KWANINI HUWA TUNAFUNDISHWA NENO LA MUNGU?


 BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Nakukaribisha tujifunze Neno la MUNGU.
Hivi kwanini huwa tunafundishwa neno la MUNGU?
 Kufundisha neno ni kumuelekeza mtu ili aelewe kwa usahihi kile anachotakiwa kuelewa kwa usahihi.
'' Maneno ya BWANA ni maneno safi, Ni fedha iliyojaribiwa kalibuni juu ya nchi; Iliyosafishwa mara saba.-Zaburi 12:6 ''
 
Zipo sababu nyingi sana za kwanini ni lazima tujifunze Neno la MUNGU.
Neno la MUNGU ni la muhimu sana kwetu.
MUNGU ametupa Neno lake katika nyakati hizi ili tujue makusudi yake. Biblia ndilo neno hai pekee la MUNGU wa kweli.
Biblia ina uvuvuo wa MUNGU mwenyewe.
Neno la MUNGU li hai.
Neno la MUNGU linatakasa.
Neno linajua zaidi yetu sisi wanadamu.
Neno  lina mamlaka kuu sana.
Neno linachoma.
YESU KRISTO ni NENO juu ya Neno la MUNGU.
Neno la MUNGU linayajua mawazo  yote ya wanadamu.
Neno hai ni la MUNGU tu.
Waebrania 4:12 ''Maana Neno la MUNGU li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.''
-Neno la MUNGU ni mhimu sana.
-Kama tunataka tumpendeze MUNGU basi ni lazima tusilikwepe Neno lake.
-Neno la MUNGU limebeba kusudi la MUNGU na mpango wa MUNGU wa Wokovu.
-Ukilidharau Neno la MUNGU hakika MUNGU atakudharau wewe.
-Neno la MUNGU ndio lililobeba siri ya baraka yako na mafanikio yako.
-ROHO MTAKATIFU ndiye  mwandishi wa Neno la MUNGU kupitia wanadamu maalumu aliowateua.
Hivyo kama kuna sehemu hatulielewi vizuri Neno la MUNGU basi ni lazima tumuulize aliyeandika Neno yaani ROHO MTAKATIFU ndipo tutajua Neno.
2 Petro 1:20-21 ''Mkijua neno hili kwanza, ya kwamba hakuna unabii katika maandiko upatao kufasiriwa kama apendavyo mtu fulani tu. Maana unabii haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa MUNGU, wakiongozwa na ROHO MTAKATIFU. ''

Kuna dada mmoja alikuwa anasumbuliwa na mapepo, kila akianza kusoma Biblia hata kabla hajamaliza mistari 5 anasinzia pale pale hadi watu watakapomwamsha. Nguvu za giza ndani yake zilikuwa zinashindwa kuhimili neno likisomwa hivyo walikuwa wanamuondoa katika neno kwa kumletea usingizi. Dada yule aliniambia kwamba alikuwa na uwezo wa kusoma gazeti hata masaa 7 bila kuchoka wala kusinzia, lakini akianza tu kusoma Biblia Takatifu anasinzia. Dada yule alinisimulia na kuonyesha jinsi anavyochukizwa na hali ile, nilimuombea kwa simu na kumwambia akaokoke na alipofanya hivyo hali ile iliondoka na sasa ni mtumishi mzuri. Kama kuna kitu shetani hataki watu wakijue basi ni neno la MUNGU. Kujua Neno la MUNGU ni kujua haki zako.

1 Petro 2:3 ''Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu;''
-Maziwa ya akili yasiyoghoshiwa ni Neno la MUNGU.
-Ili tukue kiroho na  ili tuukulie Wokovu basi hakika ni lazima tuyanywe mazima ya akili yasiyoghoshiwa ambayo ni neno la MUNGU.
 Luka 11:28 ''  Afadhali, heri walisikiao neno la MUNGU na kulishika.''
Biblia ndio neno sahihi ambalo linatakiwa kufuatwa na kila mtu.
Kuna watu wana maneno lakini hawana Neno la MUNGU.
Kuna watu wamekariri maandiko lakini hawana Neno la MUNGU ndani yao.
Yohana  5:38 ''Wala neno lake hamnalo likikaa ndani yenu, kwa kuwa ninyi hammwamini yule aliyetumwa na yeye.''
Unakuta mtu amekariri maandiko 20 na kila siku anayatumia katika maombi lakini kitendo cha kusikia paka analia kwenye paa ya nyumba yake tayari ndugu yule anahama mtaa. Huyo alikuwa na maandiko lakini Neno la MUNGU hana.
Unakuta mtu anaumwa malaria tu lakini wakati wa kuumwa kwake anasema sijui kama nitapona na kuomba anaomba kila siku. Huyo ana maandiko ila hana Neno la MUNGU.
Neno la MUNGU li hai na halijawahi kufa hata siku moja.
BWANA anasema 
''Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe.-Mathayo 24:35''

 Sababu 7 za kwanini huwa tunafundishwa neno la MUNGU.

    1.  Ili tuwe na nguvu za kiroho.

-Mtoto mmoja aliniuliza swali hili '' kwanini huwa tunakula chakula''
Nikamjibu, Tunakula Chakula ili tuishi.   Ni kweli kabisa tunakula Chakula ili tuishi. Na Kiroho pia Neno la MUNGU ndio chakula cha roho zetu hivyo kazi ya chakula hiki ni kutufanya tukue na pia kutufanya tusife kiroho.
 Yohana 6:27 ''Msikitendee kazi chakula chenye kuharibika, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele; ambacho Mwana wa Adamu atawapa, kwa sababu huyo ndiye aliyetiwa muhuri na Baba, yaani, MUNGU.''

    2.  Ili tujue ni nini jema litupasalo kutenda.


Kila jema ambalo tunatakiwa wanadamu kulitenda au kulifuata linatakiwa liwe lile ambalo linampendeza MUNGU wa mbinguni. Neno la MUNGU likituongoza hakika hatutamkosea MUNGU. Neno linatakiwa liwe ndio tochi yetu ya kutumulikia mbele yetu ili tuone na tujue jambo jema la kutenda.
Zaburi 119:165  '' Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu. ''

  3.  Ili tujue tunaishi katika nyakati gani.

Biblia inazungumzia kila nyakati za kuishi wanadamu hadi siku ya mwisho na tena Biblia iko wazi kabisa juu ya  mbingu mpya itakavyokuwa.
Katika kitabu cha Ufunuo Sura ya 2 na sura ya 3 kuna maandiko kuhusu makanisa saba ya kiunabii. Makanisa hayo yanawakilisha nyakati ambazo zilizopita na zilizopo.
Pia Neno la MUNGU ndilo linalosema siku za mwisho zitakuaje na tukiisoma Biblia tunajua kabisa tuko katika nyakati gani sasa.  
1 Timotheo 4:1-3 ''Basi ROHO anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani; kwa unafiki wa watu wasemao uongo, wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe; wakiwazuia watu wasioe, na kuwaamuru wajiepushe na vyakula, ambavyo MUNGU aliviumba vipokewe kwa shukrani na walio na imani wenye kuijua hiyo kweli.   ''

   4.  Ili tujue MUNGU husema na sisi kwa njia gani.


MUNGU husema na sisi kwa njia ya Neno lake.
Ona mfano huu.
Yeremia 18:2-6 '' Ondoka, ukashuke mpaka nyumba ya mfinyanzi, na huko nitakusikizisha maneno yangu. Basi nikashuka mpaka nyumba ya mfinyanzi, na tazama, alikuwa akifanya kazi yake kwa magurudumu. Na chombo kile, alichokuwa akikifinyanga, kilipoharibika mkononi mwake yule mfinyanzi, alikifanyiza tena kuwa chombo kingine, kama alivyoona vema yule mfinyanzi kukifanya.  Ndipo neno la BWANA likanijia, kusema,  Ee nyumba ya Israeli, je! Siwezi mimi kuwatendea ninyi vile vile kama mfinyanzi huyu alivyotenda? Asema BWANA. Angalieni, kama udongo ulivyo katika mkono wa mfinyanzi, ndivyo mlivyo ninyi katika mkono wangu, Ee nyumba ya Israeli.'' 
-Hapo tunajifunza kwamba MUNGU husema na wanadamu kwa njia ya Neno lake hivyo kama Neno lake tutalikataa hakika hata Neno lake la ufunuo halitakuja kwetu.
Neno la MUNGU ndio hutufundisha njia ambazo MUNGU anazitumia kusema na sisi. Kama hatutajifunza Neno lake ni vigumu sana Kujua kama MUNGU amesema na sisi.
Neno hutuonyesha kwamba  MUNGU husema na sisi kwa njia nyingi mojawapo;
MUNGU husema na sisi kwa Neno lake.
MUNGU husema na sisi kwa ndoto na maono.
MUNGU husema na sisi kwa Mazingira.
MUNGU husema na sisi kupitia watu wengine.


   5.  Ili tujue haki zetu.


Yohana 8:31-32 '' Basi YESU akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru.''
-Neno hutufanya kuijua kweli.
-Neno hutufanya kujua haki zetu na wajibu wetu. 

   6.  Ili tumjue MUNGU na kusudi kake kwetu.


Yohana1:1-4, 12-14 ''Hapo mwanzo kulikuwako NENO, naye NENO alikuwako kwa MUNGU, naye NENO alikuwa MUNGU. Huyo mwanzo alikuwako kwa MUNGU. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika. Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu. Bali wote waliompokea(NENO) aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake;
 waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa MUNGU. Naye NENO alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa BABA; amejaa neema na kweli.   ''


   7.  Ili tujue tutakuwa wapi baada ya kufa kwetu kutokana na matendo yetu ya sasa.


Mathayo 13:49-50 ''Ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia; malaika watatokea, watawatenga waovu mbali na wenye haki, na kuwatupa katika tanuru ya moto; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.'' 
-Neno ndilo linalosema hatima ya kila mmoja.
Kama umemkataa YESU na hutaki kuishi maisha matakatifu kumbe kuna tanuru la moto, ndio maana injili kama hii inahubiriwa ili watu waokoke na waende uzima wa milele.

Zaburi 119:11 ''Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi.''
-Ukiliweka Neno la MUNGU moyoni mwako na ukalitii hakika hutatenda dhambi. 
Ndugu yangu, Kujiachilia ili upokee mafundisho huleta uponyaji.
Hakuna sababu ya mwanadamu yeyote kulikataa Neno la MUNGU.
-Neno la MUNGU humjenga mtu.
-Neno la MUNGU humwimalisha mtu.
-Neno la MUNGU hutengeneza mabadiliko ndani ya mtu kama mtu huyo ataliruhusu.
-Neno la MUNGU huleta nuru ndani yetu.
Neno hutakasa.

1 Petro 1:25 ''Bali Neno la BWANA hudumu hata milele. Na neno hilo ni neno lile jema lililohubiriwa kwenu.''

Ndugu yangu, naamini kuna kitu umejifunza hivyo nakuomba chukua hatua ya kwenda kanisani na kumpokea YESU KRISTO kama BWANA na MWOKOZI wa maisha yako na baada ya hapo hudhuria fundisho kanisani ili uimarike na upate nguvu za kuwasaidia na wengine.
MUNGU akubariki sana.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
mabula1986@gmail.com.
0714252292.

Comments