JINSI YA KUYAEPUKA MAJARIBU YA KUJISABABISHIA.

 Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
BWANA YESU atukuzwe.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Kuna aina nyingi sana za majaribu.
Kuna majaribu yanayokuja kwa sababu tu umepunguza au umeacha maombi.
Kuna majaribu ya hila ambapo watu hukujaribu wewe.
Kuna majaribu ya kujisababishia wewe.
Kuna majaribu yanayotokana na tamaa ya mtu.
Kuna majaribu kama kipimo cha MUNGU kwa mtu wake ampendae, haya huja mara chache sana na ni kwa watu wachache tu.
Kuna majaribu hutoka kwa shetani na mawakala wake.
Kuwepo  mahali  fulani kwa  wakati usio  sahihi inaweza kuwa jaribu kwako.
Kuna upana mkubwa sana katika kufafanua majaribu na aina zake.

Maana mojawapo ya  neno ''Majaribu''   ni fikra zinazomshawishi  mtu kutenda jambo ambalo ni machukizo kwa MUNGU.
Maana nyingine Ya Neno jaribu ni ushawishi wa kipepo unaomfanya mwanadamu kutenda jambo baya au au ovu.
Kuna maana nyingi za majaribu.

Leo nataka nizungumzie tu aina moja ya majaribu yaani majaribu ya mtu kujisababishia mwenyewe.

Marko 14:38 '' Kesheni mwombe, msije mkaingia majaribuni, roho i radhi ila mwili ni dhaifu.'' 

roho i radhi kutenda mema lakini mwili ni dhaifu sana.
Majaribu yanaweza kumpata mtu kama atautii Mwili , lakini maombi yanaweza kuutiisha mwili hata mtu wa MUNGU asiingie majaribuni.
Kulitii Neno la MUNGU kunaweza kukuondolea baadhi ya majaribu katika maisha yako. Kwanini nimesema hivyo? kwamba ''baadhi ya majaribu'' ni kwa sababu kuna wakati MUNGU mwenyewe anaweza pia kukujaribu kwa njia ya kukupima kama umefaulu katika viwango vya kiroho avitakavyo.
Kuenenda kwa ROHO MTAKATUFU kunaweza kukuondolea baadhi ya majaribu katika maisha yako.
Kuenenda kiroho kunaweza kuwa msaada wa kushinda majaribu kwa urahisi sana.

 1 Timotheo 6:9-10 '' Lakini hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu. Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi. ''

Mali inaweza kuwa jaribu kwa mtu hata kumkosesha uzima wa milele.
Madaraka ya mtu yanaweza kuwa jaribu kwake hata kumkosesha uzima wa milele.
Pesa za mtu zinaweza kuwa jaribu kwake hata kumkosesha uzima wa milele.
Kazi ya mtu inaweza kuwa jaribu kwake hata kumkosesha uzima wa milele.

 Kuna watu hujaribiwa katika mambo mengi, mengi katika hayo ni haya;


1.  Kuna watu hujaribiwa kwa sababu ya kiburi chao.

Mithali 16:18 '' Kiburi hutangulia uangamivu; Na roho yenye kutakabari hutangulia maanguko.''

Kuna vitu unaweza usivipate kabisa katika maisha yako kwa sababu tu ya kiburi, kiburi kinaweza kuwa jaribu kwako.
Unaweza ukafukuzwa kazi kwa sababu ya Kiburi chako na kiburi hicho kikawa jaribu kwako.
Kuna watu kwa sababu ya viburi hawashauliki hata kidogo. Onekana una kiburi kwa kukataa mambo ya dhambi hapo utaheshimiwa na MUNGU, lakini sio wewe uonekana una kiburi kwa kung'ang'ania mambo ya dhambi, kiburi hicho kinaweza kuwa jaribu kwako.

 
2.  Kuna watu hujaribiwa kwa sababu ya uongeaji wao usio na mipaka.


Ayubu 33:2 ''Tazama basi, nimefunua kinywa changu, Ulimi wangu umenena kinywani mwangu.''

Kinywa kazi yake ni kunena, lakini pia kinywa hicho hicho kina uwezo wa kunena mabaya au mazuri. Maneno ya kinywa chako yanaweza kukuweka majaribuni hakika.
Unaweza ukatamka vitu ambayo huwezi kuvitekeleza. unaweza ukasema uongo na ukanasa kwenye dhambi. unaweza ukaahidi mbele za watu likawa jaribu kwako kama hutalitimiza.

Yakobo 1:26 ''Mtu akidhani ya kuwa anayo dini, wala hauzuii ulimi wake kwa hatamu, hali akijidanganya moyo wake, dini yake mtu huyo haifai.''

Ndugu kama unaingia sana katika majaribu kwa sabnabu ya kinywa chako kisichokuwa na bleki nakusihi omba MUNGU akuwekee mlinzi kwa maombi ili usije ukaongea mambo yatakayokuweka katika majaribu.

Zaburi 141:3 '' Ee BWANA, uweke mlinzi kinywani pangu, Mngojezi mlangoni pa midomo yangu. ''

3  Kuna watu hujaribiwa kwa sababu hawaombi maombi sahihi.


Yakobo4:2-3 ''Mwatamani, wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi! Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu.''

Unaweza ukajikuta katika majaribu mengi na mbalimbali kwa sababu tu huna maombi.
shetani anaweza akaweka makazi katika moyo wako au vitu vyako au mipango yako kwa sababu tu huna uwezo wa kumfukuza kwa sababu hufanyi maombi. Ni muhimu sana kuwa muombaji maana kwa njia hiyo kuna majaribu hata hayatagusa maisha yako daima. BWANA YESU yuko siku zote akisubiri tu umwite naye atakuitikia na utakaa salama, ila ni lazima umwite na hakuna njia ya kumwita ila njia ya maombi na utakatifu.


4.  Kuna watu hujaribiwa kwa sababu uchungu ambao uko mioyoni mwao maana hawataki kusamehe.


Waebrania 12:15 '' mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya Mungu; shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo.''

Uchungu wa mambo mbalimbali uliyotendewa unaweza kukuweka majaribuni siku zote. Uchungu unaweza kukufanya ukachukua kitu ili umpige aliyekukosea na jambo hilo likakufanya uende gerezani, uchungu umekuwa jaribu.
Uchungu unasababishwa na kutokusamehe na kusahau.
 Taarifa Muhimu Ni Kwamba; Ukikaa Muda Mrefu Ukiwa Na Uchungu Na Mtu Nguvu Za MUNGU Ndani Yako Zinaondoka.


Mathayo 6:14-15 ''Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na BABA yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala BABA yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu. ''

Kusamehe ni jambo la lazima maana hata wewe unahitaji usamehewe na MUNGU.
Kanuni ya MUNGU ni kwamba uwe mtu wa kuwasamehe watu na wewe ndipo utasamehewa na MUNGU.
Usiposamehe watu mambo waliyokukosea huwezi kuingia uzima wa milele, hivyo zingatia sana kusamehe watu makosa yao ili na wewe usamehewe. uchungu wa kutokusamehe unaweza kuwa jaribu baya katika maisha yako.

5.  Kuna watu hujaribiwa kwa sababu ya kujiona kwamba wao tu wenye uwezo na maarifa na sio mwingine yeyote.


 Mithali 12:15 '' Njia ya mpumbavu imenyoka machoni pake mwenyewe; Bali yeye aliye na hekima husikiliza shauri.''

Kujiona kwako kunaweza kukukufanya uwadharau wengine, hilo likawa jaribu baya sana.
Elimu yako inaweza ikageuka jaribu kwako kama elimu hiyo itakutumia wewe ili uwadharau watu wengine.
Kudharau watu ni dhambi hivyo jitenge na kuwadharau watu.
Kuna mtu kwa sababu ya kiburi chake cha kujiona, anaweza hata akakosa vitu vizuri kutoka kwa watu , hilo linaweza kuwa jaribu kwake.

Wafilipi 2:3 ''Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake. ''

6.   Kuna watu hujaribiwa kwa sababu ya tamaa.

Yakobo 1:14-16 '' Lakini kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa. Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti. Ndugu zangu wapenzi, msidanganyike. ''

Hapa ndipo watu wengi sana hunasa.
Tamaa yako ya vitu fulani inaweza kuwa jaribu baya hata ukaja kujuta baadae.
Kuna watu kwa sababu ya tamaa ya maisha ya kifahari wamejikuta na Ukimwi au magonjwa mengine ya zinaa.
Kutamani utajiri kuwewafanya baadhi ya watu kujiunga katika kumwabudu shetani, hilo ni jaribu baya sana.
Kuna watu wamejikuta wanaua wazazi wao au ndugu zao au watoto wao kwa sababu tu ya mali kulikopelekea kudanganywa na waganga.
Binti anaweza akajikuta ana mimba kwa sababu tu ya kumtamani kijana tajiri na kujikuta hata kuolewa haolewi, hilo likawa jaribu lake.
Tamaa mbaya inaweza kuzaa mtoto aitwaye dhambi na dhambi inaweza kuzaa kufa kiroho na hata dhambi inaweza kuzaa mauti yaani jehanamu kama mtu huyo hatatubu.


7.  Kuna watu hujaribiwa kwa sababu ya vipaji vyao ambavyo ni machukizo kwa MUNGU aliye hai.


Yakobo 4:7 '' Basi mtiini MUNGU. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia. ''


Kila mtu anapaswa kumtii MUNGU katika mambo yote.
Kuna watu hujitenga na MUNGU kwa sababu tu ya vipaji alivyowapa MUNGU.
Mfano mtu anaweza akajiona ana sauti nzuri lakini badala ya sauti hiyo kuitumia kumtukuza MUNGU kwa kuimba nyimbo za injili yeye anaanza kuimba nyimbo za kidunia za machukizo na hiyo kuwa jaribu lake baya sana maana kwa kuimba nyimbo za kidunia atakuwa anajitenga na MUNGU.
Unaweza kuwa na kipaji cha kuongea vizuri na hiyo ikakupeleka ukawa unatoa matangazo ya biashara ya makampuni fulani, matangazo hayo yakawa ya kuwaalika watu kwenda kumtukuza shetani, hilo likawa ni jaribu lako.
Kuna mabinti kwa sababu ya sura zao nzuri huwekwa eneo la mapokezi katika maofisi au mahoteli. Huvalishwa nguo za nusu uchi ili kuwavuta wateja, lakini kwa sababu jambo hilo ni baya hugeuka kuwa jaribu kwa binti yule, maana kwanza watu watamuona kuwa kama kahaba na pia atawaingiza watu dhambini kwa kumtamani kipepo, hilo ni jaribu baya sana linalotokana na kipaji au kipawa cha mtu.
 Unatakiwa umtii MUNGU katika kipaji chako, sura yako na muonekano wako.


8.  Kuna watu hujaribiwa kwa sababu ya kudhani wataishi duniani milele bila kufa.


Ayubu 14:1-2 “Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke, siku zake za kuishi si nyingi, naye hujaa taabu. Yeye huchanua kama vile Ua, kisha hukatwa; hukimbia kama kivuli, wala hakai kamwe”

 

Kuna watu hupanga mipango mingi ya miaka mingi sana ijayo  kana kwamba watakuwepo muda huo, wanasahau kama kuna kufa, hilo linaweza kuwa jaribu kwa mtu husika.

Kuna watu leo wengi sana hupanga kwamba wataokoka siku wakizeeka lakini ukweli ni kwamba kifo hakina mzee bali hata kijana au mtoto, hilo linaweza kuwa jaribu linalowapeleka pabaya sana.

Mimi Peter Kwa kuhubiri injili nimewahi kutukanwa sana na watu ninaowahubiria. MUNGU ananipa Neno la kuwasaidia ili wazinduke katika usingizi wa dhambi waliomo lakini sio wote huelewa. Siku ya mwisho i karibu lakini sio wote hutengeneza njia zao sasa.

Unaweza kujiona una nguvu na bado mdogo kiumri hivyo jambo hilo likakupelekea ukaamua kufanya anasa zote za dunia lakini kifo hakika hodI hivyo ukimkimbia BWANA YESU na wokovu wake ni heri sana kwako.

9. Kuna watu hujaribiwa kwa sababu ya kupenda Pesa. 

1 Timotheo 6:9-10 '' Lakini hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu. Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi. ''

Pesa imekuwa jaribu kwa watu wengi sana.
Kuna watu leo ni vilema kwa sababu tu walijaribu kuiba ili kupata pesa, hilo ni jaribu baya sana.
Kuna watu wanajiuza kwa sababu tu ya pesa,
hilo ni jaribu baya sana.
Kuna watu leo wametajirisha waganga kwa sababu tu ya kusaka utajiri feki,hilo ni jaribu baya sana.
Kuna watu leo wamemuacha YESU kwa sababu tu ya pesa,  hilo ni jaribu baya sana.
 Kuna watu leo kanisani wana miaka zaidi ya 2 hawajaenda kwa sababu tu ya pesa, hilo ni jaribu baya sana.




10.. Kuna watu hujaribiwa kwa sababu ya kuwadharau watu.

Marko 12:31'' Na ya pili ndiyo hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi. ''

Kama unawapenda watu huwezi kuwadharau.
Unaweza ukamdharau sasa kijana fulani lakini miaka 10 ijayo akawa ndio bosi wako kazini, ukapata jaribu la ghafla sana kama atataka kulipiza.
Unaweza kuwachukia aina fulani ya watu kwa sababu tu unaona hawana kitu hata kimoja cha kukusaidia lakini ukasau kwamba, wakati mwingine maskini wa leo anaweza kuwa ndiye tajiri sana wa kesho, huko tajiri sana wa leo akawa ndiye maskini zaidi wa kesho. Hapo unaweza kujikuta kwenye jaribu zito kwa sababu tu ya kuwadharau watu.


Waebrania 13:1-2 ''Upendano wa ndugu na udumu. Msisahau kuwafadhili wageni; maana kwa njia hii wengine wamewakaribisha malaika pasipo kujua. ''


Kuna watu wamewahi kupokea malaika, je kama wangewadharau malaika wa MUNGU wangepata miujiza yao iliyoletwa na malaika hao? 
jibu ni hapana.
Hata aina fulani ya watu wanaweza kuwa ni malaika kwako kwa sababu wametumwa na MUNGU kwa ajili yako ili kukupa mema, je kama unawadharau utapokea baraka hiyo?
Jibu ni hapana. Mambo ya kuwadhaharu watu yanaweza kugeuka jaribu kwako baya sana.

Je wewe unajaribiwa na nini? 
Je umechukua hatua gani za kuyashinda majaribu yako ambayo mengi ni machukizo kwa MUNGU aliye hai?



Kuna watu hupenda kuwa jaribu Kwa wengine lakini wao wakijaribiwa hulalamika sana.
Ndugu mmoja kabla hajawa mchungaji alikuwa akimlaumu mchungaji wake sana. Akisema yeye akiwa mchungaji kanisa litastawi sana. Alikuwa akitumika kama jaribu baya Kwa mchungaji wake na kumfanya mchungaji wake awe kama hajaitwa na MUNGU, mchungaji alidharaulika Kwa kila Mtu kanisani. Yule bwana maneno akasomea uchungaji kisha akaja kukabidhiwa kanisa kuchunga. Alikabidhiwa kanisa likiwa na waumini 300 lakini miaka 2 baadae kanisa lile likuwa na waumini 40. Alikuwa jaribu Kwa mchungaji wake ambaye hakuna na tatizo hata moja lakini na yeye baada ya kuwa mchungaji yamemshinda.
Huu ni mfano mmoja tu katika mifano mingi ya watu ambao hupenda kuwa jaribu Kwa watu lakini wao hawapendi kujaribiwa.

Najua kuna vitu unajifunza kupitia somo la leo, ila jua na hili kwamba;
 ''Mtu ajaribiwapo, asiseme, Ninajaribiwa na Mungu; maana Mungu hawezi kujaribiwa na maovu, wala yeye mwenyewe hamjaribu mtu.-Yakobo 1:13 '' 

 Asante kama unanielewa ndugu yangu.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.

Comments