![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO atukuzwe mpendwa, karibu ujifunze kitu cha kukusaidia kushinda vita ya kiroho uliyopo dhidi ya nguvu za giza, dhidi ya wachawi, wakuu wa giza, majeshi ya pepo wabaya na dhidi ya kila wakala wa shetani.
✓✓Ninachotaka ujifunze leo ni hiki, kila vita ya kiroho ina kanuni zake za kushinda.
Ngoja tuangalie mfano mmoja ndani ya Biblia, kanuni walizotumia Waisraeli ili kupata ushindi dhidi ya Yeriko.
✓✓Kwenye somo la leo nataka utafakari vita yako ya kiroho, kama ipo, ili utafute kwa maombi na kutafakari neno la MUNGU namna ya kushinda vita hiyo ya kiroho.
Kupitia kanuni walizotumia Israeli basi na wewe katika vita yako ya kiroho utajifunza Neno la MUNGU kuhusu vita yako na utajua namna ya kushinda hiyo vita.
Ilikuwa hivi katika vita ya kiroho kati ya Waisraeli na Mji wa Yeriko.
Yoshua 6:2-5 " BWANA akamwambia Yoshua, Tazama, nimeutia Yeriko katika mkono wako, na mfalme wake, na mashujaa wake. Nanyi mtauzunguka mji huu, watu wote wa vita, mkiuzunguka mji mara moja. Fanya hivi siku sita. Na makuhani saba watachukua tarumbeta saba za pembe za kondoo waume, mbele ya hilo sanduku; na siku ya saba mtauzunguka mji mara saba, nao makuhani watapiga tarumbeta zao. Kisha itakuwa watakapopiga hizo pembe za kondoo waume kwa nguvu, nanyi mtakaposikia sauti ya tarumbeta, watu wote watapiga kelele kwa sauti kuu; na ukuta wa mji utaanguka chini pale pale, na hao watu watapanda, kila mtu akiendelea mbele kukabili."
Kumbe kanuni ya kushinda vita ya kiroho dhidi ya Yeriko ilikuwa haya.
1. Kanuni ya kwanza ilikuwa kuizunguka Yeriko mara moja kila siku kwa siku saba.
Yoshua 6:14 "Siku ya pili wakauzunguka mji mara moja, wakarejea kambini; ndivyo walivyofanya siku sita."
✓✓Hata wewe unaweza kuwa katika vita ya kiroho na rohoni mwako unasukumwa kufunga siku labda 3 au 4 au 7 au 10 n.k kutegemea na vita yako na kutegemea na maelekezo uliyoyapokea kutoka ulimwengu wa roho, watu wengi hawafuati kanuni za namna ya kushinda kama wanavyoelekezwa kwenye ulimwengu wa roho.
Siku moja mimi Peter Mabula nilifunuliwa kwa ndoto kwamba nifunge siku 3 ili kufanya maombi kutokana na vita ya kiroho niliyokuwa nayo, nilifunga siku moja na nusu nikafungua lakini vita ile haikuisha hivyo baada ya muda nilijikuta nafunga siku 3 mara mbili, nini nataka kukuambia?
✓✓Kufuata kanuni ya ushindi unayoipata ni jambo muhimu sana ili usije ukatumia gharama kubwa baadae kutoka kwenye tatizo hilo hilo.
◼️Hakikisha unaisikia sauti ya ROHO MTAKATIFU anayokupa.
◼️Zingatia neno la MUNGU linalosema na wewe wakati huo juu ya vita Yako ya kiroho.
◼️Zingatia ufunuo wa maono au ndoto au msukumo wa rohoni na namna yeyote kwako ambayo utajilidhisha kwamba ni MUNGU amesema na wewe, iwe ni kupitia watumishi wake au mafundisho mbalimbali ya Neno la MUNGU, hata kupitia somo hili unaweza kushangaa kuna mahali MUNGU amesema na wewe, ukigundua fanyia kazi kwa Maombi.
Kutoka 23:22 "Lakini ukiisikiza sauti yake kweli, na kuyatenda yote ninenayo mimi; ndipo mimi nitakuwa ni adui wa adui zako, na mtesi wa hao wakutesao."
Kipindi fulani nilikuwa katika vita kali ya kiroho, niliona uzito rohoni mwangu usio wa kawaida, niliona hali haikuwa nzuri hata kidogo kwenye ulimwengu wa roho kuhusu mimi, Sikuelewa kabisa nini nifanye zaidi ya maombi tu, muda mchache baadae rafiki yangu mmoja kutoka Congo aliota ndoto kuhusu mimi akanijulisha, ujumbe wa ndoto ile kwamba inanipasa kujitenga na rafiki yangu mmoja ambaye tulipotezana miaka 20 iliyopita, nikaambiwa rafiki huyo amebeba ajenda za kuzimu za hatari sana ili kunivuruga mimi kiroho na kimwili, sikuwa najua kuhusu hilo hadi siku najulishwa ndoto hiyo, na ajabu ni kwamba siku najulishwa ndoto ndio siku rafiki huyo ananipigia simu kwa mara ya kwanza baada ya tangu miaka 20 iliyopita tulipoonana, mtu huyo akanipigia simu akijaribu kunishawishi mambo ya ajabu sana, alizungumza muda mrefu sana kwenye simu na alikuwa safarini kuja nilikokuwa, yaani ni ghafla mipango mipango mingi sana alinishirikisha. Namshukuru sana MUNGU maana ulimwengu wa roho ulikuwa umeshaona hivyo nikazingatia ya rohoni kwa kujitenga na mtu huyo kwenye ulimwengu wa roho na ulimwengu wa mwili, sikuwasiliana naye tangu siku hiyo moja na hatujawahi kuonana hadi leo.
Nini nataka niseme?
✓✓Kanuni ya ushindi wangu ilinitaka kujitenga na rafiki mbaya, inawezekana na wewe umekwama na hujui utashindaje vita ya kiroho, kumbe inakupasa kujitenga mbali na baadhi ya watu ambayo sio watu wazuri kwako.
✓Kanuni za ushindi dhidi ya nguvu za giza ziko nyingi hivyo tafuta kwenye neno la MUNGU kanuni ya kushinda kwako tafuta sauti ya MUNGU kwenye Maombi.
2. Kanuni ya pili ilikuwa kuizunguka Yeriko mara saba katika siku ya saba.
Yoshua 6:15 "Ikawa siku ya saba wakaondoka asubuhi na mapema wakati wa mapambazuko, wakauzunguka mji vivyo hivyo mara saba; ila siku hiyo waliuzunguka huo mji mara saba."
Hapa tunaweza kusema ilikuwa kuchochea zaidi maana ushindi ulikuwa uko karibu sana.
Nini nataka niseme?
Inawezekana umefunga na kuomba sana na sasa umekata tamaa, umegoma tena kuomba na kuhudhuria mikesha ya maombi.
Kumbe wakati huu kwako ndio unatakiwa uwe wakati wa kuchochea zaidi maombi lakini wewe umeacha maombi, umesahau Neno la MUNGU linasema Luka 18:1 "........ imewapasa kumwomba MUNGU sikuzote, wala wasikate tamaa."
Inawezekana wewe umemtolea MUNGU sadaka nzuri kwa muda mrefu lakini kwa sasa umeacha, umegoma ukidhani labda unawakomesha wachungaji waaminifu ambayo usiku na mchana wanakuombea, inawezekana huu ndio wakati wako wa kuzunguka Yeriko mara saba kwa siku moja na sio mara moja kwa siku moja, yaani huu ni wakati wa kuchochea na sio kupunguza spidi, inategemea na mahitajio ya ulimwengu wa roho kuhusu ushindi wako.
Sina maana ujilazimishe kutoa bali fuata sauti ya ROHO MTAKATIFU ndani yako, fuata msukumo wa ki MUNGU ndani yako, hapa sizungumzii mtumishi kukushawishi bali maelekezo ya ndani yako mwenyewe au kutokana na ulivyojifunza neno la MUNGU na kulielewa.
✓✓Kwa Waisraeli kama wangechoka na kuamua kuzunguka Yeriko mara moja tu hata siku ya saba basi wasingeshinda vita ya kiroho waliyokuwa nayo.
Kila vita ya kiroho ina kanuni zake ili ushindi, kanuni yao ya pili ilikuwa kuizunguka Yeriko mara saba ndani ya siku moja.
Je ukiambiwa siku fulani uombe mara 7 ndani ya siku hiyo moja tena kila ukianza kuomba awamu moja uombe dakika 45, kama maelekezo ndio hayo kwako basi utaomba karibu masaa 6 kwa siku hiyo.
◼️Kuna vita ya kiroho nyingine ili ushinde lazima ujue namna ya kushinda.
Muhimu tu zingatia kanuni za kiroho zinazotokana na Neno la MUNGU juu ya kile unahitaji ushindi.
3. Kanuni ya tatu ilikuwa kupiga kelele za ushindi.
Yoshua 6:16 "Hata mara ya saba makuhani walipozipiga tarumbeta, Yoshua akawaambia watu, Pigeni kelele; kwa maana BWANA amewapeni mji huu."
Ni kanuni ya ajabu sana lakini ndio ilionyesha ushindi wa wana wa Israeli.
Mambo ya ulimwengu wa roho wakati mwingine yanahitaji sana kufuata maelekezo ya Neno la MUNGU.
Siku moja mimi nilikuwa nawaombea watu fulani ili MUNGU awajibu mahitaji yao, kabla sijajua niwaombee nini watu hao nilisikia rohoni sauti hii "Tangaza mwaka wa ushindi kwa kila mmoja kama Isaya 61:2" Kutangaza mwaka wa BWANA uliokubaliwa, na siku ya kisasi cha MUNGU wetu; kuwafariji wote waliao;"
Siku hiyo maombi yalikuwa ni kutangaza tu ushindi kwa kila nilimuombea, aliyehitaji mume nilisema anapata mume, asiye na kazi nilisema ni wakati huu anaenda kupata kazi, anayeumwa nilimtangazia kupona, niliomba maombi mengi na kwa watu wengi huku nikifuata kanuni ya rohoni niliyopewa siku hiyo kwamba kutangaza ushindi.
◼️Sasa Waisraeli walipewa kanuni ya kupiga kelele za ushindi, walipozingatia kanuni hiyo Biblia inasema wakautwaa huo mji kwa ushindi mkuu maana kelele zao ziliangusha ukutwa mkubwa uliokuwa umeuzunguka mji.
Yoshua 6:20 "Basi watu wakapiga kelele, na makuhani wakazipiga tarumbeta; hata ikawa, hapo watu waliposikia sauti ya tarumbeta hao watu wakapiga kelele kwa sauti kuu sana, na ule ukuta wa mji ukaanguka nchi kabisa, hata watu wakapanda juu, wakaingia katika mji, kila mtu akiendelea kukabili mbele; wakautwaa huo mji."
Kama wasingefuata kanuni ya kupiga kelele basi ukuta usingeanguka na wasingeweza kushinda vita, ulimwengu wa roho una maajabu sana, hapa tunaona kelele za Waisraeli ndizo zilihitajika ndipo ukuta uanguke, wangetumia njia nyingine wasingefanikiwa.
◼️ Inawezekana wewe ili ushindi basi mtumikie Bwana YESU KRISTO, kama hiyo ndio kanuni ya ushindi wako basi changamka.
Kutoka 23:25 "Nanyi mtamtumikia BWANA, Mungu wenu, naye atakibarikia chakula chako, na maji yako; nami nitakuondolea ugonjwa kati yako."
◼️Kama moja ya kanuni ya ushindi wako ni sadaka basi changamka.
Zaburi 20:3-4 " Azikumbuke sadaka zako zote, Na kuzitakabali dhabihu zako. Akujalie kwa kadiri ya haja ya moyo wako, Na kuyatimiza mashauri yako yote."
Tumeiona kanuni za wa Waisraeli dhidi ya Yeriko, kanuni hiyo inaweza kuwa tofauti kidogo na kanuni ya ushindi wako dhidi ya mawakala wa shetani.
Unachotakiwa kufanya ni kuijua kanuni ya ushindi wako dhidi ya nguvu za giza.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(ushauri , ushuhuda, sadaka ya kuipeleka Injili, whatsapp, Maombi n.k).

Comments