SIFA SAHIHI ZA MUME MWEMA

 1.Aliyesimama katika imani na Mwenye uwezo wa kuiongoza familia yake: - 1 Wakorintho 11:3 “Lakini nataka mjue ya kuwa kichwa cha kila mwanamume ni Kristo, na kichwa cha mwanamke ni mwanamume, na kichwa cha Kristo ni Mungu.” Napenda uelewe kwamba Kristo ni kichwa cha kila mwanamume, kama vile mume alivyo kichwa cha mkewe, na Mungu ni kichwa cha Kristo. Waefeso 5:23 “Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili.” naye mwenyewe Kristo ni Mwokozi wa kanisa. Ikumbukwe huyu ndiye ana uamuzi wa mwisho katika familia akiamua kuukana ukristo, kurudi nyuma inakuwa na athari kubwa sana katika familia. Hivyo hii ndio nguzo ya ndoa ya Kikristo.

Inashangaza kuona baadhi ya waume hawawezi kusimama kama viongozi katika nyumba zao. Wanasahau kama Mungu kawaweka kama viongozi wa familia na mke ni msaidizi wake. Utakuta wengine wanaaacha jukumu hilo kwa mkewe kwa kupenda au kwa kutokupenda na wengine wanajikuta wamewafanya wazazi wao au ndugu zao wengine kusimama kama viongozi wa familia. Biblia inaweka wazi kuwa mume ni kichwa cha ndoa, ni lazima kila mume atambue hilo na ahakikishe anasimama kwenye nafasi yake kwa uaminifu bila kujali hali yake, wadhifa, kipato, huduma au chochote kile.

2.Awe mwenye kumcha Mungu: - Mume mwema ni yule anayeheshimu nafasi ya Mungu katika maisha yake, anayemcha Mungu na kuepukana na uovu wa kila aina. Anatambua kwamba Mungu ndiye anayepaswa kuongoza maisha yake na si vinginevyo. Kumbukumbu la Torati 6:5 “Nawe mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote.”

3.Mwenye kumheshimu mke wake: - Imezoeleka kuwa mke ndiye anayepaswa kumheshimu mume, lakini biblia inawataka pia waume kuwaheshima wake zao na kuishi nao kwa akili. Haipaswi mume kufanya maamuzi yoyote yanayohusu familia bila kumshirikisha mke wake, yawe madogo kama lini mgeni fulani aje hadi makubwa kama ujenzi au kuanzisha biashara. Mke ni sehemu ya mume hivyo ni lazima mume ampe heshima yake na kuthamini mawazo yake na mchango wake hata kama mke hafanyi kazi ya kuingiza kipato. Kumbuka mke anabeba jina la mume wake na ni sehemu ya mume wake, inahuzunisha kuona wanaume wengine wakiwadharau wake zao mbele ya ndugu zao au marafiki. Haipasi kabisa kumgombeza au kumsema vibaya mke wako mbele za watu, iwe ni ndugu, watoto au mwingine yeyote. 1 Petro 3:7 “Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe.”

4.Mwenye kumpenda mke wake kama nafsi yake: - Kumpenda mke wake zaidi ya kitu chochote iwe ni wazazi, kazi, biashara, watoto n.k. Mume mwema siku zote huthamini nafasi ya mke katika maisha yake na mara zote mke wake ni namba moja kwake. Waefeso 5: 25, 28 “Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe.”

Waefeso 5:33 “Lakini kila mtu ampende mke wake kama nafsi yake mwenyewe; wala mke asikose kumstahi mumewe.” Upendo ni nguzo ya Pili na pia ni moja ya tunda la Roho katika ndoa. Hapa naomba nieleze hii ndoa inayoongelewa ni ya Kikristo hivyo upendo huu hauwezi kuutenga na upendo wa Kristo kwa ujumla, je upendo unaelezwaje katika Biblia:

a.Huleteana heshima Warumi 12:10 “Kwa pendo la udugu, mpendane ninyi kwa ninyi; kwa heshima mkiwatanguliza wenzenu” Pia Waheshimuni wengine kuliko mnavyojiheshimu wenyewe.

b.1 Wakorintho 13:4-8 “4 Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; 5 haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; 6 haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; 7 huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote. 8 Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika.”

Hapo Tunajifunza Upendo Kuwa:

a)Hufadhiliana: Atakupa mahitaji yako bila kujali nani anazalisha zaidi, hatajali cheo au elimu yako. Maana katika ndoa mwingine anaweza panda zaidi ya mwingine lakini sio sababu ya kumwacha kwa kujiona utaonekana duni. (kuwa na kiburi). Mstari wa 4

b)Hauna ubinafsi; husameheana: Hatatunza makosa yake moyoni atasamehe na kusahau, haujihesabii haki. Mstari wa 5

c)Huonyana: atakwambia kama unakosea na siyo kukuacha upotee na marafiki wabaya. Mstari wa 6
d)Hustahimiliana: hata uwe mgumba, mlemavu, unakasoro gani atakuvumilia. Mstari wa 7

e)Hauna ukomo au mipaka: Atakupenda hadi kifo sio siku anaamka “mimi na wewe basi.” Mstari wa 8

5.Heshima na huruma: - Heshima humfanya mtu ajione unamjali, wanaume wengine atasema anapenda lakini anamwita mwenzie hajasoma, ametoka familia duni, hafanani na hali yangu, kwakweli huku ni kumdhalilisha mwenzio 1 Petro 3: 7-9 “Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe. Neno la mwisho ni hili; mwe na nia moja, wenye kuhurumiana, wenye kupendana kama ndugu, wasikitikivu, wanyenyekevu; watu wasiolipa baya kwa baya, au laumu kwa laumu; bali wenye kubariki; kwa sababu hayo ndiyo mliyoitiwa ili mrithi Baraka”

6.Amtimizie haja zake za kimwili: - 1 Korintho 7: 3-5 “Mume na ampe mkewe haki yake, na vivyo hivyo mke na ampe mumewe haki yake. Mke hana amri juu ya mwili wake, bali mumewe; vivyo hivyo mume hana amri juu ya mwili wake, bali mkewe. Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkajiane tena, Shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu.”

7.Mwenye kulea na kuwafundisha watoto njia inayopasa: - Mume ndiye baba pia hivyo asiishie kupenda mke tu watoto hajui wanasoma vipi, wanaishi vipi, anaacha malezi na makuzi yote kwa mama, siku watoto wakiharibika anaanza kumlaumu mama. Watoto wanahitaji wazazi wote wawili ili kukua katika mwenendo mzuri wa maadili ya Kikristo. 1 Timotheo 3:4 “mwenye kuisimamia nyumba yake vema, ajuaye kutiisha watoto katika ustahivu” Aweze kuisimamia nyumba yake vizuri akiwafanya watoto wake kuwa wanyenyekevu na wenye heshima katika hali zote.

Mume kama kiongozi wa familia anajukumu la kuwafundisha watoto njia inayofaa akisaidiana na mke wake. Waume wengi wanafikiri kazi ya kuwafundisha watoto ni ya mama wao ni kutoa tu adhabu pale wanapoona mtoto amekosea lakini hawajishughulishi katika kuwafundisha. Mume mwema lazima alitambue jukumu lake la kuwafundisha watoto neno la Mungu na misingi ya maisha ya mkristo. Kumbukumbu la Torati 6: 6-7 “Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako; nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo.”

Waefeso 6:4 “Nanyi, akina baba, msiwachokoze watoto wenu; bali waleeni katika adabu na maonyo ya Bwana.”

8.Mwenye Kuihudumia Familia Yake: - Mume mwema lazima ahakikishe anafanya kazi na kuipatia familia yake mahitaji ya kila siku. Haijalishi mkewe anafanya kazi au la, yeye kama mume anajukumu la kuihudumia familia yake na hii ni sehemu ya uongozi wake. Hapa pia inajumuisha na kuilinda familia yake juu ya hatari zote na kuhakikisha wana furaha na amani ya kudumu. Ili mke na watoto waweze kuwa na amani ni lazima wahakikishiwe usalama wao kimwili, kiroho na kiuchumi. 1 Timotheo 5:8 “Lakini mtu ye yote asiyewatunza walio wake, yaani, wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana Imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini.”

9.Aiheshimu ndoa / asiwe mzinzi: - Kuna wanaume ambao anaweza kukupatia mahitaji yote muhimu, lakini ni mzinzi tena wala hafichi, hii kwakweli ndio sababu kubwa ya kuvunjika ndoa nyingi sasa hivi. Ulipoapa mbele za Mungu utampenda mwenzio hadi kifo iweje uchangie upendo huu na wengine, hapa ni kama umesema “nilikupenda lakini sasa nimepata mwingine hivyo unamruhusu aondoke katika ndoa yenu” wengine hawaishii hapa anafukuza na kuoa mwingine kabisa. Mwanamke anahitaji kuona kuwa yeye ndiye pekee anayepewa upendo huu na mumewe na sio kuchangia na msururu wa wenza. Waebrania 13:4 “Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu.” na wenye ndoa wawe waaminifu kwa wenzi wao; maana Mungu atawahukumu wazinzi na waasherati. Mathayo 19:9-11 “Nami nawaambia ninyi, Kila mtu atakayemwacha mkewe, isipokuwa ni kwa sababu ya uasherati, akaoa mwingine, azini; naye amwoaye yule aliyeachwa azini. Wanafunzi wake wakamwambia, Mambo ya mtu na mkewe yakiwa hivyo, haifai kuoa. Lakini yeye akawaambia, Si wote wawezao kulipokea neno hili, ila wale waliojaliwa.”

10.Anayejitegemea kwa kimawazo na mali: - Kuna waume ambao pamoja na umri wa kuoa bado anategemea baba, mama, kaka, dada kwa mahitaji yake na pia hata mawazo afanye nini. Sio vibaya kukaa na ndugu hasa kama ni wema na wanatabia nzuri pia wasioingilia ndoa yako. Na ni vizuri pia kupata ushauri wa waliotuzidi katika mambo mbalimbali unayotaka kufanya lakini isiwe ni kikwazo cha upendo, heshima na uhuru wa ndoa yenu. Mume awe anajitegemea awe mbunifu akimshirikisha mkewe ili pamoja waweze kujitegemea na sio kutegemea wazazi hadi kutawaliwa hapa hata uimara wa Imani yake unaegemea huko anakofadhiliwa.

Marko 10:7 “Kwa sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe” Hapa ina maana aweze kumtunza mkewe na familia pamoja na kumwezesha, ila wanawake tuwe na kiasi katika kutumia hiki kifungu hususan mavazi yatupasayo.

1 Petro 2: 3 – 6 “ikiwa mmeonja ya kwamba Bwana ni mwenye fadhili. Mmwendee yeye, jiwe lililo hai, lililokataliwa na wanadamu, bali kwa Mungu ni teule, lenye heshima. Ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mmejengwa mwe nyumba ya Roho, ukuhani mtakatifu, mtoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na Mungu, kwa njia ya Yesu Kristo. Kwa kuwa imeandikwa katika maandiko Tazama, naweka katika Sayuni jiwe kuu la pembeni, teule, lenye heshima, Na kila amwaminiye hatatahayarika.”

Kujipamba kwenu kusiwe kwa nje, yaani: kwa kusuka nywele, kujipamba kwa dhahabu na kuvaa mavazi maridadi. Bali kujipamba kwenu kuwe katika utu wa ndani wa moyoni, kwa uzuri usioharibika, wa roho ya upole na utulivu. Uzuri wa namna hii ni wa thamani sana mbele za Mungu. Maana ndivyo walivyojipamba wanawake watakatifu wa zamani, waliomtumaini Mungu na kuwa wanyenyekevu kwa waume zao.

1Timotheo 2: 9 – 10 “Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani; bali kwa matendo mema, kama iwapasavyo wanawake wanaoukiri uchaji wa Mungu.”

KWA UJUMLA SIFA ZA MUME MWEMA ni:

1.Ametulia si macho juu juu kama nzi kila akionacho hata kichafu chaliwa.
2.Anajiheshimu, anamuheshimu mkewe, ndugu wa pande zote, watu wengine pamoja na majirani pia.
3.Mwenye huruma na mapenzi ya kweli kwa mke na familia kwa ujumla.
4.Mtunzaji wa familia na si bahili au mfujaji wa mali.
5.Mcha mungu, au mwenye utu.
6.Mchapa kazi, asiye kata tamaa, si mvivu na goi goi
7.Msaidizi, sio mke na jembe na kuni yeye kashika bakora anapunga mkono, shughuli zote za uzalishaji mali na utunzaji familia kamuachia mke.
8.Mwenye kupenda kujadiliana, sio amri ikitoka imetoka hata kama pumba zenye madhara mradi yeye kasema basi naibaki kuwa hivyo.
9.Mwenye kutimiza wajibu wake kwenye masuala ya unyumba, sio mume jina, "chakula" anakula barabarani mkewe anabaki na “njaa”
10.Mwenye kuona wivu kwa mkewe sio kila mtu basi ruksa kula "chakula" nyumbani kwake ilimradi yeye kaoa basi kaolea jamaa na marafiki.

________________________________________

Comments