SABABU SABA(7) ZA MUNGU KUKUITA WEWE.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la uzima.
 Waliompokea YESU hao wameitikia wito wa kuitwa kwao na MUNGU lakini mambo haya saba ni ya lazima kwa kila aliyeitwa na MUNGU.

1. MUNGU anakuita ili upate wokovu wake.

1 Timotheo 2:3-4 ''Hili ni zuri, nalo lakubalika mbele za Mungu Mwokozi wetu; ambaye hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli.''
Wokovu ni mpango wa MUNGU kumuokoa mwanadamu.
Kupata wokovu wa MUNGU maana yake ni kuokoka.
MUNGU ameandaa njia moja tu ya wokovu ambayo ni kupitia Mwanaye YESU KRISTO ambaye ndiye Mwokozi.
Anayemkataa YESU maana yake ameukataa wito wa MUNGU.
Anayemkataa YESU maana yake amemkataa MUNGU.
Yohana 3:18 ''Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU.''
 Aliye kwa YESU yeyote ni lazima sana ampokee YESU kama Mwokozi wake, huko ndiko kuitikia Wito wa MUNGU.
Kama wewe unaenda tu kanisani lakini hujaokoka maana yake wewe hujaitikia wito wa MUNGU kukuita wewe.

2. MUNGU anakuita ili uwe safi na sio mchafu tena.

Mathayo 5:8 '' Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona MUNGU.''
Wenye mioyo safi hao ni watakatifu.
Usafi ni hali ya kutokuwa na uchafu.
Wenye moyo safi ni wale waliotakaswa kwa damu ya YESU na wanaishi maisha matakatifu ya wokovu wa KRISTO.
Njia ya kuitikia wito wa MUNGU kwako unatakiwa uwe safi na sio mchafu. Msafi ni yule anatetubu kisha anaanza kuishi maisha matakatifu katika KRISTO.
Yakobo  4:8-10 ''Mkaribieni MUNGU, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili. Huzunikeni na kuomboleza na kulia. Kucheka kwenu na kugeuzwe kuwa kuomboleza, na furaha yenu kuwa hamu. Jidhilini mbele za BWANA, naye atawakuza.'

Hivyo mtu anayetubu dhambi zake na kuziacha huyo ndiye aliyeitikia wito wa MUNGU wa kuitwa kwa mtu huyo na MUNGU.
Kama uko kanisani lakini hujatubu dhambi zako wala hujaziacha, wewe hujaitikia wito wa MUNGU wa kukuita.


 3. MUNGU anakuita ili uwe mtumishi wake.

Kumb 10:12 '' Na sasa, Israeli, BWANA, Mungu wako, anataka nini kwako, ila umche BWANA, Mungu wako, na kwenda katika njia zake zote, na kumpenda, na kumtumikia BWANA, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote; ''

Waisraeli walitwa na MUNGU kama vile ambavyo mimi na wewe kama kanisa tumeitwa na MUNGU.
Kuitwa na MUNGU ili umtumikie maana yake umwabudu yeye kisha ufanye kusudi lake.
Kufanya matendo mema aliyokuagiza MUNGU huko ndiko kumtumikia.
Wanaomwabudu MUNGU katika KRISTO na kutenda mema na kufanya kazi yake, hao ndio wameitika wito wa kuitwa kwao na MUNGU.
1 Kor 4:1 ''Mtu na atuhesabu hivi, kuwa tu watumishi wa KRISTO, na mawakili wa siri za MUNGU.''

 4. MUNGU anakuita ili umwabudu katika roho na kweli.

Yohana 4:24 '' MUNGU ni ROHO, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.''
Kuna maana mbili za neno Kuabdudu.
A. Kuabudu ni kuomba au kufanya ibada  kwa unyenyekevu mkubwa kwa MUNGU.
B. Kuabdudu ni kupenda kitu kupita kiasi.
Ni heri tukampenda MUNGU kupita kiasi na tukajishughulisha katika kazi yake, huko ndio kumwabudu MUNGU.
Kumpokea YESU kama Mwokozi wako ndio mwanzo wa kumwabudu MUNGU .
Baada ya kuokoka unatakiwa umwabudu MUNGU katika roho na kweli.
Wanaomwabudu MUNGU katika roho na kweli hao ndio wameitikia wito wa MUNGU wa kuitwa kwao na MUNGU.
Hatutakiwi kumwabudu MUNGU katika roho zetu tu bali ni muhimu pia kumwabudu MUNGU katika ROHO MTAKATIFU .
Turuhusu ROHO MTAKATIFU atutawale hapo ndipo roho zetu zitajua kumwabudu MUNGU katika roho na kweli.
Kama wewe humwabudu MUNGU katika roho na kweli hakika wewe bado hujaitikia wito wa kuitwa kwako na MUNGU, Hata kama kanisani unaenda.
Zaburi 96:7-9 '' Mpeni BWANA, enyi jamaa za watu, Mpeni BWANA utukufu na nguvu. Mpeni BWANA utukufu wa jina lake, Leteni sadaka mkaziingie nyua zake. Mwabuduni BWANA kwa uzuri wa utakatifu, Tetemekeni mbele zake, nchi yote.''

5.  MUNGU anakuita ili uwe mtakatifu.
 
 Waefeso 1:4-5 '' kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo. Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake.''
 Mtakatifu ni mtu aliyetakaswa dhambi zake na makosa yake.
Kutakasa maana yake ni kusafisha hivyo walio watakatifu kwa MUNGU ni wale tu ambao wametakaswa na damu ya YESU.

Watakatifu ni wale waliosafishwa kwa damu ya YESU.
Watakatifu ni wakristo waliotengwa na MUNGU ili waliishi kusudi lake.
2 Kor 7:1 '' Basi, wapenzi wangu, kwa kuwa tuna ahadi hizo, na tujitakase nafsi zetu na uchafu wote wa mwili na roho, huku tukitimiza utakatifu katika kumcha MUNGU.''
Anayeishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO huyo ndiye aliyeitikia wito wa MUNGU.
Ni vyema sana kuishi maisha ya utakaso.
Ni muhimu sana kujitakasa kila siku na kuacha uovu wote na kujitenga na kila dhambi.
Wanaoishi maisha ya utakaso hao ndio walioitikia wito wa MUNGU wa kuitwa kwao.
 1 Petro 1:15 '' bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;''
 Kama wewe huishi maisha matakatifu katika KRISTO hakika wewe hujaitikia wito wa MUNGU kukuita.
Kama wewe ni kiongozi kanisani au mwimbaji au muumini mzuri, hata kama una upako kiasi gani lakini kama huishi maisha matakatifu ya wokovu wa KRISTO hakika wewe bado hujaitikia wito wa MUNGU wa kukuita wewe.

6. MUNGU anakuita ili uwe mwenye haki.

 1 Yohana 2:29 ''Kama mkijua ya kuwa yeye ni mwenye haki, jueni ya kuwa kila atendaye haki amezaliwa na yeye.''
YESU ni mwenye haki hivyo wewe ukiishi maisha ya haki hakika hakika utakuwa unatokana na KRISTO.
Ukiishi maisha ya haki utakuwa umeitikia wito wa MUNGU kukuita.
Maisha ya haki ni maisha ya kuishi kwa kufuata kanuni ya MUNGU ambayo ni Neno la MUNGU.

1 Petro 3:12-13 '' Kwa kuwa macho ya BWANA  huwaelekea wenye haki, Na masikio yake husikiliza maombi yao; Bali uso wa BWANA ni juu ya watenda mabaya. Naye ni nani atakayewadhuru, mkiwa wenye juhudi katika mema? ''
Ni lazima sana kuishi maisha ya haki kwa MUNGU na kwa wanadamu.
Mteule hutakiwi kutoa wala kupokea rushwa, Hayo sio maisha ya haki.
Mteule hutakiwi kuonea mtu au kumsingizia, hayo sio maisha ya haki.
Mteule hutakiwi kusengenya watu, hayo sio maisha ya haki.
Mteule hutakiwi kuiba wala kuzomea watu, hayo sio maisha ya haki.

Wafilipi 1:10-11 '' mpate kuyakubali yaliyo mema; ili mpate kuwa na mioyo safi, bila kosa, mpaka siku ya KRISTO; hali mmejazwa matunda ya haki, kwa njia ya YESU KRISTO, kwa utukufu na sifa ya MUNGU.'' 

7. MUNGU anakuita ili uwe na yeye milele.

1 Thesalonike 4:16-17 '' Kwa sababu BWANA mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya MUNGU; nao waliokufa katika KRISTO watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki BWANA hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na BWANA milele.''
 
Kufanya mambo sita Tuliyoaanza nayo katika somo hili hapo juu kutatengeneza jambo la saba ambalo ni MUNGU kuwa na wewe milele.
Ni muhimu sana mimi na wewe tufikie hatui hii ya kuwa na MUNGU milele.
Lakini ili tufikie hatua ya kuishi na MUNGU ni kwanza lazima.
=Tuitikie wito wa MUNGU wa Wokovu.
=Ni lazima tuitikie wito wa MUNGU wa sisi kuishi maisha safi.
=Ni lazima tuitikie wito wa kumtumikia MUNGU.
=Ni lazima tuitikie wito wa MUNGU wa sisi kumwabudu yeye katika roho na kweli.
=Ni lazima tuitikie wito wa MUNGU wa sisi kuwa watakatifu.
=Na ni lazima sisi tuitikie wito wa MUNGU wa sisi kuishi maisha ya haki.
Hakika baada ya hayo kuna uzima wa milele.
Baada ya hayo kuna kuishi na MUNGU.
MUNGU atusaidie mimi na wewe ili tuifikie hatua hii na kuishi na MUNGU milele kama watakatifu wake.
 Ufunuo 21:3-4 '' Nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, Tazama, maskani ya MUNGU ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye MUNGU mwenyewe atakuwa pamoja nao. Naye atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita.''
 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana Na nakuomba nisaidie kushare kwa marafiki zako ili na wao wajifunze Neno la MUNGU.


Comments