MAOMBI YA KUOMBEA FAMILIA YAKO NA UKOO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

 Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU wa mbinguni kisha tuombe maombi ya ushindi.
Kila mmoja ama ana familia au anatoka katika familia fulani au ukoo fulani.
Hata kundi fulani la watu wa MUNGU ambao mnafanya kazi ya MUNGU pamoja, ninyi ni familia.
Hata  kanisani kwenu unakomwabudu MUNGU mkiwa  kundi, ninyi ni familia.
Neno familia katika Biblia sijawahi kuliona lakini Biblia katika kuelezea familia hutumia neno ''Ndugu'' au ''Jamaa''
Na hilo neno ''Jamaa'' linapatikana zaidi ya mara mia katika Biblia.
Jamaa ina maana ya watu wa ukoo mmoja au familia moja.
Maana nyingine ya neno jamaa ni watu wenye uhusiano fulani.
Sehemu ya kwanza ambako neno jamaa linaonekana katika Biblia ni hapa, Mwanzo 7:1 '' BWANA akamwambia Nuhu, Ingia wewe na JAMAA yako yote katika safina; kwa maana nimekuona wewe u mwenye haki mbele zangu katika kizazi hiki.''
Siku moja niliomba mbele za MUNGU maombi ya kuuliza ni roho gani zinawaathiri wana ukoo wengi katika ukoo ninakotoka wakati huo ili niwaombee kuhusu hilo?. Baada tu ya kuomba hivvyo nilipata ufunuo wa ajabu sana, na hiyo ilikuwa ni mwaka 2011 yaani miaka mitatu baada ya mimi kuokoka. Niliambiwa kwamba ''Ukoo wako unateswa  sana  na roho ya uzinzi na uasherati, roho ya uchawi na roho ya kutegemea waganga wa kienyeji''  niliambiwa kwamba sio roho hizo tu zinazowatesa ukoo wangu bali ziko nyingi ila hizo tatu zimewaathiri wengi zaidi katika ukoo. Nilianza kuombea nikiharibu roho hizo za kishetani ili ziwaachie watu wa ukoo wangu.
Ndugu, hata wewe inawezekana familia yako au ukoo wako wanateswa na roho za pombe, uongo, kuabudu sanamu n.k.
Inawezekana familia yako imegeuka nyumba ya kukaa majini na mizimu.
Inawezekana familia yako wako kwenye adhabu za kipepo siku zote.
Yako mambo mengi sana yanaweza kuwatesa watu tu wa ukoo fulani au familia fulani.
Ndugu mmoja siku moja aliniambia jambo la ajabu sana akisema kwamba anaumwa kisukari, kisha akaniambia kwamba kila mwanaume katika familia  yao akifikisha miaka 40 anaugua kisukari, Akasema hata baba yake na babu yake wote walikufa katika daraja hilo la umri na kifo chao kilikuwa ni cha ugonjwa wa aina moja tu yaani kisukari.
Ndugu unayesoma ujumbe huu naomba tambua kwamba maombi ya kina kuhusu familia yako au ukoo wako ni ya muhimu sana sana maana unaweza kufuta hata ratiba za kishetani zilizoamuriwa katika ulimwengu wa giza ziwapate.
Kuna familia kila mwaka lazima wazike mtu mmoja au zaidi, yaani kila mwaka lazima iwe hivyo, mengine ni hila za shetani na sio mapenzi ya MUNGU.
Wewe uliyeokoka kumbuka sana kwamba wewe ni lango, unahitaji kusimama imara kimaombi ili watu wa familia yako wafunguliwe vifungo vya kipepo.
Inawezekana MUNGU ametafuta sana mtu aliyeokoka katika ukoo wenu atakayesimama imara kimaombi ili kuwafungua watu wa ukoo wenu walioathiriwa na shetani.
Ezekieli 22:30 '' Nami nikatafuta mtu miongoni mwao, atakayelitengeneza boma, na kusimama mbele zangu mahali palipobomoka, kwa ajili ya nchi, nisije nikaiharibu, lakini sikuona mtu.''
Wewe uliyeokoka ndiye unayetakiwa kuitengeneza boma, kutengeneza nchi kimaombi na kutengenea familia yako na ukoo kimaombi.
 Bwana YESU anapokuokoa huwa anakupa na mamlaka ya kuharibu nguvu zote za yule adui shetani na mawakala zake ''Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru.-Luka 10:19''
Hakikisha sasa unaitumia mamlaka hiyo ya KRISTO katika maombi ili kuwafungua ndugu zako.

Baadhi ya mambo ya kiroho yanayoweza kuathiri familia yako au ukoo wako ni haya.

1. Kuzaliwa hatiani.
Zaburi 51:5 '' Tazama, mimi naliumbwa katika hali ya uovu; Mama yangu alinichukua mimba hatiani.'' 
Kuzaliwa hatiani ina maana hizi kwa ufupi.
a. Ulikuwa matokeo ya uzinzi na uasherati.
Yaani mama yako alikuwa katika kufanya dhambi ya uasherati au uzinzi ndipo ukazaliwa wewe, (nashuhudiwa rohoni sasa kuna mtu ataogopa sana baada ya kusoma ujumbe huu.)
Wako wanawake huzaa bila kuwa katika ndoa, ndugu huo sio mpango wa MUNGU. Dawa ni kuacha uzinzi na uasherati, ukitoa mimba ili kukwepa kumzaa mtoto hatiani wewe unakuwa mjinga mara mia kuliko anayezaa mtoto hatiani, Hivyo epuka sana uzinzi na uasherati bali subiria ndoa yako.
Wako watu wengi sana wamezaliwa hatiani yaani mama zao walichukua mimba zao hatiani, kama ni wewe tubu kwa MUNGU sasa na hakikisha sasa hurudii kosa la mama yako.

b. Kutumia uganga ili kupata mtoto.
Wako watu mama zao walichukua mimba zao hatiani yaani walikwenda kwa waganga kutumia nguvu za giza ili wapate watoto, huko ni kuzaliwa hatiani.

c. Maneno mabaya kuhusu mtoto atakayezaliwa.
Inawezekana ulizaliwa hatiani kwa sababu wazazi wako walikukataa tangu kabla hujazaliwa, inawezekana ulifungwa vifungo kabla hata hujazaliwa.

d. Wazazi wako au mababu zako kuingia agano la kishetani kabla hujazaliwa.
Ngoja nikupe mfano, kuna nchi zinatawaliwa kifalme, hivyo inakuwa inajulikana tangu kabla mtoto hajazaliwa kwamba ni mtoto wa ngapi wa nani atakuja kuwa mfalme au malikia, hilo ni agano jema lakini sasa wako watu huingia agano baya la kipepo kwa ajili ya watoto wao baada yao.
Inawezekana umezaliwa hatiani kwa sababu wazazi wako au mababu zako kabla hujazaliwa walikupangia nafasi mbaya na za kipepo, kuna koo mtoto fulani anapozaliwa wanafanya sherehe kubwa na kufanya matambiko na maagano wakisema kwamba mtoto aliyezaliwa atarithi mikoba ya bibi au ya babu, ukiuliza hiyo mikoba  utashangaa ni mikobo ya uchawi na uganga.

 2. Kurithi mambo mabaya na ya kipepo.
Maombolezo 5:7-8 ''Baba zetu walitenda dhambi hata hawako; Na sisi tumeyachukua maovu yao.  Watumwa wanatutawala; Hakuna mtu wa kutuokoa na mikono yao.''
 Biblia inaonyesha kwamba wazazi au mababu wanaweza wakakosea na uzao wao kuja kurithi makosa hayo au maovu hayo.
Inawezekana ukoo wenu mmerithi ulevi hivyo kila mtoto katika ukoo wenu tangu akiwa mtoto mdogo anakuwa mlevi, hapo utambue kwamba mnateswa na madhabahu za kipepo za pombe.
Ukichunguza famili yako au ukoo wako kwa jicho la rohoni utagundua kabisa nini ukoo wako wamerithi kibaya kutoka kwa mababu.
Inawezekana kabisa madhabahu ya shetani ya uganga, uchawi n.k  inaishi katika ukoo wako au familia yako.
Inawezekana ninyi sasa ni watumwa wa mawakala wa shetani kwa sababu tu ya mambo ya kurithi ya ukoo.
Mambo ambayo familia inaweza kuyarithi kutoka katika ukoo au mababu baadhi ni haya;
1. Kurithi dhambi, makosa na uovu.
2. Kurithi adhabu za kipepo ambazo zilitokana na makosa ya mababu zako au wazazi wako.
3. kurithi maagano ya kishetani.
4. Kurithi vifungo vya giza.
5. Kurithi tabia mbaya za kipepo.
6. Kurithi mapokeo au mafundisho ya kishetani.
 Ndugu yangu, Bwana YESU anasema jililieni ninyi na watoto wenu.
Luka 23:28  '' ........  bali jililieni nafsi zenu na watoto wenu.''
Ni nafasi yako leo kulia mbele za MUNGU ukiwaombea ndugu zako ili Bwana YESU awafungue vifungo vya giza.
Inawezekana hata wewe kuna mambo mabaya yanayokupata kwa sababu kuna maneno mabaya babu yako alitamkiwa zamani sana ambayo yanafuatilia kizazi chake chote, unahitaji kufuta maneno hayo kwa damu ya YESU KRISTO.
Kuna familia au koo hakuna hata mmoja amewahi kufunga ndoa takatifu kanisani.
Kuna familia wanawake wote walizalia nyumbani na kuolewa imekuwa shida.
Wakati mwingine wewe uliyeokoka unaweza kunielwa vizuri zaidi maana ulipookoka ulikutana na vita kubwa kutokea familia au ukoo kwa sababu tu wewe unaomba ili kutoka katika agano la kipepo la ukoo n.k
Inawezekana familia yako au ukoo wako hawakumcha MUNGU ndio maana shetani alipata nafasi katika ukoo na kuwawekea kalenda ya kipepo ya vifungo ambayo inampata kila mwana ukoo.
Ona mfano huu ambapo MUNGU anawashangaa waliomwacha yeye na kufuata ubatili, ni hatari mno.
Yeremia 2:5 '' BWANA asema hivi, Baba zenu waliona dhuluma gani kwangu, hata wakafarakana nami, wakafuata ubatili, nao wakawa ubatili? ''
Ndugu uliyeokolewa na Bwana YESU hakika unayo nafasi sana ya kuombea sana ukoo wako au familia yako.
Ayubu yeye alikuwa anaiombea familia yake hata kuwatolea sadaka kwa MUNGU ili MUNGU awarehemu.
Ayubu 1:5 '' Basi ilikuwa, hapo hizo siku za karamu zao zilipokuwa zimetimia, Ayubu hutuma kwao akawatakasa, kisha akaamka asubuhi na mapema, na kusongeza sadaka za kuteketezwa kama hesabu yao wote ilivyokuwa; kwani Ayubu alisema, Yumkini kwamba hawa wanangu wamefanya dhambi, na kumkufuru MUNGU mioyoni mwao. Ndivyo alivyofanya Ayubu sikuzote.''
 Ndugu unahitaji sana kuombea familia yako, ombea uzao wako, ombea watoto wako na hata ukipata msukumo wa kutoa sadaka kwa ajili yao toa maana sadaka inaishi siku zote.
Itabilie mema familia yako.
Wako watu bado wanatembea na laana za mababu au laana za wazazi wao au laana za ndugu zao.
Na kanuni ya laana ni kwamba mkubwa kiroho ndiye humlaani mdogo kiroho.  Ili laana ifutike inahitaji nguvu kubwa zaidi kuliko mtoa laana.
Ndio maana Bwana YESU alikuja ili kuharibu nguvu zote za giza.
1 Yohana 3:8 ''........ Kwa kusudi hili Mwana wa MUNGU alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi.''
 Hivyo ni damu ya YESU KRISTO pekee iliyo na nguvu kuliko watoa laana wote duniani.
Kirahisi kabisa unaweza kwa damu ya YESU KRISTO kufuta laana zote kuhusu wewe, muhimu tu hakika uko ndani ya YESU KRISTO yaani umempokea kama Mwokozi wako na unaishi maisha matakatifu ya wokovu katika yeye.
Ukiita damu ya YESU KRISTO ya agano hakika itafuta laana zote, haijalishi watoa laana ni wakubwa kiasi gani.
Jina la YESU KRISTO liko juu ya watoa laana wote, hivyo kwa jina la YESU KRISTO laana kufutika ni jambo la muda mfupi sana.
Nguvu za ROHO MTAKATIFU zinaweza kukutenga mbali na laana zote kwa muda mfupi sana.
Neno la MUNGU la ufunuo wa ROHO MTAKATIFU linaweza kutangaza mwisho wa laana zote kwako na kwa uzao wako.

 Baadhi ya maombi muhimu ya kuombea familia yako au ukoo wako ni haya.

1. Tubu kwa ajili ya makosa ya wana familia au ukoo wako.

2. Omba Neema ya wokovu wa KRISTO kwa wahusika wote wa familia yako au ukoo.

3. Haribu vifungo vya giza vilivyowafunga wana familia au ukoo.

4. Watenge ndugu zako na maagano ya kishetani.

5. Haribu na kufuta kila tabia mbaya  za kurithi, dhambi za kurithi, mila za kurithi za kipepo pamoja na mizimu ya ukoo iharibu.

6. Nyunyuzia damu ya YESU KRISTO ya agano katika kila kifungo cha giza au mikataba ya giza, ukiamuru vifungo hivyo na mikataba hiyo ifutike na kuwaachia ndugu zako na jamaa yako.

7. Futa adhabu za kipepo zote zinazotokana na mikataba ya kishetani katika familia au ukoo.

8. Omba Bwana YESU amiliki na kutawala roho  ya kila mwana familia au ukoo.

9. Haribu mbinu za kishetani  za kuivuruga familia au kuisambalatisha.

10. Omba roho ya msamaha kwa kila mwana familia.
Luka 6:37 '' Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa.''

 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane na nitakujulisha jinsi ya kukipata na  Naamini kitakusaidia sana.
Hapa chini ni
MAOMBI YA KUOMBEA FAMILIA YAKO NA UKOO.  Maombi haya naomba yamsaidie mtu yule ambaye hajui kuomba ili katika kuomba kwa kutumia hayo basi atakumbuka mahitaji yake na kuyataja katika maombi yake. Haya hapa chini ni maombi ya kuanzia tu katika maombi yako ili uendelee zaidi kuomba
Kwa waombaji wazoefu naamini baada tu ya kulisoma somo na kulielewa basi anajua aombee nini maana alikuwa anaandika points za kuombea. Kumbuka pia fundisho ni muhimu kuliko maombi hivyo wewe ambaye huwa unahusika na maombi tu hakikisha unajifunza kwanza somo lote ndipo utapata nguvu za kuomba na kushinda. 

 
 
MAOMBI YA KUOMBEA FAMILIA YAKO NA UKOO.

 MUNGU wangu  wa mbinguni ninakuabudu, naungana na maserafi na makerubi  na malaika wote wa nuru kukuabudu wewe YAHWEH MUNGU wa pekee.
Niko mahali hapa mimi na familia yangu na ukoo wangu nikiomba toba kwa ajili ya makosa ya wana familia yangu na wana ukoo wangu wote.
Eee MUNGU Baba naomba utusamehe makosa yetu yote, dhambi zetu zote na maovu yetu yote.
Tusamehe Eee MUNGU kwa makosa ya kiukoo yaliyosababisha laana au balaa zisizoisha katika familia yangu na ukoo wangu, naomba utusamehe na sasa balaa hizo na migogoro hiyo ifutike kwa damu ya YESU KRISTO.
Nisamehe MUNGU wangu kwa ajili yangu mwenyewe, nisamehe kwa ajili ya familia yangu, nisamehe kwa ajili ya ukoo wangu, nisamehe kwa ajili ya ndugu zangu na nisamehe kwa ajili ya uzao wangu na uzao wa tumbo la mama yangu na bibi yangu.
Ninawaombea neema ya wokovu wa KRISTO ndugu zangu wote, naomba neema hiyo ya wokovu iwapate baba zangu wote walio hai, mama zangu wote walio hai, watoto wangu wote na kila ndugu yangu katika ukoo. Eee Bwana YESU uliyeokoa wengi naomba na ndugu zangu uwakumbuke katika ufalme wako, wape neema yako ya wokovu na wape kuishi maisha matakatifu siku zote za maisha yao.
Naomba Eee Bwana YESU KRISTO umiliki na kutawala kila roho ya mwana familia, miliki Bwana YESU kila roho ya kila mmoja ili asiende upotevuni bali aingie katika raha yako ya milele.
Nawaombea pia ndugu zangu kila mmoja moyo wa msamaha.
Wako ndugu waliokosana na ndugu wengine na kubeba visasi vikali moyoni, Eee MUNGU wa uzima ninaomba uwaumbie moyo wa msamaha.
Neno lako   Bwana YESU linasema '' Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa.-Luka 6:37 ''
Waumbie moyo wa msamaha kila mmoja, kila aliyekosewa aachilie na sio kubeba visasi. Tusaidie Eee MUNGU Muumbaji wetu ili kama familia tusiwe na matengano, mafarakano wala migogoro.
Niko pia mahari hapa nikiharibu kila kifungo cha kichawi au cha kiganga kilichowafunga ukoo wangu au familia yangu, Nakifuta kifungo hivyo kwa damu ya YESU KRISTO.
Kila kifungo cha dhambi na kifungo cha laana, Nakifuta kifungo hivyo kwa damau ya YESU KRISTO.
Kila kifungo cha pombe na sigara,Nakifuta kifungo hivyo kwa damau ya YESU KRISTO.
Kila kifungo cha uzinzi na uasherati, Nakifuta kifungo hivyo kwa damau ya YESU KRISTO.
Kila kifungo cha mizimu na majini mahaba, Nakifuta kifungo hivyo kwa damau ya YESU KRISTO.
Kila kifungo masengenyo, wivu na husuda, Nakifuta kifungo hivyo kwa damau ya YESU KRISTO.
Kila kifungo kutoka madhabahu za giza kuja kwenye familia yangu au ukoo wangu, Nakifuta kifungo hivyo kwa damau ya YESU KRISTO.
 Kila kifungo cha magonjwa ya kutengenezwa kichawi, Nakifuta kifungo hivyo kwa damau ya YESU KRISTO.
Enyi wakuu wa giza na kazi zenu tokeni katika familia yangu na ukoo wangu, kwa jina la YESU KRISTO nawaamuru sasa mtoke na msirudi tena.
Enyi majini na mizimu katika familia yangu na ukoo wangu, kwa jina la YESU KRISTO nawaamuru sasa mtoke na msirudi tena.
Enyi roho za nyoka na roho za mbwa na mbuzi katika familia yangu na ukoo wangu, kwa jina la YESU KRISTO nawaamuru sasa mtoke na msirudi tena.
Nahabribu kila hila ya kishetani ya kuivuruga familia yangu au ukoo wangu, kwa jila la YESU KRISTO nimeharibu mbinu hizo za giza na hazitakuja kwetu tena milele.
Nakataa  na kufuta kila adhabu ya kipepo ya kifamilia au kiukoo.
adhabu zote kutoka ulimwengu wa roho wa giza nazifuta kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Kila adhabu ya magonjwa na ajali vilivyoamuriwa kipepo ili viipate familia yetu, naziharibu adhabu hizo na kuzitoweshwa kwa jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu aliye hai. 
Kila adhabu ya kutengwa na kuonewa, naziharibu adhabu hizo na kuzitoweshwa kwa jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu aliye hai. 
Kila kifo kinachopangwa kipepo ili kimpate yeyote katika familia yangu au ukoo wangu nafuta mpango huo na sasa tutaishi katika jina la YESU KRISTO.
Kila adhabu ya kichawi ya kuzuiliwa kufanikiwa kiuchumi,naziharibu adhabu hizo na kuzitoweshwa kwa jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu aliye hai.
Kila adhabu ya kiganga au kichawi na kila adhabu ya majini au mizimu au wakuu wa giza, naziharibu adhabu hizo na kuzitoweshwa kwa jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu aliye hai.
 Kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO nazifuta na kuzitowesha kila tabia mbaya  za kurithi, dhambi za kurithi, mila za kurithi za kipepo pamoja na mizimu ya ukoo naiharibu kwa damu ya YESU KRISTO.
 Nanyunyuzia kwa  damu ya YESU KRISTO kwenye kila kifungo cha kipepo kilichomfunga mtu wa familia yangu au ukoo wangu, na sasa namuru kwa damu ya YESU KRISTO nikifuta vifungo hivyo vyote.
Mimi ni mshindi kwa sababu YESU KRISTO ndiye Mwokozi.
Katika jina la YESU KRISTO nimeomba na najua nimeshinda.
Ninakushuru MUNGU Baba maana umenipa ushindi mkuu.
Katika jina la YESU KRISTO nimeomba na kupokea ushindi na sasa ninashukuru.
 Amen Amen Ameeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeen.
Hakika umeshinda. Ukiweza kufunga unaweza kufunga hata siku 1 au 3 au 4 au hata 5 au zile ambazo wewe utaona unaweza ukihusika kila siku na kipengele kimoja kuombea na kumbuka baada ya maombi ya kufunga au hata maombi ya bila kufunga fanya tendo la imani kwa MUNGU kwa kutoa sadaka nzuri itakayoambatana na maombi  juu ya ukomo wa kuteswa na maadui zako katika ulimwengu wa roho
Nawaonya pia wanaotumia masomo yangu vibaya na kwa manufaa yao waache tabia hiyo.
 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? 
Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsap).
+255786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments