FAIDA ZA NGUVU ZILIZOMFUFUA YESU KRISTO ZILIZOMO NDANI YAKO.

Na Mwl. Christopher Mwakasege.
Bwana Yesu asifiwe milele!
Je umeokoka? Ikiwa umeokoka, ujue basi ya kuwa, nguvu za Mungu zilizomfufua Kristo toka kwa wafu, zimo ndani yako! Nguvu hizi zimebebwa na Roho Mtakatifu aliye ndani yako! Hii ni kwa sababu imeandikwa hivi “lakini ikiwa Roho yake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu” (Warumi 8:11).
Je, unajua faida kwa ajili yako – sasa wakati huu – yaani katika ulimwengu huu, kwa nguvu za Mungu zilizomfufua Kristo kukaa ndani yako? Na kama unazijua – je; unazitumia na kufaidika kwa kiwango kipi katika maisha yako? Hebu tafakari faida chache zifuatazo:


Faida 1: Nguvu zilizomfufua Yesu zilizomo ndani yako zinakupa uwezo wa kukusaidia kubadili mfumo na kiwango chako cha kufikiri!...ili uwe na mawazo yaliyo bora kuliko ya wale wanaokuzunguka! Biblia inasema: “Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo…yafikirini yaliyo juu…mkivaa utu mpya, unaofanywa upya upate ufahamu sawasawa na mfano wake yeye aliyeuumba” (Wakolosai 3:1, 2,10). Nguvu zilizomfufua Yesu zinakupa nafasi ya kuweza kujua “mawazo” ya Mungu juu ya mambo yanayokuhusu (Isaya 55:8,9 na Yeremia 29:11) – ili katika mawazo hayo ya ki – Mungu uweze kujenga mfumo wako wa maisha, na wa utendaji wako wa kazi (Mithali 23:7a)!
Jizoeze kutumia nguvu zilizomfufua Yesu zilizomo ndani yako kupambana na kuondoa “mawazo” ndani yako, yanayozuia au yanayokandamiza, kiwango cha mafanikio yako, kisifikie kiwango kile alichokikusudia Mungu kwa ajili yako! “Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome) tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo”.
Uwezo huu wa Mungu umo ndani yako! Ni uwezo unaoweza kubadili kufikiri kwako, kwa kiasi cha kukupa kuwaza na kufahamu mambo kama Mungu atakavyo! Je, unatumia na kuufaidi uwezo huu kwa kiwango gani?
Tunakuombea ili kiwango chako cha kufaidika na nguvu zilizomfufua Yesu zilizomo ndani yako kiongezeke, na uone matokeo yake katika maisha yako!


 Kumbuka ya kuwa kama Kristo hakufufuka – biblia inatuambia ya kwamba “Imani yenu ni bure” (1 Wakorintho 15:14, 17). “Bure” maana yake “haina faida”. Lakini kwa kuwa Kristo alifufuka, basi, Imani yetu si bure! Kwa tafsiri nyingine ina maana tunatakiwa tufaidike, kwa Kristo kufufuka!
Faida za kufufuka kwa Yesu, zinatakiwa zidhihirike katika maisha yetu, kwa msaada wa nguvu za Roho aliyemfufua Yesu aliye ndani yetu (Warumi 8:11). 


 faida ya 2  ni hii:

“Nguvu zilizomfufua Yesu zilizomo ndani yako, zinakupa kuketi pamoja na Kristo upande wa kuume wa Mungu, na kukuwezesha kunufaika na yale yanayopatikana hapo!”
Biblia inasema hivi: “Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu” (Waefeso 2:6). Na kufuatana na Waefeso 1:20, tumeketi na Yesu kwenye “mkono wa kuume” wa Mungu!
Usipojua kwenye mkono wa kuume wa Mungu kuna nini kwa ajili yako, itakuwa vigumu kuwa na Imani itakayokuwezesha kufaidi ipasavyo msaada wa nguvu zilizomfufua Yesu zilizomo ndani yako.
Kwa mfano:
Baadhi ya mambo ambayo yanatakiwa yawe yanaonekana katika maisha yako unapokuwa umeketi na Yesu mkono wa kuume wa Mungu ni haya yafuatayo:
Haki zako upewe. Usionewe kiasi cha kupoteza au kunyang’anywa haki zako (Zaburi 48:10; Isaya 41:10)
Kuwa na mamlaka ya kutawala na kuthibiti mambo katika ulimwengu wa roho kunakojidhihirisha katika ulimwengu wa kimwili (Waefeso 2:6; Waefeso 1:20, 21).
Mungu kukupigania dhidi ya adui zako hadi uwashinde (Zaburi 110:1 na Waebrania 10:12, 13).
Mungu kukulinda ili utumie vizuri siku zako za kuishi hapa duniani (Mithali 3:16).

Ukiendelea kusoma yote yaliyomo upande wa kuume wa Mungu, utashangaa kuona ya kuwa, unakwama katika maeneo kadhaa kwenye maisha yako, wakati nguvu zilizomfufua Yesu zimo ndani yako kukusaidia ili usikwame!

 Faida ya 3 unayotakiwa kunufaika nayo nguvu zilizomfufua Yesu zinapokuwa ndani yako ni hii: “Unakuwa mrithi halali wa aina mbili za urithi”!
Urithi wako wa kwanza ni huu: “Warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo”. Imeandikwa ya kuwa: “Na kama tu watoto, basi tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo” (Warumi 8:17).
Urithi wako wa Pili ni huu: “Warithi wa Ibrahimu”. Imeandikwa ya kuwa: “Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Ibrahimu, na warithi sawasawa na ahadi “(Wagalatia 3:29)
Hii ina maana chochote alichopewa Yesu kama mrithi wa Mungu – na sisi tu warithi wa vitu hivyo pamoja naye. Na chochote alichoahidiwa Ibrahimu na Mungu kiwe urithi wake na wa uzao wake – na sisi tuna uhalali wa kuwa warithi wa vitu hivyo!
Kuwa mrithi na kutokujua ya kuwa wewe ni mrithi – ni sawa na ya kwamba wewe si mrithi! Kujua ya kuwa wewe ni mrithi, na usijue mambo uliyorithi – ni sawa na ya kwamba wewe si mrithi! Ndiyo maana nataka ujue ya kuwa, ikiwa umeokoka, basi, nguvu zilizomfufua Yesu zimo ndani yako!
Na ikiwa nguvu zilizomfufua Yesu zimo ndani yako, basi, ujue wewe ni mrithi pamoja na Kristo – kwa Mungu na kwa Ibrahimu! Ni jukumu lako kusoma biblia ili ujue urithi wako kwa Mungu ni upi, na urithi wako kwa Ibrahimu ni upi!
Kwa mfano: Biblia inasema; “Ahadi ile ya kwamba atakuwa mrithi wa ulimwengu alipewa Ibrahimu na uzao wake” (Warumi 4:13). Na kufuatana na Wagalatia 3:29 – mkristo, aliye na Kristo moyoni mwake, ni “uzao wa Ibrahimu” na mrithi “Sawasawa na ahadi”
Je, unalijua jambo hili lina maana gani kwako, na ukilijua unalipataje? Ni muhimu ulijue hili – maana unaweza ukaishi maisha ya dhiki na taabu – huku wewe ni mrithi mkubwa wa utajiri wa kiroho na wa kimwili!
Ndani ya Kristo – kwa mfano – mtu anakuwa mrithi wa jina la Yesu (Waebrania 1:4); na mrithi wa wokovu (Waebrania 1:14); na mrithi wa “baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho”(Waefeso 1:3). Je, faida za urithi huu unazifaidi kwa kiwango kipi?
Ni muhimu kwako na kwa kila mkristo kukua kiroho kwenye eneo hili la kuujua urithi tuliopewa na kujua namna ya kuupata na kuutumia! Hii ni kwa sababu: “mrithi, wakati wote awapo mtoto, hana tofauti na mtumwa, angawa ni bwana wa yote, bali yu chini ya watunzaji, hata wakati uliokwisha kuamriwa na baba” (Wagalatia 4:1,2).
Mungu aendelee kukubariki katika eneo hili!

Somo hili litaendelea......................

Comments