KARAMA AMBAYO ANATAKIWA KUWA NAYO KILA MTEULE.


Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujfunze Neno la MUNGU la uzima.
Kila Mteule Wa KRISTO Ni Kuhani Kwa Maana Amekabidhiwa Siri Za Ufalme Wa MUNGU.
1 Kor 4:1 '' Mtu na atuhesabu hivi, kuwa tu watumishi wa KRISTO, na mawakili wa siri za MUNGU.''

Kumbe wateule wa KRISTO wote ni watumishi wa KRISTO na mawakili wa siri za MUNGU.
Kazi yetu ya uwakili iko katika kuipeleka injili ya KRISTO kwa watu wote.

Marko 16:15-16 ''Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. ''

Injili Ni Habari Njema Za Ufalme Wa MUNGU Hivyo Jukumu La Kutangaza Habari Njema Za Ufalme Wa MUNGU Ni La Wakristo Wote. 
Kuhubiri Injili Sio Kazi Ya Watu Fulani Tu Bali Ni Kazi Ya Wateule Wote. 
Ndugu, Timiza Wajibu Wako Kama Kuhani Na Mwana Wa Ufalme Wa MUNGU.

Dunia inahitaji wauhubiri injili lakini wakati mwingine hatutimizi malengo ya MUNGU sisi wateule ya kuitwa kwetu na MUNGU kwa sababu hatuipeleki injili yake kwa watu wote.
BWANA YESU anasema kwamba anao kondoo ambao ni sisi aliotuokoa lakini pia BWANA YESU anaendelea kusema kwamba kuna kondoo wengine hawako zizini sasa yaani hawako katika kanisa lake lakini inatupasa na hao kondoo walio nje tuwalete sisi ili BWANA YESU awaokoe.
BWANA YESU anasema;
 ''Na kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta; na sauti yangu wataisikia; kisha kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja.-Yohana 10:16''

Leo Watu Wanaotangaza Kwamba Hakuna Mtu Mtakatifu Duniani  Kwa Sababu Wao Binafsi Wamefeli Mtihani Wa Kuishi Maisha Matakatifu, Unahitajika wewe mteule wa KRISTO uwafundishe watu hao jinsi ya kuishi maisha matakatifu ambayo huanza kwa kumpokea YESU kama Mwokozi.
 Watakatifu Wapo Wengi Duniani Lakini Sizungumzii Wale Wanaopeana Vyeo Vya Utakatifu Wakati Sio Watakatifu Ila Nazungumzia Waliookolewa Kwa Damu Ya YESU Tena Wamezaliwa Mara Ya Pili Kwa ROHO MTAKATIFU Na Kwa Maji. Utakatifu Ni Kukamilishwa Na MUNGU Kupitia Wokovu Wa KRISTO. 
Ndugu, Ishi Maisha Matakatifu Maana Ndivyo Atakavyo MUNGU Muumbaji ili uwasaidie na wengine kuishi maisha matakatifu ya wokovu wa KRISTO.
 MUNGU Mwenyewe Anawatambulisha Watakatifu Walioko Duniani Kwamba Anapendezwa Sana Nao.
Zaburi 16:3 '' Watakatifu waliopo duniani ndio Walio bora, Hao ndio niliopendezwa nao. ''

 Kumbuka Nje Na Wokovu Wa KRISTO Hakuna Utakatifu Wala Mtakatifu, hivyo ukitaka kuishi maisha matakatifu unatakiwa kuokoka na kuanza kuishi maisha matakatifu.
Ukidhani unaishi maisha mataktifu lakini hujaokoka tambua kwamba wewe huishi maisha mataktifu ila unajifurahisha tu maana maisha matakatifu huanzia kuokoka kisha ukiokoka ROHO MTAKATIFU anakuja ndani yako na kukusaidia kuishi maisha matakatifu katika kusudi la MUNGU kama tu ukimtii ROHO MTAKATIFU.
Ili kudumu katika utakatifu ni lazima pia uwe mtu wa maombi na uwe unatendea kazi Neno la MUNGU unalojifunza. Kama huhudhurii ibada basi utapwaya kiroho hivyo inakupasa sana kuwa unahudhuria ibada katikati ya wiki na jumapili, hudhuria mikesha na jitoe kabasa maisha yako ili kumtumikia MUNGU na kumtukuza.
1 Petro 1:14-16 '' Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.''

Kwa sababu mteule wa MUNGU anatakiwa kuwa kielelezo cha matendo mema basi tena inampasa sana mteule huyo wa KRISTO kuipeleka injili ya KRISTO inayookoa kwa watu wote.
Ni kazi yako kuhubiri injili kwa watu wote.
MUNGU Haangalii Unahubiri Vipi Ila Anaangalia Unahubiri Nini Kisha Anaangalia Amekupa Nini.
 Je Unachohubiri Ndicho Ulichopewa Na KRISTO?
 Je Unahubiri Nini?
 Je Unalijua Kusudu La MUNGU Ndani Ya Hicho Unachohubiri?. Nimekupa Changamoto Ili Utende Vyema Katika Wito Wako Uliotiwa Na MUNGU Katika Injili Ya Wokovu Wa KRISTO.
Hutakiwi kunyamaza kuwashuhudia injili ndugu zako, wazazi wako au wafanyakazi wenzako. Kazi yako ni kuwaambia kwamba YESU anaokoa hivyo wampokee ili awaokoe na awatenge na ziwa la moto.
Hutakiwi kunyamaza ndugu, kuna sehemu umenyamaza na ndio maana kuna watu wanaendelea kuangamia. Usinyamaze tena wakati huu bali hubiri injili ya wokovu wa KRISTO siku zote.
Kuhubiri sio lazima maneno mengi bali hata maneno matatu yanatosha, hata  kuwapa watu vipeperushi vye neno la KRISTO inatosha sana, hata kumtumia tu mtu wimbo wa injili unaohubiri kweli ya MUNGU ni vyema sana, hata kuwaalika tu watu kanisani au kwenye mkutano wa injili au kwenye semina ni jambo jema sana.
Usinyamaze wakati huu ndugu yangu.
MUNGU amekupa agizo hivyo hakikisha unaipeleka injili yake kwa watu wote wanaokuzunguka. Kazi ya kuokoa ni ya MUNGU ila kazi yako wewe ni kuwaambia tu.
Usinyamaze ndugu yangu wakati huu bali ipeleke injili ya KRISTO.
Kama unaona huna nafasi au umebanana basi toa pesa yako ili walio tayari kuipeleka injili waipeleke na wewe utakuwa umehubiri injili kwa njia hiyo, dhawabu yako ya mhubiri wa injili iko pale pale maana umetoa pesa zako ili kuipeleka injili. Mpango wa MUNGU ni kwamba injili yake iende kwa watu wote.
Usinyamaze wakati huu ndugu.
Yeremia 47:7A Biblia inasema '' Utawezaje kutulia, Ikiwa BWANA amekupa agizo? ''
Na Yeremia 48:10A Biblia inasema '' Na alaaniwe mtu afanyaye kazi ya BWANA kwa ulegevu''

Ni jukumu lako mteule kuamua ama kumpendeza Mwokozi wako kwa kuipeleka injili yake au uamue kupendeza dunia kwa kukataa kuipeleka injili ya KRISTO huko duniani.
Maamuzi yako ndani yako ila mimi nakushauri ipeleke injili ndugu yangu.
 
Jambo jingine muhimu kujua ni kwamba Watumishi Wa MUNGU Wanaweza Wakabembeleza Lakini Neno La MUNGU Halibembelezi. 
Wachungaji Na Maaskofu Wanaweza Wakabembeleza Lakini Neno La MUNGU Halibembelezi. Wainjilisti, Mitume, Manabii Na Walimu Wanaweza Wakabembeleza Lakini Neno La MUNGU Halibembelezi. 
Ukipenda Sana Kubembelezwa Na Watumishi Utakuwa Na Ugumu Sana Kwenye Wokovu Wako. Lakini Kwa Sababu Neno La MUNGU Halibembelezi Litii Hilo Utaona Wepesi Kwenye Wokovu Wako Ulio Wa Thamani Sana.

Wakolosai 4:5-6 ''Enendeni kwa hekima mbele yao walio nje, mkiukomboa wakati. Maneno yenu yawe na neema siku zote, yakikolea munyu, mpate kujua jinsi iwapasavyo kumjibu kila mtu.'' 

  Pia ni lazima sana kwa Wateule  Kujua Kwamba Karama Au Vipawa Tulivyopewa Na MUNGU Havitakiwi kutufanya Tujidai, Tujisifu Au Tujiinue Bali Karama Zetu Zinatakiwa Zitufanye Tumwinue KRISTO Aliyetupa Karama Hizo. Inatakiwa Kupitia Karama Yako KRISTO Atukuzwe Na Sio Wewe Kujitukuza. 

Wafilipi 2:3-11 '' Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake. Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine. Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya KRISTO YESU; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya MUNGU, naye hakuona kule kuwa sawa na MUNGU kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu;  tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.
  Kwa hiyo tena MUNGU alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la YESU kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa MUNGU Baba. ''


 Jambo la jingine muhimu kujua ni hili; Ni Hatari Sana Kuweka Miujiza Mbele Ya Injili. 
Miujiza Inatakiwa Iwe Matokeo Ya Injili Na Sio Injili Kuwa Matokeo Ya Miujiza. 
Ni Vyema Tukawaite Watu Waje Wafunguliwe Na Neno La MUNGU Kuliko Kuwaita Watu Waje Kupokea Miujiza Yao Tu. Ukweli Ni Kwamba Tukiwaita Watu Waje Kwenye Injili Miujiza Wataipata Tu Kama Wakiitii Injili Hiyo Ya KRISTO. Injili Ina nguvu Ya Kuokoa Iwepo Miujiza Au Isiwepo. 
Injili Inaweza Kuzaa Uzima Wa Milele Lakini Miujiza Tu Haiwezi Kuleta Uzima Wa Milele Kwa Mtu

 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili

Comments