NAMNA NNE(4) ZA KUMTAFUTA MUNGU.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Sijui kama wewe huwa unamtafuta MUNGU, lakini ni faida kuu kumtafuta MUNGU.
Watu wengi humtafuta MUNGU na lakini wengine hukosea katika kumtafuta MUNGU.
Lakini ni MUNGU mwenyewe ameahidi kwamba atapatikana kama tukimtafuta kwa bidii.
 Kumbu 4:29 '' Lakini huko, kama mkimtafuta BWANA, Mungu wako, utampata, ukimtafuta kwa moyo wako wote, na roho yako yote. ''


Jumapili moja wakati wa maombi ya asubuhi kabla Ibada haijaanza nilisikia sauti ikisema kwamba ''Kila kitu lazima kifanyike katika utaratibu wa MUNGU, kwa  mapenzi ya MUNGU, Kwa kusudi la MUNGU na kwa lengo la Ki MUNGU.'' 
 Nililazimika kukatisha maombi na nikachukua notebook yangu ya masomo na kuandika ujumbe huo kisha nikarudi kuendelea na maombi. Baadae nilikuwa katika tafakari nzito juu ya ujumbe huo. Kwa haraka haraka niligundua kwamba kuna watu hufanya mambo ya ki MUNGU lakini sio katika utaratibu wa MUNGU ndio maana huwa hawafanikiwi. Kuna watu hufanya mambo katika utaratibu wa Ki MUNGU lakini sio kwa kusudi la MUNGU kwa wakati huo na pia sio mapenzi ya MUNGU kwa wakati huo. Ujumbe huo siku moja nitaufafanua kama somo kamili lakini kwa leo kwa ufupi tunaweza kugundua kwamba kumtafuta MUNGU pia kuna kanuni na taratibu zake hivyo kuna wengine hukosea. MUNGU anaweza akamsemesha mtu lakini mtu asizingatie lakini baadae akihitaji jambo ambalo kulipata kwake ni pale ambapo angemtii MUNGU zamani, wakati huu mtu huyo hutumia nguvu nyingi sana bila mafanikio, kumbe angeitii sauti ya MUNGU mwanzo basi kitu hicho wala kisingehitaji mambo mengi kukipata. Ndugu, sijui kama huwa unamtafuta MUNGU lakini kumtafuta MUNGU ni jambo la muhimu sana sana.
Kwa ufupi naweza kusema kwamba Kumtafuta MUNGU ni kuishi.
Kumtafuta MUNGU ni kuutafuta uzima.
Tangu zamani agizo la MUNGU tumtafute maana Kumtafuta yeye ni kuishi, ni kupona na ni kushinda.
Amosi 5:4 " Maana BWANA awaambia hivi nyumba ya Israeli, Nitafuteni mimi, nanyi mtaishi;"


Ni heri sana kila mmoja katika wateule wa KRISTO Kumtafuta MUNGU.
Wazazi ni vyema sana kuwafundisha watoto wao jinsi ya Kumtafuta MUNGU.

1 Nyakati 28:9 " Nawe, Sulemani mwanangu, mjue MUNGU wa baba yako, ukamtumikie kwa moyo mkamilifu, na kwa nia ya kumkubali; kwa kuwa BWANA hutafuta-tafuta mioyo yote, na kuyatambua mawazo yote ya fikira; ukimtafuta, ataonekana nawe; ukimwacha, atakutupa milele."

Kuna njia nne(4) nimekuandalia za Kumtafuta MUNGU ambazo zote zinatakiwa ziwe na wewe katika maisha yako yote.

1. Kuishi maisha matakatifu ya kumcha MUNGU.

 Nehemia 1:9 ''bali mkinirudia mimi, na kuzishika amri zangu na kuzitenda, watu wako waliofukuzwa wajapokuwa katika pande za mwisho za mbingu, hata hivyo nitawakusanya kutoka huko, na kuwaleta mpaka mahali pale nilipopachagua ili kuliweka jina langu hapo. '' 
Katika andiko hili kuna habari za waisraeli ambao wameenda kinyume na maagizo ya  MUNGU. Kwa Neema MUNGU anasema kwamba yuko tayari kuwasaidia lakini kama wakianza kuzishika sheria zake. Watu hawa Neno lao la wakati wao lilikuwa ni tolati ya Musa hivyo kushika tolati ilikuwa ni njia ya kumtafuta MUNGU. Kwetu sisi Neno letu ni injili ya YESU KRISTO, Kuitii Injili ya YESU KRISTO ambayo jina lingine inaitwa Fundisho la KRISTO ndiko kumtafuta MUNGU aliye hai.
Kumbe kutii maagizo ya MUNGU ni njia ya kumtafuta MUNGU hata akusaidie.
 1 Nyakati 16:11 '' Mtakeni BWANA na nguvu zake; Utafuteni uso wake siku zote. '' 

Watu hawa Waisraeli  waliambiwa kwamba wakimrudia MUNGU na kuanza kutii Neno lake yeye atawakusanya na kuwarudisha katika nchi yao aliyowapa zamani. Wako watu leo baraka zao walizopewa na MUNGU kwa sasa maadui zao ndio wamezikalia kwa sababu ya dhambi.
Wapo watu fursa zao na kila baraka zao shetani kupitia mawakala zake amezishikilia, lakini ahadi ya MUNGU ni kwamba watu wake wakianza kumtii na kulitii Neno lake hakika hiyo ni njia ya kumtafuta na atakuwa sasa upande wao. MUNGU akiwa upande wako hakika adui zako watakuogopa na kukimbia mbele zako.
Kuishi maisha matakatifu katika Wokovu wa KRISTO hakika huko ni kumtafuta MUNGU. Ndio maana akasema tumtafute kwa Bidii Tutamuona, tumtafute tukiwa watakatifu  sio waovu ndipo tutamuona.

Yeremia 29:13 '' Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote.''

 Kama huwa humtafuta MUNGU kwa kuishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO basi anza leo.
Unaweza ukatamani karama fulani lakini ukiokoka na kuanza kuishi maisha matakatifu ndipo moja kwa moja ROHO MTAKATIFU atakutumia katika karama hiyo uliyokuwa unaitafuta tangu zamani.

2. Kumtafuta MUNGU kwa maombi.


Maombi ni njia kuu ya kumtafuta MUNGU na kumwona.
2 Nyakati 7:14 '' ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao. '
Watoto  wa MUNGU au wateule wa MUNGU  ni wale tu waliookolewa na Bwana YESU(Yohana 1:12-13 ''Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu. '')  Hawa wakimtafuta MUNGU hakika MUNGU ataonekana kwao na kuiponya nchi yao.
Kwa njia ya maombi hakika tunamkaribia MUNGU.
Maombi ni mlango mrefu na mkubwa  kuliko zote wa kupokea kutoka ulimwengu wa roho wa nuru.

 Zaburi 34:4 '' Nalimtafuta BWANA akanijibu, Akaniponya na hofu zangu zote. ''

Kama huwa humtafuta MUNGU kwa kuishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO basi anza leo.

3. Kumtafuta MUNGU kwa kumsifu.

Matendo 16:24-26 ''Naye akiisha kupata amri hii akawatupa katika chumba cha ndani, akawafunga miguu kwa mkatale. Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba MUNGU na KUMWIMBIA NYIMBO ZA KUMSIFU, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza.
 Ghafula pakawa tetemeko kuu la nchi, hata misingi ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka, vifungo vya wote vikalegezwa.'

Huu ni mfano hai wa watu waliomtafuta MUNGU kwa kumsifu kwa nyimbo mablimbali.
Kumsifu MUNGU kumebeba siri kubwa sana ambayo watu wengi hawajui.

Kumsifu MUNGU sio kwa kuimba nyimbo tu bali hata kwa kukiri tu ukuu wa MUNGU hakika huko ni kumsifu.
Ayubu japokuwa alikuwa katika wakati mgumu sana lakini hakuona ajabu kumsifu MUNGU na kukiri nguvu zake ndio maana alishinda na kubarikiwa mara mbili kuliko mwanzo.

Ayubu 19:25 ''Lakini mimi najua ya kuwa Mteteaji wangu yu hai, Na ya kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi.''

Huku ni kumsifu MUNGU.

Hana alikuwa tasa yaani mwanamke asiyezaa lakini kwa kumsifu MUNGU na kujitabiria ushindi hakika alibarikiwa watoto 6 akiwemo mtumishi mkubwa wa MUNGU ambaye ni nabii Samweli.

1 Samweli 2:1-4 ''Naye Hana akaomba, akasema, Moyo wangu wamshangilia BWANA, Pembe yangu imetukuka katika BWANA, Kinywa changu kimepanuka juu ya adui zangu; Kwa kuwa naufurahia wokovu wako; Hakuna aliye mtakatifu kama BWANA; Kwa maana hakuna ye yote ila wewe, Wala hakuna mwamba kama MUNGU wetu.  Msizidi kunena kwa kutakabari hivyo; Majivuno yasitoke vinywani mwenu; Kwa kuwa BWANA ni MUNGU wa maarifa, Na matendo hupimwa na yeye kwa mizani.  Pinde zao mashujaa zimevunjika, Na hao waliojikwaa wamefungiwa nguvu. '' 
Hana alimtukuza MUNGU kwa kusema ''Hakuna aliye mtakatifu kama BWANA; Kwa maana hakuna ye yote ila wewe, Wala hakuna mwamba kama MUNGU wetu.''
Kumsifu MUNGU kuna faida kubwa sana.
Ndugu, usipomsifu MUNGU na kumtukuza yeye tu utamtukuza nani?
Hayupo aliye kama JEHOVAH MUNGU wetu hivyo mtukuze yeye tu.
Yeremia 10:6 ''Hapana hata mmoja aliye kama wewe, Ee BWANA; wewe ndiwe uliye mkuu, na jina lako ni kuu katika uweza. '' 

Wamtafutao MUNGU watamsifu.
 ''Zaburi 22:26 '' Wapole watakula na kushiba, Wamtafutao BWANA watamsifu; Mioyo yenu na iishi milele. ''


Biblia inatufundisha sana kuhusu kumsifu MUNGU.
Matendo makuu ya MUNGU huonekana baada ya kumsifu.
Zaburi 150:1-6 ''Haleluya. Msifuni MUNGU katika patakatifu pake; Msifuni katika anga la uweza wake.  Msifuni kwa matendo yake makuu; Msifuni kwa kadiri ya wingi wa ukuu wake.  Msifuni kwa mvumo wa baragumu; Msifuni kwa kinanda na kinubi;  Msifuni kwa matari na kucheza; Msifuni kwa zeze na filimbi;  Msifuni kwa matoazi yaliayo; Msifuni kwa matoazi yavumayo sana.  Kila mwenye pumzi na amsifu BWANA. Haleluya.''


4. Kumtafuta MUNGU kwa kumtolea matoleo.


Njia nyingine kubwa sana ya kumtafuta MUNGU ni kupitia matoleo yaani zaka na sadaka.
Malaki 3: 10-11 ''
Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema BWANA wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la. Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu ''

Njia hii ni ya muhimu sana kwa wanaomtafuta MUNGU.
Lakini ni muhimu sana kujua kwamba kumtafuta MUNGU kwa njia ya matoleo ni lazima sana tuwe watakatifu na tutoe kwa moyo wa kumpenda MUNGU na kumtii.
Ndio maana MUNGU anasema akusanyiwe wateule wanamcha hata kwa matoleo yao.
Matoleo yanaweza kutengeneza agano na MUNGU, Na ukitengeneza agano na MUNGU ujue maagano ya kipepo yatakuachia hata kama mawakala wa shetani hawataki.
Zaburi 50:5 ''Nikusanyieni wacha MUNGU wangu Waliofanya agano nami kwa dhabihu.''

Kuna siri kubwa sana na ya ushindi mkubwa sana katika matoleo yanayotoka katika moyo wa kupenda na hiari ya mtu mnyoofu.
Matoleo ni kumtafuta MUNGU na ukitumia njia hiyo kwa uaminifu ni lazima MUNGU akutendee miujiza mingi sana na kuyajibu mahitaji yako yote maana kwenye utoaji MUNGU hutazama unyenyekevu na utii kwake.
Ona maandiko haya yanayoonyesha kwamba ukimtafuta MUNGU kwa matoleo hakika atakubariki.
Zaburi 20:3-4 ''Azikumbuke sadaka zako zote, Na kuzitakabali dhabihu zako.  Akujalie kwa kadiri ya haja ya moyo wako, Na kuyatimiza mashauri yako yote.''
 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu

Comments