DHAMBI HUFUTIKAJE?

Na Mtumishi Peter Mabula.

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Nakukaribisha tule chakula cha kiroho ambacho ni Neno la MUNGU aliye hai.
Dhambi hufutikaje?
Dhambi hufutika baada ya aliyetenda dhambi hiyo kutubu kwa MUNGU kupitia KRISTO YESU.

 1 Yohana 1:6-10 ''Tukisema ya kwamba twashirikiana naye, tena tukienenda gizani, twasema uongo, wala hatuifanyi iliyo kweli; bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake YESU, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.  Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo mwetu.''

Hakuna mwanadamu hata mmoja ambaye hajawahi kutenda dhambi. 
Kwa sababu wanadamu wote wamewahi kutenda dhambi, dhambi zao kama hawajatubu bado ziko hata kama wamezitenda dhambi hizo miaka zaidi ya 60 iliyopita.
Kumpokea YESU kama BWANA na Mwokozi ndiko kunaweza kumtenga mtu na dhambi zake zote za zamani hata jina lake likaandikwa katika kitabu cha uzima. Hakuna msamaha wa dhambi nje na KRISTO ndio maana kitendo tu cha kukataa kumpokea YESU kama mkombozi ambaye damu yake itakusafisha dhambi zote, kitendo hicho tu ni dhambi ambayo inaweza kumpeleka mwanadamu jehanamu.

1 Yohana 5:11-12 '' Na huu ndio ushuhuda, ya kwamba MUNGU alitupa uzima wa milele; na uzima huu umo katika Mwanawe. Yeye aliye naye Mwana(YESU), anao huo uzima; asiye naye Mwana wa MUNGU hana huo uzima. ''

Ndugu, hata kama dhambi yako umeisahau lakini napenda kukuambia kwamba kama hujaitubia dhambi hiyo hakika bado iko na kama hutaitubia na kuiacha bado itaendelea kuwepo, na Biblia iko wazi ikisema mwisho wa wenye dhambi(ambao hawajatubu) ni ziwa la moto
Kiu Huondolewa Na Maji Wala Sio Mchuzi Wa Nyama, Na Dhambi Huondolewa Kwa Damu Ya YESU Wala Sio Kwa Kutawadha Miguu Na Mikono. 
Kuna Watu Hufanya Baadhi Ya Vitu Wakidhani Kupitia Vitu Hivyo Watasamehewa Kumbe Sio.
 Kuna Watu Ni Wagumu Sana Kutubu Kwa MUNGU, Watu Hawa Hufanya Vitu Fulani Vizuri Wakidhani Kupitia Vitu Hivyo Watasamehewa Kumbe Dhambi Yao Bado Inakaa. Hawa Hujaribu Kama Kuondoa Kiu Kwa Kunywa Soda, Matokeo Yake Hata Kama Wamekunywa Soda 10 Bado Kiu Watakuwa Nayo. 
Ndugu Zangu, Dawa Ya Kuondoa Dhambi Ni Kutubu Toba Ya Kweli Na Kuachana Na Dhambi Hizo Tena.

Matendo 3:19 '' Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA;''

Jambo la kujua ni kwamba BWANA YESU Atakaa Kwenye Kiti Cha Enzi, Atakifungua Kitabu Cha Uzima, Kisha Yatasomwa Majina Ya Wanadamu Walioshinda Duniani. 
Watu walioshinda duniani ni wale waliompokea YESU, Wakatubu na kuanza kuishi maisha matakatifu.
Hata kama kuna wakati katika maisha yao ya wokovu walijikwaa kwa kutenda dhambi, bado walitubu na kuacha uovu huo na kuendelea mbele na wokovu wa BWANA YESU ulio wa thamani sana.
Je,Unawaza Nini Juu Ya Hilo la kusomwa majina katika kitabu cha uzima?
Kuna watu majina yao yatakuwamo na wengine majina yao hayatakuwemo.
Ambayo majina yao yatakuwa katika kitabu cha uzima hao wataurithi uzima wa milele na ambao majina yao hayatakuwemo watapelekwa ziwa la moto.

Ufunuo 20:12-15 '' Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao. Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake; na Mauti na Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Wakahukumiwa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake. Mauti na Kuzimu zikatupwa katika lile ziwa la moto. Hii ndiyo mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto. Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto. ''

Kuna watu hufanya matendo mema bila kutubu wakidhani kupitia matendo yao mema watasamehewa juu kwa juu bila kutubu, huo ni uongo wa shetani.
Ni muhimu sana  kujua kwamba sadaka haiwezi kufuta dhambi.
kuwasaidia yatima na wajane hakuwezi kufuta dhambi.
Sio kwamba vitu hivyo ni vibaya Bali ni vizuri sana ila nataka kupitia ujumbe huu niwasaidie watu wengi ambao wakati wa sikukuu, wakati wa mwisho wa mwaka au wakati wowote hutoa misaada yao kwa wagonjwa, wahitaji, Yatima na wajane wakitumia njia hiyo wakidhani ni njia ya kusamehewa dhambi kumbe wala haiko hivyo.
dhambi inafutwa kwa damu ya YESU tu baada ya mwenye dhambi kutubu.
Najua kabisa matajiri wengi hawajaokoka lakini hutumia zawadi kwa wahitaji kama njia yao ya kutaka kutakaswa baada ya uovu mwingi walioutenda. hata hivyo ukweli wa MUNGU ni kwamba sadaka au msaada kwa watu haufuti dhambi Bali ukitaka dhambi zako zifutwe basi nenda kanisani ukaokoke na kutubu.
pia usiache kuwasaidia wajane, Yatima na wahitaji maana ni jambo jema sana ingawa haliwezi kufuta dhambi.

BWANA YESU anasamehe dhambi na atakuandika jina lako kwenye kitabu cha uzima kama ukimpokea na kutubu.

 Marko 2:10 '' Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi ''


Inawezekana Malengo Yako Wiki Ijayo Unataka Kwenda Kwa Mganga Sangoma Gwiji, Lakini Taarifa Muhimu Leo Ni Kwamba Hayo Ni Malengo Feki Na Ya Kishetani. 
Mathayo 3:2 ''Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia. ''

 Habari za ufalme wa MUNGU zinahubiriwa.
Wenye masikio ya kusikia wanasikia, wenye kufunguliwa wanafunguliwa.
Lengo kuu la ufalme wa MUNGU ni watu wapate uzima wa milele.
Mfalme wa ufalme wa MUNGU na BWANA YESU na yuko tayari kumuokoa mtu yeyote atakayependa kuokoka.


 Hutachuma Matunda Katika Mti Wa Mwenzako Bali Utachuma Matunda Katika Mti Wako. Kama Matunda Ya Mti Wako Yanaitwa Dhambi Ni Hayo Utakayo Kula Baadae, Ni Hayo Yatakuliza Baadae Kama Hutatubu. Kila Mtu Matendo Yake Ndio Hutengeneza Matunda Ambayo Mtu Huyo Atakula Baadae.

 Kuna Watu Wana Juhudi Lakini Sio Juhudi Katika MUNGU Aliye Hai. Mtu Anaweza Kuwa Na Juhudi Ya Kuabudu Kila Baada Ya Robo Saa Lakini Kama Hamwabudu JEHOVAH Juhudi Zake Huyo Mtu Ni Bure Na Hazitamsaidia Lolote. Unakuta Mtu Hajawahi Kukosa Kipindi Cha Mafundisho Kanisani Lakini Kama Mtu Huyo Hautaki Wokovu Wa BWANA YESU Juhudi Yake Mtu Huyo Ni Bure. Hakikisha Unakuwa Na Juhudi Katika MUNGU Aliye Hai Sio Kuwa Na Juhudi Katika Vinyago Na Kuabudu Miungu.

1 Kor 10:14-15 ''Kwa ajili ya hayo, wapenzi wangu, ikimbieni ibada ya sanamu. Nasema kama na watu wenye akili; lifikirini ninyi ninenalo. ''

 Kuna Watu Wana Wokovu Wa Msimu. 
Wakati Wa Matatizo Anaokoka, MUNGU Akimuondolea Matatizo Anarudi Kuwa Mpagani. 
 Ndugu Nakuonya Katika Jina La YESU KRISTO. 
Kama Umeamua Kuwa Wa Shetani Hakikisha Unakuwa Wa Shetani Hata Wakati Wa Matatizo Na Kumbuka Kuwa Kuendelea Kuwa Upande Wa Shetani Huwa Kuna Jehanamu Baadae, Kama Umeamua Kuwa Wa BWANA YESU Hakikisha Unakuwa Mtakatifu Hata Wakati Wa Raha. Mwenye Sikio La Kusikia Na Asikie Leo.
 Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichaka chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.


Comments