MAOMBI YA KUFUTA KILA ALAMA YA KISHETANI.

Na Mtumishi Peter Mabula.

BWANA YESU asifiwe.
Leo nataka tuombe maombi ya kufuta kila alama ya kishetani.
shetani anaweza kukuwekea alama ili akuonee zaidi, hata kama ungekuwa mbali naye lakini akiiona tu alama yake anaanza kukutesa. Leo nataka tufute kila alama za kipepo miilini mwetu na maishani mwetu.
ona mfano huu Ayubu 13:17 ''Waitia miguu yangu katika mkatale, na kuyaaua mapito yangu yote; Wajiandikia alama kuzizunguka nyayo za miguu yangu; '' 
Si kila alama ni alama nzuri.
Kuna watu wana alama za kipepo katika miili yao.
Ngoja nikupe shuhuda 2 fupi.
Kuna Dada mmoja yeye alikuwa na utisho wa kipepo, kwenye kundi lao hakuwa kiongozi lakini hata kama wanafuraha kiasi gani akitokeo tu huyo dada kila mtu kimya, akiongea kitu hakuna wa kupinga hata kama ni kibaya. Watu walikuwa wanatoa maoni lakini akitokea tu huyo dada kila mtu kimya utadhani huyo dada ni mkali kumbe ana alama ya kipepo inayompa utisho wa kipepo.
Dada huyu aliichukia hali hiyo maana alijaribu kucheka na kila mtu lakini haikuwezekana, aliumia na alikuwa anaomba sana lakini wala hali hiyo haikuisha, alidhani ndivyo alivyoumbwa kumbe ana alama za kipepo hadi alipofunguliwa.
Kuna watu wengi tu wana alama za kipepo kiasi kwamba kuna vitu haviendi huku wao wakidhani ni gundu kumbe alama za kipepo katika miili yao.
Kuna mabintiambao  wakaka wanawaogopa kuliko Simba au chui na hakuna mwenye mpango wa kuwachumbia na hata wao hawajui tatizo ni nini, kumbe ni alama za kipepo ambazo ziko kwa siri sana hata wao hawajui. unakuta binti mrembo tena hana upungufu hata mmoja lakini kuchumbiwa hakuna kumbe adui amepanda alama yake hata uzuri wa yule binti hauonekani ila kinachoonekana ni kitu kingine kumbe ni alama za kipepo.
Ushuhuda wa pili ni huu; kuna binti mmoja yeye alikuwa na alama ya kipepo ya kutamaniwa na wanaume.
Binti yule akipita njiani kila mwanaume atamwita na kumwambia hadharani hata mbele za watu kwamba anamtaka na yuko tayari kwa lolote. sio kwamba binti yule ni mzuri sana kuliko wengine lakini kumbe ni alama ya kipepo iliyokuwa usoni kwake, kila siku alikuwa anasumbuliwa sana, havai nguo za kikahaba hata siku moja lakini kutongozwa ilikuwa kero kwake na kila anayemtongoza anachotaka ni ngono tu na sehemu kubwa ya waliokuwa wanamtongoza ni waume za watu tu. binti yule aliteseka sana na akagundua kabisa kwamba inawezekana ana jini na kweli kumbe ilikuwa ni alama ya kipepo, binti yule licha ya kusumbuliwa na wanaume kupita kawaida lakini hakukuwa na muoaji hata moja na alikwenda sana umri hadi alipogundua kwamba ana alama ya kipepo usoni mwake ambaye alama hiyo kila mwanaume akimwangalia usoni tu anataka kuzini nae, yaani ni kama alikuwa na kwanga usoni mwake yake akikutanisha macho tu na mwanaume yeyote ni kosa maana huyo mwanaume atamfatilia kupita kawaida, alama hiyo ilisababisha binti huyo kubaka zaidi ya mara 3 na wanaume watatu tofauti, niliumia sana aliponisimulia. binti huyo wala hakuwa malaya na hakuwahi kumkubali mwanaume hata mmoja lakini kila mwanaume ambaye hajaokoka sawasawa alikuwa lazima amtongoze. ilipotoka hiyo alama ya kipepo binti akashangaa na kujua kwamba haikuwa kawaida yeye kusumbuliwa na wanaume na kwa sasa ana mume na maisha mazuri ya ndoa yanaendelea.
Ndugu zangu alama za kipepo zipo na kuna watu wana alama za kipepo kwenye miiili yao na wengine katika koo zao na wengine wanaishi kwenye eneo lenye alama za kipepo. ndugu yangu nimekufundisha haya ili uombe kuharibu alama za kipepo zote. Najua baada ya ujumbe huu kuna maelfu ya watu watanipigia simu au kuniandikia meseji lakini ndugu yangu msaada wala mimi sina ila msaada ni kwa BWANA YESU tu, kama hujaokoka okoka leo, kama umerudi nyuma okoka upya na kama umeokoka lakini hujawahi kufunguliwa kwenye eneo hilo basi omba ndugu yangu na hata funga ili kufuta alama zote za kipepo zinazokusumua. Waone wachungaji katika eneo lako na waeleze watakuombea na utakuwa huru.
Yeremia 31:21 ''Jiwekee alama za njia; jifanyie miti ya kukuongoza; uuelekeze moyo wako kwenye njia kuu, njia ile ile uliyoiendea; rudi tena, Ee bikira wa Israeli, irudie hii miji yako.''
Andiko hilo linatufundisha kwamba alama zipo haijalishi ni alama gani lakini pia hata alama za kipepo zipo na hizo ni lazima tuzifute kwa jina la YESU KRISTO.
Kuna watu watakuwa na alama ya shetani yaani 666 ndivyo Biblia inavyosema, na alama hiyo sio kwamba wanadamu wanaiweka bali shetani ndiye atakayewawekea.
Ndugu Yangu, neema ya BWANA YESU bado ingalipo hivyo futa alama zote za kishetani na kama umejitenga na YESU rudi  leo baada tu ya kusoma ujumbe huu.

MAOMBI YA  KUFUTA ALAMA ZOTE ZA KIPEPO.

JEHOVAH-MACCADDESHEM yaani MUNGU wa kutakasa niko mbele zako BWANA katika jina la YESU KRISTO, ninatubu dhambi zangu zote na naomba BWANA nipate neema mbele zako. mimi ni mwanadamu mwenye mapungufu mengi hivyo kwa akili zangu siwezi lolote BWANA na naomba unihurumie Mfalme wa mbinguni.. Neno lako linasema katika Isaya 55 mstari wa 6 hadi wa 7 kwamba  '' Mtafuteni BWANA, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu; Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie BWANA, Naye atamrehemu; Na arejee kwa MUNGU wetu, Naye atamsamehe kabisa.''
BABA wa mbinguni ninarejea leo na naomba unisamehe MUNGU wangu, kwa upya kabisa nampokea YESU KRISTO kama BWANA na Mwokozi wangu maana imeandikwa katika Warumi 10 msitari wa 13 kwamba '' kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la BWANA ataokoka.''
BWANA YESU leo najikabidhi kwako MUNGU wa uzima, nakuomba BWANA ulifute jina langu katika kitabu cha hukumu na uliandike katika kitabu cha uzima, kuanzia leo mimi ni wako BWANA YESU.
BWANA naomba kwa jina lako takatifu kila mashtaka kunihusu mimi kwenye ulimwengu wa roho yafutike kwa jina lako BWANA YESU. Kwa jina la YESU KRISTO kila alama ya kipepo iliyonisababishia mateso ifutike sasa kwa damu ya YESU na kwa jina la YESU KRISTO.
Imeandikwa katika Ufunuo 12 mstari wa 11 kwamba tunamshinda shetani kwa damu ya YESU KRISTO na neno la ushuhuda wetu. kuanzia sasa nafuta alama zote za kipepo kwa Damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO. Tena namshinda shetani kwa neno la ushuhuda na neno langu la leo la ushuhuda ni hili ''  kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa MUNGU . ''  Kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Luka sura ya kwanza na msitari wa 37 hivyo leo BWANA MUNGU wangu anabatirisha kila kazi ya alama ya kishetani iliyokuwa imenikamata, tena BWANA YESU anaifuta kila alama ya kipepo maana hakuna jambo lisilowezekana kwa MUNGU hivyo hata hili la alama zote za kipepo kufutika linawezekana dakika hii kwa jina la YESU KRISTO.
Kila alama ya kipepo naifuta na itoke katika mwili wangu, maisha yangu , ukoo wangu na katika aridhi yangu, ninafuta kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Kila alama ya kipepo iwe ililetwa na majini, wachawi, waganga, ndugu au majirani naifuta kwa damu ya YESU na kwa jina la YESU KRISTO.
Neno hai la MUNGU linasema  katika Mithali 18 mstari wa 10 kwamba ''Jina la BWANA ni ngome imara; Mwenye haki huikimbilia, akawa salama. '' Kuanzia leo nitakuwa salama kwa jina la YESU KRISTO maana jina la YESU KRISTO ni ngome imara na mimi nimeshatubu hivyo ni mwenye haki na ndio maana nimekimbilia jina la YESU ili nikae salama.
Asante BABA wa mbinguni maana umeshishindia.
Asante BWANA YESU maana umenihamisha kutoka kuteswa na alama za kipepo na sasa niko huru maana wewe BWANA YESU umeniweka huru kama neno lako linavyosema katika Yohana 8 mstari wa 36.
Nitakutukuza milele BWANA YESU na nakuomba BWANA unishike mkono siku zote ili nibaki pendoni mwako.
Asante ROHO MTAKATIFU kwa kuufunua ushindi wangu leo.
Ni katika jina la YESU KRISTO aliye hai nimeomba na kupokea Amen AMen.
MUNGU akubariki sana na ni hakika umeshinda kwa jina la YESU KRISTO.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mbula.
Mabula1986@gmail.com.
0714252292.

Comments