JE UNATAMANI KUKUA KIROHO? UJUMBE HUU UKUSAIDIE KUKUA KIROHO.

Na Mtumishi Peter Mabula.

BWANA YESU atukuzwe.
Karibu tuinuane kiroho.
Haya yanamhusu kila mkristo anayetamani kukua kiroho na kuzidi sana katika kumjua MUNGU na Neno lake. Nimekuletea maandiko kadhaa ambayo ukiyaelewa hakika hutarudi nyuma wala hutadumaa kiroho bali utastawi sana na kuendelea sana katika Kumjua MUNGU BABA na Neno lake.

Maandiko ni haya na yakusaidie kwa jina la YESU KRISTO.

=Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya KRISTO amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.-2 Wakorintho 5:17
-Hakikisha unakuwa mpya katika mwenende, tabia na matendo yako yote. hakikisha unakuwa na mwenendo unaombariki MUNGU, uwe na tabia njema na pia hakikisha matendo yako yote ni mema katika BWANA.


= Lakini yeye aijua njia niendeayo; Akisha kunijaribu, nitatoka kama dhahabu.-Ayubu 23:10
-Wakati mwingine majaribu huja lakini mche MUNGU hata katika magumu yako yote.


= Kwa kuwa BWANA ampendaye humrudi, Kama vile baba mwanawe ampendezaye. -Mithali 3:12
-Ishi maisha ya toba siku zote, ukikosea kwa bahati mbaya tubu na kuendelea mbele maana kulikimbia kanisa haitakusaidia hata kidogo. ila usikubali kutenda dhambi huku ukijua kabisa ni dhambi uitendayo.


=Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba;- Mathayo 7:24
-Dumu katika kujifunza na kulitafakari neno la MUNGU siku zote na tendea kazi neno la MUNGU unalojifunza.

= Akasema, Simoni, Simoni, tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano; lakini nimekuombea wewe ili imani yako isitindike; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako.-Luka 22:31B, 32
-Ukipitia magumu vumilia na omba sana, magumu mengine yana sababu ambaye inaweza kukusaidia baadae.


= Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi.-Yohana 12:24
-Hakikisha mwili wako unakufa kwa habari ya dhambi. uzike mwili wako katika damu ya YESU na hakikisha unautiisha mwili wako kwa maombi makali ili usirudi tena dhmbini.


= Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa; na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa. Yohana 15:2
-BWANA YESU anaahidi kukutunza na kukutumia vizuri katika kumletea MUNGU utukufu lakini unatakiwa kujitahidi sana katika matendo mema na ushuhudiaji wa injili kwa wengine.

= Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu.-Yohana 15:4
-Kaa katika Wokovu wa BWANA YESU siku zote na kukaa kwako huko katika Kweli hiyo ya MUNGU kutakufanya upate faida nyingi sana na faida ya kwanza ni uzima wa milele pamoja na kulindwa na MUNGU N.k.

= wala msiendelee kuvitoa viungo vyenu kuwa silaha za dhuluma kwa dhambi; bali jitoeni wenyewe kwa MUNGU kama walio hai baada ya kufa, na viungo vyenu kwa MUNGU kuwa silaha za haki. -Warumi 6:13
 -Jitoe kwa MUNGU kwa mambo yote, dumu katika kuwasaidia na wengine ili wampokee YESU KRISTO.

= Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake MUNGU, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza MUNGU, ndiyo ibada yenu yenye maana. Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya MUNGU yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu. -Warumi 12:1- 2
-Jitoe kwa MUNGU na wala usifuatishe anasa za kidunia ambazo zimejaa ubatili na maagano ya kishetani.

= Kwa hiyo hatulegei; bali ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, lakini utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku. Maana dhiki yetu nyepesi, iliyo ya muda wa kitambo tu, yatufanyia utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi sana;-2 Wakorintho 4:16-17
-Kuna furaha ya milele kama ukidumu katika utakatifu autakao MUNGU hivyo vumilia yote ya dunia.

= Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila MUNGU ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili. -1 Wakorintho10:13
-MUNGU ni mwaminifu na hatakuacha ujaribiwe kuzidi uwezo wako.

=Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika MUNGU hata kuangusha ngome;)-2 Wakorintho 10:3, 4
-kwa kuwa unaye YESU KRISTO hakika unayo mamlaka ya kimbingu hivyo kwa maombi yako ya kila siku ngome zote za adui zitapomoja, kuangamia, kuharibika na kuteketea.

=Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa KRISTO ukae juu yangu. Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya KRISTO. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu. 2 Wakorintho 12:9-10
-Vumilia ndugu.

=Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya KRISTO YESU; -Wafilipi 1:6.
-MUNGU atakutumia katika vipawa na karama alizokupa kama tu ukibaki katika kusudi lake la wokovu.

=Piga vita vile vizuri vya imani; shika uzima ule wa milele ulioitiwa, ukaungama maungamo mazuri mbele ya mashahidi wengi. -1 Timotheo 6:12
-Shika ungamo lako la kumkiri YESU na kuamua kuishi maisha matakatifu. Uliongozwa sala ya toba na kuapa kabisa kwa hiari yako kwamba utamfuata YESU milele hivyo usigeuke kwa namna yeyote.

= Ushiriki taabu pamoja nami, kama askari mwema wa KRISTO YESU. -2 Timotheo 2:3
-Wewe ni askari mwema wa KRISTO kwa ajili ya kuwaeleza wanadamu ukweli hivyo vumilia wakija na dhihaka zao lakini ukweli usiache kuwaambia siku zote.

= Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali; mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi. -Yakobo 1:2-3
-Furaha hata wakati wa majaribu lakini usiache kuomba sana maana utukufu ujao ni mkuu kuliko uliopita.

= Basi mtiini MUNGU. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.- Yakobo 4:7
-Kanuni bora ya kuishi ni hii yaani kumtii MUNGU na wakati unamtii MUNGU hakikisha unampinga shetani na kila lililo lake.

=Mnafurahi sana wakati huo, ijapokuwa sasa kwa kitambo kidogo, ikiwa ni lazima, mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna mbalimbali; ili kwamba kujaribiwa kwa imani yenu, ambayo ina thamani kuu kuliko dhahabu ipoteayo, ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto, kuonekane kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima, katika kufunuliwa kwake YESU KRISTO.- 1 Petro 1:6-7
-Iko furaha kuu kwa washindi hivyo endelea kuvumilia.

= Wapenzi, msione kuwa ni ajabu ule msiba ulio kati yenu, unaowapata kama moto ili kuwajaribu, kana kwamba ni kitu kigeni kiwapatacho. Lakini kama mnavyoyashiriki mateso ya KRISTO, furahini; ili na katika ufunuo wa utukufu wake mfurahi kwa shangwe.- 1 Petro 4:12-13
-Waza uzima wa milele ndipo utapata nguvu na kushinda.

= Akatia wimbo mpya kinywani mwangu, Ndio sifa zake MUNGU wetu. Wengi wataona na kuogopa, Nao watamtumaini BWANA -Zaburi 40:3
-Wana heri wanaomtumaini BWANA maana hakuna kama yeye.

=Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama. -Ezekieli 36:26
-Kiburi hakifai lakini kama ukiendelea kunyenyekea ukiwa ndani ya Wokovu wa BWANA YESU huku ukishika utakatifu hakika MUNGU atakutengeneza  hata usipate hasara ya milele ambayo ni jehanamu, bali utapata faida ya milele ambayo ni uzima wa milele.

=Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama KRISTO alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa BABA, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima. -Warumi 6:4
-Ndugu, enenda katika upya wa KRISTO ulioupokea.

= Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya KRISTO amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya. -2 Wakorintho 5:17

-Lazima uwe kiumbe kipya maana uko ndani ya KRISTO. Kiumbe kipya hakiwezi kuwa mlevi, mzinzi, muongo, mchawi na kila aina ya dhambi. kiumbe kipya kinashika utakatifu, utii kwa MUNGU na kutoa ushuhuda mwema .

= Na mfanywe wapya katika roho ya nia zenu; mkavae utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya Mungu katika haki na utakatifu wa kweli. -Waefeso 4:23-24

-ROHO MTAKATIFU ndiye msimamizi wa Wokovu hivyo, kwa sababu umeokoka hakikisha unamruhusu ROHO wa MUNGU kutawala maisha yako yote.

= Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele; nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa MUNGU katika KRISTO YESU.-Wafilipi 3:13- 14

-Sahau yaliyopita, kaza mwendo, ongeza maombi na baki siku zote katika BWANA YESU aliye na uzima wako wa milele.
MUNGU akubariki sana.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.

Mabula1986@gmail.com.

Comments