NA IWAPO MTU YEYOTE HAKUONEKANA AMEANDIKWA KATIKA KITABU CHA UZIMA, ALITUPWA KATIKA ZIWA LA MOTO.

 

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la uzima.
Ujumbe huu MUNGU ameuweka ndani yangu kwa muda mrefu na kwa wakati huu muda wa kuandika masomo umekuwa mdogo sana kwangu.
Lakini namshukuru MUNGU kwa leo kupata nafasi hii.
Tii neno hili la MUNGU maana linafunua kilichopo mbeleni mwako na mbeleni mwa kila mwanadamu.

 Ufunuo 20:15 ''Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto.''

Huo ndio ujumbe niliopewa nikuletee ili kukuonya na nyakati hizi mbaya unazoishi katika ulimwengu huu.
Huu ni ujumbe unatoa majibu ya wapi kila mwanadamu atakuwa baada ya kifo pamoja na baada ya siku ya mwisho.

Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto.
Inaposemwa ''Yeyote'' anaweza kuwa yeyote bila kujali jinsia yake, dini yake, elimu yake au nyadhifa yake, ilimradi tu hayumo katika kitabu cha uzima cha YESU KRISTO.
-Inaposemwa ''Yeyote'' hii ina maana yeyote haijalishi ni shemasi, mzee wa kanisa, Padri, Mchungaji, Askofu, Mwenyekiti wa wamama, Mwenyekiti wa vijana, Nabii, Mtume au mtu Yeyote maadamu jina lake halitaonekana kwenye kitabu cha uzima, huyo atatupwa katika ziwa la moto.
-Haijalishi ana huduma gani au ana ufahamu kiasi gani lakini kama jina lake halikuonekana katika kitabu cha uzima, huyo atatupwa katika ziwa la moto.
Ziwa la moto ataenda kila mwenye sifa ya kwenda huko na uzima wa milele ataenda kila mwenye sifa ya kwenda huko. Hukumu ya MUNGU ni ndio na hakika,  
  ''Mtu akiwa na sikio na asikie.-13:9"

Ni hatari sana lakini ni heri sana tukaambiwa ili tupone kabla ya kuondoka kwetu duniani na kabla ya siku ya mahesabu.
Siku ya kufa iko mbele ya kila mwanadamu, Kadri unavyoiona siku mpya ndio vilevile unavyoikaribia siku yako ya kuondoka duniani. MUNGU BABA amekupa kuiishi siku ya leo ili utengeneze njia zako na maisha yako na ili kuanzia sasa uanze kuishi maisha matakatifu katika KRISTO YESU, ili ziwa la moto lisikuhusu.

Ndugu zangu, Siku ya BWANA i karibu sana.
Kuna watu hufanya dhambi huku wakisema kwamba mbona siku ya BWANA haifiki?
Lakini hao hao wakifa ndipo wanajua ya kwamba siku ya BWANA imefika kwao maana mtu mwovu akifa hutengwa na watakatifu. Watakatifu wakifa wanaenda mbinguni lakini watenda dhambi wakifa wanaenda kuzimu.
Kila mtu atalipwa sawasawa na matendo yake.
Kama alimpokea YESU na kuanza kuishi maisha matakatifu, huyo atalipwa uzima wa milele.

Obadia 1:15 '' Kwa maana hiyo siku ya BWANA i karibu juu ya mataifa yote; kama ulivyotenda, ndivyo utakavyotendwa; malipo yako yatakurudia juu ya kichwa chako mwenyewe. '' 

-Malipo ya kila mtu yatakuwa juu ya kichwa chake.
-Kama uliishi maisha matakatifu ya Wokovu wa BWANA YESU hakika jina lako litakuwa kwenye kitabu cha uzima.
-Kama ulikuwa unaishi maisha ya kuigiza, itajulikana siku hiyo.
-Kama uligeuza kanisa kama kichaka chako cha kufichia maovu yako , siku hiyo itajulikana.
-Kama unamtegemea nabii wako basi siku hiyo hata yeye huyo nabii wako atakuwa anahukumiwa sawasawa na matendo yake.
-Kama ulimtegemea mtume wako, siku hiyo na yeye atakuwa analipwa sawasawa na matendo yake. Ni BWANA YESU tu ndio atakuwa kimbilio la wote ambao wanastahili uzima wa milele. na kimbilio hilo linatafutwa  sasa na sio siku hiyo.
-Kama ulikuwa  unampenda YESU kwa mdomo tu huku moyo wako wote umemkabidhi shetani, siku hiyo itajulikana.
Hapo juu andiko linasema  ''malipo yako yatakurudia juu ya kichwa chako mwenyewe.''

Ndugu yangu, tunaishi katika kipindi cha Mwisho kabisa. Kibiblia wakati huu unaitwa wakati wa NEEMA au Wakati wa KANISA.
Wakati huu ni wakati wa neema kiasi kwamba mtu mwenyewe anaamua aishi maisha gani, lakini kumbuka kwamba  ''malipo yako yatakurudia juu ya kichwa chako mwenyewe.''
Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto.

Muda wa kuyasalimisha maisha yako ni sasa, ni leo wala sio kesho.
Kesho ina mambo yake ambayo yanaweza kuwa uzima wa milele au  ziwa la moto kutegemea na leo yako umeamuaje.
MUNGU kwa upendo wake mkuu anaionyesha njia pekee ya uzima wa milele ambayo kila mwanadamu atakayetii hakika jina lake litakuwa kwenye kitabu cha uzima.
Yohana 3:16-21 ''  Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU. Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu.''Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa. Bali yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru, ili matendo yake yaonekane wazi ya kuwa yametendwa katika MUNGU.'' 

-Ndugu uamuzi ni wako leo, maana hakuna njia nyingine yeyote inayoweza kukufanya jina lako liandikwe kwenye kitabu cha uzima, na kumbuka kwamba Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto.
-Njia ya uzima wa Milele ilitoka mbinguni(Yohana 3:31) ili mimi na wewe tupite ndani ya njia hiyo kwenda uzima wa milele, na njia hiyo  moja tu(Yohana 14:6)
Njia pekee ya kwenda uzima wa milele ni BWANA YESU KRISTO(Matendo 4:12) Hata kitabu cha uzima kinaitwa kitabu chake.
Waabudu shetani na watenda dhambi hawamo katika kitabu cha uzima. Ufunuo 13 inaeleza ujanja wa shetani wa kutaka aabudiwe yeye, shetani ndio anayewafanya watu majina yao yasiwe katika kitabu cha uzima cha Mwanakondoo YESU KRISTO.

Ufunuo 13:7-9 ''Tena(Wakala wa shetani) akapewa kufanya vita na watakatifu na kuwashinda, akapewa uwezo juu ya kila kabila na jamaa na lugha na taifa. Na watu wote wakaao juu ya nchi watamsujudu, kila ambaye jina lake halikuandikwa katika KITABU CHA UZIMA CHA MWANA-KONDOO, aliyechinjwa tangu kuwekwa misingi ya dunia. Mtu akiwa na sikio na asikie.''

-Mwana-kondoo ni YESU KRISTO na waabudu shetani hawamo katika kitabu cha uzima, watenda dhambi hawamo katika kitabu cha uzima, wanaomkataa BWANA YESU hawamo katika kitabu cha uzima.
Ndugu sikia leo injili hii ili uyasalimishe maisha yako kwa YESU. Leo unabembelezwa kuokoka lakini siku hiyo utajua kwamba Kuokoka duniani ni jambo la lazima kwa kila anayetaka kwenda uzima wa milele.
Ndugu yangu, Siku ya mwisho i karibu sana, Mtume Yohana aliiona  kwa njia ya maono alipokuwa anaonyeshwa na Malaika wa BWANA, Mtume Yohana anasema   ''  Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao. 
 Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake; na Mauti na Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Wakahukumiwa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake. Mauti na Kuzimu zikatupwa katika lile ziwa la moto. Hii ndiyo mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto. Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto. -Ufunuo 20:12-15'' 
-Mimi nimemaliza na kazi imebaki kwako, kumpokea YESU na kuanza kuishi maisha matakatifu au kuendelea na mambo yako lakini kumbuka kwamba
Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto.

-Ndugu,Naamini umejifunza na utachukua hatua njema ya kumpokea BWANA YESU kama hujaokoka ili awe BWANA na MWOKOZI wako tangu leo na utaanza kuishi maisha matakatifu.

KAMA UNATAKA KUTUBU RUDIA MANENO HAYA  KWA KUAMUA KUTOKA MOYONI KISHA TAFUTA KANISA LA KIROHO UKAJIUNGE NA KUANZA KUISHI MAISHA MATAKATIFU.

''BABA katika jina la YESU KRISTO Niko mbele zako mimi mwenye dhambi, lakini leo nimetambua kosa langu na naomba unisamehe dhambi zangu zote, nisamehe dhambi ninazozikumbuka na pia zile ambazo sizikumbuki. futa jina langu katika kitabu cha hukumu na uliandike jina langu katika kitabu cha uzima. Neno lako katika Warumi sura ya 10 Mstari wa 9 na wa 10 Neno lako linasema ''Kwa sababu, ukimkiri YESU kwa kinywa chako ya kuwa ni BWANA, na kuamini moyoni mwako ya kuwa MUNGU alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu '' . BWANA YESU mimi nimekuamini leo na hivyo naamini sasa napokea wokovu wako na hakika nimeokoka. Kuanzia leo Naufunga ukurasa wa dhambi na ninaufungua ukurasa wa matendo mema na matakatifu. BWANA nipe ROHO wako Mtakatifu ili aniwezeshe kushinda dhambi na anasa zote za dunia. Kuanzia leo mimi nimeokoka na ni mtoto wa MUNGU mwenye haki zote. ninafuta laana zote na kila roho ya shetani inayonifuatilia naiharibu kwa jina la YESU KRISTO kama neno la MUNGU linavyosema katika Yeremia sura ya kwanza mstari wa 10. BWANA YESU nakushukuru sana kwa kuniokoa. Yote haya kwa imani nimepokea na niko tayari sasa kwa ROHO MTAKATIFU kunitumia. Katika jina la YESU KRISTO nimeomba na kupokea . Amen.''

Kama umetubu toba ya kweli hakika wewe kuanzia sasa ni mshindi na ni shujaa. Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine. ulishindwa kumpokea BWANA YESU nafasi yako bado ipo na muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA. MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula
+255714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili

Comments