KAZI SABA(7)ZA MAADUI ZAKO WA KIROHO KWAKO NI:

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu. 
Karibu tujifunze mambo ya kutusaidia kiroho.
Sijui kama unafahamu kwamba una maadui katika ulimwengu wa roho ambao hupanga mipango yao kipepo dhidi yako ili tu kukuletea madhara. Kama hujanielewa ngoja nianze hivi;
Adui ni nini?
Kuna maana mbili za Neno adui.
Adui ni  mtu au kiumbe  yeyote anayemtendea mwingine uovu.  
Maana ya pili ya neno adui ni Mshindani anayeshindana na wewe ili ukose kitu fulani muhimu kwako au maishani mwako.
Nadhani sasa umenielewa, hivyo tunavyoendelea kujifunza somo hili nakuombea kwa MUNGU upate ufahamu utakaokusaidia kuwadhibiti maadui zako wote katika ulimwengu wa roho. Hakuna njia nyingine ya kuwashinda maadui zako kiroho ila ushindi wako pekee utaupata kupitia Jina la YESU KRISTO, Damu ya YESU KRISTO, Nguvu za ROHO MTAKATIFU  na Neno la MUNGU.
 Na vyote hivyo hutenda kazi katika maombi na utakatifu wa kweli.
Najua kabisa kuna maadui wengi MUNGU huwa anakupa kuwajua kupitia ndoto na maono lakini huombi inavyotakiwa ndio maana huwa wanakushinda. Leo haribu chanzo na sio kuharibu tukio. Ukimharibu anayekutumia majini utashinda zaidi kuliko kuyaharibu tu majini yanayotumwa kwako, maana utayaharibu lakini kesho yatatumwa mengine maana mtumaji hujamharibu. 

Biblia inasema kuhusu maadui hao kwamba;
 ''Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za MUNGU, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.-Waefeso 6:12-13 ''  

Leo nazungumzia maadui waliozungumzwa na Biblia ambao ni;
=Falme za shetani ambazo huwakilisha roho za kishetani zote ambazo hutumwa kwako ili kukutawala kipepo.
=Mamlaka za kishetani ambazo huwakilisha utawala wa shetani kupitia wanadamu walio upande wa shetani dhidi yako.
=Wakuu wa giza ambao ni wachawi, waganga wa kienyeji, wasoma nyota, wasihiri, wasoma bao na kila mfanyakazi wa shetani.
=Majeshi ya pepo wabaya ambayo ni majini yote, mizimu  na kila roho za kishetani.

Hayo ndio makundi manne ya maadui ambao wanaweza kushindana na wewe ili kukuharibia.
roho hizo za shetani hutumiwa wanadamu hivyo utamuona mwanadamu akitumika kipepo dhidi yako ili kukuharibia kumbe amebeba roho ya shetani. Pambana na ushetani huo ili uwe huru.


Kuna kazi saba nimeziandaa ambazo huzitumia sana maadui zako ili kukudhuru au kukuharibia hivyo omba maombi kupitia jina la YESU KRISTO ukienda kinyume na kila kazi za maadui zako kiroho ambazo nimezitaja katika somo hili.

 Kazi saba za maadui zako kiroho ni;

1. Kukudhoofisha na Kukudhuru kiroho.

Zaburi 69:4 ''Wanaonichukia bure ni wengi Kuliko nywele za kichwa changu. Watakao kunikatilia mbali wamekuwa hodari, Adui zangu kwa sababu isiyo kweli. Hata mimi nalilipishwa kwa nguvu Vitu nisivyovichukua.''

 Andiko hili linathibitisha jinsi ambavyo wakati mwingine unaweza ukajikuta una maadui wengi wenye lengo la kukudhoofisha au kukudhuru.
Ukitumiwa roho ya magonjwa au ukipangiwa ajali kiroho maana yake maadui zako hao waliotuma mipango hiyo ya kishetani lengo lao ni kukudhoofisha au kukudhuru au kukuharibia katika eneo walilokusudia. Ukiugua muda mrefu ugonjwa ambao hata vipimo havionyeshi basi kama unafanya kazi itapelekea hata bosi wako kukuachisha kazi hivyo maadui zako wanakuwa wamefaulu katika kukudhoofisha maana hutakuwa na kazi na utayumba kiuchumi, huo ni mfano mmoja tu katika mifano mingi ya kazi za maadui zao. Kazi yako sio uwachukie bali mwite YESU asiyeshindwa ili aje akushindie. Wewe kupata ajali sio kusudi la MUNGU, Wewe kuumwa umwa sio mpango wa MUNGU, Wewe kuteseka wala sio mpango wa MUNGU. Hujasimama katika zamu yako katika maombi na utakatifu ndio maana mabaya hayo yanakupata. MUNGU hapendi wewe uteseke ndivyo neno lake linasema.
Biblia inasema kwamba,  
''Maana(MUNGU) moyo wake hapendi kuwatesa wanadamu. Wala kuwahuzunisha.-Maombolezo 3:33''

2. Kukuibia au kukuondolea  baraka uliyonayo.

Kutoka 15:9 ''Adui akasema, Nitafuatia, nitapata, nitagawanya nyara, Nafsi yangu itashibishwa na wao; Nitaufuta upanga wangu, mkono wangu utawaangamiza.'' 

Andiko hili linaonyesha jinsi ambavyo adui zako hupanga mipango yao juu  yako. huwezi kuwazuia kupanga mipango yao lakini wewe mwite YESU KRISTO katika maombi yako ili yeye YESU awaabishe maadui zako na mipango yao. Ni kweli wanapanga kukuibia, kukunyang'anya baraka zako na vitu vyako.
Nimewahi kushuhudia binti mmoja aliyekuwa ana akili sana darasani lakini siku ya mitihani kuanza ilipofika  aliugua ghafla ugonjwa usiojulikana na akalazwa. Adui anajua kwamba huyu binti atafaulu mitihani hivyo atakuja kupata kazi nzuri, adui akamuondolea baraka hiyo ya kufaulu mitihani. Ndugu zangu tunatakiwa tuombe sana na mipango yetu yote tuifunike kwa damu ya YESU KRISTO. Ndoa yako ifunike kwa damu ya YESU KRISTO. Shetani anaweza akaiba furaha ya ndoa yenu ndio maana sasa kila siku mnabigana makofi tu na mateke, furaha haipo tena. Maombi yanaweza kuirudisha furaha hiyo kwa jina la YESU KRISTO. Wokovu wa KRISTO, Utakatifu na maombi ndivyo pekee vinavyohitajika.
Wakati mwingine unapopanga mipango yako mizuri ndivyo adui zako pia wanapopanga mipango mibaya kinyume na mipango yako, usipomkabidhi BWANA YESU mipango yako hakika adui anaweza kukushinda.
BWANA YESU anasema;
'' Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili BABA atukuzwe ndani ya Mwana. -Yohana 14:13''

3.Kukuchonganisha na watu muhimu kwako.

Mithali 30:10 ''Usimchongee mtumwa kwa bwana wake; Asije akakulaani, ukaonekana una hatia.''

Kuna watu leo wameachishwa kazi kwa sababu tu ya uchonganishi uliofanywa na maadui zao.
Kuna watu hawajapanda vyeo miaka mingi sana kwa sababu tu ya uongo uliopenyezwa na adui zao katika ulimwengu wa roho.
Kuna familia zina migogoro kwa sababu ya uchonganishi uliofanywa kipepo na maadui.
Kuna huduma njema zinazomhubiri KRISTO kwa usahihi kabisa ila hazikui kwa sababu ya uongo ulifanywa na wakala wa shetani dhidi ya huduma hizo.
Kuna watu hawasalimiani, kuna familia hazisalimiani kwa sababu tu ya kazi ya shetani ya kuchonganisha.
Kuna watu wameachwa na wachumba zao kwa sababu tu ya uchonganishi uliowafanywa na mawakala wa shetani. Ndugu yangu futa maneno yote mabaya uliyonenewa, funga vinywa vyote vya kipepo vinavyotamka jambo kukuhusu, funga kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Mpinge shetani kwa maombi hakika atakukimbia.
Mwite BWANA YESU utashinda na zaidi ya kushinda.

4. Kukulaani.


 Zaburi 10:7 ''Kinywa chake kimejaa laana, Na hila na dhuluma. Chini ya ulimi wake kuna madhara na uovu,''

Laana ni kitu ambacho kinakushikilia kipepo ili usifanikiwe katika jambo fulani zuri maishani mwako.
Kazi ya maadui zako ni kukulaani ili tu usifanikiwe au usifikie viwango uvitakavyo.
Laana ni apizo ambalo linatolewa na adui zako ili yakufike mabaya.
Kukulaani maana yake ni kukuombea maovu.
Kuna watu wanatembea katika laana mbalimbali.
Unaweza kuwa umetokea katika familia iliyolaaniwa.
Kazi mojawapo ya BWANA YESU ili kufuta laana zote zinazokutesa, Mkimbilie YESU tu na laana hizo zitaondoka.
Hakuna laana ambayo haiwezi kufutika katika damu ya YESU.
Damu ya YESU ndio mwisho wa laana zote, itumie damu ya YESU katika maombi na laana zote zitaondoka katika maisha yako.
Kumbuka laana ni kitu kinachokushikilia kipepo. Umasikini unaweza kukushikilia kipepo kiasi kwamba kila ukijaribu kujinasua basi unarudi tena kwenye umaskini huo, huo ni mfano mmoja katika mifano hai mingi ya jinsi laana inavyoweza kutesa maisha yako.


5. Kutamani upatwe na mabaya siku zote.


Isaya 59:3 ''Kwa maana mikono yenu imetiwa unajisi kwa damu, na vidole vyenu vimetiwa unajisi kwa uovu; midomo yenu imenena uongo, ndimi zenu zimenong'ona ubaya.''



Dalili rahisi zaidi ya kumjua adui yako ni pale ambapo utapatwa na mabaya yeye atacheka na kufurahi.
Kazi ya adui zako kiroho.ni kutamani wewe upatwe na mabaya.
Kama mtu anatamani upatwe na mabaya basi tambua kabisa kwamba mtu kama huyo hukuombea wewe mabaya yakupate.
Kazi yako ni kufuta kila baya lililotamkwa kukuhusu. Tumia damu ya YESU na jina la YESU kufuta kila maneno mabaya yanayonenwa kukuhusu wewe.
Ukiomba kupitia jina la YESU neno la MUNGU linakupa ushindi wa ajabu sana dhidi ya adui zako, Neno linasema 
 '' Adui zangu wote wataaibika na kufadhaika, Watarudi nyuma, kwa ghafula wataaibika.-Zaburi 6:10 ''

6. Kukuondoa kwenye kusudi la MUNGU.


Mathayo 24:24 '' Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule.''


Adui yako mkuu kwenye ulimwengu wa roho ni shetani ambaye naye ana mawakala zake ambao na wao lengo lao ni moja tu yaani kukuondoa katika kusudi la MUNGU.
Hapo juu mwanzoni mwa somo tumeona maadui zako ambao wanafanya kazi ya shetani dhidi ya maisha yako. Japokuwa adui zako hao hupanga mengi mabaya kukuhusu lakini naomba utambue kwamba lengo lao la kwanza ni kuhakikisha wewe unapishana na kusudi la MUNGU maishani mwako.
Kusudi la MUNGU la kwanza ni wewe uokoke na uishi maisha matakatifu katika YESU KRISTO. shetani hutaka sana uondoke kwa YESU ili ukose uzima wa milele. Hizi ni siku za mwisho ambazo manabii wa uongo na wafanya kazi wa shetani watakuwa wengi, lengo lao ni moja tu yaani wakutoe katika wokovu wa KRISTO ulio wa thamani sana.
Ukiona Mchungaji yeyote anahubiri watu waondoke kwa YESU huyo ni nabii wa uongo na muone kana tu anayetumika kipepo, yaani yuko upande wa adui wako wa kiroho.
Ukiona Askofu au padri au mzee wa kanisa anakataza watu kuokoka, huyo muone kwamba anatumika kipepo dhidi yako, huyo yuko upande wa adui. BWANA YESU alikuja ili tuokoke hivyo ukiona mtu anakuondoa katika Wokovu wa BWANA YESU basi tambua kwamba huyo anatumika kipepo dhidi yako.
YESU anaokoa hivyo hakuna haja ya kukataa Wokovu wake.
Yeye BWANA YESU anasema'
'' Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. -Mathayo 11:28''

Maadui tu ndio wanaoweza kukuondoa kwa YESU hivyo wapinge hadharani na wapinge kwa maombi siku zote, ukinyamazisha mipango yao kwa jina la YESU KRISTO.

7.Kwenda kwa waganga na wachawi kwa ajili yako ili kukudhuru.


Zaburi  58:5-11 '' Asiyeisikiliza sauti ya waganga, Ijapo wanafanya uganga kwa ustadi. Ee MUNGU, uyavunje meno yao vinywani mwao; Ee BWANA, uyavunje magego ya wana-simba. Na watoweke kama maji yapitayo kwa kasi; Akiielekeza mishale yake, iwe imetiwa ubutu. Kama konokono ayeyukaye na kutoweka, Kama mimba iliyoharibika, isiyoliona jua, Kabla ya masufuria yenu kupata moto wa miiba, Ataipeperusha kama chamchela, Iliyo mibichi na iliyo moto. Mwenye haki atafurahi akionapo kisasi; Ataiosha miguu yake katika damu ya wasio haki. Na mwanadamu atasema, Hakika iko thawabu yake mwenye haki. Hakika yuko MUNGU Anayehukumu katika dunia.''

Yuko MUNGU anayehukumu katika dunia.
Ni kweli wamekuendea kwa waganga na kwa wachawi, wewe wala usiogope kazi zao hizo ila mwite BWANA YESU awahukumu na kazi zao.
Adui zako ni kweli kabisa wanakuendea kwa waganga lakini wewe waendee kwa YESU na wataabibika na uganga wao.
Jina la YESU ukilitumia katika maombi litawaharibu waganga na uganga wao, litawaharibu wachawi na uchawi wao, litawaharibu washirikiana na ushirikina wao na litawaharibu wakuu wa giza na hiza lao.
 
Lakini licha ya maadui zako kukupanga mabaya juu yako lakini  liko jina la YESU KRISTO lenye uzima na ushindi kwako. Ni jukumu lako kumpokea BWANA YESU na kisha kuishi maisha matakatifu harafu omba maana adui hao watakuogopa maana kila watakalolipanga likupate wewe litawapata wao.
Yeremia 1:19 ''Nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, asema BWANA, ili nikuokoe. ''
 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili

Comments