JE! NI KITU GANI?

Na Frank Philip Seth.
“Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu” (Warumi 8:35-39).
Leo nimetafakari sana hii mistari katika Warumi 8 na kuona jambo ambalo sikuliona siku za nyuma. Nimejiuliza ni kwanini Paulo anaandika habari ya KUTEGWA na upendo wa Kristo akihusianisha na MATATIZO, MAHITAJI, MAJANGA au WATU wenye mamlaka/nguvu, nk.?
Nikatazama na kuona jambo hili, kama kuna mahali watu wamemwacha Mungu ni pale ambapo wanakutana na mambo MAGUMU, hasa kutoka kwa watu wasio tarajia. Nikajiuliza tena, nini thamani ya WOKOVU wako kama hujafika mahali pa KUCHAGUA kati ya mambo mawili? Yaani unafika mahali unasema, nina dhiki, sawa, ninatishiwa maisha, sawa, nisipotii hii mamlaka nitapoteza kazi, sawa, laikini NACHAGUA kusimama na KRISTO! Hii ndio maana ya “kumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa”. Yaani ukiangalia kila HALI inakupinga, hakuna watu wa kukufariji, mume/mke ndio kabisaa anakukatisha tamaa, ukigeukia wazazi ni kama vile hawakujui, na marafiki tena uliowategemea wamekupa kisogo! Unafika mahali alipofika mfalme Daudi, “unainua macho unaona milima tu, unajiuliza msaada wako utatoka wapi?” Kumbuka, msaada wako utatoka kwa BWANA, na wala usiwatumaini wanadamu hata kama wameitwa kwa jina gani kwa maana iko siku watageuka kwako na kuwa JARIBU na hutajua pa kukimbilia.
Nikajiuliza jambo jingine, hivi Ibilisi alipomwambia Mungu, “… Je! Huyo Ayubu yuamcha BWANA bure? Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi. Lakini nyosha mkono wako sasa, uyaguse hayo yote aliyo nayo, naye atakukufuru mbele za uso wako” (Ayubu 1:9-11). Ibilisi alikuwa na uhakika na anakichosema! Huku anampandishia Mungu wetu kifua! Ona hiyo kauli kisha upige picha anavyosema kwa kujitapa, ".. naye atakukufuru mbele za uso wako"! Fikiri Mungu anaambiwa hayo maneno na Ibilisi na kweli unamuumbua Mungu wako mbele za Adui zake! Jina lake linatukanwa mchana na usiku kwa ajili yako, maana watu watasema, "unamwona yule mlokole aliyepoteza mwelekeo?", hawatakaa kimnya mbele za BWANA kwa ajili yako.
Umewahi kujiuliza ni wakati gani Mungu anafurahishwa na wewe? Usidhani ni pale upelekapo sadaka nono mbele zake, uimbapo pambio za sifa mbele za watu wengi, au uhubiripo na kufanya kazi ya huduma. Umewahi kujiuliza kwamba thamani ya kuwa MCHAMUNGU kwa vile mambo yako vizuri, mume/mke anakutii/penda, kazini mambo safi, hela iko, hakuna ugonjwa, nk. Fikiri sasa mambo yako kinyume nawe, je! Unasimama katika imani au “atamkukufuru Mungu mbele za uso wake”?
Kumbuka jambo hili, hiyo shida inayokushikilia chini itadumu hadi ujue KUMHESHIMU Mungu awezaye kukuponya nayo. Ukisema, nitaendelea kuzini, kuiba, kusema uongo, kula rushwa, nk. hadi mambo yatakapokuwa mazuri kazini/ndoa/familia/nk., utasubiri hapo bila kuvuka kwa maana kadri umkoseavyo Mungu unajipunguzia nguvu za kushinda. Laiti ungefanya uamuzi leo na kusema, “Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu”.
Angalia jambo hili, ukisha kusema hayo, kuvuka kwako hakutakuwa kwa ghafla. Kama akina Shedrack, Meshack na Abednego, bado watakuja kukufunga kamba, kuchochea tanuru na kukutisha ili wajue MSIMAMO wako. Ndipo BWANA hukusubiria kwenye moto, ndani ya tanuru na si nje! MWISHOWE ukitupwa motoni utagundua hujaungua, kwenye maji mengi, utagundua hukufurikishwa! Huku ndiko kuitwako kushinda na zaidi ya kushinda! Saa hiyo umefungwa kamba, huwezi kujitetea zaidi yakusema “simwachi Yesu”, naye huja na kukupigania na wewe utakaa kimya.
Kama umehesabiwa kama kondoo wa kuchinjwa uwe tayari kwa kisu, lakini jua neno hili, atakayevumilia mpaka mwisho ndiye atakayeokoka. BWANA anasema, “Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha” (Luka 9:24) Je! Uko tayari kuvumilia mpaka mwisho?
Jiulize maswali haya, je! Ni NANI ameweza KUKUTENGA na upendo wa Kristo? Je! Ni JAMBO gani lililo la thamani kuliko Kristo ambalo kwa hilo umemwacha? Je! Unadhani msiba wako ukiisha ndio ukamtii Mungu utii wako utahesabiwa kuwa kitu?
Tazama, yu malangoni. Neema ya Kristo iwe nanyi tangu sana na hata milele, AMEN.
Frank Philip Seth.

Comments