Yohana 14:16-17‘Nami nitamwomba baba, naye atawapa msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata akae milele; ndiye roho wa kweli amabye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui bali ninyi mnamtambua , maana anakaa kwenu na atakuwa ndani yenu.Kabla Bwana wetu Yesu hajapaa kwenda mbinguni aliyasema maneno hayo hapo juu akiwaeleza kwamba si muda mrefu yeye ataondoka kwa kuwa wajibu alioujia ameumaliza (Yohana 17:4) na kwa sababu hiyo atamwomba baba (Mungu) ili awape msaidizi mwingine yaani Roho mtakatifu. Kwa lugha nyepesi hapa Yesu alikuwa akimtambulisha Roho mtakatifu kwa wanafunzi kama msaidizi mwingine badala yake. Lengo la waraka huu ni kujifunza, je Roho mtakatifu kwa namna gain ni msaidizi?
Roho mtakatifu ni msaidizi katika nyanja zifuatazo;
*Msaidizi katika kutufundisha na kutukumbusha.
Ndani ya biblia kuna mafumbo mengi sana ambayo bila msaada wa Roho kutusaidia kuyafunua kwetu hakuna anayeweza kuyaelewa wala kuyajua. Hivyo Roho mtakatifu ni wa muhimu kwetu kwani anatusaidia kuyaelewa mawazo ya Mungu katika neno lake.
*Msaidizi katika kutushuhudia juu ya Yesu (Yohana 15:26).
Hapa Roho mtakatifu anafanya kazi ya kutushuhudia hata sasa juu ya uweza na nguvu za Yesu Kristo na utendaji wake. Mfano mzuri ni pale baada ya Yesu kupaa na kuwaacha mitume na walipoanza kuandika nyaraka zao, ni Roho mtakatifu aliyewashuhudia na kuwakumbusha zaidi kimapana juu ya uweza wa Yesu .Neno atanishuhudia lina maana Roho mtakatifu atawafunulia habari zangu(Yesu) na kuwahakikishia kwamba mimi ndiye ninayewaagiza.
*Kuuhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, haki na hukumu.
(Yohana 16;8) Huu wajibu unahusishwa na kufanya maamuzi, hapa msaada wa Roho mtakatifu upo katika kutujulisha lipi ni dhambi na lipi sio hasa katika yale unayotaka kufanya, pia lipi ni la haki na lipi sio. Mwisho anatusaidia katika kufanya maamuzi, neno hukumu linawakilisha kuamua, hivyo roho mtakatifu anatusaidia kuchukua uamuzi ambao ni mzuri na wa kufaa ili kusudi la Mungu kwetu lifikiwe.
*Msaidizi kama kiongozi mwnye kututia kwenye kweli yote na mwenye kutupasha habari za mambo yajayo (Yohana 16:13).
Katika zaburi 32:8 neno linasema nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea,nitakushauri jicho langu likikutazama. Roho mtakatifu ndiye anayefanya kazi ya kutuongoza na kuhakiksha tunadumu katika kweli ya neno la Mungu kwa kila tulifanyalo.
Ni imani yangu kwa kuwa umejua, Roho mtakatifu anafanyikaje msaidizi basi utamtumia vizuri. Nafasi ya Roho ni sawa kabisa na nafasi ya chakula katika mwili wako. Nafikiri unajua usipokula kwa muda mrefu utakufa tu kwa lazima. Na hii ina maana ni lazima utumie chakula, hivyo basi ili uweze kulitumikia kusudi la Bwana katika kizazi chako ni lazima umtumie vizuri Roho mtakatifu kama msaidizi.
POKEA UWEZA WA ROHO MTAKATIFU NDANI YAKO, KWA JINA LA YESU
Comments