MAKOSA YA ESAU YALIHARIBU HATIMA YAKE NJEMA.

 

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 


Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe Ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.

Yeremia 49:10 "Lakini nimemwacha Esau hana kitu, nimepafunua mahali pake pa siri, wala hataweza kujificha; kizazi chake kimeangamizwa, na ndugu zake, na jirani zake, naye mwenyewe hayuko."

✓✓Kuna makosa huwa ni ya hatari sana ukiyafanya maana yanaweza kukutoa katika mstari hata kama umetubu na kusamehewa.
Mfano wake ni kama Mtu kuua Kisha akakamatwa na kufungwa jela, hata akitubu atasamehewa ila bado atatumikia kifungo jela na utakatifu wake baada ya toba.

Mfano Mwingine Mtu anaweza kufanya ujambazi akakamatwa na kukatwa mkono, akitubu atasamehewa na mkono wake bado hatakuwa nao.
Hii ni mifano kuonyesha Kuna dhambi huwa Zina gharama hata baada ya kusamehewa, Esau alifanya makosa yaliyomghalimu Maisha yake.

Malaki 1:3 "bali Esau nimemchukia na kuifanya milima yake kuwa ukiwa, na urithi wake nimewapa mbweha wa nyikani."

✓✓Inawezekana kabisa Esau alifanya makosa mengi katika Maisha yake kama Mwanadamu lakini makosa haya ya Esau usiyafanye Wewe katika Maisha Yako.

Makosa ya Esau yaliyoharibu hatima yake.

1. KOSA LA KUKOSEA KUOA.

Mwanzo 26:34-35 " Esau alipokuwa mwenye miaka arobaini, akamwoa Yudithi, binti Beeri, Mhiti, na Basemathi, binti Eloni, Mhiti. Roho zao Isaka na Rebeka zikajaa uchungu kwa ajili yao."

Akina Isaka na Rebecca walikuwa Watumishi wa MUNGU na hawakutaka Kijana wao aoe Binti mpagani yaani Binti mwabudu miungu ndio maana roho zao zilijaa uchungu walipoona Kijana wao ameoa mabinti wawili waabudu shetani.

◼️Kosa kama hilo usije ukalifanya Wewe Mteule wa KRISTO kwa kuoa au kuolewa na Mtu wa dini nyingine zinazokataa Wokovu wa KRISTO YESU.
Ndoa na mwabudu shetani inaweza kukuondoa katika Wokovu au mkazaa watoto wanaomfuata shetani na sio MUNGU katika KRISTO YESU.
Jifunze kwa Yakobo aliyekatazwa kuoa waabudu shetani.

Mwanzo 28:1 "Basi Isaka akamwita Yakobo, akambariki, akamwagiza akamwambia, Usitwae mke wa binti za Kanaani."

◼️Binti Usikubali kuolewa na Mtu asiye na YESU KRISTO na Wewe Kijana Usikubali kuoa mwabudu shetani maana ukifanya hivyo hata hatima Yako ya uzima wa milele katika KRISTO YESU inaweza kuwa mtihani kwako kwa sababu ya Ndoa, mwenzi wako mwabudu shetani atakushawishi kumwacha YESU hivyo utapishana na uzima wa milele.

✓✓Wapo mamilioni ya Vijana na mabinti wanaomcha MUNGU katika KRISTO YESU, tafuta mmoja kati yao ufunge nae Ndoa na sio kutafuta waabudu shetani.

2. KOSA LA KUUZA HAKI YAKE YA UZALIWA WA KWANZA KWA TAMAA YA CHAKULA.

Waebrania 12:16 "Asiwepo mwasherati wala asiyemcha MUNGU, kama Esau, aliyeuuza urithi wake wa mzaliwa wa kwanza kwa ajili ya chakula kimoja."

Kuzaliwa wa kwanza haukuwa mpango wa Wanadamu Bali mpango wa MUNGU Mwenyewe lakini Esau alidharau kuwa mzaliwa wa kwanza ndio maana Biblia katika andiko hapo juu inamwita "Asiye Mcha MUNGU "

◼️Esau kwa kosa hilo alionekana hamchi MUNGU.
Kosa lenyewe lilikuwa hili hapa chini.

Mwanzo 25:33 "Yakobo akamwambia, Uniapie kwanza. Naye akamwapia, akamwuzia Yakobo haki yake ya mzaliwa wa kwanza."

Kuna vitu vya kuuza ila sio uzaliwa wa kwanza kama Kuna agano la MUNGU.

✓✓Esau hakutambua thamani ya baraka ya MUNGU ya mzaliwa wa kwanza.

✓✓Uzaliwa wa kwanza ulikuwa urithi wa ki MUNGU uliobeba baraka na kibali, kwa kosa hilo lilimtenga mbali na kibali Cha ki MUNGU ndio maana baada ya hapo ikawa ni rahisi MUNGU kusema na Yakobo na sio Esau.
Mfano ni 

Mwanzo 28:12 "Akaota ndoto; na tazama, ngazi imesimamishwa juu ya nchi, na ncha yake yafika mbinguni. Tena, tazama, malaika wa MUNGU wanapanda, na kushuka juu yake."

3. KUMCHUKIA NDUGU YAKE NA KUTAKA KUMUUA KWA AJILI YA BARAKA YAKE.

Mwanzo 27:41" Esau akamchukia Yakobo kwa ajili ya ule mbaraka babaye aliombarikia. Esau akasema moyoni mwake, Siku za kumlilia baba yangu zinakaribia, ndipo nitakapomwua ndugu yangu Yakobo."

◼️Kwanza ukisoma andiko hili unagundua Esau alikuwa anamtakia kufa hadi Baba yake mzazi ili Baba akifa amuue Mdogo wake, hii ni hatari mbaya sana.
Ni kitu kibaya sana Mtoto atamani Mzazi wake afe, huko ni kijiunganisha na laana mbaya.

Mathayo 15:4 "Kwa kuwa MUNGU alisema, Mheshimu baba yako na mama yako, na Amtukanaye baba yake au mama yake kufa na afe."

◼️Ndugu haijalishi Baba Yako au Mama Yako amezeeka kiasi gani au anaumwa kiasi gani usimtakie kufa, mzazi anaweza kuwa na hatima ya Mtoto wake maana ni yeye ndio aliyemzaa, usijaribu kumtakia kufa mzazi wako yeyote.
Kumbuka unaweza usiishi miaka mingi kwa kushindwa tu kuwaheshimu wazazi wako.

Waefeso 6:1-3 " Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika BWANA, maana hii ndiyo haki. Waheshimu baba yako na mama yako; amri hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi, Upate heri, ukae siku nyingi katika dunia."

◼️Licha ya kosa hilo kwa Esau kosa lingine lilikuwa kumchukia Ndugu yake kwa ajili ya baraka yake.

✓✓Inawezekana Kuna Ndugu Yako amebarikiwa na MUNGU, hakuna haja ya kumchukia kwa ajili ya baraka yake.

◼️Kumbuka chuki ya Esau kwa Yakobo haikupunguza chochote kwa Yakobo.

◼️Hakuna haja ya Mtu yeyote kuwachukia waliobarikiwa na MUNGU.
Asante kwa kujifunza Neno la MUNGU siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments