VYANZO SABA(7) VYA NDOA KUWA NA MIGOGORO

Na Mtumishi Peter Mabula
BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Leo ndoa nyingi zimejaa migogoro mingi.

Waefeso 5:31 '' Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja.''
 
Baada  ya wanandoa kuanza kuishi pamoja ndipo wakati mwingine kwa baadhi yao huibuka migogoro.
Vikao vingi vya kusuruhisha wanandoa leo viko kila kona.
Kulaumiana ni kwingi kwa wanandoa. hakuna anayekubali kushindwa.
Kila mwanandoa ni mjuaji na anajiona yeye ana haki kuliko mwenzi wake.
Amani imeondoka katika ndoa nyingi. Kuaminiana kumekuwa kudogo sana.
Ndoa nyingi zimegeuka ndoana.
Wamama wengi wanazikimbia ndoa zao na wababa wengi pia wanazikimbia ndoa zao.
Ndoa sasa kwa baadhi ya watu sio ndoa takatifu bali imegeuka ndoa tukutu.
Kuna wanandoa wanatamani wenzi wao wafe ili wawe huru kuolewa au kuoa wale wanaowataka.
Kuna wanandoa wanatamani wenzi wao wazime kama mshumaa unavyozima ili wawe huru.
Binafsi mimi Peter Nimekutana na maombi mengi sana ya kuombea ndoa baada ya migogoro.
Ndoa katika baadhi ya watu imekuwa mzigo mzito usiobebeka.
Wanandoa wengi hawajui chanzo cha hayo yote katika ndoa yao.
Wengine hata wanajilaumu na kusema walikosea kuchagua kumbe wala hawakukosea kuchagua ila ni kutokujua tu jinsi iwapasavyo kutenda katika utakatifu na maombi.

Wafilipi 2:14 '' Yatendeni mambo yote pasipo manung'uniko wala mashindano,'' 

Leo nataka nizungumzie vyanzo vya ndoa kuwa na migogoro.


Vyanzo 7 vya ndoa kuwa na mgogoro ni.

1. Shetani kupewa nafasi katika ndoa hiyo.

Waefeso 4:27 ''wala msimpe Ibilisi nafasi.''

-shetani akipewa nafasi katika ndoa huitumia vizuri sana kupanda magugu ambayo sio rahisi kuyang'oa.
-shetani anaweza kupanda chuki na kiburi.
-shetani anaweza kupanda dharau na kutokuaminiana.
-shetani anaweza kupanda tamaa za kipepo na kila aina ya uovu. haitakiwi wanandoa kumpa nafasi hata moja shetani.
-Kumpa shetani nafasi hata kidogo tu kunaweza kusababisha mgogoro mkubwa katika ndoa ambapo mgogoro huo unaweza kuwasumbua hata miaka 10 kama msipojua jinsi ya kumuondoa shetani na pando lake kwenu.

2. Mume kutokukaa katika nafasi yake kiroho na kimwili.

Waefeso 5:28 '' Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe. ''
-Hili ni agizo kwa kila mume kutoka kwa MUNGU.
Hata huwa sijui kwanini mume ndio kaambiwa ampende mke kama mwili wake mwenyewe. 
-Kama mume hatakaa katika nafasi yake kiroho na kimwili lazima tu hali hiyo itaibua migogoro katika ndoa yake.
-Mume kama hampendi mkewe kama anavyopenda mwili wake ni makosa.
-Nafasi ya mume katika ndoa ni kumpenda mkewe kama anavyojipenda mwili wake.
-Hapendi kuupiga mwili wake hivyo asimpige mkewe.
anavyouthamini mwili wake na mkewe anatakiwa kumthamini hivyo.
Mume asipojitambua katika hili lazima ndoa itakuwa na migogoro na mapigano yasiyokoma.

3. Mke kutokukaa katika nafasi yake kiroho na kimwili.

Wakolosai 3:18 '' Ninyi wake, watiini waume zenu, kama ipendezavyo katika BWANA. ''
-Mke ana agizo kutoka kwa MUNGU linalosema kwamba mke amtii mume wake katika BWANA yaani katika mema yampendezayo MUNGU.
-Mama akiondoa katika nafasi yake ya utii hakika ndoa itageuka ndoano.
-Haki sawa ya kibiblia ni mume akae kwenye nafasi yake na mke akae kwenye nafasi yake.
-Mama asipokuwa mtii kwa mumewe hakika atamsema vibaya mumewe kwa watu. atatoa siri za ndoa yake kwa marafiki na kuleta aibu itakayompata yeye mwenyewe.
Mwanamke asipokuwa mtii hawezi hata kumpikia mumewe, hawezi hata kutandika kitanda, huyo sio mtii na hajitambui.
Migogoro mingi katika ndoa inaweza kusababishwa na wamama kutokuwa watii kwa waume zao. Hakuna agizo la kumtii mumeo katika kila kitu hata kama ni dhambi bali ni lazima umtii katika BWANA.
Kumfulia nguo ni agizo kwako, kupika na kusafisha nyumba ni agizo katika BWANA. Mtii mumeo na ndoa yenu itadumu kama utaweka utii na maombi na utakatifu.

4. Kukosa hofu ya MUNGU kwa wanandoa.

Mithali 1:33 ''Bali kila anisikilizaye atakaa salama, Naye atatulia bila kuogopa mabaya.''
-Hofu ya MUNGU hutufanya tumche MUNGU na kulitii Neno lake.
-Hofu ya MUNGU hutufanya tumsikilize MUNGU kabla ya yote.
-Kumsikiliza MUNGU kupitia Neno lake ni sababisho la kukaa salama ndoa yenu, kukaa salama na maisha yenu kukaa salama.
-Hofu ya MUNGU huondoa hofu za kipepo.
-Kama mume katika ndoa hana hofu ya MUNGU hakika huyo dhambi kwake litakuwa ni jambo la kawaida na dhambi hizo kuzaa migogoro katika ndoa.
-Kama mke hana hofu ya MUNGU kutapelekea kufanya maovu mengi na maovu hayo kuzaa migogoro mingi katika ndoa.
Kukosa hofu ya MUNGU kwa wanandoa ni jambo la hatari sana.

5. Ahadi za wakati wa uchumba ambazo hazitekelezeki wakati wa ndoa.

Waefeso 4:25 ''Basi uvueni uongo, mkaseme kweli kila mtu na jirani yake; kwa maana tu viungo, kila mmoja kiungo cha wenzake.''
 -Wakati wa uchumba hutoka ahadi nyingi ambazo kwenye ndoa hushindwa kutekelezeka.
-Mfano kijana ameahidi kumsomesha mchumba wake pindi tu wakioana lakini baada ya kuingia katika ndoa mume huyo anasema marufuku mkewe kusoma. ni mbaya sana hiyo maana inaweza kusababisha mume kutokuaminika maneno yake yote hata kama atasema maneno ya kweli.
Biblia inasema ''Basi uvueni uongo, mkaseme kweli kila mtu na jirani yake''
-Wachumba wakiuvua uongo na kuambizana kweli siku zote za uchumba hadi ndoa hakika jambo hilo litawasaidia katika ndoa yao kuwa na amani na furaha, lakini uongo mwingi wakati wa uchumba unaweza kuleta migogoro mingi wakati wa ndoa. Mfano binti wakati wa uchumba anadanganya kwamba hajawahi kuzaa kumbe ana watoto wawili, jambo hilo likija kuwa wazi hataaminika tena na inaweza kuwa chanzo kikuu cha migogoro katika ndoa. kijana umesema hujazaa kumbe una mtoto na kwa bahati mbaya mkiingia katika ndoa mke wako akawa hazai na wewe hukumwambia kama una mtoto, mgogoro wa hapo wa kuumaliza ni MUNGU tu.
Binti wakati wa uchumba unajisemea kwa kujiamini kabisa kwamba uko bikra wakati ukweli umewahi kutembea na watu wengi hadi waume za watu, umewahi hadi kutoa mimba. mambo hayo yakijakugundulika ndoa hiyo itakuwa kwenye wakati mgumu sana.
 ''uvueni uongo, mkaseme kweli kila mtu na jirani yake''
 
6. Marafiki wabaya wa ndoa hiyo.

Mithali 18:24 '' Ajifanyiaye rafiki wengi ni kwa uangamivu wake mwenyewe; Lakini yuko rafiki aambatanaye na mtu kuliko ndugu. ''
-Ndoa nyingi huwa na migogoro kwa sababu ya marafiki wabaya.
Ndugu na wazazi wanaweza kuwa ni moja ya marafiki wabaya kama watatumika vibaya kuharibu ndoa yenu.
Biblia inasema '' Ajifanyiaye rafiki wengi ni kwa uangamivu wake mwenyewe  '' 
Kuna marafiki ndoa zao zimewashinda hivyo wanatamani na ndoa yao ivunjike. ukiwahusudu sana marafiki hakika migogoro katika ndoa itakuwa mingi sana.
Sio kwamba marafiki wote ni wabaya lakini uwe makini na marafiki zako, wengine wanataka urafiki na wewe ili wazini na mkeo/mumeo na kukuachia maumivu na migogoro mikubwa sana katika ndoa.
Mama umeolewa na mume mmoja hivyo msikilize zaidi mumeo na msahihishane nyie bila kuingiliwa.
Baba umeoa mke mmoja tu ambaye ulimchagua kuwa anafaa kuliko wanawake wote duniani, hivyo msikilize zaidi mkeo kuliko wengine.
Ukiwahusudu sana marafiki yaani watu wa nje ya ndoa yako hakika unaweza kuja kupata migogoro katika ndoa yako.
'' Ajifanyiaye rafiki wengi ni kwa uangamivu wake mwenyewe  ''

7. Wanandoa kutegemea akili zao na sio MUNGU.

Yeremia 17:5 '' BWANA asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha BWANA.'
-Ndoa yenu inatakiwa  iongozwe na MUNGU ambaye ndiye mwanzilishi wa ndoa yenu.
-Kuzitegemea akili zenu huku MUNGU mmemwacha ni hatari sana.
-MUNGU pekee ndio anaijua kesho yenu na kesho ya ndoa yenu hivyo ni muhimu sana kuwa waombaji ili MUNGU awasaidie.
Kuna wanandoa mara ya mwisho kuombea ndoa yao ni siku walipofunga ndoa miaka zidi ya 10 iliyopita.
Kuna wanandoa mara ya mwisho kuombea ndoa yao ni siku walipopigana na kupelekea kupelekana kwa mchungaji ndipo walipoombea ndoa yao.
Ndoa haiwezi kusimama kwa akili za wanandoa tu,.
Ndoa bila BWANA YESU itawashinda tu na kupelekea migogoro.
Ni laana kumtegemea mwanadamu huku moyoni umemwacha MUNGU.
Ni laana kujitegemea wewe mwenyewe huku moyoni umemwacha BWANA YESU.
''Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha BWANA.''

Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili

Comments