SIRI YAKO NI ULINZI WAKO

Na Frank P. Seth

"Wakati huo Merodaki-baladani, mwana wa Baladani, mfalme wa Babeli, alipeleka barua na zawadi kwa Hezekia; kwa maana amepata habari kwamba amekuwa hawezi, na kwamba amepona. Hezekia akawafurahia, akawaonyesha nyumba yake yenye vitu vyake vya thamani, fedha na dhahabu, na manukato, na marhamu ya thamani, na nyumba yote yenye silaha zake za vita, na vitu vyote vilivyoonekana katika hazina zake; hapakuwa na kitu nyumbani mwake wala katika ufalme wake asichowaonyesha. Ndipo Isaya nabii akamwendea mfalme Hezekia, akamwambia, Watu hawa walisema nini? Nao wametoka wapi kuja kwako? Hezekia akasema, Wametoka katika nchi iliyo mbali, wakaja kwangu toka Babeli. Ndipo akasema, Wameona nini katika nyumba yako? Hezekia akajibu, Wameviona vitu vyote vilivyomo nyumbani mwangu; hapana kitu katika hazina zangu nisichowaonyesha. Ndipo Isaya akamwambia Hezekia, Basi, lisikie neno la BWANA wa majeshi. Tazama, siku zinakuja, ambazo vitu vyote vilivyomo nyumbani mwako, na hivyo vilivyowekwa akiba na baba zako hata leo, vitachukuliwa mpaka Babeli; hapana kitu cho chote kitakachosalia; asema BWANA" (Isaya 39:1-6).
Mojawapo ya mambo muhimu sana ya KIVITA ni kuhakikisha ADUI hajui SIRI ya nguvu zako au uwezo wako. Ukitaka kujua ninamaanisha nini kumbuka anguko la Samson, ni kutoa SIRI ya nguvu zake kwa Delilah (ADUI).
Vita nyingi sana ambazo tumeshindwa, sio kwa sababu nguvu zetu za kupigana zimepungua, ila tumesema maneno ambayo yamefungua mlango wa vita husika na kwa sababu tumeweka MAUNGO yetu wazi kwa ADUI basi tumepigwa kwa urahisi.
Nitakufundisha jambo hili, kukaa kimya juu ya mipango yako, hasa ile ya msingi ya kimaisha ni hekima. Angalia tena, sijasema kuacha kushirikisha watu wa muhimu, ila kusema hovyo kwa kila umkutaye ukidhani utasifiwa kumbe unajiweka mahali pa utelezi na anguko lako linakuja punde.
Jifunze kujua watu wa kubeba mambo yako kama yao kwa maana hakuna apendaye mambo yake NYETI yasemwe hovyo. Sio kila mara utakutana na WATUMISHI waaminifu ambao utawaambia SIRI zako na zikawa salama, uwe makini. Na hata kwa wenye ndoa, sio kila mara mambo ya NDANI kabisa yatakuwa salama, jufunge viuno yako kwa hekima, ufundishe ulimi wako kuwa na akili wakati wa kusema.
Jifunze jambo hili, mtu asemaye SIRI zako kwa wengine, hasa baada ya kukatazwa kusema, huyo ni fungu moja na adui zako. Jichunge naye. Jifunze kutunza SIRI za watu ili uwe mtu wa MUHIMU kwao. La sivyo, utajikuta ukiwekwa fungu moja na adui.
Ni vigumu au haiwezekani kufuta neno ulilosema, ila unaweza kulizuia kwa kutolisema. Angalia, kama unataka jambo fulani liwe binafsi, chagua SANA wa kumshirikisha au kaa KIMYA, utakuwa salama.
Frank P. Seth

Comments