TUNASHINDAJE DHAMBI NA MAMBO YA DUNIA? HIZI HAPA NJIA 10 ZA KUFUATA ILI USHINDE DHAMBI NA MAMBO YA DUNIA.

Na Peter M Mabula. Maisha ya ushindi.
BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze neno la uzima.
1 Yohana 5:4-5 ''  Kwa maana kila kitu kilichozaliwa na MUNGU huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu. Mwenye kuushinda ulimwengu ni nani, isipokuwa ni yeye aaminiye ya kwamba YESU ni Mwana wa MUNGU? '' 
-Utashinda ya dunia kwanza kwa wewe kuhama kutoka kwenye kutawaliwa na dunia na kuingia katika ufalme wa MUNGU kwa kumpokea YESU KRISTO.
-Tunashinda ya dunia kama tu tukiishika kwa usahihi imani ya KRISTO ambayo ndiyo imani ya uzima wa milele.
Ukishampokea YESU na kuanza kuishi maisha ya wokovu unatakiwa usitende mabaya tena na hakikisha unayashinda mabaya hayo kwa wewe kutenda mema. kama pombe ulikuwa ndio ubaya wako basi sasa usinywe tena pombe maana ni dhambi na badala yake ule muda uliokuwa unautumia kunywa pombe basi anza kuutumia katika maombi na kujifunza neno la MUNGU. 
Warumi 12:21 ''Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema. '' 
-Kama zamani ubaya wako ulikuwa uzinzi au uasherati basi sasa muda ule ambao ulikuwa ukiutumia kwa kuzini utumie katika kuwatembelea wagonjwa au utumie katika kumtembelea mchungaji wako na kumuuliza maswali ambayo yanakutatiza, au muda huo utumie katika kwenda kwenye mikutano ya injili au semina za kiroho.
Isaya 43:18 '' Msiyakumbuke mambo ya kwanza, wala msiyatafakari mambo ya zamani. '' 
 
Waliookoka Tumeamriwa Tuushinde Ulimwengu. 

Je Tunashindaje? 
Hapa nimekuandalia njia 10 za kukusaidia kushinda dhambi na mambo ya dunia.

       1.     Tunashinda Ulimwengu Kwa Maombi Ya Imani Kupitia Jina La YESU KRISTO. 
Marko 14:38 '' Kesheni mwombe, msije mkaingia majaribuni, roho i radhi ila mwili ni dhaifu.''
-Maombi ni maisha na maombi ni mkono mrefu wa kupokea kutoka kwa MUNGU.
''Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba.-1 Yohana 5:14-15''.
-Tena maombi ni agizo kwako.
Ombeni bila kukoma;- 1 Thesalonike 5:17''

        2.    Tunashinda Kwa Neno La MUNGU likikaa kwa wingi ndani yetu na tukilitendea kazi neno hilo.
Yohana 8:31-32 ''Basi YESU akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru.''
-Siku ile BWANA YESU alizungumza na wayahudi lakini leo neno lile lile anazungumza na wewe. 

Zaburi 119:11 ''Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi''
-Kumbe neno la MUNGU ukiliweka moyoni kwa wingi litakusaidia kutokutenda dhambi.
 
          3.    Tunashinda Kwa Kuenenda Na Kuongozwa Kwa ROHO. 
 Warumi 8:5-9 '' Kwa maana wale waufuatao mwili huyafikiri mambo ya mwili; bali wale waifuatao roho huyafikiri mambo ya roho. Kwa kuwa nia ya mwili ni mauti; bali nia ya roho ni uzima na amani.  Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya MUNGU, kwa maana haitii sheria ya MUNGU, wala haiwezi kuitii. Wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza MUNGU. Lakini ikiwa ROHO wa MUNGU anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na ROHO wa KRISTO, huyo si wake.''
 
        4.   Tunashinda Kwa Kujifunza Neno Na Kulitafakari Neno La MUNGU. 
 Zaburi 119:130''Kufafanusha maneno yako kwatia nuru, Na kumfahamisha mjinga. ''
-Neno la MUNGU lina nuru ndani yake na ukifahamishwa neno la MUNGU itakusaidia kushinda ya dunia na kushinda dhambi.
 
2 Timotheo 2:15 '' Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na MUNGU, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli.''
-Tumia neno la MUNGU kwa uhalali, usililazimishe neno likufuate wewe bali wewe ndio ya kulifuata neno. Usilisahihishe neno bali litii na utashinda dhambi na mambo yote ya dunia.
 1 Petro 2:2''Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu;''
-Neno la MUNGU ni maziwa safi ya akili yasiyochanganywa na chochote hivyo kunywa maziwa haya kila mara ndipo utasimama imara katika kusudi la MUNGU la uzima na utakaa mbali na kutumikishwa na dunia wala dhambi.

          5.    Tunashinda Kwa Kuishi Kama Wasafiri Tu Duniani Hivyo Wakati Wowote Tunaondoka. 
1 Petro 2:11-12 '' Wapenzi, nawasihi kama wapitaji na wasafiri, ziepukeni tamaa za mwili zipiganazo na roho. Mwe na mwenendo mzuri kati ya Mataifa, ili, iwapo huwasingizia kuwa watenda mabaya, wayatazamapo matendo yenu mazuri, wamtukuze MUNGU siku ya kujiliwa.'' 
-Duniani hatujafika ila tuko safarini kwenda kwetu mbinguni. tunatakiwa tuwe tayari muda wote kuchukuliwa. huko ndiko kuna furaha timilifu, huko ndiko tutarukaruka kama ndama kwa furaha, huko ndiko tutafurahi na BWANA YESU aliyetuokoa.
Wafilipi 3:20-21 '' Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, BWANA YESU KRISTO; atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote viwe chini yake. '' 

       6.   Tunashinda Kwa Kuhudhuria Ibada, semina za Neno la MUNGU au mikutano ya injili na kutii fundisho la Biblia tunalojifunza katika ibadaau mikutano hiyo ya kiroho.
Waebrania 10:25 '' wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia. ''

        7.   Tunashinda Kwa Kujishughurisha Na Mambo Ya MUNGU. 
Zaburi 2:11-12 ''Mtumikieni BWANA kwa kicho, Shangilieni kwa kutetemeka. Shikeni yaliyo bora asije akafanya hasira, Nanyi mkapotea njiani,Kwa kuwa hasira yake itawaka upesi,Heri wote wanaomkimbilia ''

       8.    Tunashinda Kwa Kujitenga Na Dunia.
1 Yohana 2:15-17 '' Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda BABA hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na BABA, bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya MUNGU adumu hata milele. ''

     9.  Tunashinda Kwa Kutokukaa Barazani Pa Wenye Mizaha wala kwenda katika njia ya wakosaji.
Zaburi 1:1-2 '' Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha. Bali sheria ya BWANA ndiyo impendezayo, Na sheria yake huitafakari mchana na usiku. ''

       10.   Tunashinda Ulimwengu Kwa Kutokufungwa Nira Moja Na Wasio Mwamini BWANA YESU. 
2 Kor 6:14-18 ''Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza? Tena pana ulinganifu gani kati ya KRISTO na Beliari? Au yeye aaminiye ana sehemu gani pamoja na yeye asiyeamini? Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la MUNGU na sanamu? Kwa maana sisi tu hekalu la MUNGU aliye hai; kama MUNGU alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa MUNGU wao, nao watakuwa watu wangu. Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema BWANA, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha. Nitakuwa BABA kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike,''

Ndugu usikubali shetani akakuzuia kuiendelea baraka yako ya uzima.
Madhara ya kuzuiliwa shetani kupita.
-Unaweza kujikuta unageuza Malengo yako
- Unaweza ukatofautiana na hatima ya maisha yako,
- Unaweza ukachelewa kufika katika hatima yako
- Unaweza kujikuta unakata tamaa ya kuendelea mbele,
- Unaweza ukatumikishwa japo hutaki.

Jambo la ajabu ni kwamba ukimtegemea BWANA YESU na kuliishi neno la MUNGU hakika shetani atakuogopa sana.
Yakobo 4:7-9 '' Basi mtiini MUNGU. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.  Mkaribieni MUNGU, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili. Huzunikeni na kuomboleza na kulia. Kucheka kwenu na kugeuzwe kuwa kuomboleza, na furaha yenu kuwa hamu. Jidhilini mbele za BWANA, naye atawakuza.''
-shetani hatakuogopa tu wewe bali ataliogopa zaidi neno la MUNGU lililo ndani yako.
Atamuogopa zaidi YESU KRISTO aliye ndani yako.
Atamuogopa zaidi ROHO MTAKATIFU maana ROHO hajawahi kushindwa na lolote.

Ushauri wangu ni huu kwa ndugu yule ambaye hajaokoka.
-Mpokee BWANA YESU kama BWANA na MKOMBOZI wako leo.
-Jitenge na mambo ya dunia yaliyo machukizo kwa MUNGU BABA.
-Hakikisha unakuwa mtu wa maombi.
-Kiri ushindi daima.
-Ongozwa na ROHO MTAKATIFU.
-Inuka uangaze maana BWANA YESU ndio ushindi wako.

Yohana 3:16-18 ''Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU.''

 Yale Anayokutendea MUNGU Ni Makubwa Sana Kuliko Mema Yote Wanayokutendea Wanadamu. Cha Ajabu Watu Wengi Huwashukuru Sana Wanadamu Kwa Matendo Yao Mema Kwao, Hupiga Magoti Kwa Unyenyekevu Mkuu Ili Kuwashukuru, Huinama Na Kuonyesha Nidhamu Ya Hali Ya Juu Kwa Watu Hao Waliowasaidia. Sio Vibaya Lakini Kumshukuru MUNGU Kungehitaji Unyenyekevu Zaidi Ya Ule Tunaouonyesha Kwa Wanadamu Maana Hata Matendo Ya MUNGU Ni Makuu Zaidi. Mara Nyingi Watu Wengi Husahau Hata Kumshukuru BWANA Kwa Makuu Aliyoyatenda. MUNGU Amewapa Afya, Amewalinda Na Mengine Mengi Lakini Ni Mara Chache Sana Kumshukuru,lakini Mwanadamu Akikupa Zawadi 2000 Unaweza Ukmshukuru Mara Kumi Kumi Lakini MUNGU Anashukuriwa Nusu Dakika Tena Huku Unatembea Kwenda Kazini. Biblia Inaagiza Kumshukuru MUNGU Siku Zote
Zaburi 136:1-9 '' Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni mwema; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Mshukuruni MUNGU wa miungu; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Mshukuruni BWANA wa mabwana; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Yeye peke yake afanya maajabu makuu; Kwa maana fadhili zake ni za milele.  Yeye aliyefanya mbingu kwa fahamu zake; Kwa maana fadhili zake ni za milele.  Yeye aliyeitandaza nchi juu ya maji; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Yeye aliyefanya mianga mikubwa; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Jua litawale mchana; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Mwezi na nyota zitawale usiku; Kwa maana fadhili zake ni za milele.   ''  
-Ndugu, Penda Kumshukuru BWANA Siku Zote, Sio Unakumbuka Kumshukuru MUNGU Siku Ya Birthday Yako Tu. Uhai Ni Zawadi Bora Kuliko Zote, Uhai Tunapewa Na MUNGU Hivyo Tumshukuru Sana Tena Sana BABA Wa Mbinguni Kwa Matendo Yake Makuu Siku Zote. Uzima wa milele tunapewa na BWANA peke yake hivyo kushukuru ni muhimu sana.
Ndugu yangu, songa mbele na BWANA YESU. Hata kama ndugu watakutenga baki kwa BWANA YESU maana yeye hatakuacha kamwe.

Zaburi 27:10 ''Baba yangu na mama yangu wameniacha, Bali BWANA atanikaribisha kwake.''
 Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA. MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako
Peter M Mabula
Maisha ya Ushindi Ministry.
mabula1986@gmail.com
+255714252292.
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili

Comments