ZIEPUKE HADAA ZA MCHUMBA.

Mr & Mrs Peter Mabula siku ya uchumba wao kutangazwa Kanisani Kawe Pentecostal Church.
BWANA YESU atukuzwe sana ndugu.
Karibu tujifunze.
Leo nazungumzia hadaa za wachumba.

Mithali 14:12 ''  Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, Lakini mwisho wake ni njia za mauti. ''

-Iko njia ionekananyo njema machoni mwa mtu lakini ni njia mbaya, ni njia ya mateso, ni njia inayoelekea kwenye ubaya na sio uzuri.
- Kuna njia unaweza kupita lakini mwisho wake ukaachwa njia panda tu. njia panda huzaliwa na njia.
-Uchumba ni njia fupi ya kuelekea kwenye njia ndefu iitwayo Ndoa.
-Kuenenda kimwili katika njia unayoiendea ya uchumba inaweza kukuletea njia panda iitwayo ndoa maana kila kitu kitakuwa kinyume na ulivyokusudia mwenyewe,  maana ulikuwa tu mwenye hekima machoni pako mwenyewe huku adui naye akikupangia mabaya, na kwa sababu hukumhusisha MUNGU lazima tu utanasa na njia hiyo haitakuwa nzuri kwako ila balaa.
Ngoja nikuambie ukweli ndugu yangu.
Ndugu Yangu, Huyo Anayetaka Kuokoka Ili Akuoe Au Umuoe Anakudanganya. Mtu Anatakiwa Aokoke Ili Kwenda Mbinguni Na Sio Anaokoka Ili Akuoe Au Umuoe. 
Dada Mmoja Mwokovu Aliniomba Ushauri Kwamba Kuna Kijana Hajaokoka Ila Anampenda Na Yuko Tayari Kubadili Dini Na Kumuoa, Yule Dada Nilimwambia Tumuombe MUNGU Maana Kipindi Ananiambia Niliona Vita Kubwa Rohoni Mwangu, Akakata Simu Na Mimi Nikaendelea Na Maombi. Ajabu Miezi 5 Baadae Akanipigia Simu Huku Analia Kwa Uchungu Mkubwa Akisema "Heri Ningekusikiliza Mtumishi", Nikamuuliza Kwa Nini? Akasema, Baada Tu Ya Kuongea Na Mimi Kipindi kile kwa simu, Walianza Mipango Ya Kutoa Mahali Na Hata Mwezi Haukuisha Wakafunga Ndoa, Yaani Yule Kaka Alikuwa Ameokoka Kwa Wiki 4 Tu Wakafunga Ndoa, Baada Ya Kufunga Ndoa Haikupita Hata Miezi 3 Timbwili Likaanza, Yule Kaka Akarudi Kwenye Dini Yake Ya Awali, Akarudia Pombe Na Bangi, Ndoa Ikageuka Ndoana. Niliumia Sana Maana Mimi Nilikuwa Bado Namuombea Kumbe Aliniomba Ushauri Huku Ameshaamua Tayari. Amenipa Kazi Mpya Ya Kuiombea Ndoa Hiyo.
Huu ni mfano wa njia ambayo machoni pa mhusika ni njema lakini mwisho ni kuingia kwenye majuto maana MUNGU wa mbinguni hawakumhusisha.
Wengi leo wanadanganywa na wachumba zao feki kwamba watabadili dini ili waoane nao.
Ndugu zangu, jambo la kujua ni kwamba hakuna hata mtu mmoja ambaye huokoka ili apate mke au mme bali anayeokoka kwa kuamua huokoka ili aupate uzima wa milele. Mchumba utamkuta huko huko kwenye wokovu na utamthibitisha wewe mwenyewe  kwamba ndie.
Kuna wengine huingia kwenye uhusiano na wapagani au watu wa dini tofauti na kujipa moyo kwamba watawabadilisha tu na wao wampokee YESU kama wao. ndugu huwezi kumuokoa mtu wewe ila neema ya MUNGU ndio inayookoa.
1 Kor 7:16 '' Kwa maana wajuaje, wewe mwanamke, kama utamwokoa mumeo? Au wajuaje, wewe mwanamume, kama utamwokoa mkeo? '' 
-Ndugu yangu kama unamkubali mtu asiye na YESU ndani yake huku ukitarajia wewe utambadilisha tambua kwamba hapo unacheza pata potea.
-Upendo una nguvu kuliko mauti ndivyo inavyosema (Wimbo 8:6), lakini pia kuna upendo usio sahihi nao pia una nguvu kuliko mauti, na nguvu ya upendo usio sahihi umewaacha wengi wakiteseka sana.
-Kigezo cha mchumba sahihi ni yule Mkristo mcha MUNGU aliye na hofu ya MUNGU ndani yake, Zaidi ya hapo ni hatari tupu.
-Vijana wengi wakishaingia katika mahusiano  huwa hawashauliki na hata mtu akiwashauri basi watamuona anatamani tu kuwa kama wao maana ya kwake watasema yamemshinda.
Kama ni mchungaji anamshauri binti aachane na kijana mlevi, mzinzi tena mpagani. Binti atashauriana na kijana yule na hata kumsema vibaya mchungaji kwamba yawezekana mchungaji ana malengo mabaya na binti kumbe laa.

Mithali 12:15 ''Njia ya mpumbavu imenyoka machoni pake mwenyewe; Bali yeye aliye na hekima husikiliza shauri.''
-Kwa mjibu wa kamusi ya kiswahili sanifu Neno Mpumbavu maana yake ni Mtu anayeshindwa kuelewa jambo hata akielezwa.
Wapo wapumbavu wengi sana maana Upendo feki huwafanya  wawe wapumbavu hata wasiweze kuelewa hata wakielezwa ukweli ambao utawasaidia wao. Upendo unaweza kumfanya mtu kuwa mpumbavu maana njia ya mpumbavu imenyooka machoni pake tu. Nisamehe kwa kutumia Neno Mpumbavu hata hivyo ni neno sahihi kabisa la kiswahili na kuna watu kabisa linawahusu sana hasa baada ya kuingia katika upendo feki ambao huwafanya wawe vipofu wasioona tena kuna wengine wamekuwa viziwi wa mapenzi hata hawawezi kusikiliza watumishi ambao wana nia njema tu.

Mithali 14:1 ''Kila mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake; Bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe.'' 

-Andiko hili haliwalengi tu wanawake ambao wako katika ndoa ambao wanaweza kuiharibu ndoa yako kwa mikono yao wenyewe bali pia wapo wanawake ambao wanaingia katika ndoa wakiwa tayari wameshaiharibu ndoa yao kwa mikono yao wenyewe wakati wa uchumba.

Mithali 14:8 ''Akili za mwenye busara ni kujua njia yake; Lakini upumbavu wa wapumbavu ni udanganyifu.'' 

-Je wewe una busara au unaufuata udanganyifu?
Kuna hadaa nyingi kutoka kwa vijana wawe wa kiume na hata wa kike.
Jiulize kijana kwanini unatenda dhambi ya uongo kwa kumdanganya huyo mchumba wako kwamba utamnunulia gari wakati hata Pesa huna?  unamdanganya utamsomesha wakati moyoni hata wazo hilo huna?
Kwanini unamdanganya wakati ukijua kwamba huyo ndio utatatikiwa uishi nae maisha yako yote?


Ndugu zangu ushauri wangu ni huu: Hakikisha unamtegemea MUNGU na omba sana maana vijana walio wengi wakishapata wachumba hata maombi huacha, kama kijana alikuwa anakesha huacha kukesha na kubaki akikesha tu akiandikiana meseji za uongo kwa simu na huyo mchumba wake.

Zaburi 111:10 '' Kumcha BWANA ndio mwanzo wa hekima, Wote wafanyao hayo wana akili njema, Sifa zake zakaa milele.''

-Ndugu nakuomba usiendelee kumng'ang'ania mchumba asiye mcha BWANA.
-Ndugu hapo juu kwenye ushuhuda kijana wa kiume hakuwa anamcha BWANA  ila aliigiza tu kumcha BWANA ili ampate yule binti aliye mcha MUNGU na matokeo yake baada ya ndoa karudi tena kwenye dhambi zake na hata uaminifu umefutika. na imefika kipindi anamkataza hata mke wake kwenda kanisani. ni hatari sana kuanza kujitenga na BWANA YESU kisa ndoa isiyo mpango wa MUNGU.

-Huwezi kuwa mcha MUNGU harafu MUNGU akakupa mchumba  mpagani. ndugu ukiona umepata mchumba mpagani tambua tu kwamba sio mpango wa MUNGU ila ni mpango wako tu. kama una mawazo ya kumbadilisha ili aokoke bado hiyo inaweza kukugharimu sana maana wengi ni wasanii tu.
Tunza ujana wako na usikubali kukaa sehemu hatalishi. 
Mche MUNGU BABA na omba kwake kwa ajili ya kupata Mwenzi wako wa maisha.
Matapeli wa uchumba na matapeli wa ndoa ni wengi sana. Enenda kwa ROHO wala usizitegemee tamaa za mwili wako.
Ndoa ni furaha na upendo na tamani ndoa yako iwe ya  aina hiyo na muombe MUNGU atakupa.
Kwa wale mlioharibu wakati wa uchumba hakikisha mnamwona Mchungaji wenu ili awaongoze sala ya toba na mtasamehewa. ila kwa wewe unayetaka kujaribu uovu ukitarajia kutubu baadae itakugharimu sana maana ipo gharama vile vile ya kuziba makovu yaliyozaliwa na uovu huo hata kama kusamehewa utasamehewa.
Uchumba sio ndoa hivyo uwe makini maana unaweza kupata mchumba na lengo lake ni kuku-enjoy tu kisha anakuacha kabla hata ya ndoa. Unaweza kumpata binti ambaye ana mtu wake hivyo anakula vya kwako kisha kabla ya ndoa anatokomea zake na kukuacha ukisema ''Nimekusamehe ila sitakusahau''
Usiishi tu kwa sababu unaishi bali ishi kwa sababu YESU KRISTO anaishi ndani yako.
Kumbuka waasherati na wazinzi MUNGU atawakuhumia adhabu kama awasipotubu, na toba hiyo iwe toba ya kweli. 
 '' Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi MUNGU atawahukumia adhabu. Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa. Hata twathubutu kusema, BWANA ndiye anisaidiaye, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini? Wakumbukeni wale waliokuwa wakiwaongoza, waliowaambia neno la MUNGU; tena, kwa kuuchunguza sana mwisho wa mwenendo wao, iigeni imani yao. YESU KRISTO ni yeye yule, jana na leo na hata milele. Msichukuliwe na mafundisho ya namna nyingine nyingine, na ya kigeni; maana ni vizuri moyo ufanywe imara kwa neema, wala si kwa vyakula, ambavyo wao waliokwenda navyo hawakupata faida.-Waebrania 13:4-9 ''

-Ndugu,Naamini umejifunza na utachukua hatua njema ya kumpokea BWANA YESU kama hujaokoka ili awe BWANA na MWOKOZI wako tangu leo na utaanza kuishi maisha matakatifu

KAMA UNATAKA KUTUBU RUDIA MANENO HAYA KISHA TAFUTA KANISA LA KIROHO UKAJIUNGE NA KUANZA KUISHI MAISHA MATAKATIFU.

''BABA katika jina la YESU KRISTO Niko mbele zako mimi mwenye dhambi, lakini leo nimetambua kosa langu na naomba unisamehe dhambi zangu zote, nisamehe dhambi ninazozikumbuka na pia zile ambazo sizikumbuki. futa jina langu katika kitabu cha hukumu na uliandike jina langu katika kitabu cha uzima. Neno lako katika Warumi sura ya 10 Mstari wa 9 na wa 10 Neno lako linasema ''Kwa sababu, ukimkiri YESU kwa kinywa chako ya kuwa ni BWANA, na kuamini moyoni mwako ya kuwa MUNGU alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu '' . BWANA YESU mimi nimekuamini leo na hivyo naamini sasa napokea wokovu wako na hakika nimeokoka. Kuanzia leo Naufunga ukurasa wa dhambi na ninaufungua ukurasa wa matendo mema na matakatifu. BWANA nipe ROHO wako Mtakatifu ili aniwezeshe kushinda dhambi na anasa zote za dunia. Kuanzia leo mimi nimeokoka na ni mtoto wa MUNGU mwenye haki zote. ninafuta laana zote na kila roho ya shetani inayonifuatilia naiharibu kwa jina la YESU KRISTO kama neno la MUNGU linavyosema katika Yeremia sura ya kwanza mstari wa 10. BWANA YESU nakushukuru sana kwa kuniokoa. Yote haya kwa imani nimepokea na niko tayari sasa kwa ROHO MTAKATIFU kunitumia. Katika jina la YESU KRISTO nimeomba na kupokea .
Amen.''
Kama umetubu toba ya kweli hakika wewe kuanzia sasa ni mshindi na ni shujaa. Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine. ulishindwa kumpokea BWANA YESU nafasi yako bado ipo na muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula
+255714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments