MKRISTO HATAKIWI KUWA MTOA RUSHWA AU MPOKEA RUSHWA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Katika jamii tunajua maneno mengi yanayoelezea ubaya wa rushwa. Tunayajua maneno kama ''rushwa ni adui wa haki'' na mengineyo. Kwa sababu Neno la MUNGU kazi yake ni kulitengeneza kanisa ili limpendeze MUNGU basi leo nimepewa ujumbe huu na ROHO wa MUNGU ili nikufundishe.
Mteule wa MUNGU hatakiwi kuwa mtoa rushwa wala mpokea rushwa.
Mithali 17:23 '' Asiye haki hutoa rushwa kifuani, Ili kuzipotosha njia za hukumu.''
 
Rushwa ni fedha au kitu cha thamani kinachotolewa na mtu ili mtu huyo mtoaji  apatiwe upendeleo.
Kuna wengine hutoa rushwa ya ngono, ni machukizo makuu.
Kuna wengine hutoa mali zao au vitu vyao ili tu wapendelewe, hiyo ni haifai kuwepo katika kundi la watu wa MUNGU.
MUNGU hataki wateule wake wawe watoa rushwa au wapokea rushwa, ni dhambi mbaya.

Amosi 5:12 ''Maana mimi najua jinsi maasi yenu yalivyo mengi, na jinsi dhambi zenu zilivyo kubwa; ninyi mnaowaonea wenye haki, mnaopokea rushwa, na kuwageuza wahitaji langoni wasipate haki yao.'' 

MUNGU kupitia Neno lake anawaonya watoa rushwa na wapokea rushwa.
Kazi Mojawapo Ya Rushwa Ni Kupofusha Macho Ili Yatoke Maamuzi Isivyo Sahihi Wala Haki. 
Rushwa Inapofusha Macho. 
Kuna Waheshimiwa Wengi Leo Ni Vipofu Kwa Sababu Ya Rushwa. Kuna Wasomi Wengi Leo Ni Vipofu Kwa Sababu Ya Rushwa. Kuna Watu Leo Ni Vipofu Kwa Sababu Ya Rushwa.
 Upofu Wa Rushwa Uko Kwenye Maamuzi. Rushwa Ni Dhambi, Haifai Kutoa Wala Kupokea Rushwa Wewe Uliyeokolewa Na KRISTO. Biblia Inasema Rushwa Hupofusha Macho. 

Kutoka 23:8 ''8 Nawe usipokee rushwa; kwani hiyo rushwa huwapofusha macho hao waonao, na kuyapotoa maneno ya wenye haki.''

Kama kanisa lisipofundishwa madhara ya rushwa basi inawezakuja kutokea siku moja kwamba kuna Askofu fulani ametoa rushwa ili ashinde uchaguzi wa kumfanya Askofu mkuu.
Tutasikia kwamba Kuna Mchungaji amehonga ili tu achaguliwe kuwa Askofu wa jimbo.
Tutasikia kwamba kuna ndugu fulani ametoa pesa ili tu viongozi wa kanisa wampe nafasi ya uzee wa kanisa au ya kuongoza idara kanisani.
MUNGU hataki wateule wake wawe watoa rushwa au wapokea rushwa, ni dhambi mbaya.
Kumbu 16:19 ''Usipotoe maamuzi; wala usipendelee uso wa mtu; wala usitwae rushwa; kwa kuwa rushwa hupofusha macho ya wenye akili, na kugeuza daawa ya wenye haki. '' 

Kama kuna kitu MUNGU wa mbinguni anakichukia basi ni rushwa.
Biblia inawaonya kanisani kutojihusisha na rushwa.
Rushwa ni dhambi kama zilivyo dhambi zingine.
rushwa ni uovu kama yalivyo maovu mengine.

Ayubu 15:34-35 '' Kwa kuwa jamii ya hao wasiomcha MUNGU watakuwa tasa, Na moto utateketeza mahema yenye rushwa. Wao hutunga mimba ya madhara, na kuzaa uovu, Nalo tumbo lao hutengeza udanganyifu.''

Mahali palipotawaliwa na rushwa hapo ni hatari sana.
 Sekta iliyotawaliwa na rushwa hiyo ni sekta hatari sana.
Kama kuna mtu anatoa pesa ili achaguliwe au apendelewe katika maamuzi tambua kwamba huyo ana lengo la kuja kuirudisha pesa yake kwa njia ya madaraka yake mtakayompa.
MUNGU hana upendeleo(Matendo 10:34) ndio maana na sisi watoto wake anatutaka tusipendelee mtu yeyote.

Kumbu 10:17 '' Kwa maana BWANA, Mungu wenu, yeye ndiye MUNGU wa miungu, na BWANA wa mabwana, MUNGU mkuu, mwenye kuogofya, asiyependelea nyuso za watu, wala hakubali rushwa.''
 
MUNGU hataki wateule wake wawe watoa rushwa au wapokea rushwa, ni dhambi mbaya.
 Watoa rushwa hawana sehemu katika uzima wa milele wasipotubu.
Kuna machozi mengi leo yanawatoka baadhi ya watu kwa sababu tu kuna rushwa ilitolewa na mtu ambayo imesababisha wao wateseke.
Kutoa rushwa ni dhambi kwa MUNGU kama ilivyo  kupokea rushwa.
MUNGU anaweza akakukataa na kukuondoa katika huduma yake kwa sababu tu ya tabia yako ya kutoa au kupokea rushwa.
Hebu ona hapa.
1 Samweli 8:1-3 ''Hata Samweli alipokuwa mzee, aliwafanya wanawe wawe waamuzi juu ya Israeli. Na jina la mwanawe mzaliwa wa kwanza aliitwa Yoeli; na jina la wa pili Abiya; walikuwa waamuzi katika Beer-sheba. Ila wanawe hawakuenda katika njia zake, bali waliziacha, ili wapate faida; wakapokea rushwa, na kupotosha hukumu.''

 Baada ya watoto wa Nabii Samweli kupewa madaraka walianza kupokea rushwa ili wapotoe maamuzi na jambo hilo likawa chukizo kwa MUNGU. Ndio maana baada ya hapo watoto wa Samweli waliondolewa katika madaraka ya kuwa waamuzi na Ufalme ukachukua nafasi na sio waamuzi tena.
 MUNGU hataki wateule wake wawe watoa rushwa au wapokea rushwa, ni dhambi mbaya.

Ezekieli 22:12-16 ''Ndani yako wamepokea rushwa ili kumwaga damu; umepokea riba na faida; nawe kwa choyo umepata mapato kwa kuwadhulumu jirani zako, nawe umenisahau mimi, asema Bwana MUNGU. Basi, tazama, nimeipigia kofi hiyo faida uliyopata kwa njia isiyo haki, na hiyo damu yako iliyokuwa kati yako. Je! Moyo wako waweza kuvumilia, au mkono wako waweza kuwa hodari, katika siku zile nitakapokutenda mambo? Mimi, BWANA, nimenena neno hili, tena nitalitenda. Nami nitakutawanya kati ya mataifa, na kukutapanya kati ya nchi mbalimbali; nami nitauteketeza uchafu wako, ili ukutoke. Nawe utatiwa unajisi ndani ya nafsi yako, mbele ya macho ya mataifa; nawe utajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.'

Kanisa likiingia kwenye rushwa huko ni kumkataa MUNGU anayekataza rushwa.
Haki huwa hainunuliwi kwa pesa.
Madaraka hayatakiwi kununuliwa kwa pesa.
Nyazifa zozote hazitakiwi kununuliwa kwa pesa au vitu.
Kanisa lazima likemee rushwa.
Watoa rushwa na wapokea rushwa inatakiwa sana waonywe na hata watengwe kwa muda maana watasababisha haki iondoke.
Ukiwa mtu wa kutoa rushwa naamini kabisa hata kwenye maombi hutaenda maana wewe unaitegemea sanamu yako iitwao pesa ya rushwa na si kumtegemea MUNGU.
Rushwa ni sanamu mbaya sana ambayo wengi wameivaa katika shingo za mioyo yao.

Mika 7:2-4 ''Mtu amchaye MUNGU ametoweka, asionekane katika nchi, wala hapana mtu mwenye adili katika wanadamu; wote huotea ili kumwaga damu; kila mtu humwinda ndugu yake kwa wavu. Mikono yao inayashika mabaya wayatende kwa bidii; mtu mkuu aomba rushwa, kadhi yu tayari kuipokea; mtu mkubwa hunena madhara yaliyomo rohoni mwake; hivyo ndivyo wayafumavyo hayo pamoja.  Mtu aliye mwema miongoni mwao ni kama mbigili; mtu aliye mwenye adili miongoni mwao ni mbaya kuliko boma la michongoma; hiyo siku ya walinzi wako, yaani, siku ya kujiliwa kwako, imefika; sasa kutatokea kufadhaika kwao.'

MUNGU hataki tuhusike na rushwa kwa namna yeyote ile.
Ndugu jitenge mbali na rushwa.
Usitoe rushwa wala usipokee rushwa.
Mtii MUNGU kwa kuikataa rushwa.
Mtii Mwokozi wako YESU KRISTO kwa kuikimbia rushwa.
Muone tu kwamba mtoa rushwa anatumika kipepo.
Muone tu mpokea rushwa kwamba ni wakala wa shetani.
Lazima watu wa MUNGU waiepuke rushwa na waikemee.
Hata kuwakalisha matajiri mbele ya kanisa hiyo ni matokeo ya rushwa.
Hata kanisani kuwapa viti vizuri matajiri na masikini kuwaweka kwenye vitu vya kawaida hiyo ni makosa makubwa, ni harufu ya rushwa.
BWANA YESU analionya kanisa lake leo kwamba rushwa isitajwe kanisani maana rushwa ni uovu. Rushwe isiwepo katika watu wa MUNGU.
Iogope rushwa, ikimbie rushwa, usitoe rushwa na usikubali kupokea rushwa.
Mithali 29:4 '' Mfalme huithibitisha nchi kwa hukumu; Bali yeye apokeaye rushwa huipindua.'' 
 
Apokeaye rushwa huipindua hukumu, huyo havai kuwapo katika kundi la waenda mbinguni.
 MUNGU hataki wateule wake wawe watoa rushwa au wapokea rushwa, ni dhambi mbaya.

 Upendo wa KiMUNGU ni hali ya kumpenda mtu bila kujali mtu huyo alivyo au ana sifa gani.
Kanisa lote linatakiwa liwe na upendo kwa watu wote bila kupendelea yeyote.
Ukipendelea maana yake umepofushwa macho na rushwa.
Rushwa haifai na hakikisha hutoi wala kupokea rushwa.
 
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili



Comments