MASAA YAMEENDA SANA NA MWISHO U KARIBU.

Na Mtumishi Peter Mabula.

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU. 
Masaa yameenda sana.
Kama kuna kitu muhimu kimebaki basi ni kuijua njia ya kwenda uzima wa milele na kuifuata.
Njia ya kwenda mbinguni ni kumpokea YESU.

Yohana 14:6 '' YESU akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa BABA, ila kwa njia ya mimi.''

ili ufike mbinguni hakikisha baada ya kuiona njia hiyo ishi maisha matakatifu.


Waebrania 12:14 '' Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona BWANA asipokuwa nao;''

Naamini umenielewa njia ya kwenda uzima wa milele ilivyo.

Njia ni YESU na tiketi ni utakatifu.
Kwanini nimesema kwamba masaa yameenda sana?
Ni kwa sababu bado kuna watu wako katika kufuata uongo na wameiacha njia ya mbinguni.

Warumi 1:25 ''Kwa maana waliibadili kweli ya MUNGU kuwa uongo, wakakisujudia kiumbe na kukiabudu badala ya Muumba anayehimidiwa milele. Amina.''

Moja ya makosa ni hili la sanamu.
Ukweli ni kwamba
Kumwabudu mariamu ni karama ya shetani na ni kuabudu kiumbe na sio MUNGU aliye hai.
Kusujudia sanamu ni karama ya shetani na ni kuabudu shetani  na sio MUNGU aliye hai.
Walio nje na KRISTO hao wako pia nje ya ufamle wa MUNGU na wako nje ya uzima wa milele, Maana uzima wa milele ni katika KRISTO YESU tu.

Waefeso 1:7 '' Katika yeye huyo(YESU), kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake.'' 

Hayo ya sanamu na kuabudi wanadamu ni machukizo na leo nataka mtu mmoja apone kupitia ujumbe huu.
Karama ya MUNGU ni kuifuata Biblia na kuitii.
Masaa yameenda sana.

Waebrania 9:27 ''Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu;''
 
Natamani nimwambie dada yule na kaka yule kwamba masaa yameenda sana.
Natamani nimwambie baba yule na mama yule kwamba masaa yameenda sana.
Ingawa yeye anadhani kwamba sasa ni asubuhi lakini ukweli ni kwamba sasa ni usiku na karibu sana kunakucha.
Ndugu huyu anaendelea na dhambi akidhani muda wa kutubu bado ni mwingi sana mbele yake lakini ukweli ni kwamba Masaa yameenda sana bado kidogo kutakucha hivyo atakua amechelewa kutubu.
Nimeambiwa nimwambue atubu sana na kuokoka maana karibia kunakucha.
BWANA YESU amemwita sana huyu ndugu ili amuokoe maana masaa yameenda sana lakini ndugu huyu ameshupaza shingo akijipangia mwaka wa kutubu kumbe karibia kunakucha na nafasi hataipata kama kutapambazuka kabla hajatubu.
Mimi nimeambiwa nimwambie maana masaa yameenda sana.
Malaika wa BWANA wanaikusanya ngano ghalani na huyu ndugu bado hajafanyika ngano hadi sasa.
Yeye bado ni magugu na magugu yatatupwa kwenye ziwa la moto.


Masaa yameenda sana hivyo nimetumwa nimwambie kwamba masaa yameenda sana hivyo atubu kabla hakujapambazuka.
Mwenye sikio la kusikia na alisikie neno hili na Uzima na atubu maana masaa yameenda sana.

Ni muhimu kila mmoja kuifikia toba kwa kutubu na kuacha uovu.

2 Petro 3:9-14 ''BWANA hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba.
Lakini siku ya BWANA itakuja kama mwivi; katika siku hiyo mbingu zitatoweka kwa mshindo mkuu, na viumbe vya asili vitaunguzwa, na kufumuliwa, na nchi na kazi zilizomo ndani yake zitateketea. Basi, kwa kuwa vitu hivi vyote vitafumuliwa hivyo, imewapasa ninyi kuwa watu wa tabia gani katika mwenendo mtakatifu na utauwa, mkitazamia hata ije siku ile ya MUNGU, na kuihimiza; ambayo katika hiyo mbingu zitafumuliwa zikiungua, na viumbe vya asili vitateketea na kuyeyuka? Lakini, kama ilivyo ahadi yake, mnatazamia mbingu mpya na nchi mpya, ambayo haki yakaa ndani yake. Kwa hiyo, wapenzi, kwa kuwa mnatazamia mambo hayo, fanyeni bidii ili mwonekane katika amani kuwa hamna mawaa wala aibu mbele yake.''



Kuna watu bado hata sasa wako katika dhambi.
Kuna viongozi wa dini hawakemei dhambi kwa sababu hata wao huzishiriki dhambi hizo.
Ndugu zangu masaa yameenda sana.
Usikubali kung'ang'ania dini ya Babu yako ambayo hata haihubiri Wokovu wa KRISTO.
Using'ang'anie dhehebu la wazazi wako ambalo halikufundishi jinsi ya kuwa mtakatifu bali linafundisho uongo likikataza watu kuokoka.
Usikubali kuangamizwa kwa sababu tu umekosa maarifa ya kiMUNGU.
Kuna watu wanaangamizwa na viongozi wao wa dini.
Kuna viongozi wa dini kwa sababu wameiacha kweli ya KRISTO, MUNGU na wao amewaacha hivyo hata kama wanaitwa watumishi lakini MUNGU amewakataa kwa sababu wanahubiri uongo.


Hosea 4:6 '' Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe, usiwe kuhani kwangu mimi; kwa kuwa umeisahau sheria ya MUNGU wako, mimi nami nitawasahau watoto wako.''

=Maarifa sahihi ni Neno la MUNGU.
-Maarifa ni elimu iliyo katika matendo.

Ukilipokea Neno la MUNGU kisha ukaliishi hakika hutaangamia
Ni muhimu kila mtu kuishi kwa kulifuata Neno la MUNGU.
Injili ni habari njema za ufalme wa MUNGU zinazoelekeza watu kuokoka na sio kuangamia.
Wokovu ni mpango wa MUNGU kuwaokoa wanadamu kupitia YESU KRISTO.
BWANA YESU ambaye ndiye mwenye wokovu anasema;
 ''Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi, wapate kutubu.-Luka 5:32''

BWANA YESU amekuja kuwaita wenye dhambi ili watubu.
BWANA YESU amekuja kuwaita wenye dhambi haijalishi hao wenye dhambi wanasali kanisa gani au wanaabudu dini gani lakini kama wakimpokea na kutubu hakika anawapa haki ya uzima wa milele. Muhimu tu ni kwamba baada ya kumpokea BWANA YESU kwa kuokoka, kisha unatubu na kuanza kuishi maisha mataktifu hakika wewe uzima wa milele ni wako.

 Matendo 3:19 '' Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA;''

Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichaka chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.


Comments

Anonymous said…
Habari mtumishi,tumebadilisha link yetu sasa ni www.grananewsmedia.blogspot.com
Samahani kwa usumbufu