NI HERI KUISHINDA DHAMBI KULIKO IKUSHINDE WEWE.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.


BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Dhambi ikifika mlangoni imekaribia kukunasa, ikikunasa ni ngumu sana kuiondoa.
Dhambi haimwachi mtu ina mtu ndio anaiacha dhambi.
Kama unafanya dhambi ukitarajia dhambi ikuache tambua kwamba dhambi haitakuacha kamwe ila ni wewe unawezeza kuiacha kama ukiamua.
Naomba amua kuacha dhambi na utabarikiwa.

Ni heri kuishinda dhambi kuliko dhambi ikushinde wewe.

2 Petro 2:14,21--22 '' wenye macho yajaayo uzinzi, watu wasiokoma kutenda dhambi, wenye kuhadaa roho zisizo imara, wenye mioyo iliyozoezwa kutamani, wana wa laana; Kwa maana wale waliokwisha kuyakimbia machafu ya dunia kwa kumjua BWANA na Mwokozi Yesu KRISTO, kama wakinaswa tena na kushindwa, hali yao ya mwisho imekuwa mbaya kuliko ile ya kwanza. Maana ingekuwa heri kwao kama wasingaliijua njia ya haki, kuliko kuijua, kisha kuiacha ile amri takatifu waliyopewa.
  Lakini imetukia kwao sawasawa na ile mithali ya kweli, Mbwa ameyarudia matapiko yake mwenyewe, na nguruwe aliyeoshwa amerudi kugaa-gaa matopeni. ''


Dhambi ni mbaya sana  na imewarudisha nyuma watu wa MUNGU wengi.
 Wengine baada ya wao kurudi nyuma waliamua kuwarudisha nyuma na wapendwa wao.
Dhambi imewafanya baadhi ya watu kuliona Neno la MUNGU kuwa ni kitu tu cha kawaida na cha kupita.
Ni heri kuishinda dhambi kuliko dhambi ikushinde wewe.
Hakikisha haipo dhambi ya kukushinda ndugu yangu.
Hakikisha unashinda dhambi zote. Usishinde uongo tu huku uzinzi umekushinda kuushinda.
Usishinde kiburi tu huku usengenyaji hujaushinda.
Shinda dhambi zote ndugu yangu.
 Ni heri kuishinda dhambi kuliko dhambi ikushinde wewe.
Usishinde rushwa tu huku tamaa mbaya hujaishinda bali shinda dhambi zote.
Usishinde pombe na ulevi tu huku usaliti hujaushinda. Bali shinda dhambi zote.

Ni heri kuishinda dhambi kuliko dhambi ikushinde wewe. Usishinde Bangi tu na sigara bali shinda hata uchonganishi.
Usishinde uasherati tu bali shinda na kuabudu sanamu.

Ni heri kuishinda dhambi kuliko dhambi ikushinde wewe.

 ''Mkaribieni MUNGU, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili. Huzunikeni na kuomboleza na kulia. Kucheka kwenu na kugeuzwe kuwa kuomboleza, na furaha yenu kuwa hamu. Jidhilini mbele za BWANA, naye atawakuza.-Yakobo 4:8-10''

Tumeitwa na MUNGU kwa ajili ya mambo mawili tu.

1. kuishi maisha matakatifu ndani ya KRISTO.
1 Petro 1:14-16 ''Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.'' 

2. kumtumikia KRISTO kwa kuipeleka injili yake kwa watu wote duniani.

Marko 16:15-16 ''Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.''

  Hayo ndio majukumu mawili muhimu ambayo kila mteule wa MUNGU amepewa. Hivyo dhambi haitakiwi kuwa kazi yetu ya kuiishi bali utakatifu ndio kazi yetu kuiishi duniani. 
Leo watu wengi wameamua kujitenga na kanisa la MUNGU kwa sababu tu hawawezi kuacha dhambi.
Dada aliyezoea kuvaa nusu uchi ni ni ngumu kutulia kanisani maana ataona kama anakosa uhuru kumbe ni shetani anamdanganya.
 Ni heri kuishinda dhambi kuliko dhambi ikushinde wewe.
Baba mmoja alisumbuliwa sana na magonjwa. Baadae akagundua kwamba msaada wake ni kwa YESU tu. Akaja kanisani na tukamuombea, Wakati nimemuwekea mkono mimi huku nikikemea madhabahu za kishetani zilizomfunga zibomoke na kuanguka ili awe huru, ndugu mmoja wa kanisani ambaye alikuwa pembeni ya mgonjwa akaja na kuninong'oneza masikioni akisema ''Huyo mgonjwa amepona maana nimeona kiti kikiwa nyumbani kwake na katika kiti kile amekaa mtu kama mganga wa kienyeji akiwa na zana zake lakini ulipokemea nikaona upanga ukimkata katikati na kukipasua kiti ndipo huku huyo mgonjwa akadondoka chini, hivyo amepona''  
Baada ya ndugu yule kuniambia hivyo niliacha kukemea na nikamwambia yule mgonjwa anajisikiaje akasema amepona. Kisha nikamwambia yale yaliyotokea akashangaa sana na kusema kwamba ni kweli zamani aliwahi kwenda kwa mganga na kupewa kiti akiambiwa kwamba kiti kile asikalie mtu yeyote, alifanya siri sana na anashangaa watu wa kanisa tumejua. Yule mzee aliapa kuanzia siku hiyo kwamba ataambatana na YESU tu. Mchungaji wetu akamuongoza sala ya toba upya na yule mzee akawa na juhudi sana kanisani, akapona na akawa anamshukuru MUNGU kila mara. Baada ya kupona kabisa hata uchumi wake ukawa mzuri ndipo alipogeuka tena na kuacha kuja kanisani. Baada ya muda akawa hata ananikwepa kila akiniona. Dhambi ni mbaya na adui alikuwa anamrudisha kwenye mamlaka yake taratibu. Ni wengi sana leo ambao husahau fadhili za MUNGU baada tu ya MUNGU kuwabariki au kuwaponya.

Ni heri kuishinda dhambi kuliko dhambi ikushinde wewe.
Ndugu zangu dhambi haitakiwi kutushinda bali yatupasa tuishinde.
Kutokaa kwenye Neno la MUNGU ni kuikaribisha dhambi.
Dhambi huwa inashindwa kwa Neno la MUNGU tu na maamuzi ya kuiacha na sio kwa viboko.
Mathayo 3:2 '' Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.'' 

Hata kama ungechapwa viboko elfu moja lakini dhambi yako kama iko iko tu. Dhambi unaweza kuishinda kwa Neno la MUNGU tu na maamuzi ya kuiacha.
 Ni heri kuishinda dhambi kuliko dhambi ikushinde wewe.
ndugu mmoja alikuwa anatembea na waume za watu. Siku moja mumewe alimfumania na kumtembeza uchi mitaani labda ataacha lakini hata miezi miwili haikuisha yule mama akakamatwa tena akiisaliti ndoa yake.
 Ni heri kuishinda dhambi kuliko dhambi ikushinde wewe.
Baba mmoja naye alifumaniwa na mke wa mtu, akapiga na kutolewa meno kadhaa. Watu wakadhani labda ataacha uzinifu wake lakini hata miezi mitatu haikuisha akakamatwa tena na kupigia na kuumizwa vibaya sana lakini baada ya miezi miwili alizini tena.

Ni heri kuishinda dhambi kuliko dhambi ikushinde wewe.
  Ndugu zangu dhambi huwa hitoki kwa sababu ya adhabu za kibinadamu ila dhambi itatoka kwa mtu husika kuamua kuikataa jehanamu na kuuchagua uzima wa milele ulio katika KRISTO YESU.
Warumi 6:23 ''3 Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika KRISTO YESU Bwana wetu.''

 Kuna dhambi kama umeshindwa kuiacha nakuomba okoka sasa na anza kuliruhusu Neno la MUNGU likutawale na kukuongoza.
Kudumu katika dhambi ni kujinunulia eneo kabisa katika jehanamu ya moto.
Kushikilia dhambi ni kushikilia kifo chako cha kiroho na hata kimwili wakati mwingine.
 Ni heri kuishinda dhambi kuliko dhambi ikushinde wewe.
1 Tiomotheo 5:24 ''Dhambi za watu wengine zi dhahiri, zatangulia kwenda hukumuni; wengine dhambi zao zawafuata.'

Jambo ambalo  MUNGU halitaki kwako ni dhambi.
Mpendeze MUNGU Muumbaji wako kwa kuiacha dhambi na kujitenga na dhambi.
Vunja urafiki na shetani.
Vunja urafiki na marafiki wanaokushawishi uingie katika dhambi.
 Ni heri kuishinda dhambi kuliko dhambi ikushinde wewe.
Amua tu kuishi maisha safi ya wokovu wa KRISTO.
MUNGU anahitaji kwako utakatifu.
Dhambi hazitakufikisha popote ndugu yangu.
Hakuna faida hata moja katika kutenda dhambi.
Mbinguni hataingia mwenye dhambi bali waliotubu na kuishi maisha matakatifu katika wokovu wa KRISTO.
Usifanye wema wa dhambi kwa watu bali ni heri wakakuchukia kwa sababu tu unakemea dhambi zao na kwa sababu tu una msimamo thabiti katika KRISTO YESU.

Waefeso 1:5-13 ''Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya YESU KRISTO, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake.  Na usifiwe utukufu wa neema yake, ambayo ametuneemesha katika huyo Mpendwa(YESU). Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake. Naye alituzidishia hiyo katika hekima yote na ujuzi; akiisha kutujulisha siri ya mapenzi yake, sawasawa na uradhi wake, alioukusudia katika yeye huyo. Yaani, kuleta madaraka ya wakati mkamilifu atavijumlisha vitu vyote katika KRISTO, vitu vya mbinguni na vitu vya duniani pia. Naam, katika yeye huyo; na ndani yake sisi nasi tulifanywa urithi, huku tukichaguliwa tangu awali sawasawa na kusudi lake yeye, ambaye hufanya mambo yote kwa shauri la mapenzi yake. Nasi katika huyo tupate kuwa sifa ya utukufu wake, sisi tuliotangulia kumwekea KRISTO tumaini letu. Nanyi pia katika huyo mmekwisha kulisikia neno la kweli, habari njema za wokovu wenu; tena mmekwisha kumwamini yeye, na kutiwa muhuri na ROHO yule wa ahadi aliye Mtakatifu. '' 
 
Wewe ni wa thamani sana mbele za MUNGU ndio maana MUNGU anataka uishi maisha matakatifu katika Mwanye YESU KRISTO ili uwe na sehemu katika uzima wa milele.
Ziko taji mbinguni ambazo zinawangoja tu watakatifu walioshinda duniani, hakikisha unakuwa mmoja wao kwa kuiacha dhambi na kuishi maisha ya wokovu.
Ni heri kuishinda dhambi kuliko dhambi ikushinde wewe.
Kazi ya YESU aliyoifanya msalabani ni kuhakikisha wewe huingii ziwa la moto bali unaingia katika uzima wa milele, ni kazi yako tu kumpokea kama Mwokozi wako na kuishi maisha mataaktifu katika yeye.

Ni heri kuishinda dhambi kuliko dhambi ikushinde wewe.
 Ndugu wala hujachelewa, acha tu dhambi na tubu kwa BWANA YESU na yeye atakusamehe dhambi zako zote.
Hakuna dhambi isiyosameheka hivyo kimbilia tu kanisani na ukamue kuokoka na MUNGU atakubariki sana.
Kwenye dhambi umepoteza pesa zako tu wala kuhupata faida.
Kuna wengine kwenye dhambi wameambulia magonjwa tu na sasa wanajuta. Ndugu hujachelewa maana BWANA YESU anakuhitaji leo ili uingie katika kundi la watakatifu waliosafishwa kwa damu yake ya thamani sana.

Wakolosai 1:12-14 ''mkimshukuru BABA, aliyewastahilisha kupokea sehemu ya urithi wa watakatifu katika nuru. Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi;''
 
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili

Comments