KIWANGO CHAKO CHA IMANI NDICHO KIWANGO CHAKO CHA KUPOKEA KUTOKA KWA MUNGU

Na Mtumishi Peter Mabula.
BWANA YESU atukuzwe mpendwa wangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Kama ulikuwa hulijui hili naomba ulijue leo kwamba  ''KIWANGO CHAKO CHA IMANI NDICHO KIWANGO CHAKO CHA KUPOKEA KUTOKA KWA MUNGU''

Waebrania 11:6 ''Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye MUNGU lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.''

Kama imani haipo kwako muombaji basi kupokea hakupo pia maana pasipo imani haiwezekani kumpendeza MUNGU.
MUNGU ni wa kuaminika hivyo  lazima tumwamini kama tunataka kupokea kutoka kwake.
Kuomba tu hakutoshi kama unaomba bila imani ya kupokea.
Kuna imani  lakini pia kuna imani ya kupokea.
Kama una imani ya kuomba basi ongeza pia imani ya kupokea ili upokee.

Waebrania 11:1 '' Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana.''

Imani ni uhakika wa mambo yajayo, na majibu ya maombi ni mambo yajayo hivyo hayo yajayo hutokea tu kama tuliomba kwa imani tena tukawa na imani ya kupokea tulichoomba.
Kiwango chako cha imani ndicho kiwango chako pia cha kupokea.
Mwenye imani ndogo katika maombi hupokea vidogo vile vile na mwenye imani kubwa hupokea vikubwa.
MUNGU hapendi watu wenye mashaka naye.

 Usijitetee, Mwache MUNGU akutetee, Usijipiganie, Mwache MUNGU akushindie lakini ni kupitia maombi katika jina kuu la YESU KRISTO.
Kuna watu wana imani ya kuombea chakula tu lakini hawana imani ya kuombea ndoa zao. mtu wa hivyo ukimwambia ombea chakula hakika ataomba kwa imani sana lakini suala la ndoa atasema ''namwachia MUNGU'' wakati kama angeomba kwa imani amani na furaha vingerejea kwenye ndoa haraka sana.

2 Kor 5:7 ''Maana twaenenda kwa imani, si kwa kuona.'' 

Kazi ya imani ni kuamini hata kama kitu hakijaonekana.
Inawezekana kabisa unaumwa sana lakini kwa maombi kupitia jina la YESU unaomba kwa imani huku ukikiri uzima wa BWANA YESU na hakika unapokea uponyaji, hiyo ndio imani.
Kiwango chako cha imani ndio kiwango chako cha kupokea.
Kama kiwango chako cha imani ni cha kukemea mapepo tu basi hutapokea kuvuka kiwango chako cha imani.
Kuna wengine kiwango chao sio cha kuishia kukemea mapepo bali kiwango chao ni kuombea wagonjwa wa ukimwi na wanapona.
Kiwango chako cha imani kinaishia wapi?
Kiwango chako cha imani katika maombi kinatakiwa kipande na kuzidi sana katika jina la YESU KRISTO ili upate kupokea vikubwa kulingana na imani yako.
Mitume mwanzoni walikuwa na imani ya kukemea mapepo tu.
ona hapa walipotumwa na BWANA YESU kwenda kuhubiri. 

Luka 10:17 '' Ndipo wale sabini waliporudi kwa furaha, wakisema, BWANA, hata pepo wanatutii kwa jina lako. ''

Lakini wakati BWANA YESU anakamatwa kwenda kusurubiwa wanafunzi hawa hawa Imani iliwatoka wa wengine wakamsaliti na kusahau kabisa kama kwa jina lake YESU walitoa pepo Soma Luka 22:54-62 na wengine wakarudi kabisa kuvua samaki na kuacha kukemea tena mapepo.
Ndugu, ongeza imani yako, palilia imani yako ili ikue.
Imani ni muhimu sana maana kwa maombi ya imani unaweza kuharibu kila hila ya shetani.
Biblia inasema neno hili kwako 
''zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.-Waefeso 6:16 ''

Tunatakiwa tuombe kwa imani lakini kama imani yetu itakuwa ndogo hakika vikubwa hatutapokea.
Kama imani yako inalegalega nakuomba ujue njia za kukuza imani yako ambazo ni;
=Kusoma neno la MUNGU na kulitafakari.
=Kuomba maombi ya muda mrefu na kufunga.
=Kuziamini kazi za MUNGU ambazo ziko katika Biblia.
=Kujumuika na wana kanisa wengine katika kazi za MUNGU kanisani. 

kumbuka mkaa usio na moto ukiuchanganya na mikaa yenye moto na wenyewe utashika moto ndio maana ni lazima sana kuhudhuria ibada na kuomba pamoja na wana kanisa wengine ili hata kama uko baridi ukawe moto. lakini kujitenga na kanisa ni kubaya sana, Kujitenga na wokovu wa BWANA YESU ni kubaya sana, kujitenga na ibada ni kubaya sana , kujitenga na Neno la MUNGU ni kubaya sana. Ni kama kaa la moto ambalo lina moto lakini ukilitenga mbali na mikaa mingine yenye moto litazima tu baada ya muda mfupi, ndivyo ilivyo kwa mtu ambaye anaacha ibada, anaacha maombi, anaacha kujifunza neno la MUNGU kanisani.
Imani ni muhimu sana.
 BWANA YESU siku zote anasubiri tu wewe uombe kwa imani ili atende muujiza.
Imani yako ya kuomba inaweza ikawaokoa hata ndugu zako na marafiki zako.
Yakobo 5:15 '' Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na BWANA atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa. ''

Naamini sasa unaona umuhimu wa imani ya kuomba na imani ya kupokea.

Ili kuinuka zaidi kiroho nakuomba uombe haya pia.

Omba MUNGU akupe Roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye na Neno lake na ili Macho ya moyo wako au macho ya rohoni yatiwe nuru. 
Efeso 1:17-18 ''MUNGU wa BWANA wetu YESU KRISTO, BABA wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye; macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo;''

Naamini hadi hapo umeona umuhimu wa kuomba kwa imani.
Omba kwa imani ndugu maana kiwango chako cha imani ndicho kiwango chako pia cha kupokea.
  1Yoh 5:14-15 ''
Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba. ''
 Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com

MUNGU akubariki sana kwa kusoma somo hili. 

Comments