Neema
Decoras (Amezaliwa Tarehe 27 Julai 1984) ni mwimbaji na mtunzi wa
nyimbo za Injili za Kikristo mwenye kipawa na hodari kutoka nchini
Tanzania ambaye amejitoa kuwa chombo imara cha Uinjilisti na kutumikia
kusudi la Mungu katika wakati wake. Alizaliwa katika jiji la Mbeya,
Tanzania na ni watatu kuzaliwa katika familia ya watoto saba.
Neema
Decoras ambaye kwa sasa ni mama wa watoto wawili wa kike na mke mpendwa
wa mume mmoja alianza uimbaji wa nyimbo za injili akiwa mdogo sana
katika shule ya Jumapili ya Kanisa La Pentekoste Tanzania (KLPT) kabla
ya kuokoka na kubatizwa na mchungaji Mwakanyamale wa Evangelistic
Assemblies of God Tanzania (EAGT) ya Ilembo, Airport, Mbeya.
Neema
Decoras aliendelea na huduma ya uimbaji katika kipindi chote alichokuwa
akisoma, kuanzia shule ya msingi hadi sekondari. Akiwa anachukua elimu
ya sekondari alikuwa mwanachama na mwalimu wa kwaya ya Christ's
Ambassadors Students Fellowship Tanzania (CASFETA) katika shule yake na
muimbaji wa nyimbo za kusifu na kuabudu katika kikundi cha kusifu na
kuabudu na Kwaya ya Tumaini ya Kanisa La Pentekoste Tanzania (KLPT). Ni
katika kipindi hicho ndipo alipoanza kuwa na haja ya kukitumia kipawa
cha uimbaji na utunzi wa nyimbo na kufanya huduma ya uimbaji kama
muimbaji wa kujitegemea.
Haja ya kuwa muimbaji wa kujitegemea
ilianza kutimia mwishoni mwa mwaka wa 2012 Neema Decoras alipofanikiwa
kurekodi wimbo wake uitwao “Mungu ni Mwema” katika studio iitwayo Twins
Records iliyopo Riverside, Ubungo jijini Dar es Salaam chini ya
mtayarishaji wa muziki aitwaye Gabriel Maulana. Mnamo January
mwaka wa 2013 mume wake alimpeleka kwa mtayarishaji wa muziki aitwaye
Ambangile Mbwanji anayejulikana sana kama Amba ambaye ni mmiliki wa
studio iitwayo Amba Records iliyoko Ukonga, Jijini Dar es Salaam,
Tanzania.
Katika studio hiyo alifanikiwa kurekodi na kutoa albamu
yake ya kwanza mwezi Julai mwaka wa 2013. Albamu hiyo iitwayo “Milele
Nitalisifu Jina Lako” ina nyimbo nane ambazo zote ameziimba kwa lugha ya
Kiswahili. Nyimbo zilizomo katika albamu hiyo ni; Milele Nitalisifu
Jina Lako, Mikononi mwa Mungu, Unapojaribiwa, Nione Leo, Mungu ni Mwema,
Rejea kwa Yesu, Ninaimba Sifa na Hakika Nimejua.
Akiongozwa na
Neno kutoka katika Zaburi 145:1-2 “Ee Mungu wangu, Mfalme, nitakutukuza,
Nitalihimidi Jina lako milele na milele. Kila siku nitakuhimidi,
Nitalisifu Jina Lako Milele na Milele” Neema Decoras anasema kamwe
hawezi kuacha kulisifu Jina la Bwana kwa kuwa Bwana ndiye mkuu mwenye
kusifiwa sana.
Kwa sasa Neema Decoras anaishi jijini Dar es Salaam
ambapo amefanya maonyesho yake mengi sana japo yuko tayari kutumika
katika Ibada, Matamasha na Mikutano ya Injili, Semina, Sherehe, na
matukio mbalimbali ambayo yanahubiri Neno la Mungu popote pale ndani na
nje ya Tanzania.
Comments