NANI ANATAKIWA AWE MWINJILISTI?


       Watu wengine, kwa kukosa mafundisho, wanafikiri kwamba kazi ya uinjilisti, inafanywa tu na Wainjilisti, Wachungaji, Walimu au Mitume na Manabii waliowekwa na Mungu maalum kwa kazi hiyo na kupewa karama mbalimbali. Hii ni mbinu ya Shetani ya kufanya kazi hii ifanyike kwa viwango vya chini, ili yeye afurahi kuona wengi wanaangamia. Wainjilisti, Wachungaji, Walimu, au Mitumne na Manabii; ni Makomanda au viongozi wa Jeshi, na watu wengine waliookoka ni askari wa jeshi hili la Kristo Yesu ( 2 TIMOTHEO 2:3 ). Je, ni jeshi gani la nchi yoyote linaloweza kushinda ikiwa watakaopigana ni makomanda wa jeshi hilo tu na askari wengine hawashiriki kupigana? Jeshi la namna hiyo, ni lazima litashindwa vibaya. Askari wa kawaida, ndiyo wengi sana na katika nchi yetu, Tanzania, wanaitwa wapiganaji, maana bila wao, makomanda hawawezi kufanya kazi hiyo wenyewe. Kazi ya makomanda ni kuwa mstari wa mbele wa mapigano, na kuwaongoza  maaskari wengine kuleta ushindi.Hivi ndivyo walivyofanya Kanisa la kwanza. Uinjilisti, haukuachwa kwa Mitume tu, pamoja na karama walizokuwa nazo; bali wote, wanaume na wanawake katika Kanisa la kwanza walishiriki katika kufanya Uinjilisti ( MATENDO 2:17-18 ).. Hata pale ambapo mitume walibaki Yerusalemu, wengine wote katika Kanisa, walitawanyika nakwenda kulihubiri Neno. Ndiyo maana, Kanisa la Kwanza, liliupindua ulimwengu wa nyakati zao ( MATENDO 8:1, 4 ). Mafundisho mengine ya Biblia, pia yanaoana na jambo hili. Kila mtu aliyeokoka, amefanywa kuwa mfalme na kuhani ( UFUNUO 5:9-10; UFUNUO 1:5-6 ).Utukufu wa Mfalme ni wingi wa watu wake, na uchache wa watu wake ni uharibifu wake ( MITHALI 14:28 ). Mtu ambaye  hana hata mtu mmoja katika milki yake, hawezi kudai kwamba ni mfalme. Mfalme wa nani? Mfalme wa hewa? Vivyo hivyo, mtu aliyeokoka ambaye hana mtu yeyote katika milki yake aliyempata kwa uinjilisti, huyu ni mfalme wa hewa. Kazi ya Kuhani pia, ni kumpatanisha mtu aliyetenda dhambi, na Mungu wake, kwa kumfanya mtu yule kupata msamaha wa dhambi kutoka kwa Mungu (MAMBO YA WALAWI 6:1-2, 6-7 ). Kwa misingi hiyohiyo, kila mtu aliyeokoka, kwa kufanywa Kuhani; amepewa na Yesu Kristo, huduma ya upatanisho, kuwapatanisha wenye dhambi pamoja na Mungu wao ( 2 WAKORINTHO 5:17-18 ). Kama Kristo alivyotumwa na Baba, anatutuma sisi pia kufanya huduma ya upatanisho. Tusipofanya uinjilisti kwa wenye dhambi, tunawafungia katika dhambi. Tukiwa wavuvi wa watu, tunafanya watu hao waondolewe dhambi, maana watamwitaje Yesu  bila kumsikia mtu akiwahubiri? ( YOHANA 20:21, 23; WARUMI 10:13-14 ). Tukiwafungia watu katika dhambi kwa kuacha kufanya uinjilisti, tunamuwekea Mungu moshi machoni pake na kumfanya atoe machozi, na vile vile tunampa siki anywe na kumfanya apate ganzi kwenye meno. Siyo vema kwetu  kumfanyia hivyo Mungu ikiwa kweli tumeokolewa ( MITHALI 10:26 ). MUNGU awabariki

Comments