NENO LA MUNGU NI LAKO BINAFSI, USILIKWEPE.

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze neno la MUNGU la uzima.
 ''Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu;-1 Petro 2:2''
-Maziwa ambayo tunaambiwa tuyatamani ni Neno la MUNGU lililo tayari kuweka mabadiliko katika maisha yetu kama tukilitii.
-Tumezaliwa kiroho kwa neno la MUNGU na ambapo tunatakiwa sasa kuendelea kunywa maziwa haya ya uzima mabyo ni neno la MUNGU.
-Neno la MUNGU ni kwa ajili ya kila mwanadmu, ni kwa ajili ya mhubiri na kwa ajili ya anayehubiriwa.
Hakuna asiyelihitaji neno maana Neno la MUNGU ni la muhimu sana kwa watu wote.
Mathayo 4:4 '' Naye akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha MUNGU.''
 -Inawezekana Kabisa Neno La MUNGU Likahubiriwa Ili Tu Kumsaidia Mtu Mmoja Tu Kwenye Ibada Ya Waumini 1000. 
Kwa Nini Mmoja Tu? 
Ni Kwa Sababu Huyo mmoja tu  Ndiye Atakayesikia Neno Hilo Na Kulitendea Kazi, Wale 998 Inawezekana Kabisa Watafundishwa Neno Hilo Lakini Wataliacha Kwenye Viti Au Mabenchi Kanisani, Wao Wataenda Majumbani Mwao Bila Hilo Neno. 
Mithali 15:5 '' Mpumbavu hudharau kurudiwa na babaye; Bali yeye aangaliaye maonyo hupata busara. ''

Mara Nyingi Tumekuwa Na Tabia Ya Kudhani Neno Linalohubiriwa Wakati Huo Halituhusu Sisi Bali Watu Fulani. 

 Waebrania 4:12 ''Maana Neno la MUNGU li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo''

Kama Kuna Mtu Hapendi Kukosa Ibada Ni Pamoja Na Mimi, Miaka Kadhaa Iliyopita Nilikuwa Kwenye Majukumu Ya Kiserikali Kwa Wiki 4 Mfululizo Hivyo Sikuhudhuria Ibada Kwa Muda Huo. Kuna Waumini Wenzangu Tukawa Tunaongea Kwa Simu Wakitoka Kanisani Na Kuniambia
 "Neno La Leo Lilikuwa Linakuhusu Wewe" 
Hiyo Ilitokea Mara Nyingi Nikawa Nawaambia Waniazime Madaftari Yao Ili Na Mimi Nijifunze Ujumbe Huo, Lakini Pia Nikawa Najiuliza "hawa Ndugu Kila Neno Wakihubiriwa Wanasema Linanifaa Mimi Peter, Je Wao Neno La Siku Ipi Ni Lao?".
 Ndugu Zangu, Neno Ni Kwa Ajili Ya Wote, Lipokee.

Yohana  21:15 ''Basi walipokwisha kula, YESU akamwambia Simoni Petro, Je! Simoni wa Yohana, wewe wanipenda kuliko hawa? Akamwambia , Naam ,BWANA, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Lisha wana-kondoo wangu.''
-Huu ni mfano wa watumishi waliopewa maagizo na MUNGU kwamba kila siku wahakikishe kondoo wa MUNGU wanakula na kushiba Neno lake.
Mara nyingi huwa Hakuna tatizo katika wachungaji ila tatizo liko kwenye kondoo maana kondoo wengi hawataki kula baadhi ya chakula. Mfano unaweza kushangiliwa sana ukihubiri kuhusu upendo na mahusiano lakini siku ukihubiri fungu la kumi na kukemea uzinzi, uongo na uchawi utashangaa kila mtu anabadilika. na kama mchungaji wa kondoo utatambua kabisa kwamba kondoo wako huwa hawapendi chakula cha kuwapa afya zaidi ila wanataka siku zote uwape chakula ambacho wakila mwezi mmoja tu mfululizo lazima waugue utapiamlo kitu ambacho kama mchungaji hukipendi.
Mithali 28:13 ''Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.''

-Ndugu zangu mara nyingi kondoo hawapendi kukemewa.ni jambo baya, ni muhimu kujua kwamba anayekukemea sio mchungaji ila ni Neno la MUNGU.
-Haitakiwi Kondoo kuwa na Nguvu kuliko Mchungaji na kupelekea kondoo kujipangia chakula cha kula siku hiyo. Ni mbaya maana wewe Mchungjai ulikabidhiwa na MUNGU hao kondoo ambapo ni wajibu wako kumuomba MUNGU ili akupe chakula stahiki kwa siku hiyo kwa ajili ya kondoo.

 2 Kor 4:2 ''Lakini tumekataa mambo ya aibu yaliyositirika, wala hatuenendi kwa hila, wala kulichanganya neno la MUNGU na uongo; bali kwa kuidhihirisha iliyo kweli twajionyesha kuwa na haki, dhamiri za watu zikitushuhudia mbele za MUNGU. ''

Kuna Ndugu Mmoja Aliniuliza
 "Kwanini Mchungaji Wangu Siku Nyingine Huwa Hanibariki Na Kupelekea Siku Hiyo Niwe Na Ibada Mbaya?" 
 Nikamuuliza Hakubariki Kivipi? Akajibu "Siku Hizo Asizonibariki, Huhubiri Shutuma Tu". 
 Nilipoendelea Kumuuliza Akasema "kila Siku Mchungaji Wangu Mahubiri Yake Ni Kukemea Uzinzi Tu, Kwani Dhambi Zingine Hazioni?"
Nilichogundua Kwa Ndugu Huyu Hataki Mahubiri Ya Kukemea Dhambi. 
-Hata Kwingine Au Hata Kanisani Kwenu Unaweza Ukasikia Maneno Ya Mtu Akisema "leo Sijabarikiwa Na Mahubiri" 
- Kumbe Alitamani Ahubiriwe Upendo Tu.
-Alitaka Atiwe Moyo Na Mhubiri Wakati Matendo Yake Ni Maovu.
 Ezekieli 3:18-19 '' Nimwambiapo mtu mbaya, Hakika utakufa; wewe usimpe maonyo, wala husemi na huyo mtu mbaya ili kumwonya, kusudi aache njia yake mbaya na kujiokoa roho yake; mtu yule mbaya atakufa katika uovu wake; lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako. Lakini ukimwonya mtu mbaya, wala yeye hauachi ubaya wake, wala njia yake mbaya, atakufa katika uovu wake; bali wewe umejiokoa roho yako. ''
 Ninachojua Mimi Anayekupenda Zaidi Ni Yule Anayekukemea, =Kama Anakufariji Pasipo hitaji Faraja Huyo Hakutakii Mema. =Kama Mahubiri Yamesemwa Yakithibitishwa Na Neno La MUNGU Bila Kulipindua Neno, Hayo Ni Mahubiri Sahihi Hata Kama Hayatakubariki. 
=Wanadamu Wengi Hutaka Biblia Inawafuate Wao Badala Ya Wao Kuifuata Biblia. 
Ndugu, Kama Hutabarikiwa Na Neno La MUNGU Basi Utabarikiwa Na Neno La shetani ambalo laitakusaidia chochote.
Ndugu tii Neno La MUNGU maana MUNGU huwatuma watumishi wake kila siku kwa ajili yako.
2 Timotheo  2:14 '' Uwakumbushe mambo hayo, ukiwaonya machoni pa MUNGU, wasiwe na mashindano ya maneno, ambayo hayana faida, bali huwaharibu wasikiao. ''

Ni Wakati wa kuwa makini sana.
BWANA Yuaja na mshahara mkononi mwake ili kumlipa kila mwanadamu sawasawa na kazi aliyoifanya akiwa duniani.

2 Timotheo 3:16-17 ''  Kila andiko, lenye pumzi ya MUNGU, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa MUNGU awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema. ''
-Neno la MUNGU ni muhimu sana kila siku na ni la lazima siku zote ili uwe na afnya sahihi ya kiroho.

Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako
Peter M Mabula
Maisha ya Ushindi Ministry.
+255714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.



Comments

Unknown said…
AMINA UBARIKIWE KWA MAFUNDISHO MAZURI