SIFA KUMI NA MBILI(12) ZA ROHO MTAKATIFU.



BWANA YESU asifiwe.
Karibu tujifunze umuhimu wa ROHO MTAKATIFU kwetu.
Mwanzo 41:38 '' ....  Tupate wapi mtu kama huyu, mwenye roho ya MUNGU ndani yake? ''
-Je ni kitu gani huwafanya watu wa nje washangae kwa mtu ambaye ana ROHO MTAKATIFU?

leo nazungumzia baadhi tu ya sifa na kazi za ROHO MTAKATIFU kwetu kanisa hai  la MUNGU.
1 Kor 2:14-15 '' Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya ROHO wa MUNGU; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni.Lakini mtu wa rohoni huyatambua yote, wala yeye hatambuliwi na mtu. ''
-kuna watu hata kuhudhuria tu ibada kwao ni mzigo kumbe ni kwa sababu wako empty yaani hawana ROHO MTAKATIFU.
-Kuna watu antena zao za rohoni hazinasi kumbe ni kwa sababu sio watii kwa MUNGU.

ROHO MTAKATIFU ni ahadi kwa waaminio wote ila wawe waaminio katika kweli, bila kuokoka ROHO MTAKATIFU wewe utamsikia tu kwenye TV watumishi wakinena na kusema mambo ambaye ROHO wa MUNGU amewaambia. 

MUNGU aliahidi kwa wote.

Yoeli 2:28-29 ''Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, waume kwa wake, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono; tena juu ya watumishi wenu, wanaume kwa wanawake, katika siku zile, nitamimina roho yangu. ''

Mfano kuna watu wanawaza kuhusu rais ajaye wa Tanzania lakini kuna watumishi wanamjua Rais huyo tangu miaka 9 iliyopita.
Kuna watu  wanaumiza kichwa juu ya ugonjwa wa ndugu zao fulani lakini kama ukisimama katika maombi na ukapata neema unaweza kabisa ukajua kwamba huyo mgonjwa atapona au atakufa. ROHO MTAKATIFU habahatishi katika jambo lolote  maana yeye ni MUNGU na anajua yote.

1 Thesalonike 5:19 ''  Msimzimishe ROHO; ''

-Kama unaye ROHO MTAKATIFU basi hakikisha humzimishi kwa wewe kutenda dhambi wala kutomtii. ukitenda dhambi au ukishindwa kumtii anaweza kuondoka kwako. akiondoka ni hatari sana kwako.

-ROHO MTAKATIFU huona mwisho kabla ya mwanzo hivyo akikukataza jambo acha tena liache kabisa. sishuhudii leo lakini nina shuhuda nyingi sana juu ya yale aliyoyafanya ROHO MTAKATIFU kwangu iwe kwa kunijulisha au hata kunionya pia.


BWANA YESU alisema tupokee ROHO MTAKATIFU, sasa wewe ambaye hata YESU humtii basi sahau kuhusu ROHO MTAKTIFU maana hawezi kuja kwako.
Yohana 20:22 '' Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni ROHO MTAKATIFU.''
Kuna kazi na sifa nyingi sana za ROHO MTAKATIFU ila hizi ni baadhi tu ya sifa na kazi hizo za ROHO MTAKATIFU.

    1.    ROHO MTAKATIFU hutujulisha yaliyopita, yaliyopo na yajayo.
    2.    ROHO MTAKATIFU hutuombea kwa kuugua kusikotamkika.
   3.    ROHO MTAKATIFU ni mtakatifu hivyo lazima akae patakatifu.
   4.    ROHO MTAKATIFU atakuwa na sisi watakatifu milele.
   5.    ROHO MTAKATIFU hutuelekeza mambo mazuri ya kutenda.
   6.    ROHO MTAKATIFU hutafasiri kwetu yale tusiyoyajua ili tuyajue.
   7.    ROHO MTAKATIFU humshuhudia KRISTO kwetu.
   8.    ROHO MTAKATIFU hutupa Karama njema kwa ajili ya utumishi.
   9.    ROHO MTAKATIFU hutupa huduma ili tutumike.
  10.  ROHO MTAKTIFU hutufariji na kutoa majibu ya nini cha kufanya.
  11.  ROHO MTAKTIFU hutupa nguvu za rohoni.
   12.  ROHO MTAKATIFU anajua yote.

1 Kor 2:10 '' Lakini MUNGU ametufunulia sisi kwa ROHO. Maana ROHO huchunguza yote, hata mafumbo ya MUNGU.  ''
Ni muhimu sana kujazwa ROHO MTAKATIFU.
-ROHO MTAKATIFU ni ahadi kwa waaminio wote wala sio baadhi tu ya waaminio.
-Kama hujampata ROHO MTAKATIFU hakikisha unampata maana Mkristo baada ya kuokoka hakuna jambo muhimu kwake kama ROHO MTAKATIFU na utakatifu.


Wagalatia 5:25 ''  Tukiishi kwa ROHO, na tuenende kwa ROHO.''
Mkristo bila ROHO MTAKATIFU ni kama gari bira mafuta na gari hilo linasafiri.
 Waefeso 6:18 ''  kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika ROHO, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;''
-Mkristo bila ROHO MTAKATIFU hawezi kuzishinda dhambi.
Kama hujazajwa ROHO MTAKATIFU nakuomba ndugu mpokee BWANA YESU na acha dhambi, kisha ishi maisha matakatifu na baada ya hapo mhitaji ROHO na yeye atakuja kwako na utaona mabadiliko makuu.
Ufunuo 2:17 '' Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa. Yeye ashindaye nitampa baadhi ya ile mana iliyofichwa, nami nitampa jiwe jeupe, na juu ya jiwe hilo limeandikwa jina jipya asilolijua mtu ila yeye anayelipokea. ''
-ROHO MTAKATIFU ni muhimu kwako kuliko chochote.
Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA. MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako
Peter M Mabula
+255714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments