HASARA YA MCHUMBA ASIYE SAHIHI.

Na  Mtumishi Peter Mabula
BWANA YESU atukuzwe ndugu zangu.
Karibu tujifunze.
Leo nazungumzia wanaotarajia kuoa au kuolewa.

Ezra 10:2 ''Hata Shekania, mwana wa Yehieli, mmoja wa wana wa Elamu, akajibu, akamwambia Ezra, SISI TUMEMKOSA MUNGU WETU, NASI TUMEOA WANAWAKE WAGENI WA WATU WA NCHI HIZI; lakini kungaliko tumaini kwa Israeli katika jambo hili.''  

Maneno haya yanatufundisha kwamba wateule wa MUNGU kuoa au kuolewa na waabudu shetani au waabudu miungu ni jambo lenye hasara kubwa kwa wateule hao.
Kuoa au kuolewa na mtu wa jinsi hiyo ni kujitenga na MUNGU pale utakaposhika mambo ya shetani kwa ushawishi wa huyo mwenzi wako ambaye hamjui MUNGU wa kweli na wala hajui kwamba nje na wokovu wa BWANA YESU ni maangamivu.
Waisraeli walijigundua kwamba wamekosea sana kuoa/kuolewa na watu wa mataifa.
Yezebeli mwabudu shetani alipoolewa tu na mfalme Ahabu alikuja na miungu yake na kusababisha taifa zima kuanza kuabudu miungu na sio MUNGU aliye hai.
BWANA aliwaadhibu kwa uovu wao japokuwa uovu huo uliletwa na Malikia ambaye alipatikana kwa sababu ya mfalme Ahabu kuoa mwabudu shetani.
Leo wengi sana husema kosea yote ila usikosee kuoa/kuolewa.
Wanazungumza maneno rahisi kabisa lakini hawajichunguzi kama wao wanaishi maisha matakatifu mbele za MUNGU aliye waumba.
 Mimi leo nataka niseme hivi ''Kama wewe ni mwasherati ni rahisi sana kumpata mwasherati mwenzako kisha mkaoana''

1 Kor 6:16 ''Au hamjui ya kuwa yeye aliyeungwa na kahaba ni mwili mmoja naye? Maana asema, Wale wawili watakuwa mwili mmoja.''

Kuna siri kubwa sana katika andiko hilo.
Kahaba ni mzinzi wa daraja la juu.
Wengi wameoana wakitokea kwenye ukahaba.
Mimi naamini wachumba kuzini kuanzia mara mbili na kuendelea huo ni ukahaba.
Hata kuzini mara moja ni dhambi kuu na haitakiwi kutokea.
Hata kuzini mara moja tu kunampasa jehanamu mzinifu huyo kama asipotubu.
Watu wengi husema ujana ni maji ya moto lakini mimi nasema;

Ujana utaitwa maji ya moto kama tu mwanadamu atautumia ujana wake kwa shetani.
Kwanini wewe ukubali kuoa/kuolewa na mtu aliyemkabidhi shetani maisha yake?

  1 Kor 5:10-11 ''Sisemi msichangamane kabisa na wazinzi wa dunia hii, au na wenye kutamani, au na wanyang'anyi, au na wenye kuabudu sanamu; maana hapo ingewalazimu kutoka katika dunia. Lakini, mambo yalivyo, naliwaandikia kwamba msichangamane na mtu aitwaye ndugu, akiwa ni mzinzi au mwenye kutamani au mwenye kuabudu sanamu au mtukanaji au mlevi au mnyang'anyi; mtu wa namna hii msikubali hata kula naye.'' 

Ngoja nikufundishe yafuatayo;
Baada ya kuumizwa kwenye uchumba unaovunjika wengi au ndoa yenye migogoro wengi ndipo wakati huo hutambua kwamba mojawapo ya haya ndio yaliyobababisha kuingia kwenye uhusiano huo uliovunjika baadae na kumuachia maumivu makali.
Baada ya uchumba kuvunjika au baada ya ndoa kuwa na migogoro isiyoisha wengi hugundua kwamba;

1= Hugundua kwamba Tamaa yake ya kumpata mtu mwenye mali ndio iliyompeleka kwenye uchumba huo au kwenye ndoa hiyo yenye vipigo kila siku.

2= Kuwaiga wengine walio na wachumba au walio kwenye ndoa ndicho kilichompa msukumo wa kuingia katika uchumba huo au ndoa hiyo.


3= Kuona muda umeenda ndivyo kilichompeleka kwenye uchumba kisha ndoa hata bila kumjua kwa kina mchumba huyo.



4= Hugundua kwamba hakumshirikisha MUNGU katika maamuzi ya kuingia katika uchumba kisha ndoa hiyo iliyogeuka ndoana.


5= Hugundua kwamba watu walimuona hafai ndio maana akaingia katika uchumba kisha ndoa kichwakichwa ili kujionyesha kwao kwamba na yeye yumo lakini madhara ya baade ndio yaliyompa kutambua ukweli huu.


6= Hugundua kwamba ngono waliyoiweka mbele yeye na mzinzi mwenzake huyo ndicho kimewaharibia.


7= Hugundua kwamba shinikizo la wazazi, ndugu au marafiki ndivyo kilichomponza na kujikuta ameingia katika uchumba kisha ndoa bila kutafakari kwa kina.


8= Hugundua kwamba huruma zake za kutaka kumsaidia mchumba wake huyo ndizo zilizompoza na sasa anaugulia maumivu mengi baada ya kuachwa au kuingia katika ndoa yenye vita kila siku.


9= Hugundua kwamba alikurupuka tu ndio maana akajikuta ameangukia kwa mtu ambaye sio.


10= Hugundua kwamba kwa sababu hajui kukataa ndio maana alijikuta akiangukia kwenye mchumba misumari kisha akaingia katika ndoa ndoano


11= Hugundua kwamba uzuri wa mchumba huyo ndio uliomzuzua na kujikuta akidandia basi(Mchumba) la kwenda jehanamu japokua yeye ana mpango wa kwenda mbinguni.


12= Hugundua kwamba aliowaomba ushauri juu ya mchumba wake huyo ndio waliomponza maana walimpamba mchumba huyo kwa sifa ambazo hata hajawahi kuwanazo ndio maana sasa ndoa imegeuka uwanja wa vita vya nyuklia


Waebrania 13:4 ''Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi MUNGU atawahukumia adhabu.'' 

Sijui wewe uchumba wako huo ambao umevunjika au haujavunjika ila ni uchumba wa kuungaunga ulianzaje.
Sijui wewe hiyo ndoa yako ilianzia wapi au ndio mlianzia katika ukahaba kwanza kisha ndoa?

Nakushauri kutunza utakatifu pamoja na kumcha MUNGU katika yote.
Nafasi ya kutengeneza na BWANA YESU KRISTO ipo wazi leo.


Matendo 3:19 ''Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA;''


Uzima wa milele ni muhimu kwako kuliko uchumba na mke au mume.
Ukitaka MUNGU akusaidie tena katika suala la uchumba au ndoa yako uliyoiingia kidhambi tubu toba ya kweli na anza upya na BWANA YESU 

Kama umekuwa na mchumba aliyejaa dhambi nakuomba achana naye na tubu kwa BWANA YESU naye atakupa mtu mtakatifu aliye sahihi ambaye ukimuona tu  utasema ''huyu ndie'' na utasema ''hakika nimepata kwa BWANA mtu aliye sahihi ambaye tutasaidiana katika maisha na tutasaidia na kuhimizana katika kuishi maisha matakatifu ili tuishi maisha mema na ya kumpendeza MUNGU.''

Kuna watu  naomba pia niwasaidie katika jambo hili.
Je shetani anao uwezo wa kufahamu mawazo  ya watu?

 Jibu ni kwamba shetani hawezi kufahamu mawazo ya mtu yeyote ila shetani ana uwezo wa kumshawishi mtu kupitia mawazo yake huyo mtu  akayafuata mawazo ya shetani ya kuyatekeleza akidhani ni ya kwake.
Kwenye suala la kutafuta mwenzi wa maisha shetani pia anaweza kudandia na kutimiza kusudi lake kwako.
Omba MUNGU sana katika uchaguzi wako.

Pia naomba niwasaidie watu wengine kwamba.   hivi Mungu anaweza kukusamehe na kufuta dhambi zao kama hujatubu na kuomba msamaha?

Wengi baada ya kupata wachumba na kuingia nao dhambini huwakimbia wachungaji wao na wengine huhama kabisa makanisa bila kutubu wala kuomba msamaha.

Majibu yangu ni haya.

MUNGU hawezi kufuta dhambi zako kama wewe hujaamua kutubu.

Mathayo 3:2 ''Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.''
 Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili

Comments