AINA ZA MANABII.

Ndugu msomaji wangu. Ninayo furaha kwa wakati huu, kukufundisha aina za manabii kama ifuatavyo:-
i. Nabii wa ndoto.
ii. Nabii wa Maono.
iii. Nabii wa mafunuo.
iv. Nabii wa maono ya Mungu Baba.
v. Nabii wa baraza
vi. Nabii wa neno
vii. Nabii wa neno,maono na mafunuo ya Mungu.
viii. Nabii anayezungumza Na Mungu mdomo kwa mdomo.......
ix. Nabii mwenye mamlaka ya kuliitia jina la BWANA na akaitikiwa.
x. Nabii wa mataifa.
xi. Nabii katika idara ya mwonaji

UFAFANUZI:
1. Nabii wa Ndoto
Hutokea usiku wakati mtu amelala usingizi mzito, Aidha ukiota kama unaangalia video, ujue neno hilo litampata mtu mwingine. Lakini ukiota na wewe upo ndani ya tukio, ujue yatakupata

Yeremia 23:22
Mara nyingi ndoto, hutokea wakati mtu amelala na amepumzika asilimia mia 100%, yaani usingizi mzito. Na mara nyingi hutokea wakati wa usiku wa manane saa sita mpaka saa tisa, au wakati wowote ule ambao utakukuta umelala usingizi mzito sana.
Mwanzo 37:9… “Akaota ndoto nyingine, akawaambia ndugu zake akasema, angalieni nimeota ndoto nyingine, natazama, jua na mwezi na nyota kumi na moja zikaniinamia”
Yeremia 23:28… “Nabii aliye na ndoto, na aseme ndoto yake; na yeye aliye na neno langu, na aseme neno langu kwa uaminifu.
Jinsi ndoto inavyofanya kazi ulimwengu wa roho:
Nabii anayefunuliwa kupitia ndoto anapata maneno haya Kama ifuatavyo;
Mungu Aliye hai anapenda kutumia mfumo wa fikra ulio ndani ya mwanadamu, kupitisha ujumbe wa picha na sauti, kwa namna ya ndoto, ili kumtaarifu mwanadamu kuhusu tukio Fulani, litakalotokea maishani mwake au hapa duniani. Kwa hiyo unapo amka kutoka usingizini unatakiwa uombe Mungu ili kuzuia ile vita uliyoiona isitokee.

2. Nabii wa Maono
Nabii wa aina hii amepewa jicho la kiroho la kuona umbali wa wastani; mfano:
Miezi kadhaa ijayo au iliyopita au ijayo.
2 Samweli 12:1-7,9
Ndipo BWANA akamtuma Nathani aende kwa Daudi.naye akamwendea akamwambiapalikuwa na watu wawili katika mji mmoja;mmoja wao alikuwa tajiri na wapili masikini. Yule tajiri alikuwa na kondoo na ng’ombe wengi sana.;bali Yule masikini hakuwa na kitu, ila mwanakondoo mmoja mdogo, ambaye amemnunua na kumlea.naye akakuwa pamoja naye, na pamoja na wanawe hula sehemu ya posho yake, na kukinywea kikombe chake na kulala kifuani mwake,akawa kwake kama binti. Hata msafiri mmoja akamfikia Yule tajiri, naye akaacha kutwaa mmoja wa kondoo zake mwenyewe au mmoja wa ng’ombe zake mwenyewe ili kumwandalia Yule msafiri aliyemfikilia, bali alimnyang’anya Yule masikini mwanakondoo wake na akamwandalia Yule aliye mfikilia, ndipo hasira ya Daudi ikawaka sana juu ya mtu Yule; akamwambia Nathani, aishivyo BWANA, mtu huyu aliyetenda jambo hili, hakika yake astahili kufa; naye atamrudishia Yule mwanakondoo mara nne. Kwa sababu ametenda jambo hili, na kwasababu hakuwa na huruma. Basi Nathani akamwambia Daudi,Wewe ndiwe mtu huyo. BWANA, Mungu wa Israeli asema hivi; nalikutia mafuta uwe mfalme juu ya Israel, nikakuokoa na mkono wa Sauli. Kwanini umelidharau neno la BWANA, na kufanya yaliyo mabaya machoni pake? Umempiga Uria Mhiti kwa upanga , nawe umemtwaa mkewe kuwa mke wako, nawe umemuua huyo kwa upanga wa wana wa Amoni”
Kwa hiyo nabii wa maono ndivyo anavyo ona katika macho yake ya rohoni. Anafunuliwa tukio lililopita siku,miezi, au miaka michache.
Na ili aweze kuona mbali zaidi inabidi aombe kwa Mungu ili apewe hatua mpya na inayofuata kutoka mbinguni ili aweze kuona mbali zaidi. Juhudi na shauku aliyonayo, itapelekea Roho Mtakatifu amfikirie na kumwongezea macho mapya yanayo ona umbali mrefu sana.

Aina Za Manabii Wa Maono:
i. Nabii wa maono anayefunuliwa mashauri ya wafalme.
ii. Nabii wa maono anayetumika na adhabu za Mungu.
iii. Nabii wa maono anayetumika na sauti ya baragumu.
iv. Nabii wa maono ya mbinguni anayetumika na radi kuu.
v. Nabii wa maono anayetumika na baragumu saba.
vi. Nabii wa maono anayefunuliwa kupitia kioo
vii. Nabii wa maono mwenye karama na matendo makuu ya miujiza ya Mungu.

Nabii wa Maono Anayefunuliwa Siri Za Wafalme: 2Samweli 12:1-10
Nabii wa aina hii,anafunuliwa siri na mashauri ya watawala au wakuu wa ki-dunia. Maranyingi Mungu anamwonyesha mashauri ya wafalme, na kumtuma kwenda kuwaonya, hasa wanapomwasi Mungu Aliye Hai. Katika hali hii, Mungu anawatumia Manabii wa aina hii kutokana na asili zao. Lakini huyu wa kuonya, ni lazima katika asili yake anakuwa mkali sana. Ndipo baada ya kuokoka na kupokea kipawa hiki cha Unabii, anatumika na kipawa hiki kwa namna alivyo.

Nabii wa Maono Anayetumika Na Adhabu Za Mungu:
Nabii wa aina hii anatumika na hasira kali za Mungu Aliye Hai kwa kiasi cha kutisha. Na anatumwa kwenda kuadhibu mtu, watu au taifa Fulani. Kwahiyo mkononi mwake amebeba hukumu na adhabu za Munga Aliye Hai.

Aina za adhabu anazotumika nazo ni;
i. Mapigo ya njaa katika uso wan chi yanayosababisha vifo vya watu wengi.
ii. Fimbo ya magonjwa makubwa ya kutisha kama tauni, inanyopelekea watu wengi kufa sana.
iii. Mapigo au fimbo ya vita katika nchi, itakayosababisha maafa makubwa sana kama ilivyotokea Afghanistani, Iraqi,Irani, Yugoslavia, na Sudani. Ifahamike kwamba tatizo la vita katika nchi Fulani, sio neno la bahati mbaya, au la kumlaumu mtu Fulani. Bali linaanzia ulimwengu wa roho, ndipo machafuko haya yanaingia na kuishukia nchi Fulani iliyokusudiwa kuadhibiwa Na Mungu Aliye Hai.
iv. 2Samweli 24:11-15…
” Na Daudi akipoondoka asubuhi,neno la BWANA likamjia Nabii Gadi, mwonaji wake Daudi, kusema, nenda ukanene na Daudi, BWANA, asema hivi;nakuwekea mambo matatu; katika haya uchague moja nikutendee hilo. Basi Gadi akamwendea Daudi akamweleza akamwambia, basi miaka saba ya njaa ikujie katika nchi yako? Au miezi mitatu ukimbie mbele ya adui yako huku wakikufuatia? Au siku tatu iwe tauni katika nchi yako?, fanya shauri sasa ufikiri, ni jawabu gani nimrudishie yeye aliyenituma. Naye Daudi akanwambia Gadi, nimeingia katika mashaka sana, basi sasa natuanguke katika mkono wa BWANA, kwa kuwa rehema zake ni nyingi; wala nisianguke katika mkono wa binadamu. Basi BWANA akawaletea Israeli tauni, tangu saubuhi hadi wakati ulioamriwa; nao wakafa watu toka Dani mpaka Beer-sheba sabini elfu”

Nabii wa aina hii akipatikana ndani ya kanisa ni lazima viongozi wote na waumini wote wa hilo kanisa wakae katika hali ya tahadhari sana, pamoja na maisha ya utakatifu, vinginevyo, kifo ni nje nje.
Nabii wa Maono Anayetumika na Sauti Ya Baragumu:
Nabii wa aina hii,anapokea unabii katika hali na namna ya utukufu na utisho wa pekee, unaoambatana na sauti yenye utisho kutoka mbinguni, inayo ambatana na nguvu kutoka mbinguni kwa Mungu aliye hai.
Ufunuo 1:10-13…”Nalikuwa katika Roho siku ya Bwana; nikasikia sauti kuu nyuma yangu kama sauti ya baragumu, ikisema, haya uyaonayo uyaandike katika chuo, ukayapeleke kwa hayo makanisa saba:Efeso na Smirna na Pergamo na Thiatira, na Sardi na Filadelfia, na Laodikia. Nikageuka niione ile sauti iliyosema nami. na nilipogeuka niliona vinara vya taa saba vya dhahabu; na katikati ya vile vinara nikaona mtu mfano wa mwanadamu, amevaa vazi lililofika miguuni, na kufungwa mshipi wa dhahabu matitini.
Wakati unabii huu unapoendelea katika hali hii, anaingia ulimwengu wa roho Ufunuo 8:7-10 na kuzungumza na Roho mtakatifu, Yesu Kristo, Mungu, au malaika.

Nabii wa maono ya mbinguni Anayetumika Na Radi Kuu:
Nabii wa aina hii anatumika na uchungu na hasira kali sana ya Mungu Aliye Hai, na nguvu nyingi za Mungu. Na amebeba unabii wenye maonyo kutoka mbinguni, maana amepewa jukumu la kufuatilia utekelezaji wa sheria za Mungu Aliye Hai ndani ya kanisa la Yesu Hapa duniani, na mahali pengine atakapoelekezwa na Uongozi wa Roho Mtakatifu.
Ezekieli 3:12-17…”
Ndipo roho ikaniinua name nikasikia nyuma yangu sauti kama mshindo wa radi kuu,ikisema na uhimidiwe utukufu wa BWANA,tokea mahali pake, nikasikia mshindo wa mabawa ya vile viumbe hai, walipogusana,, na mshindo wa yale magurudumu kando yao, mshindo wa radi kuu, basi roho ikaniinua ikanichukua mahali pengine name nikaenda kwa uchungu na hasira kali rohoni mwangu, na mkono wa BWANA ulikuwa juu yangu kwa nguvu. Ndipo nikawafikia watu waliohamishwa, huko tel-abibu, walikuwa wakikaa karibu na mto kebari, nikafika huko walikokuwa wakikaa; nikaketi huko miongoni mwao, muda wa siku saba, katika hali ya mshangao mwingi. Hata ikawa mwisho wa siku saba neno la BWANA likanijia kusema. Mwanadamu nimekuweka kuwa mlinzi wa nyumba ya Israeli, basi sikia neno hili litokalo katika kinywa change, ukawape maonyo haya yatokayo kwangu”.

Miiko na maadili ya kiroho yapovunjwa; Nabii huyu anakuwa mkali sana. Wakati wa kuonya akiwa katika hali ya mafuriko ya Roho Mtakatifu, anajaa nguvu za Roho Mtakatifu kwa wingi sana, na hasira kali za BWANA wakati wa maombi au ibada. Ndipo utisho wa hali ya juu sana unatawala mahali alipo. Vile vile anatumika na Roho ya Utakatifu akiwa katika hali hii.
Warumi 1:4…
”Na kudhihirishwa kwa uweza kuwa, mwana wa Mungu, kwa jinsi ya roho ya utakatifu, kwa ufufuo wa wafu, Yesu Kristo Bwana wetu”.

Nabii Wa Maono Anayetumika Na Ngurumo Saba:
Nabii huyu wa maono anapokea ujumbe wa unabii kutoka mbinguni kwa namn ya utisho sana, unao ambatana na ngurumo saba. Ndani ya kila ngurumo inayomjia, inaambatana na ujumbe wa sati na picha au atakavyopenda Mungu mwenyewe.
Ufunuo 10:1,3.
“Kisha nikaona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni, amevikwa wingu na upinde wa mvua,juu ya kichwa chake na uso wake ulikuwa kama jua, na miguu yake kama nguzo za moto, naye akalia kwa sauti kuu, kama samba angurumavyo. Na alipolia zile ngurumo saba zikatoa sauti zao

Ngurumo Saba:
Ngurumo hizi saba zina faida sana, maana zinaleta pia fundisho la maneno ya uzima ya kujenga, kuimarisha,kuonya na kuinua. Uzuri wa nabii wa aina hii, amepewa neema na uwezo wa kufundisha madhabahuni kwa sura ya Mwalimu.
Nabii huyu ni muhimu sana kwa kanisa, maana amepewa ufunuo wa neno (RHEMA). Na wakati anafundisha, anaweza kuangalia ulimwengu wa roho na kupata mafunuo yanayo wahusu wale anaowafundisha (MARA), wakati akiwa madhabahuni. Hakika huyu ndiye mwalimu wa pekee anayehitajika kanisani hivi sasa, ili kusaidia wengi wenye mahitaji.

Nabii Wa Maono Anayefunuliwa Kupitia Kioo:
Nabii wa aina hii anaona na kufunuliwa kupitia kioo maalum kutoka mbinguni. Kioo hiki kina akisi picha ambayo Roho Mtakatifu anataka nabii huyo aione, na kuileta mbele ya macho yake ya rohoni. Hii ni kama teknolojia katika somo la nuru ndani ya taaluma ya fizikia
(topic of light and mirror in the subject of physics)
1Korintho 13:12
“Maana wakati wa sasa tunaona kwa kioo, kwa jinsi ya fumbo;wakati ule tutaona uso kwa uso, wakati wa sasa nafahamu kwa sehemu;wakati ule nitajua sana, kama mimi name nilivyojuliwa sana”.
Nabii huyu anaweza kuliona neno ambalo Manabii wenzake hawajaliona. Maneno yaliyofichika sana kutoka ulimwengu wa roho, yeye amepewa neema ya ziada inayomwekea kioo ili aone kwa ufasaha.1Korintho 2:10 Roho Mtakatifu anawasaidia manabii wa aina hii, kupata mafunuo au unabii kupitia kioo maalum cha mbinguni. (Heavenly sight mirror) Ufunuo 4:6.

Nabii Wa Maono Mwenye Karama Na Matendo Makuu
Ya Miujiza Ya Mungu:
Nabii wa aina hii anatumika sana na maajabu ya Mungu Aliye Hai. Vile vile anatumika na nguvu za uumbaji wa ki-Mungu na nguvu za zamani zijazo kutoka mbinguni, kwa hali ya juu sana, inayopita uwezo wa kufikiri wa mwanadamu.
Waebrania 6:4… “ Kwa maana hao waliokwisha kupewa nuru, na kukionja kipawa cha mbinguni, na kufanywa washirika wa Roho Mtakatifu”.
Mfano wa nguvu za zamani zijazo:
i. Marko 6:47-51--------- Yesu kutembea juu ya maji.
ii. Kutoka 7:19 ------------ Musa anageuza maji kuwa damu
iii. Kutoka 8:17------------- Musa anageuza vumbi kuwa chawa.
iv. Kutoka 17:6,7----------- Musa analipiga jabali na linatoa maji ya kunywa.
v. Kutoka 14:15-18-------- Musa anaigawanya bahari na njia inatokea.

Kuheshimu Manabii
Nabii wa aina hii anaweza kukiita kitu chochote na kikatokea, katika hali ya kushangaza sana. Akitamka neno hata kama ni la kwake linatukia wakati uo huo.
Yoshua 10:12.
“Ndipo Yoshua akanena na BWANA, katika siku hiyo ambayo, BWANA aliwatoa waamori, mbele ya macho ya wana wa Israeli, akasema mbele ya macho ya waisraeli, wewe jua simama juu ya Gibeoni; na wewe mwezi simama katika bonde la Aiyaloni. Ndipo jua likasimama na mwezi ukatulia, Hata hilo taifa lilipokuwa, limekwisha jipatilizia juu ya adui zao……………”.
Katika andiko hili Joshua alisimamisha jua na mwezi katika bonde la Aiyaloni wakati akilipiza kisasi……Hatari iliyopo kwa aina hii Nabii, ukishindana naye au kumpinga na kumwonyesha jeuri na dharau, lazima utakufa.
Maana atakutamkia neno katika haira ya Mungu na kukufagia mpaka futi sita ardhini. Na hii ndio ole kwa wale wote wanaopiga vita manabii kwa kutumia madhabahu( yaani kutumia biblia au maandiko Fulani ndani ya biblia na kuwashambulia Manabii).
Manabii ni wa kuheshimiwa sana maana wamepewa neema ya kusimama mbele za Mungu Aliyeumba mbingu na nchi. Manabii ni wahudumu wa muhimu sana kanisani au katika mwili wa Yesu Kristo. Tuwapende na kuwakubali kwa kuwa ni watumishi maalum sana.

3. Nabii wa Mafunuo
Nabii wa aina hii, amepewa jicho la kuona mbali sana. Mfano; miaka ijayo mingi sana au iliyopita.
Ufunuo 21:10
“Akanichukua katika Roho mpaka mlima mkubwa mrefu, akanionyesha ule mji mtakatifu, Yerusalem ukishuka kutoka mbinguni kwa Mwenyezi Mungu”
Nabii wa mafunuo anaweza kuzijua siri zako tangu ungali tumboni mpaka utu uzima wako. Na kama akipewa karama za matendo ya miujiza na uponyaji, inakuwa faida kubwa sana, maana watu wengi wanaokuja kanisani watasaidika sana, na kupokea uponyaji wa watatizo na magonjwa ya aina mbali mbali.
Kwakuwa wana uwezo katika Mungu kujua chanzo cha matatizo au magonjwa ya watu. Na wanafunuliwa jinsi ya kuomba kwa msaada wa Roho Mtakatifu.

Faida Za Nabii Wa Mafunuo Kiuchumi,Kijamii:
Katika aina hii ya nabii, vilevile kuna ambao wana neema ya kuonyeshwa, maneno ya elimu na aina mbalimbali za ufundi,sayansi na teknolojia, kwa ajili ya maendeleo na ustaharabu.
Manabii wa aina hii wameisaidia sana Ulaya na Marekani, kuendelea kisayansi na kitekinolojia, na kufikia kufanikiwa sana kielimu na kiuchumi.

Jinsi Afrika Ilivyoathirika Kutokana na Kuipiga Vita Huduma Ya Unabii:
Sababu hii imeifanya Afrika kuwa nyuma sana kimaendeleo na kisayansi na kiteknolojia kwa kuwa, huduma ya unabii imekuwa ikipigwa vita sana, hasa na Wachungaji wa makanisa Fulani la kilokole. Mwisho wa siku wamesababisha Afrika kuwa fukara sana, bila ya wao kujua hili. Ndiyo maana wazungu hawakufundisha maneno ya Huduma ya Unabii Afrika, kwa kuwa hawakutaka mwafrika aifikie fahari ya kimbingu waliyoipokea, bali walipokuja huku Afrika walifundisha; kuokoka, ubatizo wa maji mengi, na ujazo wa Roho Mtakatifu kwa sehemu ndogo sana. Maneno haya matatu ni kiwango cha darasa la pili kiroho. Ndio maana watumishi wengi wa Tanzania hawajui mafundisho ya Unabii, hawawezi na hawajui kuwalea waumini wenye Kipawa hiki cha Unabii. Kipawa hiki ni mali sana kina faida; za kiroho,kimwili, kiuchumi na kijamii. Kwa ajili hii unapokataa kipawa hiki cha Unabii, umekaribisha ufukara wa hali ya juu katika nchi.
Kutoka 31:1-4,
“BWANA akanena na Musa na kumwambia, angalia nimemwita kwa jina lake Bezaleli, mwana wa Uri, mwana wa Huri, name nemjaza roho ya Mungu katika hekima, na maarifa na ujuzi, na mambo ya kazi za kila aina, ili abuni kazi za ustadi, kuwa fundi wa dhahabu, fundi wa fedha na wa shaba”,

4. Nabii wa Maono Ya Mungu Baba.
Ezekieli 8:1-3.
“Naye akanyosha mfano wa mkono, akanishika kwa kishungi kimoja cha nywele, za kichwa change, nayo roho ikaniinua kati ya dunia na mbingu, ikanileta katika maono ya Mungu mpaka Yerusalemu, mpaka mlango wa kuingilia ua wa ndani, uelekeao upande wa kaskazini; mahali palipokuwa pamewekwa sanamu ya wivu,itiayo wivu.
Nabii wa aina hii amepewa neema ya kuvishwa mwili wa MALAIKA, kiasi cha kushangaza. Anaweza kutoweka na baadaye kurejea kama malaika.
2Korintho,12:1-4.
Nabii wa aina hii amepewa neema ya kuona na kusikia siri za wanadamu na na za Mungu aliye Hai. Namna yake ya kuona ni hii; anapelekwa mahali Fulani na kuonyeshwa maneno.
Na ikumbukwe kuwa hawaendi kwa mapenzi yao wenyewe, bali wanapelekwa na Mungu. Nabii wa aina hii analetwa na Roho mtakatifu mpaka ndani ya nyumba Fulani na kuonyeshwa siri za ndani sana za wanadamu.

5. Nabii Wa Maarifa
Nabii wa aina hii,anafunuliwa madawa ya mimea na chakula. Na vilevile , ana uwezo wa kufunuliwa chanzo cha tatizo lako Ezekiel,47:12
“Nakaribu na mto juu ya ukingo wake, upande huu na upande huu, utamea kila mti wa chakula, ambo majani yake hayata nyauka, wala matunda yake hayatatindika kamwe, utatoa matunda mapya kila mwezi, kwasababu maji yake yanatoka mahali patakatifu, na matunda yake yatakuwa ni chakula, na majani yake yatakuwa ni dawa.

Nabii wa maarifa anapotumika katika utumishi wake, anapata mafunuo ya Roho Mtakatifu ya uponyaji, kupitia; mimea, nafaka, na matunda. Kwa ajili ya uponyaji wa matatizo au magonjwa ya aina mbalimbali.
Namba yake ya utumishi inatembea katika mchepuo huu, tofauti na Manabii wa aina nyingine.

Ufunuo 22:2,3
“katikati ya njia kuu yake, na upande huu na upande huu wa ule mto, ulikuwapo mti wa uzima uzaao matunda aina kumi na mbili, wenye kutoa matunda yake kila mwezi, na majani ya mti huo ni ya kuwaponya mataifa. Wala hapatakuwa na laana yo yote tena. Na kiti cha enzi cha Mungu, na cha Mwanakondoo kitakuamo ndani yake, na watumwa wake watamtumikia.
Nabii huyu wa maarifa anatumika na aina hii ya utumishi, uanaotoka katika kiti cha enzi, kwa kuwa mungu ndiye aliyeumba mimea kwa ajili ya wanadamu na viumbe vingine. Mungu anautumia uumbaji wake katika uponyaji wa magonjwa waliyonayo wanadamu kwa jina la Yesu.
Watu wengi walifundishwa kumtumikia shetani tangu wangali tumboni, kupitia mila na desturi za makabila. Kuna baadhi ya makabila motto anapozaliwa , wanachukua kitovu na kukifanyia mila za kishetani. Baada ya hapo, wamekuwa wakiingia maagano na shetani bila ya kujua.
Zaburi 51:5
“Tazama mimi naliumbwa katika hali ya uovu, mama yangu alinichukua mimba hatiani”
Kutokana na hali hii laana huingia katika malango ya makabila mbalimbali, na kuleta uharibifu. Ndio maana Nabii wa maarifa ufunuliwa jinsi ulivyo ingia katika mtego wa shetani, na Mungu wa mbinguni, anampa maarifa ya kimbingu ili kumkomboa mwanadamu.
Isaya 28:18
“Na agano lenu mliloagana na mauti litabatilika, tena mapatano yenu mliyopatana na kuzimu, hayatasimama; pigo lifurikalo litakapopita ndipo ninyi mtakapokanyagwa nalo”.

Kutokana na maagano ambayo wanadamu walifanya na kuzimu kupitia mila za kishetani, zinasababisha laana kwa njia ya maarifa ya giza au kipepo.
Sasa ili mtu wa aina hii afunguliwe na kuponywa kupitia jina la Yesu, inahitaji vilevile karama ya maarifa ya upande wa NURU, kutoka kwa Roho Mtakatifu ifanye kazi ya kufungua, kama vile Roho Mtakatifu apendavyo.
1Korintho 12:8
“Maana mtu m’moja kwa Roho hupewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo Roho yeye Yule”.
Nabii wa Maarifa anatumika na KARAMA ya neno la Hekima na Neno la Maarifa, wakati anawafungua wagonjwa wanaohitaji huduma ya ukombozi na maarifa, ili kuondoa vifungo vya giza.

Upinzani Anaoupata Nabii Wa Maarifa:
Matendo 7:51, 52
Enyi wenye shingo ngumu, msio tahiriwa mioyo wala masikio, siku zote mnampinga Roho Mtakatifu, kama baba zenu walivyofanya, na ninyi ni vivyo hivyo. Ni yupi katika Manabii ambaye baba zenu hawakumuudhi? Nao waliwaua wale waliotabiri habari za kuja kwake Yule mwenye haki, ambaye sasa ninyi m’mekuwa wasaliti wake mkamwua”
Nabii wa maarifa anapingwa sana hasa na baadhi ya watumishi, kwa kuwa, wanafananisha kile anachokifanya upande wa NURU, na kila anachokifanya shetani na watu wake upande wa giza.
Wengi wanaompinga Nabii wa maarifa, wamekosa ufahamu wa neno, na hawana nuru ya ufahamu, (Efeso 1:17, 18). Lakini watumishi wenye NURU YA UFAHAMU, wanalijua hili, wala haliwapi taabu kulielewa.

6. Nabii wa Baraza
1Falme22:5-22
“1Wafalme 22:19
“Mikaya akasema sikia basi neno la BWANA; nalimwona BWANA ameketi katika kiti chake cha enzi, na jeshi lote la mbinguni wamesimama upande wake wa mkono wake wa kuume na wa kushoto”
Nabii wa aina hii, anahudhuria baraza au vikao vya mbinguni. Maneno yake ni ya kanuni sana. Akipatikana kanisani mtu kama huyu, kanisa litafaidika kiroho na kiuchumi. Kwa sasa Manabii wa aina hii ni wachache sana. Maana macho ya aina hii ni ya daraja la juu sana na adimu hapa duniani. Wakati wote Mungu Anapo kaa vikao mbinguni, Nabii wa baraza na yeye anaenda kuhudhuria vikao vya mbinguni. Kila kitakachozungumzwa na kuamriwa, yeye ataona na kusikia kwa ufasaha na ukanuni. Na unabii wa mtu huyu ni wa ukanuni na umenyooka vizuri.

7. Nabii wa Neno
Isaya38:1-5, Anatoa unabii wa papo kwa hapo. Amejaa unabii tumboni. Wakati wowote, yeye ana uwezo wa kutoa unabii. Ndani ya Nabii wa neno, kuna aina ya Nabii anayetumika na wapiganaji wa mbinguni.
Nabii huyu anatumika sana kuwakomesha watu wote wanaothubutu kuitukana kazi ya Mungu kwa jeuri 2Wafalme 20:1-10. Katika Biblia Nabii Isaya alitumia katika eneo hili wakati ulani wa enzi za mfalme Hezekia.

8. Nabii Na Kuhani
Ezekiel 1:3
“Neno la BWANA lilimjia Ezekieli kuhani, mwana wa Buzi kwa dhahiri, katika nchi ya wakaldayo, karibu na mto Kebari; na mkono wa BWANA ulikuwa hapo juu yake”.
Yeremia18:18,
“ hapo ndipo waliposema, njoni na tufanye mashauri juu ya Yeremia; maana sheria haitampotea kuhani, wala shauri halitampotea mwenye hekima,wala neno halitampotea Nabii…………..”.
Nabii wa aina hii ana sehemu ya Ukuhani ndani yake. Amekirimiwa uwezo wa kubariki, kuwaongezea wanadamu siku za kuishi. Na ni mtetezi wa watu mbele za Mungu Aliye Hai. Sio kila mtu ni kuhani, kama wengi wanavyodhani, bali kuhani ni mtumishi mwenye heshima ya juu kiroho kuliko nabii mbele za Mungu. Na unawekwa na Mungu mwenyewe, sio wewe kujiweka, au kupewa na wanadamu kienyeji.
Katika biblia nabii Samweli alitumika katika ngazi hii, wakati wa utumishi wake, siku za biblia.

9. Nabii Anayezungumza Na Mungu Mdomo kwa Mdomo.
Hesabu,12:8
“Kwake nitanena mdomo kwa mdomo, maana, waziwazi, wala si kwa mafumbo; na umbo la BWANA yeye ataliona……………”
Nabii huyu, anatokewa waziwazi, na Yesu, Roho Mtakatifu na Mungu baba, na kuongea nao ana kwa ana. Kutoka,33:3-12.
Nabii wa aina hii anatokewa na aidha;malaika,Yesu Kristo, au Mungu baba waziwazi bila kificho. Luka 9:28-34, aina hii ya Nabii hufunuliwa maneno kutoka mbinguni peupe na waziwazi, kwa neno la kitaalamu la Kigiriki ni; MARA.
Nabii huyu amepewa uwezo wa hali ya juu sana katika kuutawala ulimwengu wa roho. Na wakati wowote Mungu akiwa na neno anajifunua kwake peupe.

10. Nabii wa Dhamiri Safi
Rumi,9:1
“Nasema kweli katika Kristo, sisemi uongo,dhamiri yangu ikinishuhudia, katika Roho Mtakatifu”
Nabii huyu,anatumika na dhamiri safi, kutoka ndani ya moyo wake kwa neema ya Roho Mtakatifu na ni fundi wa Imani

11. Nabii wa Neno, Maono na Mafunuo ya Mungu:
Hii ni ngazi ya juu ya Nabii,anayetabiri na kufunuliwa maneno kutoka kwa Mungu moja kwa moja(straight). Na amepewa mamlaka ya juu sana, na anachokitaka moyoni mwake kinakuwa saa hiyohiyo, na akitamka neno linatokea saa iyo hiyo. Vilevile Nabii huyu amepewa kibali cha juu sana, na anaweza kubariki na kulaani. Ni nabii wa pekee sana. Na aina hii ya manabii ni adimu hivi sasa hapa duniani.
Hesabu 24:1-5

12. Nabii katika Idara ya Mwonaji:
Kazi ya Nabii wa aina hii ni kuangalia mashauri ya Mungu juu ya kazi yake, juu ya jamii, na watu binafsi. Lengo la Mungu hapa ni:
i. Kutahadharisha wanadamu wasimwasi Mungu.
ii. Kukosoa pale inapobidi au inapo onekana kasoro ndani ya taifa,jamii au kanisani.
iii. Kujenga kiroho na kuimarisha kazi ya Mungu hapa duniani.

Katika aina hii, anaitwa; Nabii kwakuwa anapata (Line) muunganiko au mtandao wa moja kwa moja kutoka kwa Mungu. Na anaitwa; Mwonaji kwa kuwa anapewa maono ya Mungu.
2Samweli 24:11-19 Yeremia 1:4-11

13. Nabii mwenye Mamlaka ya Kuliitia jina la BWANA na Akaitikia:
Nabii wa aina hii ni moja ya wale waliopewa mamlaka ya juu sana katika utumishi, mwenye neema ya kuliitia Jina la BWANA, na akasikilizwa na kuitikiwa papo hapo. Pia nabii wa aina hii amepewa mamlaka ya kushusha mbingu chini na utukufu
(shakaina glory), na BWANA Anateremka kupitia nguzo ya wingu, Wingu linaloshuka hapa linaleta mambo yafuatayo:- 1Samweli 12:18
i. Mambo ya kutisha Sana kutoka mbinguni.
ii. Matendo makuu ya Mungu Aliye Hai.
iii. Maajabu kutoka mbinguni.
iv. Katika hali hii ya utukufu mwingi, (Shakaina Glory) kila hitaji lililopo linapata jibu au majawabu.
Zaburi 99:6-8

14. Nabii Wa Mataifa:
Nabii wa aina hii amepewa neema ya kuhudumu katika mataifa mbalimbali katika kazi ya:
i. Kung’oa .
ii. Kubomoa.
iii. Kuharibu.
iv. Kuangamiza.
v. Kujenga .
vi. Kupanda.

Yeremia 1:4, 10
“Neno la BWANA, likanijia kusema, angalia nimekuweka leo juu ya mataifa, na juu ya falme,ili kung’oa na kubomoa, na kuharibu na kuangamiza, ili kujenga na kupanda”.

Ufafanuzi:
i. Kung’oa :
Hii ni kazi maalumu ya kung’oa kila pando la shetani, alilolipanda ndani ya watu, ardhi, eneo au nchi.
ii. Kubomoa:
Nabii katika upako huu anapewa mamlaka ya kubomoa ngome na falme za giza kwa jina la Yesu na kwa ufunuo atakaopewa na Roho Mtakatifu.
iii. Kuharibu:
Nabii wa aina hii amepewa mamlaka ya kuharibu kazi za shetani, kazi za mizimu, kazi za wachawi na kila aina ya mitego ya kishetani wanayotegeshewa wanadamu.
iv. Kuangamiza:
Nabii wa namba hii amepewa nguvu za kuangamiza majeshi ya pepo wabaya waliotumwa kuwatesa wanadamu na maisha yao.
v. Kujenga :
Nabii wa mataifa amepewa kibali cha kuujenga Ufalme wa Mungu kwa neema ya pekee, aliyokirimiwa na Mungu katika utumishi wake.
vi. Kupanda:
Upako mwingine wa nabii huyu ni kupanda mbegu njema ya neno na kazi ya Mungu hapa duniani.

MWL: JORDAN G. TWARINDWA
MOB: 0717 963078

Comments