KWA AKILI ZAKO UMESHINDWA, SASA MKABIDHI BWANA YESU JAMBO HILO UTASHINDA.


BWANA YESU atukuzwe ndugu zangu.
Karibu nikupe njia ya kufanya wakati magumu yanapokukabili na huoni msaada wa kutokea.
Je umeshawahi kuomba kijasiri namna hii ukimweleza MUNGU kwa ujasiri kama watumishi wa MUNGU wa zama za Biblia walivyofanya?
Mtumishi huyu baada ya kuona vita imekuwa kubwa na peke yake hawezi aliamua kusema maneno haya.
''Ee BWANA, utete nao wanaoteta nami, Upigane nao wanaopigana nami.-Zaburi 35:1''

-Yawezekana na wewe uko katika wakati mgumu na msaada huoni.
-Yawezekana kila mtu amegeuka adui yako na kila unalofanya haufanikiwi. ndugu napenda ujue kwamba bado liko tumaini kwa BWANA YESU na bado uko msaada kwa MUNGU wa Israeli.
Maombi ndio sauti ya kumwita MUNGU aliye hai ili akushindie.
BWANA YESU akija kwako haji kukusaidia ila kukushindia.
Siku moja katika maombi nilipata ufunuo wa ajabu sana.
Kuombea matatizo yangu sita na hata kama liko tatizo la 7 bado BWANA YESU atanishindia.

Ayubu 5:19-21 '' Yeye atakuokoa na mateso sita; Naam, hata katika saba hapana uovu utakaokugusa.Wakati wa njaa atakukomboa na mauti; Na vitani atakukomboa na nguvu za upanga.Utafichwa na mapigo ya ulimi; Wala usiogope maangamizo yatakapokuja. ''
-Licha ya kuisoma Biblia yote lakini siku napata ufunuo wa kuomba kwa kutumia maandiko hayo hapo ilikuwa kana kwamba tangu nizaliwe sikuwa nimewahi kusoma maandiko hayo katika Biblia. Nilipata nguvu za ajabu za kuomba na hakika nilianza kutaja kila teso ambalo lilikuwa katika maisha yangu na BWANA ni Mwaminifu maana yeye hajipingi na Neno lake na siku zote yeye analiangalia neno lake ili alitimize.
=Nilipata siri za ajabu kupitia maandiko hayo hapo juu.
-Nilijua kwamba MUNGU anajibu maombi, mateso au shida 6 zinazonisumbua nikimwita BWANA YESU hakika nitashinda. shida ya saba imebeba shida zote duniani maana saba ni namba na ukamilifu kwa MUNGU, Hata kama ndugu una mateso 77 bado yote yako katika saba na MUNGU anasema hata katika teso la saba hakuna uovu utakaokugusa (Ayubu 5:19).
-Katika vita yako dhidi ya wachawi , majini au uganga wa kienyeji, MUNGU bado atakushindia(Ayubu 5:20)
-Watu wakikunenea mabaya au wakikulaani kwa midomo yao bado ukiamua kuomba kwa MUNGU katika KRISTO YESU yeye MUNGU atakuficha na mapigo yote ya ulimi(Ayubu 5:21).
Ulimi una mapigo maana kama mtu kupitia waganga wa kienyeji atakutamkia mabaya yakupate hakika yatakupata kama usipokuwa mtu wa maombi na hasa usipokuwa mteule wa BWANA YESU. Ndugu maombi ni muhimu sana. penda kuomba mwenyewe sio kutegemea kuombewa tu wakati wewe umelala.

Ndugu yangu ukiomba kwa imani hakika BWANA atakuja kukushindia. Biblia iko wazi kabisa inasema
''Waambieni walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo, msiogope; tazama, MUNGU wenu atakuja na kisasi, na malipo ya MUNGU; atakuja na kuwaokoa ninyi.-Isaya 35:4''

BWANA YESU ndio msaada pekee kwako kwa ajili ya wewe kushinda. kama kuna watu walitoa kafara ya kuku au mnyama yeyote kumbuka damu ya mnyama huyo bado inakutamkia mabaya wewe na damu huwa haifi hivyo ili upone katika hayo mkimbilie BWANA YESU maana damu ya YESU pekee ndio inayoweza kufuta laana na balaa zote.
BWANA YESU kwa kinywa chake anasema '' Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.-Mathayo 11:28 ''
-Ndugu yangu amini katika BWANA YESU, omba katika BWANA YESU pekee na hakikisha unaomba kwa imani bila mashaka yeyote.
Mtumishi mmoja wa MUNGU kwa imani alisema maneno haya
''BWANA ataniokoa na kila neno baya, na kunihifadhi hata nifike ufalme wake wa mbinguni. Utukufu una Yeye milele na milele. Amina.-2 Timotheo 4:18''

-Huyu aliyasema haya kwa sababu alikuwa na imani. hata wewe unaweza kuomba kwa imani na ukapokea ushindi mkuu.
usilie ndugu bali omba maombi ya imani.
Usikate tamaa ndugu maana ushindi wako uko karibu sana kama ukiomba.

Maadui hawatakuweza kama ukisimama kwa imani katika maombi katika KRISTO YESU.
''Hata twathubutu kusema, BWANA ndiye anisaidiaye, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini?-Waebrania 13:6''
-Ndugu kama umeomba maombi ya kawaida basi anza kufunga kabisa, kama umeomba maombi ya kuomboleza basi sasa anza kuomba maombi ya vita. kama umeomba huku hujui unachoomba basi sasa anza kuomba maombi katika ROHO wa MUNGU.
''Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na MUNGU nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia.-1Yohana 4:4''
Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA. MUNGU akubariki sana.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula
Maisha ya Ushindi Ministry.
+255714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments