UKO TAYARI KUKUTANA NA SIKU ILIYO KUU?

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze neno hai la MUNGU.
Karibu tuijue siku iliyo kuu na tujue tufanyeje sasa ili siku hiyo tuitwe heri na sio ole.

Ufunuo 6:17 '' Kwa maana siku iliyo kuu, ya hasira yao, imekuja; naye ni nani awezaye kusimama? ''

Kwa binadamu leo siku Siku iliyo kuu huwa inamaana kubwa sana.
-Kuna watu siku iliyokuu kwao ni siku ya kuzaliwa. 
-kuna wengine siku yao kuu ni siku ya kufunga ndoa. 
-Kuna wengine siku yao kuu ni siku ya kufa. 
-Kuna watu siku yao kuu ni siku ambayo waliajiriwa. 
-Kuna watu siku iliyokuu ni siku walipoondokewa na wazazi wao.
Hizo ni siku zilizozo kuu lakini ipo siku iliyokuu kuliko hizo. inaitwa siku ya BWANA iliyo kuu. hiyo ni siku ya BWANA lakini itawahusu wanadamu wote.
Je katika siku hiyo iliyo kuu utakuwa wapi ndugu?

Sefania 1:14-18 '' Hiyo siku ya BWANA iliyo kuu i karibu; I karibu, nayo inafanya haraka sana; Naam, sauti ya siku ya BWANA; Shujaa hulia kwa uchungu mwingi huko! Siku ile ni siku ya ghadhabu, Siku ya fadhaa na dhiki, Siku ya uharibifu na ukiwa, Siku ya giza na utusitusi, Siku ya mawingu na giza kuu, Siku ya tarumbeta na ya kamsa, Juu ya miji yenye maboma, Juu ya buruji zilizo ndefu sana. Nami nitawaletea wanadamu dhiki, hata watakwenda kama vipofu, kwa sababu wamemtenda BWANA dhambi; na damu yao itamwagwa kama mavumbi, na nyama yao kama mavi. Fedha yao wala dhahabu yao havitaweza kuwaokoa katika siku ile ya ghadhabu ya BWANA; bali nchi yote pia itateketezwa kwa moto wa wivu wake; maana atawakomesha watu wote wakaao katika nchi hii, naam, ukomo wa kutisha.''
-Siku ya BWANA i karibu sana.
-Ni siku ya mahesabu, ni siku ya kupokea majibu ya mtihani ulioufanya kipindi uko duniani.
-BWANA YESU Atakuja  Siku hiyo iliyo kuu. 
BWANA YESU Atakuja Siku hiyo Ndugu. 
Ufunuo 22:12-13 '' Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo. Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, wa kwanza na wa mwisho. '
-BWANA YESU Atakuja Kumlipa Kila Mwanadamu Sawa Na Matendo Yake. 
Ndugu yangu, Vitu Vyote Vya Dunia Ndugu Vitapita, Wanadamu Na Anasa Vyote Vitapita. 
-Jitahidi Ndugu Yangu Usitende Dhambi. BWANA YESU Yu Karibu. 
-Maisha Yako Ndugu Yangu Mpe BWANA YESU, Ujana Wako Ndugu Yangu Mpe BWANA YESU, Ishi Maisha Ya Wokovu Utafanya Vyema. BWANA YESU Yu Karibu.

 Sefania 3:8 '' Basi ningojeni, asema BWANA, hata siku ile nitakapoondoka kuteka mateka; maana nimeazimia kuwakusanya mataifa, ili nizikutanishe falme, nipate kuwamwagia ghadhabu yangu; naam, ukali wote wa hasira yangu; kwa maana dunia yote itateketezwa kwa moto wa wivu wangu.''
-Ndugu zangu, tukishindwa kumtii MUNGU tutamtii nani?
-Tukishindwa kulitii neno la MUNGU tutalitii neno la nani?
MUNGU anaagiza tutende mema, anaagiza tuishi maisha ya wokovu katika yeye. 
Hata leo BWANA anawaagiza watumishi wake ili wawaambie wanadamu wote kwamba mwisho u karibu.
BWANA anaagiza kwa watumishi wake

Yoeli 2:1 '' Pigeni tarumbeta katika Sayuni, Pigeni na kelele katika mlima wangu mtakatifu; Wenyeji wote wa nchi na watetemeke; Kwa maana siku ya BWANA inakuja. Kwa sababu inakaribia; '' 
-Hata somo hili limekuijia kwa sababu tu ya kuitii sauti ya MUNGU ya kuwaonya wanadamu.
-Napiga kelele nyingi kwa njia ya ujumbe huu ili tu mwenye sikio la kusikia na asikie.
Masomo kama haya kuyandaa sio suala la dakika 5, inahitaji kuomba na kumsikiliza ROHO MTAKATIFU na kutumia muda mwingi katika uwepo wa BWANA ndipo unaandaa ujumbe kama BWANA atakavyo. kuna jumbe huandaliwa hata miezi kadhaa ili tu wanadamu wageuke na kuifuata njia ya uzima ambayo ni BWANA YESU. Muda naandaa ujumbe kama huu ningeweza kuutumia kulala au kwenda kutembea lakini kwa kutii agizo la BWANA YESU ni muhimu kutumika maadamu tuna muda mfupi duniani ukilinganisha na milele ijayo. kwa hiyo kwa njia ya ku-post somo kama hili na mengine kila siku huko ni kulitimiza agizo la MUNGU kwamba tupige kelele ili wanadamu wageuke.

Ezekieli 7:19-20 ''Watatupa fedha yao katika njia kuu za mji, na dhahabu yao itakuwa kama kitu cha unajisi; fedha yao na dhahabu yao hazitaweza kuwaokoa siku ya ghadhabu ya BWANA; hawatajishibisha roho zao, wala hawatajijaza matumbo yao; kwa sababu zilikuwa kwazo la uovu wao. Na uzuri wa pambo lake, yeye aliuweka katika enzi, lakini wao walifanya sanamu za machukizo yao, na vitu vyao vichukizavyo, ndani yake; ndiyo maana nimeifanya kuwa kama kitu cha unajisi kwao.''
-Fedha na ufahari wowote wa kidunia hautaweza kumuokoa mwanadamu yeyote siku hiyo. 
-Utajiri hautasaidia siku hiyo.
-Siku hiyo ni siku ya kutolewa maamuzi ya milele.
Hakuna utani juu ya siku hiyo ila kupokea kila mtu kile kipimo chake stahiki sawasawa na matendo yake duniani.
ROHO MTAKATIFU amenipa  huu sasa ni ujumbe kama wa 4 au zaidi juu ya suala hili tu moja kwamba SIKU YA MWISHO I KARIBU na katika jumbe zote hizo kuhusu siku hiyo kila ujumbe una vitu vyake vya msisitizo.


Ni faida kuu kumpokea BWANA YESU na kaunza kumtii. yeye anasema
 ''Wote anipao BABA watakuja kwangu; wala ye yote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe. Kwa kuwa mimi sikushuka kutoka mbinguni ili niyafanye mapenzi yangu, bali mapenzi yake aliyenipeleka. Na mapenzi yake aliyenipeleka ni haya, ya kwamba katika wote alionipa nisimpoteze hata mmoja, bali nimfufue siku ya mwisho. Kwa kuwa mapenzi yake BABA yangu ni haya, ya kwamba kila amtazamaye Mwana na kumwamini yeye, awe na uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho-Yohana 6:37-40'' 
 Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA. MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako
Peter M Mabula
Maisha ya Ushindi Ministry.
mabula1986@gmail.com
+255714252292.
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments