KUWEKWA ALAMA YA DAMU YA MWANAKONDOO WA MUNGU ALIYE HAI * sehemu ya pili *

Na mtumishi wa MUNGU Gasper Madumla


Bwana Yesu asifiwe...
Haleluya...

Karibu katika muendelezo wa fundisho hili zuri kabisa,ikiwa leo ni siku ya pili ya fundisho hili. Ninachojua ni jambo moja tu,kwamba siku ya leo utapokea neno lenye kukutoa sehemu fulani na kukupeleka sehemu fulani iliyo nzuri kuliko sehemu hiyo uliyopo.

Siku ya leo nina neno fupi juu yako,yamkini wewe usomaye ujumbe huu umekusudiwa kujifunza kitu fulani hivi mahali hapa hapa.Najua yupo mmoja aliyekusudiwa siku ya leo apokee.

Ninaposema habari za kuwekwa kwa alama ya damu ya mwanakondoo wa Mungu ilikuwa ni kulipa gharama ya dhambi ndani yako na KUKUTAMBULISHA RASMI kwamba wewe si mali ya ibilisi tena bali ni mali ya Mungu aliye hai.Damu ya mwanakondoo ni damu ya thamani sana kuliko kupita maelezo yawayo yote awezayo kueleza mtu chini ya jua hili nchi idumupo.

Damu hiyo ya Bwana Yesu,ililipa gharama zako zote;
Gharama za dhambi,
Magonjwa yote,
Kila udhaifu,
Kuonewa na mapepo,
Yeye Bwana alilipa yote hayo pale msalabani,kwa nini sasa uteseke mpendwa?

Haleluya...

Tulisoma andiko hili kama andiko la msingi wa fundisho letu,anasema;

" Kisha akamsongeza kondoo mume wa pili, huyo kondoo wa kuwaweka wakfu; na Haruni na wanawe wakaweka mikono yao kichwani mwa huyo kondoo.
Kisha akamchinja; na Musa akatwaa katika damu yake, na kuitia katika ncha ya sikio la kuume la Haruni, na katika chanda chake cha gumba cha mkono wake wa kuume, na katika kidole cha gumba cha guu lake la kuume. " Walawi 8:22-23

Zoezi mojawapo alilokuwa akilifanya Musa ni kumuweka alama Haruni kwa DAMU YA KONDOO. Musa akahakikisha alama ile ya damu ya kondoo anawaweka pia na wanawe Haruni.Haruni akitambulishwa rasmi kwa alama ya damu ya kondoo wa kuchinjwa sawa sawa na agizo la BWANA Mungu.
Nasi pia tunatambulikana kwa damu ya Paska wetu naye ndie Yesu Kristo.

Haleluya...
Nasema;
haleluya,haleluyaa...

Kwa damu mtu hutambulikana,hata wana sayansi wa leo wamegundua siri ya utambulisho,ni kupitia damu tu.
Leo hii mtu akiwa na mashaka juu ya mtoto wake basi mtu huyo atakimbilia uthibitisho wa kupima DAMU yake akilinganisha na damu yake.

Ndiposa mtu huyo atahitajika kuchukuliwa vipimo vya damu yake.Kupitia vipimo hivyo ukweli utajulikana,kwamba ni mtoto wake au lah!
Sisi nasi tunatambulikana kwa kupitia DAMU YA BABA YETU KWA NJIA YA YESU KRISTO kwa sababu tumeungamana naye kwa njia ya damu.Nje ya damu ya Yesu sisi si wakristo.

• Kuna nguvu halisi ndani ya damu ya Yesu Kristo.
• Upo uweza wa ajabu usioelezeka ndani ya damu ya Yesu Kristo.
• Hata injili ya kweli huzaliwa ndani ya damu ya mwanakondoo,damu ya msalaba.

Mkristo hujulikana kwa alama ya damu ya mwanakondoo aliye hai,kama vile mtu amjuavyo mtoto wake kwa njia ya damu.
Ikumbukwe kwamba hata wana wa Israeli walitofautishwa na wana wengine kwa alama ya damu ya mwanakondoo aliyechinjwa.
Tunasoma;

" Hapo ndipo Musa akawaita wazee wa Israeli, na kuwaambia, Nendeni, mkajitwalie wana-kondoo kama jamaa zenu zilivyo mkamchinje pasaka.

Nanyi twaeni tawi la hisopu, mkalichovye katika ile damu iliyo bakulini na kukipiga kizingiti cha juu, na miimo miwili ya mlango, kwa hiyo damu iliyo katika bakuli; tena mtu ye yote miongoni mwenu asitoke mlangoni mwa nyumba yake hata asubuhi. " Kutoka 12:21-22

Haleluya...

Musa anawatambulisha wana wa Israeli mbali na Wamisri kwa alama ya damu,Musa anawaambia wazee wa Israeli mambo makubwa sana,anasema watu wote walio ndani ya alama ya damu wasitoke nje ya alama hiyo,ila wakitoka nje ya alama ya damu,watapigwa,wala hawatatambulika tena kama walikuwa wana wa Mungu.

Hali hii inafanana kabisa na leo hii katika safali yetu ya maisha ya wokovu maana nasi tumewekewa alama ya damu ya mwanakondoo wa Mungu aliye hai,na ikiwa tutatoka nje ya alama ya damu hiyo basi ujue tutapigwa.
Anasema;

" Na ile damu itakuwa ishara kwenu katika zile nyumba mtakazokuwamo; nami nitakapoiona ile damu, nitapita juu yenu, lisiwapate pigo lo lote likawaharibu, nitakapoipiga nchi ya Misri. " Kutoka 12:13

Damu ilikuwa ishara kwa wana wa Israeli,na kupitia hiyo ishara Bwana Mungu akawatofautisha na watu wengine,kama leo jinsi tulivyotengwa mbali na mataifa kwa alama ya damu ya msalaba.
Maana kama isingelikuwa damu ya msalaba,basi ukristo wetu ni bure kabisa,wala tusingekuwa na wokovu. sababu msalaba wa Yesu ulituokoa toka dhambini ,ukatutakasa na zaidi sana tukapewa uwezo wa kushinda dhambi kwa msaada wa Roho Mtakatifu.

Haleluya...

Watu wengi tumetoka nje ya alama ya damu ya msalaba,kwa kuendelea kutenda dhambi. Na kujikuta tukipigwa na muharibu wetu,ibilisi;tukipigwa kwa magonjwa,mapepo na hata uchumi wetu pia huangamizwa.Misoto tunayoipata siku hizi za leo ya kuonewa na ibilisi ni kwa sababu ya kukaa nje ya damu ya mwana kondoo,damu ya msalaba.

Mahali pale wana wa Israeli walipoambiwa wasitoke nje ya nyumba zao,unafikiri kwamba kama wangetoka nje ingekuwaje?
Hakika wakepigwa na muharibu.

Bwana Yesu asifiwe...

Leo hii tunajifunza jambo moja kubwa mahali hapa;
Kwamba nje ya damu ya Yesu Kristo ni kupigwa na adui tu.
Uponyaji wa kweli hupatikana ndani ya damu ya Yesu Kristo,na hata usalama wetu wa maisha upo ndani ya damu ya msalaba,na ndio maana tunaona kwamba wana wa Israeli wanaambiwa kamwe wasitoke nje ya damu.

Kwa lugha nyingine,Musa alichopewa na BWANA Mungu awaeleze waisraeli ni kwamba awaambie maisha yao yamesitiriwa ndani ya alama ya damu ya kondoo iliyopakwa juu ya miimo ya nyumba zao walizokuwepo.
Kama vile nasi maisha yetu yamefichwa ndani ya damu ya Yesu Kristo...

ITAENDELEA...

Usikose!

• Kwa huduma ya maombi na maombezi,usisite kunipigia namba yangu hii hapa chini;
• 0655111149.

UBARIKIWE...

Comments