rejea Mwanzo 3:1-23 Kwa hivyo Ule mfano na sura ya Mungu, (utakatifu) Kwa Adamu na Hawa ukaondoka, kwa sababu Mungu hataki kukaa na mwenye dhambi, akawafukuza kwenye bustani na kuweka ulinzi ili wasiweze kuingia mle.
Mwanzo 3: 23 kwa hiyo Bwana Mungu akamtoa katika bustani ya Edeni, ailime ardhi ambayo katika hiyo alitwaliwa.
24 Basi akamfukuza huyo mtu, akaweka Makerubi, upande wa mashariki wa bustani ya Edeni, na upanga wa moto uliogeuka huko na huko, kuilinda njia ya mti wa uzima.

UTAKATIFU: Ulio sura ya Mungu ulipo mwondoka Adamu, watoto wake aliowazaa, wakaanza kuzaliwa kwa mfano na sura ya Adamu (Dhambi) na si kwa Sura na mfano wa Mungu tena, kama ilivyokuwa Mwanzo,
Mwanzo 5: 3 Adamu akaishi miaka mia na thelathini, akazaa mwana kwa sura yake, kwa mfano wake, akamwita jina lake Sethi.
Kwa hivyo Dhambi Iliondoa kabisa utukufu wa Mwanadamu kwa Mungu, NDIYO maana unaona leo watu tunawaogopa wanyama wa porini, wakati wao ndo walitakiwa kutuogopa sisi, Mamba nae aishie kwenye maji, nae tunamuogopa wakati sisi ndo tulitakiwa tuogopwe, nae,
kwa hivyo Ujumbe wa Mungu kwa wanadamu waliozaliwa na Adamu, wa kuwataka warejee kwenye mfano na sura yake ni Utakatifu tu, ndiyo maana Mungu akasema.

Walawi 19: 2 Nena na mkutano wote wa wana wa Israeli, uwaambie, Mtakuwa watakatifu; kwa kuwa mimi Bwana, Mungu wenu, ni mtakatifu.
Mtakuwa watakatifu kwa sababu Mungu wenu ni Mtakatifu: Huu ni urejesho wa mwanadamu kwa Mungu, awe mfano na sura ya Mungu, maana huwezi Kumkaribia Mungu kama wewe siyo Mtakatifu,, Kama ambavyo watu wa Mwanzo walivyoweza kukaa Pamoja na Mungu, walipokuwa Watakatifu, sisi nasi watoto wa Adamu, ambao tumezaliwa chini ya dhambi, tukitaka kumuona Mungu, na kuwa pamoja nae, kama Maandiko yasemavyo.
Ufunuo 21: 3 Nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao.
4 Naye atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita.

Ni lazima tuutafute UTAKATIFU…
Waebrania 12: 14 Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;
15 mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya Mungu; shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo.
16 Asiwepo mwasherati wala asiyemcha Mungu, kama Esau, aliyeuuza urithi wake wa mzaliwa wa kwanza kwa ajili ya chakula kimoja.

Kumbuka Mussa alikataliwa na Mungu asiweze kuuona Uso wake, hapa duniani, kwa sababu Mwanadamu, aishie hapa Duniani, hawezi kuuona uso wa Mungu na akaishi
Kutoka 33;20 Kisha akasema, Huwezi kuniona uso wangu, maana mwanadamu hataniona akaishi.
Kwa hivyo sisi tutamuona Mungu Mbinguni, tukiishi Maisha Matakatifu hapa Duniani.
UTAKATIFU TUNAUPATA KUPITIA KWA MWOKOZI WETU YESU KRISTO, MAANA YEYE ALIKUJA NA KUISHI BILA KUFANYA DHAMBI, KWA HIVYO YEYE NDIYE MWENYE KUUREJESHA UTUKUFU TULIOUPOTEZA.
1 Petro 1: 14 Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu;
15 bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;
16 kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.
17 Na ikiwa mnamwita Baba, yeye ahukumuye kila mtu pasipo upendeleo, kwa kadiri ya kazi yake, enendeni kwa hofu katika wakati wenu wa kukaa hapa kama wageni.
18 Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu;
19 bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo.
20 Naye amejulikana kweli tangu zamani, kabla haijawekwa misingi ya dunia; lakini alifunuliwa mwisho wa zamani kwa ajili yenu;
21 ambao kwa yeye mmekuwa wenye kumwamini Mungu, aliyemfufua katika wafu akampa utukufu; hata imani yenu na tumaini lenu liwe kwa Mungu.
22 Mkiisha kujitakasa roho zenu kwa kuitii kweli, hata kuufikilia upendano wa ndugu usio na unafiki, basi jitahidini kupendana kwa moyo.
23 Kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika; kwa neno la Mungu lenye uzima, lidumulo hata milele.
24 Maana, Mwili wote ni kama majani, Na fahari yake yote ni kama ua la majani. Majani hukauka na ua lake huanguka;
25 Bali Neno la Bwana hudumu hata milele. Na neno hilo ni neno lile jema lililohubiriwa kwenu.

Yesu yeye ndiye njia kweli na uzima, Mtu hafiki kwa Baba nje na njia ya Yesu, kwa hivyo utakatifu huwezi kuupata kwa mwingine nje na Kristo, (Yohana 14;6) kwa maana huwezi kumuona Mungu ukiwa nje na Kristo, kwa sababu Kristo ni mfano na sura yake Mungu.
2 Wakorintho 4: 4 ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu.
TAHADHARI: Kama wewe unafanyamatendo haya mwili kamwe huwezi kujiita wewe ni mfano na sura ya Mungu.
Wagalatia 5: 19 Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi,
20 ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi,
21 husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.

Aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu anaepukana na dhambi, kwa hivyo tujitahidi sana kutenda mapenzi ya Mungu, tuwe Watakatifu, Ili mamlaka yetu yarejeshwe, Kumbuka Daniel Alikuwa Mtakatifu, alipotupwa kwenye Himaya ya Simba, wale Simba hawakumtafuna, Ni vipi kama angekuwa mtu muovu angesalimika? Yesu ametoa mamlaka ya kukanyaga nge na nyoka, na nguvu zote za yule muovu, wala hakuna kitu kitacho tudhuru, Sasa kama tusipokuwa Watakatifu, ni vipi tutaweza kuyachukua mamlaka hayo? TUREJEENI KWENYE MWANZO WETU WA KUUMBWA…. Ili siku ile ya Mwisho tukamuone Mungu.

Comments